Friday, February 11, 2022

MAWAZIRI WA SEKTA YA NISHATI WA EAC WASISITIZA UMUHIMU WA KUPATIKANA KWA NISHATI YA UHAKIKA

Mawaziri wa Sekta ya Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekutana leo tarehe 11 Februari 2022 jijini Arusha, Tanzania kwa lengo la kuhudhuria Mkutano wa 15 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya hiyo.

Mkutano huu ulitanguliwa na mikutano ya awali ngazi ya Wataalamu/Maafisa waandamizi uliofanyika tarehe 8 na 9 Februari 2022 na kufuatiwa na mkutano ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 10 Februari 2022.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huu umeongozwa na Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba (Mb.) ambaye ameambatana na; Katibu Mkuu Wizara ya Nishati - Tanzania Bara, Mhandisi Felschesmi Mramba; Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini -Zanzibar; Dkt. Mngereza Miraji; Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio; Kamishna wa Petroli na Gesi kutoka Wizara ya Nishati; Bw. Michael Mjinja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa ujumla.

Akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Waziri Makamba aliwakaribisha nchini wajumbe wa mkutano huo na kuwahakikishia kuwa mkutano utafanikiwa kuyafikia malengo yake kufuatia uongozi imara wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Peter Mathuki.

Vilevile akaeleza ukanda wa Afrika Mashariki umejaaliwa rasilimali nishati za kutoka hivyo, ni wakati sasa kwa kila nchi kuwa na mikakati imara ya kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana ili kuihakikishia jamii upatikanaji wa huduma zote zinazohitaji nishati.

“Tukiwa tunapitia changamoto za ugonjwa wa COVID-19 tumeshuhudia namna gani nishati zilihitajika katika kusaidia kuleta nafuu na kuokoa maisha ya wananchi wetu” alisema Mhe. Makamba.

Naye mwenyekiti wa mkutano huo na Waziri wa Nishati wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. Monica Juma alitumia nafasi hiyo kuwashukuru Watalamu na Makatibu Wakuu kwa kufanya maandalizi mazuri ya Mkutano huo na kusisitiza kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika ni moja ya viashiria vya kukua kwa uchumi wa nchi yeyote.

Pia akaeleza kukua kwa uchumi husaidia kupunguza utegemeze na hivyo jitihada za makusudi zinahitajika kuziwesha Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya uzalishaji wa kutosha viwandani na katika sekta ya kilimo.

Mkutano huu wa 15 wa Baraza la Mawaziri wa Kisekta la Nishati pamoja na mambo mengine utapitia na kutoa maamuzi juu ya; Tarifa ya hali ya utekelezaji wa maagizo ya mikutano iliyopita; Hatua iliyofikiwa hadi sasa katika sekta za Nishati Jadidifu, Nishati ya Umeme na Nishati ya Mafuta; pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Kitaifa na Kikanda ya Sekta za Nishati inayotekelezwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kadhalika mkutano huu utajadili kwa kina utekelezaji wa mradi wa kituo cha Nishati Jadidifu cha Afrika Mashariki; Mradi wa Kufua Umeme wa Nsongezi; Mradi wa kufua Umeme wa Murongo/Kigagati (14MW) na Taasisi ya Mamlaka ya udhibiti wa Nishati katika Nchi za Afrika Mashariki.


===================================================

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akiongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 15 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika leo tarehe 11 Februari 2022 jijini Arusha Tanzania.

Picha ya pamoja meza kuu; Wapili kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Mkutano na Waziri wa Nishati wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Monica Juma akiongoza mkutano huo, kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Peter Mathuki na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Bw. Christophe Bazivamo na mwisho kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati kutoka Jamhuri ya Kenya Mej. Gen. Dr. Gordon Kihalangwa wakifatilia mkutano.

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba (wa pili kutoka kushoto) pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati (Tanzania Bara), Mhandisi Felschemi Mramba (wa kwanza kushoto); Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini -Zanzibar, Dkt. Mngereza Miraji (wa pili kulia ) na Kamishna wa Petroli na Gesi Wizara ya Nishati, Bw. Michael Mjinja (wa kwanza kulia )wakifatilia mkutano. 

Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota akifuatilia majadiliano wakati wa mkutano huo.

Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio na Kamishna Msaidizi Maendeleo ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila wakifuatilia majadiliano. 

Maafisa Waandamizi kutoka Wizara za Nishati Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Maafisa Waandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)

Kutoka kushoto ni Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Mgeta Sabe pamoja na maafisa waandamizi kutoka Taasisi za Nishati wakifuatilia mkutano 

Ujumbe kutoka Kenya

Ujumbe kutoka Uganda


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.