Wednesday, June 29, 2022

TANZANIA NA CUBA KUFUNGUA MAENEO MAPYA YA USHIRIKIANO

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Mhe. Bruno Rodriguez Parrilla walipokutana kwa mazungumzo tarehe 29 Juni 2022 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yamefanyika baada ya Mhe. Parrilla kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kufuatia mwaliko wa Mhe. Waziri Balozi Liberata Mulamula.

Akifafanua dhumuni la ziara hiyo, Mhe. Balozi Mulamula ameeleza kuwa ziara hii inafanyika kwa lengo la kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo.  Maeneo mapya ya ushirikiano yanatarajiwa kufunguliwa katika sekta za kilimo, utalii, usimamizi wa masuala ya zimamoto na ukoaji, viwanda na biashara, na utamaduni na michezo.

“Urafiki na misingi ya kitaifa iliyowekwa na waasisi wa mataifa yetu imetuwezesha kuangalia namna bora ya kuimarisha ushirikiano wetu wa kidiplomasia katika kukuza sekta za maendeleo,” alisema Mhe. Balozi Mulamula.

Pia akaeleza umuhimu wa ushirikiano katika ya Tanzania na Cuba hususan wakati huu ambapo dunia inapitia changamoto mbalimbali ili kujenga mshikamano imara katika utatuzi wa changamoto hizo.

Vilevile akasisitiza umuhimu wa kuimarisha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya mataifa hayo mawili ili maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa yaweze kusimamiwa na kupewa ufuatiliaji wa karibu kwa manufaa ya pande zote mbili.

Naye Mhe. Parrilla ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufungua ofisi ya Ubalozi nchini Cuba pamoja na mapokezi mazuri ya Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Yordenis Despaigne.

Kadhalika, amefurahishwa kusikia habari za Filamu ya Tanzania the Royal Tour iliyonadiwa kwake na Mhe. Waziri Mulamula katika mazungumzo yao. Mhe. Parrilla aliahidi kuiangalia filamu hiyo ili kujifunza mazingira ya asili ya kitanzania na vivutio vya utalii vilivyotangazwa kupitia filamu hiyo.

Katika hatua nyingine viongozi hao wamekubaliana kuboresha utendaji wa kiwanda cha viuadudu kilichopo Kibaha, Pwani ili malengo ya uwekezaji pamoja na yale ya kudhibiti malaria yaweze kufikiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Mhe. Bruno Parrilla katika ofisi ndogo za Wizara tarehe 29 Juni 2022 jijini Dar es Salaam. 

Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme, Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Valentino Mlowola, Afisa Mambo ya Nje, Bi. Salma Rajab na Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Seif Kamtunda wakifuatilia mazungumzo.


Mazungumzo yakiendelea.

Picha ya pamoja Mhe. Balozi Mulamula na Mhe. Parrilla
Mhe.Waziri Mulamula akimkabidhi zawadi ya picha ya Tingatinga Mhe. Parrilla.







WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA CUBA AWASILI NCHINI KWA ZIARA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Mhe. Bruno Rodrieguez Parrilla amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 29 hadi 30 Juni 2022.

Akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Parrilla amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb).

Wakati wa mapokezi hayo, Mhe. Balozi Mulamula ameeleza madhumuni ya ziara hiyo ni kuimarisha na kukuza ushirikiano wa kihistoria ulioasisiwa na Wasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Fidel Castor aliyekuwa Rais wa kwanza wa Taifa la Cuba.

Tanzania na Cuba zimeendelea kushirikiana katika maeneo ya afya, elimu, viwanda, na biashara. Pamoja na maeneo hayo, serikali hizo mbili zinatarajia kufungua maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za Kilimo, utalii, ushirikiano katika usimamizi wa masuala ya zimamoto na uokoaji, utamaduni pamoja na michezo.

Aidha, akiwa nchini Mhe. Parrilla pamoja na mambo mengine, atakutana na kufanya  mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Liberata Mulamula na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Mhe. Bruno Rodriguez Parrilla mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 29 Juni 2022 jijini Dar es Salaam.

Mhe. Balozi Mulamula na Mhe. Parrilla wakiteta jambo wakati wa mapokezi, nyuma ya viongozi hao wa kwanza kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Valentino Mlowola na pembeni yake ni Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Yordenis Despaigne. 

Kulia ni  Balozi Mulamula akiongea na Mhe. Parrila ambao alieleza kuwa ziara yake ni muhimu kwakuwa ina lenga kuimarisha na kukuza uhusiano wa kihistoria baina ya mataifa hayo mawili.
Kutoka kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Valentino Mlowola, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Salma Rajab wakifuatilia mazungumzo.

Mazungumzo yakiendelea.



BALOZI MULAMULA AFAFANUA USHIRIKI WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA CHOGM ULIOFANYIKA RWANDA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola uliofanyika nchini Rwanda tarehe 19 hadi 25 Juni 2022

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola uliofanyika nchini Rwanda tarehe 19 hadi 25 Juni 2022

Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakimsikiliza 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula alipoongea na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam  kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola uliofanyika jijini Kigali, nchini Rwanda tarehe 19 hadi 25 Juni 2022

Hotuba kamili ya Mhe. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 

TAARIFA YA MHESHIMIWA BALOZI LIBERATA MULAMULA (MB.), WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU USHIRIKI WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA 26 WA WAKUU WA SERIKALI WA JUMUIYA YA MADOLA TAREHE 29 JUNI 2022.

Ndugu wanahabari, Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ............. Kazi iendelee!!

Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo tukiwa na afya njema. Pia nitumie fursa hii kuwashukuru kwa namna ya pekee kwa kufika kwenu. Ni matarajio yangu kuwa kupitia vyombo vya habari mnavyoviwakilisha, watanzania na dunia kwa ujumla itaweza kufahamu nilichopanga kukiwasilisha kwenu leo.

Ndugu Wanahabari, nimewaita hapa leo kuwapa taarifa kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 26 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliofanyika Kigali, Rwanda kuanzia tarehe 19 hadi 25 Juni 2022.

Kama mnavyofahamu, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanachama hai wa Jumuiya ya Madola toka nchi yetu ilipopata uhuru mwaka 1961 na imeendelea kuwa mwanachama baada ya Muungano mwaka 1964. Kufuatia uanachama huo, Tanzania imekuwa ikinufaika na kushiriki shughuli zote za Jumuiya hiyo.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliofanyika Kigali uliongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ambaye alimwakilisha Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkutano huu wa 26 umefanyika baada ya kuahirishwa mara mbili (2020 na 2021) kutokana na janga la UVIKO-19 ambalo linaendelea kuitesa dunia hadi sasa. Mojawapo ya mijadala ya mkutano huu ilikuwa ni namna gani dunia itakavyoweza kujikwamua kiuchumi na kijamii kutokana na janga hili.

Ndugu Wanahabari, Mkutano huu wa 26 ulihudhuriwa na Wakuu wa Serikali 27 kati ya nchi 54, ambapo wakuu wengine wa Serikali wapatao 27 waliwakilishwa. Mkutano ulifanyika chini ya kaulimbiu, “Delivering a Common Future: Connecting, Innovating and Transforming” ambayo ilijikita kwenye maeneo makuu ya kipaumbele ya utawala bora, utawala wa sheria na haki za binadamu; vijana; afya; teknolojia na uvumbuzi; na uendelevu kwenye masuala ya uchumi, biashara, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na utunzaji wa mazingira. 

Ukichunguza vizuri maeneo hayo ya vipaumbele yanalingana kabisa na vipaumbele vya Serikali ya awamu ya sita, kitu ambacho kilitusukuma kushiriki kwa nguvu kubwa katika mkutano huu.

Ndugu Wanahabari, Mkutano wa CHOGM ulikuwa na matukio mengi ambayo kutokana na muda, haitakuwa rahisi kuyaeleza hapa yote, hivyo, naomba mnipe ruhusa, ni yataje machache. CHOGM 2022 ilitanguliwa na mikutano kadhaa iliyohusisha Majukwaa ya Jumuiya ya Madola; mikutano ya Mawaziri wa Mambo ya Nje, mikutano ya pembezoni (side events) na mikutano ya uwili (bilaterals meetings).

 

Jukwaa la Biashara

Ujumbe wa Tanzania kwenye Jukwaa la biashara ambalo pamoja na mambo mengine lilijadili fursa za biashara na uwekezaji kwenye Jumuiya ya Madola na Bara la Afrika na changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hizo zikiwemo athari zitokanazo na janga la Uviko-19 na mgogoro kati ya mataifa ya Ukraine na Urusi, uliongozwa na Dkt. Hashil Twalib Abdallah, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Wajumbe wengine walitoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Benki za CRDB na KCB na Chama cha Wakulima wa Maua, Mbogamboga na Matunda (TAHA) na (CTI). Ujumbe wa Tanzania pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji kwenye Jukwaa hili, uliwasilisha kwa wawekezaji orodha ya miradi 115 iliyopo katika sekta mbalimbali nchini kwa ajili ya kutafuta wabia kwenye miradi hiyo kwa utaratibu wa Public Private Partnerships (PPP).

Jukwaa la Wanawake

Ujumbe wa Tanzania kwenye Jukwaa la Wanawake (Commonwealth Women’s Forum) uliongozwa na Bibi Abeida Rashid Abdallah, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Pamoja na ushiriki wa Serikali Asasi mbalimbali za Kiraia kutoka Tanzania nazo zilishiriki. Jukwaa hili lilijadili usawa wa kijinsia na kuwainua wanawake kwenye nyanja zote; kuongeza nafasi za uongozi kwa wanawake; kutoa elimu bora kwa watoto wa kike na namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri haki za wanawake.

Jukwaa la Vijana

Vijana saba kutoka Tazania walishiriki Jukwaa la Vijana lililojadili masuala ya ajira kwa vijana, kuendeleza ujuzi na vipaji kwa vijana; elimu kwa vijana; kusaidia vijana wajasiriamali; matumizi ya teknolojia kwa vijana; kujiajiri; na kuongeza udhamini kwenye shughuli za vijana.

MIKUTANO YA MAWAZIRI

Ndugu Wanahabari, katika Mikutano hii, Mawaziri wa Mambo ya Nje, walikutana kwenye mikutano miwili: mmoja ulijadili Mkutano wa Wakuu wa Serikali na mwingine ulizungumzia masuala mbalimbali yanayohusu nchi ndogo (small states).

Kwa upande wa Mkutano wa Mawaziri kuhusu nchi ndogo uliofanyika chini ya Uenyekiti wenza wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda na St. Vincent and Grenadines ulijadili changamoto za nchi ndogo hususan kufuatia janga la UVIKO-19, athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi na mgogoro unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine pamoja na upatikanaji mdogo wa fedha za maendeleo.

Baada ya mkutano huo, iliazimiwa kutumia mkakati ujulikanao kama United Nations-Commonwealth Advocacy Strategy, kujenga ubia wa kukabiliana na changamoto zinazokabili nchi ndogo.

Mkutano mwingine wa Mawaziri wa Mambo ya Nje ulikikita kwenye kuandaa Mkutano wa Wakuu wa Serikali (Pre-CHOGM Commonwealth Foreign Ministers’ Meeting) kwa kujadili nyaraka mbalimbali za mkutano zilizopokelewa kutoka kwenye mikutano ya Maafisa Waandamizi na mkutano wa watendaji wakuu wa Serikali ambao ulihusisha Makatibu Wakuu-viongozi (Chief Secretaries).

Nyaraka hizo ni: matamko kuhusu usimamizi bora wa matumizi ya ardhi (Commonwealth Living Lands Charter – A Call to Action on Living Lands (CALL)), ukuaji endelevu wa miji (Declaration on Sustainable Urbanization) na huduma na ulinzi kwa watoto (Kigali Declaration on Childcare and Protection Reform). Vikao hivyo vilijadili pia Tamko la Mwisho la Mkutano(Communiqué).

 

MKUTANO WA WAKUU WA SERIKALI WA JUMUIYA YA MADOLA

Ndugu Wanahabari, Ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola ulifanyika tarehe 24 Juni, 2022. Sherehe hizo zilihudhuriwa na Mwana wa Mfalme wa Uingereza, Charles, The Prince of Wales, aliyemwakilisha Malkia Elizabeth II wa Uingereza ambaye ndiye Mkuu wa Jumuiya hiyo; Mhe. Rais Paul Kagame, Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Madola kwa kipindi cha mwaka 2022-2024; Mhe. Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madola tangu mwaka 2018; Wakuu wa Serikali wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola walioshiriki CHOGM 2022; na baadhi ya wajumbe wa nchi wanachama walioshiriki Mkutano huo.

Baada ya ufunguzi wa Mkutano huo, ulifanyika uchaguzi wa Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola. Wagombea waliojitokeza walikuwa ni Bi. Kamina Johnson Smith, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamaica na mgombea kutoka Tuvalu, Sir Iakoba Italeri, ambaye aliingia dakika za mwisho.

Baada ya raundi mbili za kura, Bi. Patricia Scotland alishinda kwa kupata kura 27 wakati Bi. Smith alipata kura 24 na Bw. Italeri alipata kura 3. Kwa matokeo hayo Bi. Scotland anaendelea kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya kwa kipindi cha miaka miwili iliyobaki ya kukamilisha kipindi cha pili cha uongozi wake hadi mwaka 2024.

Ndugu Wanahabari, baada ya uchaguzi, Wakuu wa Serikali au wawakilishi wao walifanya vikao vya utendaji chini ya uenyekiti wa Mhe. Rais Kagame. Niliiwakilisha Jamhuri ya Muungano ya Tanzania baada ya Mhe. Makamu wa Rais kurejea nyumbani kuendelea na majukumu mengine.  Vikao hivyo vilijadili mada zifuatazo:

Mjadala kuhusu Mada ya Utawala Bora na Utawala wa Sheria

Ndugu Wanahabari, chini ya mada hii, mkutano ulijadili umuhimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kuimarisha demokrasia, utawala bora, na kuheshimu mipaka kati ya mihimili mitatu ya dola ili kufikia mustakabali wenye usawa kwa wote. Ajenda hii ni muhimu kwa nchi za Jumuiya ya Madola ikiwemo Tanzania kwa kuwa zinakabiliwa na changamoto katika maeneo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii zinazohitaji misingi mizuri ya demokrasia, amani na utawala bora kupata utatuzi wake.

Katika mjadala huu, Tanzania ilieleza umuhimu inaotoa kwa kanuni za utawala bora na utawala wa sheria tangu kupata uhuru. Vilevile, Tanzania ilisisitiza umuhimu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola kusaidia nchi wanachama kutekeleza programu za kukuza uelewa miongoni mwa watendaji wa taasisi za umma na binafsi ili kutambua majukumu waliyonayo katika kuhudumia wananchi, hivyo kuepuka rushwa na vitendo ambavyo vinakinzana na kanuni za utawala bora na utawala wa sheria.

Mjadala wa Maendeleo Jumuishi na Endelevu

Ndugu Wanahabari, mjadala chini ya eneo hili ulihusu kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanahusisha vipengele muhimu kuhusu utunzaji wa mazingira na ujumuishwaji wa makundi mbalimbali ya jamii nzima. Chimbuko la mada hii ni namna ambavyo mabadiliko ya tabianchi yanavyoweza kuathiri mafanikio ya nchi yaliyopatikana kupitia uwekezaji; pamoja na umuhimu wa makundi yote ya jamii kujumuishwa kwenye mipango ya maendeleo ya nchi.

Tanzania ilisisitiza umuhimu wa vijana, wanawake na walemavu kujumuishwa kwenye sera za kitaifa na kimataifa kwenye kutunza mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kukuza biashara na uwekezaji.  Vile vile ilieleza ulazima wa nchi maskini zaidi duniani kushirikishwa kikamilifu na kwa usawa kwenye mfumo wa kibiashara wa kimataifa; na umuhimu wa nchi zinazoendelea kujengewa uwezo, kupatiwa teknolojia na fedha ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

 

MIKUTANO YA PEMBEZONI

Ndugu Wanahabari, Wakati wa Mkutano wa CHOGM, kulifanyika mikutano mingine mingi ya pembezoni ambayo ilijadili nada mbalimbali. Mikutano miwli kati ya hiyo ilijadili Malaria na Magonjwa yasiyopewa kipaumbele. Malengo ya Mkutano huu yalikuwa ni kupokea mikakati ya viongozi katika kukabiliana na malaria na magonjwa yasiyopewa kipaumbele. Mhe. Makamu wa Rais alieleza changamoto kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania kukabiliana na magonjwa haya wakati ambapo mapambano dhidi ya UVIKO-19 yanaendelea. Aidha, alieleza uzoefu, mafanikio na mikakati ya Tanzania kukabiliana na magonjwa hayo.

 

Mkutano wa Kuzuia na Kupambana na Viashiria vya Ugaidi

Dkt. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu aliongoza ujumbe wa Tanzania ulioshiriki kwenye mkutano wa pembezoni kuhusu kuzuia na kupambana na viashiria vya ugaidi. Mkutano huu ulijadili athari kwa vijana na wanawake kutoka nchi za jumuiya, ambayo ni makundi yanayoathirika kwa kiasi kikubwa na madhara yanayotokana na masuala ya ugaidi. Mkutano huo ulianisha mikakati kadhaa ya kupambana na changamoto hiyo ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidigitali na kupambana na uenezaji wa propaganda za itikadi kali na ugaidi, hususani kwa vijana.

Tanzania ilishiriki mkutano huu kwa kuzingatia kuwa Sekretatarieti ya Jumuiya ya Madola imekuwa ikishirikiana na Jeshi la Polisi, Magereza na Kituo cha Kupambana na Ugaidi nchini kukuza uelewa na kujengea uwezo vyombo hivyo vya usalama kukabiliana na viashiria vya ugaidi nchini Tanzania na eneo la Afrika Mashariki kwa ujumla.

MIKUTANO YA UWILI

Ndugu Wanahabari, Mheshimiwa Makamu wa Rais na mimi mwenyewe tulifanya mikutano ya uwili na viongozi mbalimbali waliohudhuria mikutano hiyo. Lengo letu lilikuwa ni kuitangaza nchi pamoja na kuvutia uwekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo za utoaji wa huduma kwa jamii.

Mhe. Makamu wa Rais alifanya mazungumzo na Bi. Melinda Gates, mwanzilishi mwenza wa taasisi ya Melinda and Bill Gates. Wakati wa mazungumzo hayo, Mhe. Makamu wa Rais aliishukuru taasisi hiyo kwa kuendelea kusaidia Tanzania katika kuboresha sekta ya afya ikiwemo kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza kupitia tafiti na kujengewa uwezo.

Vilevile, Mhe. Makamu wa Rais alieleza ukubwa wa changamoto ya malaria nchini Tanzania ambapo alifafanua kuwa zaidi ya asilimia 94 ya wananchi wapo kwenye hatari ya maambukizi ya ugonjwa huo. Kadhalika, Mhe. Makamu wa Rais alifafanua jitihada za kukabiliana na malaria ikiwemo Mkakati wa Taifa wa Mwaka 2021-2025 unaolenga kupunguza maambukizi ya malaria hadi kufikia chini ya asilimia 3.5 ifikapo mwaka 2025 na kutokomeza kabisa ugonjwa huu ifikapo mwaka 2030. Aidha, alieleza upungufu wa bajeti uliopo wa kiasi cha dola za Marekani milioni 540 ili kutekeleza mpango huo kikamilifu.

Ndugu Wanahabari, mimi mwenyewe pia nilikuwa na mkakati maalum wa kutumia fursa ya mkasinyiko huo wa viongozi kufanya nao mazungumzo. Nilifanikiwa kufanya mazungumzo rasmi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore, Mhe. Dkt. Vivian Balakrishnan; Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe.  Subrahmanyam Jaishankar; Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Mhe. Hina Rabbani Khar, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Amina Mohammed na Mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza na Mwanzilishi wa Mfuko wa Cherie Blair, Bibi Cherie Blair.

Viongozi Wakuu niliokutana nao sio kwa mazungumzo rasmi, lakini nilifanikiwa kuwapa salamu za Rais Samia ni pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza, Mhe. Boris Johnson, Waziri, Mkuu wa Canada, Mhe. Justin Trudeau; Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame; Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema; Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta; na Rais wa Nigeria, Mhe.  Muhammadu Buhari.

Ujumbe wangu katika mazungumzo hayo ni kuhusu maboresho yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita katika mazingira ya biashara na uwekezaji na kwamba Tanzania ni eneo salama kwa wawekezaji. Maeneo niliyosisitiza ni kilimo, utalii, afya na usafiri wa anga na Uchumi wa buluu hasa katika usimamizi na uendeshaji wa bandari na mafunzo ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

Ndugu Wanahabari, baada ya kusema hayo, ninawashukuru sana kwa mwitikio wenu, na ni matarajio yangu kuwa mtatumia vyombo vyenu vya habari kueneza tarifa hii ili iwafikie wananchi.

Ndugu Wanahabari, nimalizie kwa kuwasalimu tena kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania……Kazi iendelee!!!



 

Tuesday, June 28, 2022

BALOZI MULAMULA APOKEA ZAWADI PICHA KUTOKA SERIKALI YA CHINA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akipokea zawadi ya picha kutoka kwa Bw. Ahmed Salim mtoto wa Dkt. Salim Ahmed Salim ambaye alikabidhiwa na Serikali ya China ikiwa ni ishara ya kuutambua mchango wa Dkt. Salim ulioiwezesha China kurejesha kiti cha Kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 1971

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (kushoto) akizungumza na  Bw. Ahmed Salim (katikati) mtoto wa Dkt. Salim Ahmed Salim ambaye alifika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam kumkabidhi zawadi ya picha iliyotolewa  na Serikali ya China ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa Dkt. Salim ulioiwezesha China kurejesha kiti cha Kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 1971


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amepokea zawadi ya picha kutoka Serikali ya China ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa Dkt. Salim Ahmed Salim ulioiwezesha nchi hiyo kurejesha kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 1971.

Zawadi hiyo ya picha imekabidhiwa na Mtoto wa Dkt. Salim Ahmed Salim Bw.  Ahmed Salim katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Bw. Ahmed amesema zawadi ya picha iliyotolewa na Serikali ya China inaonesha picha za Dkt. Salim katika vikao vya Umoja wa Mataifa, alama na nembo za Serikali ya China ambazo zinaonesha heshima ya nchi hiyo kwa Dkt. Salim.

 




Monday, June 27, 2022

WAZIRI MULAMULA AMUAGA BALOZI WA UBELGIJI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameagana na Balozi wa Ubelgiji nchini Mhe. Peter Van Acker ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini.

Akizungumza na Mhe. Balozi Peter walipokutana katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, Waziri Mulamula amesema Tanzania na Ubelgiji zimekuwa na uhusiano wa karibu tangu nchi hiyo ilipofungua Ubalozi wake hapa nchini mwaka 1980.

“Uhusiano kati ya Tanzania na Ubelgiji umekuwa unakuwa na kuimarika………. kupitia awamu zote za serikali tumeshuhudia uwepo wa mipango ya maendeleo katika sekta za maji, elimu , nishati pamoja na biashara na uwekezaji,” amesema Balozi Mulamula.

Waziri Mulamula ampongeza Mhe. Balozi kwa kumaliza utumishi wake nchini na kuacha uhusiano kati ya Tanzania na Ubelgiji ukiwa imara.

Balozi Mulamula amesema pamoja na kwamba Balozi Peter anaondoka nchini amemhakikishia kuwa kundi la wafanyabiashara kutoka Ubelgiji litakuja nchini mwaka huu ikiwa ni mwendelezo wa kukuza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji.

Kwa upande wake, Balozi wa Ubelgiji nchini, Mhe. Peter Van Acker ameongelea kuridhishwa kwake na uhusiano uliopo baina ya Ubelgiji na Tanzania na kuahidi kuwa balozi mwema wa Tanzania.

“Nimeishi vizuri hapa Tanzania na nimefurahia kuwa hapa wakati wote wa uwakilishi wangu, kuna mengi ya kujivunia kufanya kazi Tanzania……asante sana, amesema Balozi Acker

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa na Balozi wa Ubelgiji nchini Mhe. Peter Van Acker katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Ubelgiji nchini Mhe. Peter Van Acker katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimkabidhi  Balozi wa Ubelgiji nchini Mhe. Peter Van Acker  zawadi ya picha






BALOZI MULAMULA AKUTANA NA NAIBU KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe, Amina Mohammed jijini Kigali, Rwanda wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola. Mazungumzo hayo yaliangazia masuala makuu matatu ambayo ni mikutano inayoandaliwa na Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Usalama wa Chakula na namna dunia itakavyojikwamua kiuchumi baada ya UVIKO-19.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula  na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe, Amina Mohammed  wakifurahia jambo wakati wa mazungumzo.yao yaliyofanyika jijini Kigali, Rwanda.
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Robert Kahendaguza akiwa katika mazungumzo ya utangulizi na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe, Amina Mohammed (mwenye kilemba). Mwingine katika picha ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiendelea na mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe, Amina Mohammed (mwenye kilemba). Wengine wanaofuatilia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Robert Kahendaguza; Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Balozi Mindi Kasiga na Afisa Dawati, Bi. Gloria Ngaiza.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe, Amina Mohammed (mwenye kilemba) wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wao walioshiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola.

 Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe, Amina Mohammed akihojiwa na Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Runinga cha Channel 10, Bw. Ezekiel Mwamboko jijini Kigali, Rwanda wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola. Pembeni ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula

 

Saturday, June 25, 2022

BALOZI MULAMULA ATUMIA MKUTANO WA CHOGM KUITANGAZA TANZANIA

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki chini ya uongozi wa Waziri Liberata Mulamula imeendelea kutumia majukwaa ya kimataifa kuitangaza nchi na fursa zake kama sehemu ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

Katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaohitimishwa leo tarehe 25 Juni 2022 nchini Rwanda na kuhudhuriwa takribani na viongozi wa kaliba na ngazi tofauti wa nchi zote 54 za umoja huo, Tanzania ilitumia fursa hiyo kuhamasisha wawekezaji na kuja nchini.

Balozi Liberata Mulamula alionekana akifanya mazungumzo rasmi na yasiyo rasmi na Mawaziri wenzake wa Mambo ya Nje na hata Mawaziri Wakuu na Marais wa nchini mbalimbali kwa lengo la kuitangaza nchi. Alisikika akiwaambia, “Rais wetu, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kuboresha mazingira ya biashara, hivyo milango ipo wazi, waambieni wafanyabiashara wenu waje kuwekeza Tanzania kwenye sekta mbalimbali na hasa kilimo ambacho ni moja ya kipaumbele cha Serikali ya awamu ya sita”.

Viongozi ambao Mhe. Waziri Mulamula alipata fursa ya kufanya nao mazungumzo rasmi ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore, Mhe. Dkt. Vivian Balakrishnan; Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe.  Subrahmanyam Jaishankar; Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Mhe. Hina Rabbani Khar na Mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza na Mwanzilishi wa Mfuko wa Cherie Blair, Bibi Cherie Blair.

Viongozi Wakuu aliokutana nao na kuwapa salamu za Rais Samia ni pamoja na Waziri Mkuu wa Canada, Mhe. Justin Trudeau; Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame; Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema; Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta; na Rais wa Nigeria, Mhe.  Muhammadu Buhari.

Katika mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula alihimiza ushirikiano katika biashara na uwekezaji, mafunzo, usafiri wa anga na utalii.  Alieleza namna Serikali ya awamu ya sita inavyofanya jitihada kuondoa vikwazo vya kibiashara na kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kushawishi wawekezaji wengi. Aliziomba Canada, Singapore, India na Pakistan kuleta wawekezaji wengi zaidi na hasa katika sekta ya kilimo ambayo ni kipaumbele cha Serikali ya awamu ya sita.

Kuhusu utalii, Mhe. Waziri aliziomba nchi hizo kutafsiri Filamu ya The Royal Tour iliyoongozwa na Rais Samia kwa lugha za nchi zao ili iwafikie watu wengi zaidi. Aidha, alizihimiza nchi hizo, hususan India na Singapore kuanzisha safari za moja kwa moja za mashirika yao ya ndege kati ya Tanzania na nchi hizo ili kuhamasisha utalii.

Aidha, Mhe. Waziri alihimiza ushirikiano na Singapore katika Uchumi wa Buluu kutokana na nchi hiyo kupiga hatua kubwa kwenye eneo hilo, hususan kwenye uendelezaji, usimamizi na uendeshaji wa bandari. Aligusia pia umuhimu wa kujengeana uwezo hususan katika eneo la rasilimali watu na mafunzo ya TEHAMA.

Wakati wa mazungumzo na Bibi Cherie Blair, alielezea utayari wa Mfuko wake wa Cherie Blair Foundation wa kushirikiana na Tanzania, kwenye kuwajengea uwezo wanasheria wa kuwa na ujuzi wa kutosha wa upatanishi na usuluhishi wa migogoro nje ya mahakama na kwamba mfuko huo pia, upo tayari kuisaidia Tanzania kwa kutoa msaada kwa mawakili katika kesi za Kimataifa zinazoikabili Serikali ya Tanzania.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola utafungwa leo jioni na Balozi Mulamula ataendeelea na mkakati wake wa kukutana na viongozi mbalimbali na atarejea nchini tarehe 26 Juni 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Waziri Mkuu wa Canada, Mhe Justin Trudeau wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Waziri Mkuu wa Canada, Mhe Justin Trudeau wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022. Mwingine katika picha ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Mhe. Mélanie Joly
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea jambo na Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame  wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Modola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2025.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea jambo na Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Modola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2025.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea jambo na Rais wa Nigeria, Mhe.  Muhammadu Buhari  wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Modola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2025.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea jambo na Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta  wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Modola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2025.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongozana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango kuingia kwenye ukumbi unaofanyika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa  Singapore, Dkt. Vivian Balakrishnan wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Modola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2025.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa  Singapore, Dkt. Vivian Balakrishnan wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Modola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2025. Balozi Mulmula alitumia fursa pamoja na mambo mengine kuwakaribisha wafanyabiashara wa Singapore kuja kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea jambo na Mkurugenzi wa Afrika katika Wizara ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz. Wengine katika picha ni Maafisa wa Mambo ya Nje, Bi. Talha Waziri (kulia) na Bi. Lilian Mukasa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Mhe. Bilawal Bhutto Zardari wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe Subrahmanyam Jaishankar wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo na na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe Subrahmanyam Jaishankar wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula (kulia) akiongea jambo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe.Netumbo Nandi-Ndaitwah wakati wakielekea kwenye ukumbi unaofanyika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sierra Leone, Mhe. Prof. David Francis wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia, Mhe. Stanley Kakubo wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaofanyika Rwanda tarehe 20 hadi 25 Juni 2022