Thursday, February 3, 2022

WAZIRI MULAMULA AFANYA MAZUNGUMZO NA UJUMBE WA SERIKALI YA URUSI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Taasisi ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Masuala ya Kibinadamu kutoka nchini Urusi Bw. Yevgeny Primakov leo tarehe 03 Februari 2022 katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Bw. Primakov ameambatana na Balozi wa Urusi nchini, Mhe. Yuri Popov pamoja na Mjumbe kutoka Serikali ya Urusi, Bw. Egor Utkin.

Wawakilishi hao kutoka Serikali ya Shirikisho la Urusi waliwasilisha ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladimirovich Putin.

Pamoja na mambo mengine viongozi hao walijadili juu ya kuimarisha ushirikiano uliopo na kwamba kwa sasa Tanzania na Urusi zinajikita zaidi katika kufungua maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji, utalii na masuala mengine ya kiuchumi kwa maslahi mapana ya mataifa hayo.

Waziri Mulamula alieleza kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano mzuri na wa kihistoria ambao uliasisiwa na Waasisi wa Mataifa hayo mawili.  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kushoto) akipokea ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia)kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladimirovich Putin

Mazungumzo yakiendelea. 

Picha ya pamoja Mhe. Waziri na Ujumbe kutoka Serikali ya Urusi.
Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme, na Kulia kwake ni Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Mhe. Fredrick Kibuta.
 Kutoka kulia kwa Mhe. Waziri ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Masuala ya Kibinadamu nchini Urusi, Bw. Evgeny Primakov, Balozi wa Urusi nchini,
 Mhe. Yuri Popov pamoja na Mjumbe kutoka serikali ya Shirikisho la Urusi, Bw. Egor Utkin.

Waziri Mulamula akikabidhi shajara.
                                                                                      
Picha ya Pamoja.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.