Tuesday, February 15, 2022

Waziri wa Mambo ya Nje wa UAE atembelea Banda la Tanzania, Dubai

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Abdullah bin Zayed tarehe 13 februari 2022 ametembelea Banda la Tanzania kwenye Maonesho ya Expo 2020 Dubai na kupokelewa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Mohamed Abdullah Mtonga ambaye pia ni Kamishna Jenerali wa Banda la Tanzania kwenye Maonesho ya Expo 2020 Dubai. 

Baada ya kuwasili kwenye banda hilo na kutembezwa, Mhe. Zayed aliipongeza Tanzania kwa kuandaa Banda lenye mvuto na linaloonyesha vivutio vya utalii pamoja na fursa zilizopo katika sekta mbalimbali kama za utalii, nishati, uchukuzi na madini. 

Kwa upande wake, Mhe. Balozi alimshukuru Mgeni wake kwa kuchagua kutembelea banda la Tanzania ikiwa ni moja ya nchi 192 zinazoshiriki maonesho hayo. Aidha, aliishukuru Serikali ya UAE kwa kuandaa vizuri Maonesho makubwa ya Expo 2020 Dubai, licha ya uwepo wa changamoto ya kuenea kwa ugonjwa wa COVID -19. 

Ushiriki wa Tanzania unatarajiwa kuwa na matokeo chanya na kuongeza idadi ya Watalii watakaoitembelea Tanzania, wawekezaji, mitaji pamoja na masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini. Katika Maonesho haya, Tanzania ni miongoni mwa nchi 50 ambapo kwa mara ya kwanza zinashiriki kwenye mabanda pekee  yaliyojengwa  kwa ufadhili wa Serikali ya UAE.

Katika hatua nyingine, Ubalozi wa Tanzania, UAE utasherehekea Siku ya Kitaifa (National Day) tarehe 27 Februari 2022. Sherehe hizo zitapambwa na shughuli mbalimbali zikiwemo Kongamano kubwa la Biashara na Uwekezaji litakalofanyika kwenye Ukumbi wa Ballon, Hoteli ya Jumeirah Beach tarehe 27 Februari 2022.

=====================================================================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Abdullah bin Zayed alipowasili kwenye Banda la Tanzania katika Maonesho ya Expo 2020 Dubai na kupokelewa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Mohamed Abdullah Mtonga 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Abdullah bin Zayed akiangalia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa nchini inayooneshwa kwenye Banda la Tanzania katika Maonesho ya Expo 2020 Dubai.

Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Mhe. Mohamed Abdullah Mtonga akibadilishana mawazo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Abdullah bin Zayed alipowasili kwenye Banda la Tanzania katika Maonesho ya Expo 2020 Dubai.


Monday, February 14, 2022

EMPLOYMENT OPPORTUNITIES


EMPLOYMENT OPPORTUNITIES

Tanzania is among 42 countries implementing a mutually agreed instrument voluntarily acceded to by someMember States of the African Union (AU) as a self-monitoring mechanism. Thegoal of the Mechanism is to foster the adoption of policies, standards and practices that lead to political stability, high economic growth, sustainable development and accelerated sub-regional and continental economic integration. The instrument thus, is a tool for sharing experiences, reinforcing best practices, identifying deficiencies and assessing capacity building needs resulting from periodic governance reviews.

The review process is overseen by the National Governing Council, which ensures credible periodic assessmentsthrough engagement of technically competent researchers coupled withimplementation of country-wide sensitisation and validation programmes. The Governing Council is supported by a National Secretariat, whose role is to implement plans and decisions of the Council in;information dissemination, sensitization, facilitating and overseeing the work of researchers, managing assessment events and their logistics, collecting public opinion and facilitating the work of external evaluators visiting the country.

Applications are hereby invited from suitably qualified candidates to fill in the following vacancies which exist in theNational Secretariat; 

Job Description
Title: Executive Secretary (ES)
Reporting to: The National Governing Council
Job Summary: 

The ES is the overall in-charge of the National Secretariat.

Key functions:

i. Chief Executive Officer and Accounting Officer of the National Secretariat;

ii. Responsible for planning, coordinating and controlling of activities of the the National Secretariat and advise the Governing Council on policies and programmes to be implemented;

iii. Ensure timely preparation of annual budgets and periodic performance reports of the Institution;

iv. Responsible for staff welfare of the Institution;

v. Chief spokes person of the Institution;

vi. Facilitate and coordinates fielding external review missions;

vii. Provide overall leadership of the NationalSecretariat;

viii. Liaise with the Government, Development Partners and other Continental bodies on the activities ofthe Institution; and

ix. Perform any other duties as may be directed by the Governing Council.

Qualifications, Skills and Experience

a) Masters degree at least in Public Administration, Economics, Business Administration, Law, Finance and Humanities related fields, a PHD will be an added advantage;

b) At least 10 years working experience at a senior level in a reputable organization;

c) Demonstrated ability to interact with Government establishment. Ability to interact with Development Partners will be an added advantage;

d) Demonstrated ability to write to a very high standard as evidenced by previous examples of relevant work accomplished in the field;

e) Fluency in spoken Kiswahili and English and ability to write lucid reports and documents in the said languages; knowledge of the other international languages will be an added advantage; 

f) Good knowledge of current development issues in Tanzania and National Development Strategies will be an addedadvantage;and

g) Outstanding peer relations.


Job Description
Title: Media and Communications Manager (MCM)
Reporting to: Executive Secretary

Job Summary:

To assist the Governing Council and the National Executive Secretary in providing the public with information on period governance review processes to be undertaken in Tanzania.

Key functions

i. Review and implement media and communication strategies of the institution;

ii. Undertake promotion of the activities of the institution and create positive image thereof;

iii. Coordinate preparation of the institution’spapers for workshops and conferences;

iv. Liaise with the media in covering events in which the institutionparticipates;

v. Coordinate press briefings for the institution;

vi. Oversees the publication of reports, leaflets, brochures etc. regarding activities of the institution;

vii. Coordinate preparation and production of the institutionarticles, programmes and news letters through various media channels;

viii. Up-date the institutioninformation in the website and other relevant online platforms;

ix. Advise other Units on the production of various documents; and

x. Perform any other duties as may be assigned by the National Executive Secretary.

Qualifications, skills and Experience

i. Minimum of Master's degree in governance, communication, marketing, media relations, journalism or related field;

ii. Minimum of 5 years of relevant professional experience in the development of public policy related to communications, including an appreciation of the role of social media and other modern communication techniques;

iii. A good understanding of governance challenges facingTanzania;

iv. Demonstrated ability to write to a very high standard as evidenced by previous examples of relevant work accomplished in the field;

v. Fluency in spoken Kiswahili and English and ability to write lucid reports and documents in the two mentioned languages; knowledge of the other international languages will be an added advantage.

vi. Demonstrated ability to communicate ideas and analyses clearly and tactfully, both orally and in writing.

vii. Outstanding peer relations;

Salary

The above positions carry a very competitive remuneration package.

Applications

Candidates should submit their applications attaching their resumes not later than20th February 2022to the following email address:



taprimreg18@gmail.com










 




Friday, February 11, 2022

MAWAZIRI WA SEKTA YA NISHATI WA EAC WASISITIZA UMUHIMU WA KUPATIKANA KWA NISHATI YA UHAKIKA

Mawaziri wa Sekta ya Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekutana leo tarehe 11 Februari 2022 jijini Arusha, Tanzania kwa lengo la kuhudhuria Mkutano wa 15 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya hiyo.

Mkutano huu ulitanguliwa na mikutano ya awali ngazi ya Wataalamu/Maafisa waandamizi uliofanyika tarehe 8 na 9 Februari 2022 na kufuatiwa na mkutano ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 10 Februari 2022.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huu umeongozwa na Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba (Mb.) ambaye ameambatana na; Katibu Mkuu Wizara ya Nishati - Tanzania Bara, Mhandisi Felschesmi Mramba; Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini -Zanzibar; Dkt. Mngereza Miraji; Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio; Kamishna wa Petroli na Gesi kutoka Wizara ya Nishati; Bw. Michael Mjinja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa ujumla.

Akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Waziri Makamba aliwakaribisha nchini wajumbe wa mkutano huo na kuwahakikishia kuwa mkutano utafanikiwa kuyafikia malengo yake kufuatia uongozi imara wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Peter Mathuki.

Vilevile akaeleza ukanda wa Afrika Mashariki umejaaliwa rasilimali nishati za kutoka hivyo, ni wakati sasa kwa kila nchi kuwa na mikakati imara ya kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana ili kuihakikishia jamii upatikanaji wa huduma zote zinazohitaji nishati.

“Tukiwa tunapitia changamoto za ugonjwa wa COVID-19 tumeshuhudia namna gani nishati zilihitajika katika kusaidia kuleta nafuu na kuokoa maisha ya wananchi wetu” alisema Mhe. Makamba.

Naye mwenyekiti wa mkutano huo na Waziri wa Nishati wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. Monica Juma alitumia nafasi hiyo kuwashukuru Watalamu na Makatibu Wakuu kwa kufanya maandalizi mazuri ya Mkutano huo na kusisitiza kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika ni moja ya viashiria vya kukua kwa uchumi wa nchi yeyote.

Pia akaeleza kukua kwa uchumi husaidia kupunguza utegemeze na hivyo jitihada za makusudi zinahitajika kuziwesha Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya uzalishaji wa kutosha viwandani na katika sekta ya kilimo.

Mkutano huu wa 15 wa Baraza la Mawaziri wa Kisekta la Nishati pamoja na mambo mengine utapitia na kutoa maamuzi juu ya; Tarifa ya hali ya utekelezaji wa maagizo ya mikutano iliyopita; Hatua iliyofikiwa hadi sasa katika sekta za Nishati Jadidifu, Nishati ya Umeme na Nishati ya Mafuta; pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Kitaifa na Kikanda ya Sekta za Nishati inayotekelezwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kadhalika mkutano huu utajadili kwa kina utekelezaji wa mradi wa kituo cha Nishati Jadidifu cha Afrika Mashariki; Mradi wa Kufua Umeme wa Nsongezi; Mradi wa kufua Umeme wa Murongo/Kigagati (14MW) na Taasisi ya Mamlaka ya udhibiti wa Nishati katika Nchi za Afrika Mashariki.


===================================================

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akiongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 15 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika leo tarehe 11 Februari 2022 jijini Arusha Tanzania.

Picha ya pamoja meza kuu; Wapili kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Mkutano na Waziri wa Nishati wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Monica Juma akiongoza mkutano huo, kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Peter Mathuki na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Bw. Christophe Bazivamo na mwisho kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati kutoka Jamhuri ya Kenya Mej. Gen. Dr. Gordon Kihalangwa wakifatilia mkutano.

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba (wa pili kutoka kushoto) pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati (Tanzania Bara), Mhandisi Felschemi Mramba (wa kwanza kushoto); Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini -Zanzibar, Dkt. Mngereza Miraji (wa pili kulia ) na Kamishna wa Petroli na Gesi Wizara ya Nishati, Bw. Michael Mjinja (wa kwanza kulia )wakifatilia mkutano. 

Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota akifuatilia majadiliano wakati wa mkutano huo.

Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio na Kamishna Msaidizi Maendeleo ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila wakifuatilia majadiliano. 

Maafisa Waandamizi kutoka Wizara za Nishati Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Maafisa Waandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)

Kutoka kushoto ni Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Mgeta Sabe pamoja na maafisa waandamizi kutoka Taasisi za Nishati wakifuatilia mkutano 

Ujumbe kutoka Kenya

Ujumbe kutoka Uganda


Balozi Kilima ateta na Wawekezaji kutoka Ujerumani

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Kilima amefanya mazungumzo na wawekezaji wa nishati ya jua kutoka Oman jijini Muscat hivi karibuni.
Wawekezaji hao ambao ni Dkt. Michael Voch na Bw. Claus Heim kutoka Ujerumani na Bw. Khalid Hamdoun M. Aljabri  na Bw. Mohammed Al Riyami kutoka Taasisi ya  IGD ya Oman wanakusudia kuwekeza katika sekta ya uzalishaji wa nguvu ya umeme wa kutumia Jua kwa teknolojia mpya inayoitwa Solar Container. Teknolojia hiyo inatumua maji kuzalisha hydrojen ambayo ndiyo inayotoa umeme na oxygen kama mabaki ya uzalishaji (byproducts)
Teknolojia hiyo tayari inatumika katika nchi za Ulaya na hivi karibuni itaanzishwa nchini Oman inaweza kutosheleza nyumba 200 Kwa kontena moja na pia inaweza kuunganishwa na Gridi ya Taifa
Wawekezaji hao pia wanakusudia kuanzisha miradi ya kilimo inayotumia Teknolojia ya Hydroponic system ambacho kinatunia eneo dogo lakini tija kubwa.
Wawekezaji imeiomba Serikali ya Tanzania kuwapatia eneo la uwekezaji pamoja na kuunganishwa na makampuni yatakayoweza kununua bidhaa watakazozalisha kama wanavyofanya nchini UAE, waneingia mkataba na Shirika la Ndege la Emirate kununua bidhaa za vyakula watakavyozalisha.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi aliwaeleza wawekezaji hao kwamba Tanzania inakarubisha uwekezaji katika sekta ya uzalishaji wa nguvu za umeme wa kutumia Jua kwani ni nishati mbadala na rahisi kutumika. Kwa upande wa mradi wa kilimo cha hydroponic, Mhe. Balozi alieleza kwamba kilimo hicho kinaweza kuwa mkombozi wa kilimo cha kutegemea mvua ambacho huwa ni cha msimu. Hivyo mradi huo unaweza kuongeza uzalishaji na kupata ziada ya kuuza nje ya nchi. 

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Kilima akizungumza na wawekezaji kutoka Ujerumani. Kulia Kwake ni Dkt. Michael Voch na Bw. Claus Heim

 

Thursday, February 10, 2022

MAKATIBU WAKUU WA SEKTA YA NISHATI WA EAC WAMEKUTANA JIJINI ARUSHA

Makatibu Wakuu wa sekta ya nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana leo tarehe 10 Februari 2022 jijini Arusha, Tanzania.

Mkutano wa Makatibu Wakuu ulitanguliwa na mkutano wa Maafisa Waandamizi uliofanyika tarehe 8 na 9 Februari 2922. Hii ni mikutano ya awali kwaajili ya maandalizi ya Mkutano wa 15 Wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika kesho tarehe 11 Februari 2022.


Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Makatibu Wakuu umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati (Tanzania Bara), Mhandisi Felchesmi Mramba ambaye ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini wa Zanzibar, Dkt. Mngereza Miraji.


Pamoja na mambo mengine Mkutano wa Makatibu Wakuu umepitia na kuandaa: Taarifa ya hali ya utekelezaji wa maagizo ya mikutano iliyopita; Hatua iliyofikiwa hadi sasa katika sekta za Nishati Umeme, Nishati Mafuta, na Nishati Jadidifu; pamoja na Utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Kitaifa na Kikanda ya Sekta za Nishati inayotekelezwa ndani ya Jumuiya ya Afrika  Mashariki.


Akiongea wakati wa ufunguzi wa mkutano mwenyekiti wa mkutano huo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati wa Jamhuri ya Kenya, Maj. Gen. Dkt. Gordon Kihalangwa, CBS alieleza kuwa uhaba wa nishati ndani ya nchi zetu na jumuiya kwa ujumla huleta changamoto kwa wananchi wote na kushusha shughuli za uchumi na pato la taifa kwa ujumla. Hivyo, akasisitiza umuhimu wa kuunganisha nguvu katika kutekeleza miradi ya nishati ya kitaifa na kikanda.


Vilevile akaeleza umuhimu wa sekta ya afya kupatiwa nishati ya kutosha na ya uhakika ili kuondoa changamoto za mara kwa mara zinazochangia kukosekana kwa huduma hizo.


 “Huduma za mama na mtoto pamoja na huduma nyingine za afya ni muhimu zikazingatia upatikanaji wa nishati ili kupunguza matatizo yatokanayo na kukosekana kwa nishati ya uhakika kwa baadhi ya vifaa vinavyohitaji nishati ya umeme na gesi” alisema Dkt. Gordon.


Mkutano huu umefanyika kwa njia ya mseto ambapo nchi za Tanzania, Kenya na Uganda wameshiriki mkutano wa ana kwa ana isipokuwa Burundi, Rwanda na Sudan Kusini wameshiriki kwa njia ya mtandao.

 

Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 15 wa Baraza la Mawaziri  la Kisekta la Jumuiya ya Afrika Mashariki la Nishati na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati (Tanzania Bara) akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini (Tanzania Zanzibar), Dkt. Mngereza Miraji wakifuatilia majadiliano kwenye mkutano huo.

Mwenyekiti wa Mkutano huo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati wa Jamhuri ya Kenya, Maj. Gen. Dkt. Gordon Kihalangwa, CBS (kati) akifungua Mkutano wa 15 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 10 Februari 2022 jijini Arusha, Tanzania. Kushoto ni Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati waJamhuri ya Kenya, Mhandisi Benson Mwakina. 

Kulia ni Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota akifuatilia majadiliano katika mkutano huo.

Kutoka kushoto Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Mgeta Sabe na Mhandisi Emmanuel Yessaya kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakifuatilia majadiliano.

Ujumbe wa Tanzania

Mkutano ukiendelea

Ujumbe kutoka Uganda

Ujumbe kutoka Kenya


WATANZANIA WAASWA KUILINDA NCHI

Imeelezwa kuwa jukumu la kulinda nchi ni la kila Mtanzania na vijana wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kwa kuwa wao ni chachu ya ukuaji uchumi wa nchi na viongozi watarajiwa wa Taifa hili.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola wakati alipokuwa anafungua semina ya siku moja kwa wanafunzi wa shule za sekondari za jijini Dodoma.

Balozi Kayola alisema Wizara imekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa wanafunzi ili wao kama vijana wawe na elimu stahiki kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa ambayo yatawawezesha kushiriki kikamilifu katika kutumia fursa za mtangamano ukiwemo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ( EAC).

Alieleza kuwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, vijana wametambuliwa kama kundi muhimu kwa maendeleo ya jumuiya hiyo, hivyo utoaji wa elimu hiyo ni muhimu ili vijana wafahamu fursa zilizopo katika nyanja mbalimbali za uchumi, utamaduni, elimu na siasa na namna na ya kuzichangamkia. 

Aliwambia wanafunzi hao kuwa Sera ya Vijana ya EAC imeweka bayana haki za vijana kuwa na uhuru wa kutembea na kuweka makazi kwenye nchi yoyote ya Jumuiya kwa madhumuni mbalimbali kama kutafuta elimu, ajira au kufanya biashara, hivyo ni muhimu kwa vijana hao wanapoelekea kuhitimisha masomo yao ya sekondari ni vyema wakaweka mipango ya kuchangamkia furza za EAC.

Balozi Kayola alihitimisha hotuba yake kwa kuwasihi vijana hao kuwa mabalozi waźuri wa Tanzania katika safari yao ya maisha na kuwaelimisha wanafunzi wenzao na jamii kwa ujumla ambao kwa sababu mbalimbali hawakuweza kupata elimu hiyo.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imejiwekea utaratibu wa kuelimisha makundi mbalimbali katika Jumuiya yakiwemo ya wanafunzi kuhusu Sera ya Mambo ya Nje. Na katika semina hiyo wanafunzi hao walielimishwa kuhusu majukumu ya Wizara, utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje, hatua za mtangamano wa EAC na fursa zake pamoja mchakato wa kuelekea shirikisho la kisiasa la EAC.

Semina ya siku moja kwa wanafunzi wa shule za sekondari za jijini Dodoma masuala mbalimbali ya Mtangamo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiendelea 

Sehemu ya wadau wakifuatilia semina ya siku moja kwa wanafunzi wa shule za sekondari za jijini Dodoma iliyofanyika kwenye ukumbi wa informatics katika Chuo Kikuu cha Dodoma

Picha ya patoja
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Balozi Agness Kayola akitoa hotuba ya ufunguzi wa semina ya siku moja kwa wanafunzi wa shule za sekondari za jijini Dodoma. Kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Bw. Emmanuel Buhohela. Wote kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Semina ikiendelea
Semina ikiendelea

Tuesday, February 8, 2022

RAIS WA BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA (AFDB) DKT. ADESINA AWASILI DODOMA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina alipowasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akisalimiana na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina alipowasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki BaloziLiberata Mulamula (katikati) akizungumza na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina (kushoto) huku Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (kulia) akiwasikiliza wakati Dkt. Adesina alipowasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma.


Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina (wa pili kushoto) akizungumza na wenyeji wake waliompokea katika Uwanja wa ndege Dodoma alipowasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma huku Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (kulia) wakifuatilia mazungumzo hayo.




Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina awasili jijini Dodoma akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini. Katika uwanja wa ndege wa Dodoma Dkt. Adesina amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba.

Dkt. Adesina yuko nchini kwa ziara ya siku tatu ambapo tarehe 09 February 2022 atashiriki katika uzinduzi wa ujenzi wa barabara za mzunguko zinazojengwa katika jiji la Dodoma utakaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Ujenzi wa barabara hizo za mzunguko zenye urefu wa kilomita 112.3 unagharamiwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na benki hiyo. Ujenzi wa barabara hizo utalifanya jiji la Dodoma kuwa na barabara za aina yake katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

MKUTANO WA 15 WA BARAZA LA MAWAZIRI LA KISEKTA LA NISHATI LA EAC WAFUNGULIWA JIJINI ARUSHA KATIKA NGAZI YA WATAALAMU

Mkutano wa 15 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki umefunguliwa leo tarehe 8 Februari 2022 jijini Arusha, Tanzania katika ngazi ya Wataalamu.


Mkutano huu utafanyika katika ngazi tatu ambapo umeanza na; Mkutano Ngazi ya Wataalamu unaofanyika tarehe 8 hadi 9 Februari 2022, utafuatiwa na Mkutano Ngazi wa Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 10 Februari 2022 na utamalizika kwa Mkutano Ngazi ya Mawaziri utaofanyika tarehe 11 Februari 2022.


Lengo la Mkutano huu ni kupitia na kuandaa taarifa ya hali ya utekelezaji wa Maamuzi/Maagizo ya mikutano iliyopita; Hatua iliyofikiwa hadi sasa katika sekta za Nishati Umeme, Nishati Mafuta, na Nishati Jadidifu; pamoja na Utekelezaji wa Miradi/Programu mbalimbali za Kitaifa na Kikanda ya Sekta za Nishati inayotekelezwa ndani ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.


Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano Ngazi ya Wataalamu unaongozwa na Kamishna Msaidizi Maendeleo ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila ambaye ameambatana na Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota, Mkurugenzi Idara ya Nishati na Madini kutoka Wizara ya Nishati na Madini Zanzibar, Mhandisi Said H. Mdungi pamoja na maafisa wengine Waandamizi kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wenye dhamana katika sekta ya nishati.


Mkutano Ngazi ya Wataalamu na Ngazi ya Makatibu Wakuu ni sehemu ya mikutano ya awali kwaajili ya maandalizi ya Mkutano wa  Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki utaofanyika tarehe 11 Februari 2022. 


Kushoto ni Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika Mkutano Ngazi ya Wataalamu na Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme katika Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila na kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota akifafanua jambo wakati wa majadiliano ya mkutano huo.

Mwenyekiti wa Mkutano Ngazi ya Wataalamu na Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu kutoka Jamhuri ya Kenya, Mhandisi Benson Mwakina (Kushoto) akiongoza majadiliano, kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Bw. Christophe Bazivamo. 

Kushoto ni Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Mgeta Sabe na wajumbe wengine wa Tanzania wakifatilia majadiliano.
Mkutano ukiendelea

Ujumbe wa Tanzania.

Sehemu nyingine ya Ujumbe wa Tanzania.



WAZIRI MULAMULA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KWENYE MKUTANO WA 46 WA DHARURA WA BARAZA LA MAWAZIRI WA EAC


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula, akiwa jijini Dodoma ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki katika Mkutano wa 46 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mkutano huu wa dharura umeitishwa kwa lengo la kujadili ripoti ya majadiliano yaliyofanyika tarehe 15 hadi 24 Januari 2022 jijini Nairobi, Kenya kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuhusu Nchi hiyo kujiunga na Jumuiya. 

Pamoja na muasula mengine yaliyojadiliwa Mkutano umekubaliana kuendelea kufanyia kazi kwa wakati hoja za pande zote mbili za majadiliano (EAC na Congo DRC), na kuandaa taarifa itakayowasilishwa kwa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ili kuharakisha uridhiaji wa maombi ya DRC

Mkutano huu wa dharura ambao umefanyika kwa njia ya mtandao umehudhuriwa na Nchi zote wanachama wa Jumuiya na kuongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo Waziri anayesimamia masuala ya Mtangamano wa Afrika Mashariki Mhe. Adam Mohamed kutoka nchini Kenya. 

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iliwasilisha maombi ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki tarehe 4 Juni 2019. 
Mkutano ukiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula, Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine (katika) na Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama Balozi Stephen Mbundi wa Wizara hiyo wakifuatilia Mkutano wa 46 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea
Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia Mkutano wa 46 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendele
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifuatilia mjadala uliokuwa ukiendelea kwenye Mkutano wa 46 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akichangia hoja kwenye Mkutano wa 46 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulifanyika kwa njia ya mtandao.