Wednesday, June 8, 2022

WAZIRI MULAMULA ATOA WITO KWA JUMUIYA ZA KIKANDA KUSHIRIKIANA KATIKA KUTEKELEZA MAKUBALIANO YA AfCFTA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula ametoa wito kwa Jumuiya za kiuchumi za Kikanda za Afrika kushirikiana katika utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

Waziri Mulamula amebainisha hayo alipokuwa akifungua Mkutano wa Pili (2) wa Uratibu wa Watendaji Wakuu wa Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda (RECs) kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliofanyika tarehe 7 Juni 2022 jijini Arusha.

Mkutano huo uliohudhuriwa na Wakuu wa Jumuiya za Kuichumi za Kikanda ulilenga kuwakutanisha Wakuu hao na Sekretariati ya AfCFTA ili kwa pamoja waweze kujadili na kuweka mikakati endelevu ya utekelezaji wa makubaliano ya AfCFTA. Mikakati hiyo ni pamoja na kubuni namna ya kupata rasilimali zitakazoiwezesha Sekretariati ya AfCFTA kuendesha shughuli zake bila kutegemea ufadhili wa nchi za nje, na kuandaa mfumo wa pamoja wa ushirikiano utakaoziwezesha pande zote mbili kutekeleza makubaliano ya AfCFTA kwa ufanisi.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo Waziri Mulamula alieleza kuwa uchumi wa Afrika utaendelea kukua kwa kasi zaidi endapo nchi za Afrika zifanikiwa kuunganisha shughuli za kiuchumi ikiwemo kuendesha biashara baina yetu wenyewe. Waziri Mulamula aliongeza kusema, anamatarajio makubwa kuwa ndoto za waasisi wa Umoja wa Afrika za kuwa na Afrika yenye umoja na iliyounganishwa kiuchumi zinaenda kutimia siku za usoni.

“Nina imani kubwa kuwa uwepo wa mikutano ya mfumo huu unaounganisha Sekretariati ya Eneo Huru la Afrika na Watendaji wa Jumuiya za Uchumi za Kikanda, utawezesha kupatikana kwa mapendekezo ya sera zinazotekelezeka na kujenga ushirikiano thabibiti ambao utawezesha kutatua changamoto mbalimbali zinazokwamisha ustawi wa biashara miongoni mwa nchi za Afrika, na hatimaye kufikia ndoto za waasisi wetu za kuwa na Afrika iliyounganishwa kiuchumi”. Alisema Balozi Mulamula

Vilevile Waziri Mulamula alieleza kuwa pamoja na jitihada za kuendelea kushirikiana katika kutekeleza makubaliano ya AfCFTA ni muhimu pia kwa Jumiya za Kiuchumi za Kikanda na Serikali za Afrika kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji inayounganisha bara la Afrika ambayo itasadia kwa kiasi kikubwa kuokoa gharama na muda wa usafirishaji wa bidhaa na huduma miongoni mwa Nchi za Afrika.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya AfCFTA, Mhe. Wamkele Mene alisema kuwa utekelezaji wa Mkataba wa AfCFTA ni wa lazima kwa maendeleo ya Afrika hivyo ni muhimu pia kwa sekta binafsi kupewa kipaumbele kwenye utekelezaji wa makubaliano ya AfCFTA.

Mhe. Wamkele aliendelea kusisitiza kuwa ni muhimu kwa nchi za Afrika kuendelea kuhimiza katika ukuzaji wa viwanda na kuwekeza katika kuboresha bidhaa zake, ili kumudu ushindani wa soko la kimataifa na hatimaye kuweza kunufaika na soko kubwa katika biashara ya kimataifa na kuongeza mchango wake katika pato la Dunia.

“Inasikitisha kuona kwamba nchi 55 za Afrika kwa sasa zinachangia asilimia 2 tu ya pato la biashara ya duniani na asilimia 3 ya Pato la Dunia huku Singapore, jiji lenye ukubwa wa maili 600 za mraba pekee, likichangia asilimia 6.2 ya biashara ya kimataifa”. Alisema Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya AfCFTA Mhe. Wamkele.

Aidha, Mhe. Wamkele alisisitiza umuhimu wa ushirikiano thabiti na utendaji wa karibu kati ya RECs na Sekretarieti ya AfCFTA ili kuhakikisha kuwa matokeo ya AfCFTA yanawiana na maendeleo ya kikanda katika ushirikiano na ukuajia wa biashara.

Mkutano huu umefanyika ikiwa ni utelekezaji wa agizo la Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali ambalo uliielekeza Sekretariati ya AfCFTA, Tume ya Umoja wa Afrika na RECs kukaa pamoja na kuandaa mfumo wa ushirikiano sambamba na kuoanisha programu na shughuli zao ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa makubaliano ya AfCFTA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifungua Mkutano wa Pili (2) wa Uratibu wa Watendaji Wakuu wa Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda (RECs) kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliofanyika jijini Arusha.
Sehemu ya Meza Kuu wakifuatilia Mkutano uliokuwa ukiendelea
Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Bernard Haule, akifuatilia Mkutano wa Pili (2) wa Uratibu wa Watendaji Wakuu wa Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliokuwa ukiendelea jijini Arusha
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili (2) wa Uratibu RECs kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliofanyika jijini Arusha.

Katibu Mkuu wa Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Peter Mathuki akizungumza kwenye Mkutano wa Pili (2) wa uratibu wa RECs kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliofanyika jijini Arusha.
Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya AfCFTA Mhe. Wamkele Mene akisisitiza jambo kwenye mkutano wa Mkutano wa Pili (2) wa Uratibu wa RECs kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliofanyika jijini Arusha.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula, Watendaji wa RECs na Viongozi Waandamizi kutoka Serikalini na Sekta binafsi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano wa Pili (2) wa Uratibu wa RECs kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliofanyika jijini Arusha kufikia tamati.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwasili katika ukumbi wa mikutano wa Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Alioambatana nao mstari wa mbele ni Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya AfCFTA Mhe. Wamkele Mene (wa kwanza kulia), Katibu Mkuu wa Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Peter Mathuki (wapili kulia), Rais wa Baraza la Biashara la Afrika Dkt. Amany Asfour (wa pili kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia Sekta za Uzalishaji na Huduma za Jamii Mhe. Chritophe Bazivamo

Saturday, June 4, 2022

WIZARA YA MAMBO YA NJE YAWAPIGA MSASA WABUNGE KUHUSU UMUHIMU WA KUDHIBITI MIGOGORO

Serikali ya Tanzania imechangia kwa kiasi kikubwa jitihada za kuleta amani barani Afrika hususan eneo la ukanda wa maziwa makuu, kupitia ushiriki wake katika kutatua migogoro na kuchangia vikosi vya kulinda amani.


Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab alipozungumza leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa warsha kuhusu Utatuzi wa Migogoro iliyotolewa na Wizara kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa lengo la kuwajengea uwezo.


Amesema kuwa, kwa miaka mingi Tanzania imeendeelea kushirikishwa kwenye utatuzi wa migogoro na kuchangia vikosi vya kulinda amani kutokana na kuaminika kwake kikanda na kimataifa kwenye eneo hilo na hii inatokana  na hali ya amani na utulivu wa kisiasa, kiuchumi na kijamii iliyopo nchini.


“Jukumu la Wizara ni kusimamia uhusiano baina ya Tanzania na nchi mbalimbali na mashirika ya kikanda na kimataifa kwa lengo la kulinda maslahi ya nchi. Ni kutokana na kutekeleza jukumu hilo, Tanzania imeendelea kuaminika na kushirikishwa katika utatuzi wa migogoro mbalimbali Afrika. Hiki ni kielelezo cha kuaminika”, amesema Balozi Rajab.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa amesema kuwa viongozi wakiwemo Wabunge wanayo nafasi kubwa katika kuchangia amani kupitia nafasi zao kwa kutoa elimu ya uzalendo kwa wananchi kwa kuwaelimisha kutojiingiza kwenye masuala yanaweza kusababisha migogoro na uvunjifu wa amani ndani ya jamii.


“Kila mmoja wetu atumie nafasi yake kuzuia migogoro katika jamii ikiwemo ile inayosababishwa na siasa. Wizara iendelee kutoa semina hizi na Kamati itaendelea kutoa ushirikiano na ushauri unaohitajika kwa Wizara”, alisisitiza Mhe. Kawawa.


Akiwasilisha mada kuhusu “Utatuzi, Udhibiti na Usuluhishi wa Migogoro” Mkufunzi kutoka Chuo cha Diplomasia cha jijini Dar es Salaam, Dkt. Ally Masabo amesema ujenzi wa imani na kujiamini kwa wananchi na siasa safi ni njia mojawapo ya kudhibiti migogoro ndani ya jamii. Pia ameongeza kuwa, Tanzania ipo mstari wa mbele katika utatuzi wa migogoro na uchangiaji wa vikosi vya ulinzi wa amani kutokana na ukweli kwamba eneo lote linaloizunguka Tanzania likiwa salama nchi inanufaika zaidi.


“Tanzania ni nchi ya 13 ulimwenguni katika kuchangia walinzi wa amani na ya sita Afrika. Hii inatokana na imani ya Tanzania kwamba amani ni chanzo cha maendeleo. Tanzania inaamini kwamba nchi zinazotuzunguka zikiwa salama nchi inanufaika kuliko zikiwa katika migogoro” amesema Dkt. Masabo.


Wakichangia mada hiyo, Wajumbe hao wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama wamepongeza utaratibu wa Wizara wa kutoa semina za aina hiyo kwao na kuongeza kuwa, ipo haja kwa Serikali kuwa na Program za uelimishaji umma kuanzia ngazi za chini kuhusu umuhimu wa amani na madhara yanayotokana na migogoro katika jamii.


Pia wamesisitiza elimu ya kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kwa kufanya kazi na kujishughulisha itolewe kwa wingi ili kuepuka migogoro inayosababishwa na wananchi kutojishughulisha na kusubiri Serikali iwanyie kila kitu.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Balozi Fatma Rajab akifungua mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama yaliyofanyika leo tarehe 4 Juni 2022 Bungeni, jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa akifafanua jambo wakati wa majadiliano kwenye mafunzo hayo.

Mkurugenzi wa Idara wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi akitoa neno la shukurani kwa jumbe wa kamati hiyo.
Mhe. Cosato Chumi akichangia hoja wakati wa majadiliano, kulia ni  Mhe. Janeth Masaburi akifatilia mafunzo.

Sehemu ya Wajumbe wa kati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, kutoka kushoto ni Mhe. Bonnah Kamol na Mhe. Fakharia Shomar Khamis wakifuatilia uwasilishaji wa mada ya migogoro.




Mhe. Abeid Ramadhani akichangia hoja wakati wa majadiliano kwenye mafunzo hayo.

Mkufunzi kutoka Chuo cha Diplomasia, Dkt. Ally Masabo akiwasilisha mada ua udhibiti wa migogoro kwa kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Mafunzo yakiendelea, wa kwanza kulia ni Mhe. Stella Ikupa akifuatilia majadiliano.


Mhe. Zahor Mohamed Haji akifafanua juu ya umuhimu wa mafunzo hayo kwa Waheshimiwa Wabunge na umuhimu wa kulinda kauli zao ili kuepuka kuwa vyanzo vya migogoro katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Felista Njau akieleza umuhimu wa Wabunge kutambua matatizo ya msingi katika jamii wanazoziwakilisha na kuyatatua kwa wakati ili kuepuka kuzuka kwa  migogoro na kuathiri amani ya Taifa.
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasiliamali Watu, Bw. Alex Mfungo akichangia jambo wakati wa majadiliano kwenye mafunzo hayo.
Kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia, Bw. Felix Wandwe na Mkurugenzi wa Idara ya Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Caroline Chipeta wakifuatitilia mafunzo.

Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifatilia mafunzo.
Sehemu nyingine ya Maafisa wa Wizara ya Mambo ya nje wakifuatilia mafunzo.


TZ, ITALIA KUONGEZA NGUVU SEKTA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI

Na Mwandishi wetu, Dar 

Tanzania na Italia zimeahidi kushirikiana kukuza na kuendeleza sekta ya biashara ya uwekezaji kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Akihutubia sherehe za maadhimisho ya 76 ya siku ya Kitaifa  ya Jamhuri ya Italia, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) alisema Tanzania imeboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kuwasihi wafanyabiashara wa Italia kuja kuwekeza nchini kwa kuwa ni salama zaidi.

“Natumia fursa hii kuwahakikishia ushirikiano wetu wa kukuza na kuendeleza biashara na uwekezaji nchini, Serikali imechukua jitihada mbalimbali za kuwavutia wawekezaji kuwekeza hapa nchini ikiwemo kuondoa vikwazo vya biashara,” alisema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula aliongeza kuwa, Tanzania na Italia zimekuwa na utamaduni wa kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kupitia majukwaa mbalimbali ya biashara na matokeo chanya ya majukwaa hayo yameanza kuonekana ambapo Disemba, 2021 kupitia kongamano la biashara na uwekezaji lililofanyika Italia, kampuni ya Kiitaliano ‘Suness Limited’ inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ilisaini makubaliano na Shirika la Taifa la madini (Stamico) kwa ajili ya kuendeleza mradi wa shaba inayopatikana Kilimanjaro.

“Ni Imani yangu kuwa kupitia kongamano la biashara na uwekezaji litakalofanyika mwezi Septemba 2022 Jijini Dar es Salaam na Zanzibar litatoa fursa nyingi zaidi kwa pande zote mbili kuchangamkia fursa zinazopatikana kwenye sekta za kilimo, viwanda, miundombinu, elimu, utalii na uchumi wa buluu,” alisema Balozi Mulamula

Pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula aliishukuru Serikali ya Italia kwa ushirikiano imara wa kuchangia maendeleo ya Tanzania ambapo wiki ijayo Tanzania na Italia zitasaini makubaliano ya mkopo wa masharti nafuu wa Euro milioni 20 kwa ajili ya kuboresha elimu ya ufundi katika mikoa ya Mbeya, Arusha, mwanza, Songwe, Zanzibar na Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi ameipongeza Tanzania kwa jitihada kubwa za kuboresha na kuimarisha mazingira ya biashara nchini.

“Kwa kweli tunafurahishwa sana na namna mazingira ya biashara yanavyoboreshwa hapa Tanzania, kwa kweli tutaendelea kuwashawishi wafanyabiashara wetu waje kuwekeza hapa kwani ni sehemu salama uya kuwekeza,” alisema Balozi Lombardi

Aliongeza kuwa kitendo cha Tanzania kuviondoa vikwazo vya biashara kimeongeza imani kubwa kwa wafanyabiashara na wawekezaji wengi duniani kuiona Tanzania ni salama. Aidha, Balozi Lombard alimpongeza Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kuimarisha Diplomasia ya Uchumi na mataifa mengine duniani.

“Napenda kuwahakikishia kuwa Italia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuimarisha uhusiano uliopo baina yetu kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” aliongeza Balozi Lombardi.

Tanzania na Italia zimekuwa zikishirikiana katika Nyanja za kilimo, afya, elimu, maji, nishati, utalii na maendeleo ya sekta binafsi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Kiongozi wa Mabalozi nchini ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini Mhe. Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed katika sherehe za maadhimisho ya 76 ya siku ya Kitaifa  ya Jamhuri ya Italia, jana jioni Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba yake katika sherehe za maadhimisho ya 76 ya siku ya Kitaifa  ya Jamhuri ya Italia, jana jioni Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi akiwasilisha hotuba yake katika sherehe za maadhimisho ya 76 ya siku ya Kitaifa  ya Jamhuri ya Italia, jana jioni Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akikata keki katika sherehe za maadhimisho ya 76 ya siku ya Kitaifa  ya Jamhuri ya Italia, jana jioni Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi wakishangilia baada ya kukata keki katika sherehe za maadhimisho ya 76 ya siku ya Kitaifa  ya Jamhuri ya Italia, jana jioni Jijini Dar es Salaam



Friday, June 3, 2022

TANZANIA, IRELAND KUONGEZA MAENEO YA USHIRIKIANO

Na Mwandishi wetu, Dar

Tanzania na Ireland zimeahidi kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano ambayo ni biashara na uwekezaji, kilimo, viwanda vya nguo pamoja na ujenzi.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipokutana kwa mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Ireland, Bw. Joe Hackett katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

“Ireland imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo kwa Tanzania katika masuala ya kijamii ikiwemo elimu, kusaidia kaya masikini na kuwajengea uwezo wanawake, kupitia kikao chetu cha leo tumekubaliana kuangalia namna ya kuongeza wigo wa ushirikiano katika sekta ya biashara na uwekezaji, kilimo hasa parachichi, viwanda vya nguo pamoja na ujenzi ili kuweza kuinua zaidi uchumi wetu kwa maslahi ya pande zote mbili,” amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa kupitia biashara na uwekezaji wafanyabiashara wa Kitanzania watapata fursa ya kuchangamkia biashara zinazopatikana nchini Ireland lakini pia wafanyabiashara wa Ireland watapata fursa ya kuwekeza nchini Tanzania.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Ireland, Bw. Joe Hackett amesema Ireland wamefurahishwa na hatua ambazo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikizichukua katika kuimarisha na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kuinganisha Tanzania na mataifa mengine ulimwenguni.

“Ireland tunaiona Tanzania ikiwa tulivu na mazingira mazuri ya kuwavutia wafanyabiashara, tutaongea na wafanyabiashara na kuwaeleza kuwa Tanzania ni sehemu salama kuwekeza,” amesema Bw. Hackett

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya uhusiano baina ya Tanzania na Ireland katika maeneo yenye maslahi kwa pande zote mbili. 

Katika tukio jingine, Balozi Mulamula ameongoza majadiliano ya mpango wa kuimarisha diplomasia ya uchumi ya Tanzania. Wengine walioshiriki katik majadiliano hayo ni Balozi wa Uswisi nchini mhe. Didier Chassot, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Zlatan Milišić na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Christine Musisi, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme pamoja na wadau wengine wa maendeleo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Ireland, Bw. Joe Hackett katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Maongezi ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Ireland, Bw. Joe Hackett yakiendelea katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Idara ya Amerika na Ulaya kutoka Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (Mwenye Koti Jekundu) akifuatiwa na Afisa Dawati Bw. Laurian Ntwale, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga pamoja na Katibu wa Mhe. Waziri, Bw. Seif Kamtunda  wakifuatilia kikao cha Balozi Liberata Mulamula na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Ireland, Bw. Joe Hackett katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Ireland, Bw. Joe Hackett katika picha ya pamoja na Balozi Mindim Kasiga, Balozi Swahiba Mndeme na Bw. Laurian Ntwale kutoka wizarani pamoja na Balozi wa Ireland nchini, Mhe. Mary O’Neil na maafisa waandamizi kutoka ubalozi wa Ireland nchini. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongoza kikao cha majadiliano ya Mpango wa kuimarisha diplomasia ya uchumi ya Tanzania katika kikao cha majadiliano ya Mpango wa kuimarisha diplomasia ya uchumi ya Tanzania katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Christine Musisi akieleza jambo katika kikao cha majadiliano ya Mpango wa kuimarisha diplomasia ya uchumi ya Tanzania katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mtaalam akiwasilisha mada katika kikao cha majadiliano ya Mpango wa kuimarisha diplomasia ya uchumi ya Tanzania katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na washiriki wa majadiliano ya Mpango wa kuimarisha diplomasia ya uchumi ya Tanzania katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 



Thursday, June 2, 2022

SERIKALI NA KAMPUNI YA LONGPIN WAKUBALIANA KUHARAKISHA UWEKEZAJI KATIKA KILIMO CHA SOYA


Viongozi,Watendaji na Maafisa Waandamizi wa Serikali wamekutana na kufanya mazungumzo na Watendaji wa Kampuni ya Longping High Tech ya China inayotarajia kuwekeza katika kilimo cha soya nchini. Mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ofisi ya Wizara ya Kilimo jijini Dodoma yalilenga kujadili namna ya kuharakisha utekelezaji wa mradi huo. 

Akizungumza katika mkutano huo Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Antony Mavunde amesema kuwa Serikali inashauku kubwa kuona uwekezaji huu ambao unaenda kuwainua wakulima wadogo kiuchumi, unaanza kutekelezwa mapema iwezekanavyo. Naibu Waziri mavunde aliongeza kuwa kwa upande wa serikali tayari imeshaweka mazingira mazuri na rafiki ya kuhakikisha kuwa mradi huu unatekelezwa kwa mafanikio nchini. 

“Pamoja na mambo mengi muhimu tuliyofanya ili kuharakisha uwekezaji huu wa kuongeza uzalishaji na ubora wa soya nchini, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kuanzia imetenga takriban hekari 27000 ambazo zitatumika katika uzalishaji wa mbegu za soya” Alisema Naibu Waziri Mavunde.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Longping High Tech Bw. Liang Shi ameeleza kuwa baada ya ziara waliyoifanya katika maeneo mbalimbali nchini wamepata mwamko zaidi wa kuanza uwekezaji haraka iwezekavyo.

“Katika kipindi tulichokuwepo hapa nchini tumetembelea maeneo mbalimbali tumeona ardhi na hali ya hewa nzuri kwa uzalishaji wa soya, utayari wa wakulima na zaidi utayari wa Serikali katika kupokea uwekezaji wetu ambao pamoja masuala mengine unatoa uhakika wa soko la soya za wakulima. Tumefarijika na kuhamasika zaidi hivyo tuna ahidi uwekezaji wetu utaanza mara moja”. Amesema Bw. Shangyang Wu

Watendaji wa Kampuni ya Longping High Tech wamekuwepo nchini kwa kipindi cha takribani wiki mbili ambapo wametembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Ruvuma, Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa na Katavi kwa lengo la kuangalia maeneo ya uzalishaji wa soya sambamba na kuonana na kufanya mazunguzmo na wadau katika sekta hiyo. 
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Antony Mavunde akizungumza wakati wa kikao baina ya Viongozi,Watendaji na Maafisa Waandamizi wa Serikali na Watendaji wa Kampuni ya Longping High Tech ya China kilichofanyika katika ofisi ya Wizara hiyo jijini Dodoma.
Balozi wa Tanzania nchini Brazil Mhe. Balozi Prof. Adelardus Kirangi akizungumza wakati wa kikao baina ya Viongozi, Watendaji na Maafisa Waandamizi wa Serikali na Watendaji wa Kampuni ya Longping High Tech ya China kilichofanyika katika ofisi ya Wizara hiyo jijini Dodoma.
Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Mbelwa Kairuki akizungumza wakati wa kikao baina ya Viongozi, Watendaji na Maafisa Waandamizi wa Serikali na Watendaji wa Kampuni ya Longping High Tech ya China kilichofanyika katika ofisi ya Wizara hiyo jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Biashara za Nje na Fedha wa Kampuni hiyo Bw. Shangyang Wu akizungumza kwenye kikao baina ya Viongozi, Watendaji na Maafisa Waandamizi wa Serikali na Watendaji wa Kampuni ya Longping High Tech ya China kilichofanyika katika ofisi ya hiyo jijini Dodoma.
Mkutano ukiendelea
Mkutano ukiendelea
Viongozi,Watendaji, Maafisa Waandamizi wa Serikali, wadau kutoka sekta binafsi na Watendaji wa Kampuni ya Longping High Tech ya nchina China wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano uliofanyika katika ofisi ya Wizara ya Kilimo jijini Dodoma

TANZANIA KUENDELEA KUCHANGIA OPERESHENI ZA ULINZI WA AMANI

Na Mwandishi wetu, Dar

Katika jitihada za kuwaunga mkono walinda amani, Tanzania imeahidi kuendelea kuchangia zaidi katika operesheni za ulinzi wa amani duniani ili kuendelea kunufaika na matunda ya amani.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipohutubia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.   

“Walinda amani wa Umoja wa Mataifa ni kiungo muhimu katika mfumo wa amani na usalama wa dunia kwani wamejitolea maisha yao kutumikia katika hali ngumu ili mamilioni ya watu ulimwenguni waishi kwa amani,” amesema Balozi Mulamula. 

Balozi Mulamula ameongeza kuwa nchi nyingi duniani zimekuwa zikifanya kazi kwa bidii ili kutekeleza na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo 2030, amani ni sehemu muhimu katika azma hiyo. 

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuendelea kupaza sauti katika kuhakikisha amani inapatikana duniani kama kaulimbiu ya mwaka huu inavyosisitiza, ni juu yetu kuchukua jukumu hili kwa pamoja, kutafuta misingi ya pamoja, kuzingatia umuhimu wa mazungumzo na upatanishi kama njia ya kutatua migogoro kwa njia za amani.

“Tanzania inajivunia kushika nafasi ya 13 kwa mchango mkubwa katika operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa duniani. Hadi Machi mwaka huu, Tanzania imechangia walinda amani 1,485 katika nchi za  Lebanon, Afrika ya Kati, Sudan Kusini  na DRC ambapo matokeo chanya ya uwepo wao katika nchi hizi yameonekana,” ameongeza Balozi Mulamula.

Awali akihutubia maadhimisho hayo kwa Niaba ya Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Zlatan Milišić ameipongeza Tanzania kwa kuungana na Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani.

“Tanzania imekuwa na mchango mkubwa katika jitihada za kuendelea kuchangia walinda amani katika mataifa mbalimbali ikiwemo DRC, Lebanon na Sudani Kusini, Amesema Bw. Milišić na kuongeza kuwa amani ni ustawi wa maendeleo kwa taifa lolote lile duniani. 

Pamoja na mambo mengine, Bw. Milišić amesema Umoja wa Mataifa unatambua mchango wa Tanzania katika kulinda amani ndani ya nchi na amani katika mataifa mengine.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongoza viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na mabalozi katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa  katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiweka ua katika  mnara wa Mashujaa uliopo Mnazi mmoja wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Zlatan Milišić  pamoja na baadhi wa viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiimba nyimbo ya taifa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa  

Meza kuu wakifuatilia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa  

Sehemu ya Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini wakifuatilia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa 

Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Zlatan Milišić akiwasilisha hotuba yake katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba yake katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa

Mabalozi pamoja na maafisa waandamizi wa vyombo vya ulinzi na usalama katika picha ya pamoja 




Wednesday, June 1, 2022

ATCL KUANZA TENA SAFARI CHINA MWEZI JUNI 2022

Serikali imesema kuanzia mwezi Juni 2022 Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limeruhusiwa kusafirisha tena abiria nchini China.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) jana jioni wakati alipokuwa akijibu hoja za wabunge kuhusu mkakati wa Wizara katika kukuza na kuetekeleza Diplomasia ya Uchumi.

“Lakini pia Mhe. Naibu Spika kuna habari njema, na Habari ambayo nimeipokea wiki hii ni kwamba kuanzia Juni mwaka huu Shirika letu la ndege limeruhusiwa kuanza tena safari zake kubeba abiria kwenda China,” alisema Balozi Mbarouk.

Machi 2020, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) lilitangaza kusitisha safari za ndege kuelekea China kutokana na kuwapo kwa ugonjwa wa virusi vya Corona.