Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewasili
nchini Rwanda tarehe 22 Juni 2022 kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na
Serikali wa nchi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth Heads of Government
Meeting-CHOGM) unaofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kigali.
Makamu
wa Rais anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia
Suluhu Hassan kwenye mkutano huo ulioanza tarehe 20 Juni na utahitimishwa
tarehe 25 Juni 2022.
Mhe.
Makamu wa Rais, mbali ya kushiriki kwenye mkutano huo ameombwa pia miadi ya
kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa Namibia, Mhe. Hage
Geingob; Waziri Mkuu wa Mauritius; Pravind Jugnauth; Waziri Mkuu wa Canada,
Mhe. Justin Trudeau na Melinda Gates.
Inaelezwa
kuwa miadi hiyo ni ishara ya dhahiri ya kuendelea kuimarika kwa diplomasia ya
Tanzania duniani chini ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia.
Hivyo, Mhe. Makamu wa Rais anatarajiwa kutumia miadi hiyo kusisitiza umuhimu wa
kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya pande mbili na hasa ushirikiano
katika eneo la uwekezaji na biashara pamoja na utoaji wa huduma za kijamii kwa
wananchi.
Aidha,
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata
Mulamula naye yupo nchini humo kushiriki Mkutano huo katika ngazi ya Mawaziri
tarehe 23 Juni 2022. Kama ilivyo kwa Makamu wa Rais, Balozi Mulamula ameombwa
miadi ya kufanya mazungumzo na Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za India,
Zambia, Botswana, Eswatini, Singapore na mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa
Uingereza, Mhe. Tony Blair, Bibi Cherie Blair ambaye ni mwanzilishi wa Cherie
Foundation.
Wakati
huo huo, mikutano ya utangalizi ya mkutano huo, inaendelea ambapo tarehe 20
hadi 23 Juni 2022 ilifanyika mikutano ya jukwaa la vijana, jukwaa la wanawake
na jukwaa la biashara. Tanzania ilishiriki katika majukwaa yote hayo
Wakati
wa mkutano wa jukwaa la biashara, washiriki pamoja na mambo mengine, walijadili
namna bora ya kufanya biashara huku dunia ikiwa bado inakabiliwa na janga la
ugonjwa wa Corona na athari za vita kati ya Urusi na Ukraine.
Ujumbe
wa Tanzaia katika mkutano huo uliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda na
Biashara katika Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah
ambaye alieleza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita za kuboresha
mazingira ya biashara na fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana nchini.
Kwa
upande wa mkutano wa jukwaa la vijana ambapo Tanzania iliwakilishwa na vijana
saba, ulisistizwa umuhimu wa kuwaendeleza vijana. Ilielezwa kuwa endapo nchi za
Jumuiya ya Madola zinahitaji kufikia maendeleo ya kweli, hazina budi kuwekeza
kwa vijana kwa sababu katika nchi hizo vijana ni zaidi ya asilimia 60.
Kuhusu mkutano wa jukwaa la wanawake,
ulisisitizwa umuhimu wa kumuendeleza mwanamke ikiwa ni pamoja na kumpatia elimu
ya kumiliki, kukuza na kufanya biashara, kuweka usawa wa kijinsia na kukomesha
vitendo vyote vya unyanyasaji dhidi ya wanawake.
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akitoa maelezo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango kuhusu maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika jijini Kigali, Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022. |
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akifafanua jambo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango kuhusu ushiriki wa Tanzania katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika jijini Kigali, Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022.
| Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akitoa maelezo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ambaye anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 26 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika jijini Kigali, Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022. |
| Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe.Dkt. Asha-Rose Migiro akifafanua jambo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango kuhusu masuala ya CHOGM |
|
|
Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Robert Kahendaguza akitoa utaratibu wa namna ya mikutano ya CHOGM itakavyoendeshwa kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango.
|
|
Afisa Dawati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Salma Rajab akifafanua jambo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango. |
|
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika kikao cha maandalizi na ujumbe wake kabla ya kushiriki kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika jijini Kigali, Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022. |
|
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akiongea na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga. |
|
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akiongea na baadhi ya viongozi wa Serikali wanaoshiriki Mkutano wa 26 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika jijini Kigali, Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022. |