Wednesday, July 6, 2022
NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI ZATAKIWA KUKUZA, KUENZI KISWAHILI
Na Mwandishi wetu, Zanzibar
Nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimetakiwa kuweka mikakati ya muda mrefu ili kukuza, kuendeleza na kueneza lugha ya Kiswahili duniani.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Bw. Khamis Abdalla Saidi aliyemwakilisha Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe.Tabia Maulid Mwita katika Kongamano la kwanza la Siku ya Kiswahili Duniani lililoanza leo tarehe 6 Julai, 2022 Zanzibar.
Kongamano hilo linalongozwa na Kauli Mbiu: “Kiswahili kwa Amani, Ustawi na Utangamano wa Kikanda” litahitimishwa kwenye siku ya Kilele cha Siku ya Kiswahili duniani tarehe 7 Julai 2022.
Katika hotuba yake, Bw. Saidi amesema kuenea kwa Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki na Mataifa mengine ni bidhaa ya bishara, hivyo umuhimu wa Kiswahili ni mkubwa katika kupiga hatua ya kimaendeleo.
“Ni jukumu la kila mmoja wetu kukifuatilia Kiswahili katika kila hatua na kutafuta na kubuni njia na mikakati ya muda mrefu na ya kisasa ya kuikuza lugha hii adhimu ya Kiswahili,” amesema Bw. Saidi.
Bw. Saidi aliongeza Lugha ya Kiswahili inatakiwa itumike kama bidhaa inayouzwa na kupata tija. Kuna haja kubwa ya kuwekeza kuwasomesha wataalamu wa lugha kuwa na stadi na uwezo unaotakiwa katika kutoa huduma ya kufundisha, ukalimani, kutafrisi na kuandaa machapisho mbali mbali kwa Kiswahili.
“Ni jukumu la vyuo vikuu vya Afrika Mashariki kutilia mkazo mikakati ya muda mrefu ya uwekezaji wa kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa kufanya tafiti mbalimbali za lugha,” ameongeza Bw. Saidi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote amesema kuwa jumuiya ya Afrika Mashariki inapaswa kushirikiana kwa pamoja na wadau wa Lugha ya Kiswahili ili kuweza kupata uzoefu wa matumizi ya Kiswahili pamoja na kujadili changamoto za lugha hiyo ili kuimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili yataimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa lugha hii ni lugha ya biashara hivyo tunapaswa kujivunia lugha hii adhimu kwa maslahi mapana ya jumuiya yetu,” amesema Mhandisi Mlote.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (MS TCDC), Bi. Yusta Mganga amesema licha ya kuimarika kwa matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ukanda huo unapaswa kuchukua hatua madhubuti zaidi kwa ajili ya kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakuzwa na kuendelezwa miongoni mwa nchi ambazo bado hazijaimarika katika matumizi ya Kiswahili.
“Kuna njia mbalimbali za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kama vile kufanya tafiti, uandaaji wa makongamano na semina mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya Kiswahili…….katika kuandhimisha siku hii muhimu ni vyema tukatafakari mafanikio ya Kiswahili katika ukanda wa Jumuiya yetu ili kuimarisha amani na utangamano wa kikanda,” amesema Bb. Mganga
Novemba 23, 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) lilitangazwa rasmi kuwa tarehe 7 Julai ya kila mwaka ni siku maalumu ya kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani.
Februari 2022, Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika katika mkutano wake wa kawaida wa 35 walipitisha Kiswahili kama Lugha ya Kazi na mawasiliano mapana Barani Afrika.
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote akitoa hotuba yake katika Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar |
Meza Kuu wakifuatilia kikundi cha ngoma za asili kutoka Zanzibar wakati wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar |
Washiriki wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani wakifuatilia kikundi cha ngoma za asili kutoka Zanzibar |
Washiriki wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani wakiimba wimbo wa Taifa |
Washiriki wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani wakifuatilia Kongamano hilo lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar |
Meza Kuu katika picha ya pamoja na wawakilishi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar |
WATANZANIA WAASWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MASOKO YA KIMATAIFA
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amewasihi Watanzania kuchangamkia fursa za masoko ya bidhaa mbalimbali nje ya nchi.
Balozi Fatma ametoa rai hiyo
leo alipotembelea Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba)
Jijini Dar es Salaam.
Balozi Fatma ameeleza Wizara
ya Mambo ya Nje kupitia Balozi zake nje imekuwa ikitatafuta fursa za uwekezaji,
masoko ya bidhaa na kutangaza vivutio vya utalii kupitia majukwaa na mikutano
mbalimbali inayofanyika katika vituo vya uwakilishi nje ya nchi.
“Fursa za masoko zinazopatikana
kwa sasa ni pamoja na; Soko la zao la ufuta, mihogo na soya nchini China; Soko
la nyama na wanyama kama mbuzi na kondoo nchini Saud Arabia; Soko la nafaka
kama maharage na mbaazi nchini Oman na Umoja wa Falme za kiarabu (U.A.E); Soko la parachichi nchini Ufaransa, India na
Uholanzi; na Soko la asali katika nchi za Scandnavia na Mashariki ya Kati.
Balozi Fatma pia ameeleza
uwepo wa soko la uyoga katika masoko ya kimataifa kufuatia umuhimu wa zao hilo
na kutoa rai kwa watanzania kuchangamkia kilimo kwa ajili ya biashara badala ya
kuzalisha kwa chakula pekee.
Aidha, aliongeza kusema
jitihada hizi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zinafanywa
kwa kushirikiana na Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Mamlaka ya
Usimamizi wa Biashara Tanzania (TANTRADE) pamoja na Wizara ya Kilimo kwa lengo
la kuhamasisha wakulima na wafanyabiashara kuchangamkia fursa mbalimbali za
masoko ili kujitangaza kimataifa na kukuza mitaji ya biashara zao.
Wakati huo huo Balozi Fatma
amezungumzia jitihada zinazofanywa na Balozi zetu katika kutangaza filamu ya “Tanzania
the Roya Tour” kwa lengo la kuongeza watalii sambamba na kuitangaza Tanzania Nje
ya mipaka kupitia mandhari na mazingira ya asili yanayo onekana katika filamu
hiyo.
Kadhalika, ameeleza fursa
zinazopatikana kutokana na jitihada za wizara kupitia Balozi zake katika kukuza
lugha ya Kiswahili duniani hususan wakati huu tunapoelekea tarehe 7 Julai 2022 kwenye
maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yatakayoadhimishwa kitaifa Jijini Dar
es Salaam.
Balozi Fatma akiwa katika viwanja vya Maonesho ya Sabasaba pia ametembelea banda la Kituo cha Mikutano cha Kitamataifa cha Arusha (AICC), Kenya, Zanzibar, pamoja na Shirika la Madini (Stamico).
BALOZI MUSHY AITAFUTIA MSHIRIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA
Balozi wa Tanzania nchini Austria, Mhe. Celestine Mushy akiwa katika kikao na uongozi wa Hospitali na Chuo Kikuu cha Tiba cha Vienna ambapo wamekubaliana kuandaa Hati ya Makubaliano (MoU) ya kuanzisha ushirikino na Hospitali ya Benjamin Mkapa ya jijini Dodoma. |
Balozi wa Tanzania nchini Austria, Mhe. Celestine Mushy |
TANZANIA NA AFRIKA KUSINI KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA ELIMU
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula
amekutana na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini, Mhe. Matsie Angelina Motshekga
ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi.
Wakati
wa kikao chao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius
Nyerere jijini Dar Es Salaam leo tarehe 5 Julai 2022, Mawaziri hao walijadili
pamoja na mambo mengine, namna nchi zao zitakavyoweza kushirikiana katika sekta
ya elimu.
Mhe.
Motshekga anayetarajiwa kusaini Hati ya Makubaliano na Waziri wa Elimu, Prof.
Adolf Mkenda kuhusu Tanzania kushirikiana na Afrika Kusini kufundisha Kiswahili
katika nchi hiyo, alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuainisha maeneo ya
kipaumbele ya aina ya elimu tunayoihitaji ili tuweze kubadilishana uzoefu
katika maeneo hayo.
Maeneo
mengine ambayo viongozi hao waliyadili ni pamoja na programu za kubadilishana
wanafunzi na walimu na changamoto zinazoikabili sekta za elimu za nchi hizo
ambazo ni pamoja na uhaba wa miundombinu, mimba za mapema, kuacha shule na
uhaba wa vitabu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberrata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini Mhe. Matsie Angelina jijini Dar Es Salaam. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberrata Mulamula na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini Mhe. Matsie Angelina wakiendelea kujadili masuala ya elimu kuhusu nchi zao huku ujumbe wa Tanzania ukifuatilia kwa makini. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberrata Mulamula akiwa na mgeni wake, Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini Mhe. Matsie Angelina baada ya mazungumzo yao. |
TANZANIA YASIFIWA INAFANYA VIZURI KATIKA CHANJO ZA UVIKO-19.
Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeratibu msauala ya UVIKO-19,
Dkt. Ted Chaibans jijini Dar Es Salaam tarehe 5 Julai 2022.
Katika kikao hicho, Balozi
Mulamula alielezea hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania za kudhibiti
ugonjwa wa UVIKO-19 na kusisitiza umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea
kushirikiana na Tanzania kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Balozi Mulamula alisema
licha ya changamoto za uhaba wa miundombinu na ukubwa wa nchi, Serikali
imejitahidi kupambana na ugonjwa huo, hususan kwa kuhamasisha wananchi
wajitokeze kupata chanjo za UVIKO-19.
Balozi Mulamula
alihitimisha mazungumzo hayo kwa kukumbushia wito wa Serikali kuhusu kupata
msaada wa Jumuiya ya Kimataifa ili Serikali ya Tanzania iweze kutimiza azma
yake ya kujenga kiwanda cha kutengeneza chanjo za Uviko-19 na magonjwa mengine.
Kwa upande wake, Dkt.
Chaibans alikiri kuwa licha ya Tanzania kuchelewa kuanza matumizi ya chanjo za
UVIKO-19 lakini imepiga hatua kubwa kuliko baadhi ya nchi zilizoanza mapema
kampeni za kuhamasisha chanjo. Alisisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea
kuhamasisha watu kwa kubuni mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwatumia
viongozi wa dini. Aliendelea kwa kutoa wito kwa Serikali ya Tanzania,
ihakikishe kuwa makundi ya kipaumbele kama Wazee, wenye maradhi ya kudumu,
watumishi wa sekta za afya, elimu na utalii wanahamasishwa ili wapate chanjo za
UVIKO-19.
Wakati huo huo, Balozi Mulamula amekutana na wajumbe wa Kamati ya Afrika ya Hydrogen inayojihusisha na uwekezaji katika nishati jadidifu (renewable energy). Wajumbe wa Kamati hiyo walimweleza Mhe. Waziri Mulamula utajiri wa vyanzo mbalimbali vya nishati ilivyonavyo Tanzania ambavyo vina fursa nyingi za kibiashara, endapo vitatumiwa vizuri. Kamati hiyo imeelezea utayari wa kufanya kazi na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa rasimali hizo zinatumika vizuri ili ziweze kuleta maendeleo endelevu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Kamati ya Afrika ya Hydrogen ambayo inajishughulisha na masuala ya kutoa ushauri na uwekezaji katika Nishati jadidifu (renewable energy).
|
Tuesday, July 5, 2022
Balozi Mulamula Apokea Nakala za Hati za Utambulisho
Kauli hiyo ameitoa leo
tarehe 5 Julai 2022 jijini Dar Es Salaam wakati akipokea nakala za Hati za
Utambulisho za Balozi Mteule wa Uganda hapa nchini, Mhe. Kanali Mstaafu Fred
Mwesigye.
Balozi Mulamula amesema
kuwa Tanzania na Uganda zina uhusiano mzuri wa kihistoria na umekuwa ukiimarika
siku hadi siku kutokana na masuala mbalimbali ya ushirikiano yanayoendelea, yakiwemo
ziara za viongozi wa kitaifa.
Alisema kuwa hivi
karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
alifanya ziara nchini Uganda ambapo makubaliano na ahadi mbalimbali zilitolewa
katika ziara hiyo. Makubaliano hayo ni pamoja na kuhakikisha kuwa sekta binafsi
za nchi hizi mbili zinawekewa mazingira mazuri ya kufanya uwekezaji na biashara
kwa faida ya wananchi wake.
Alielezea matumaini
yake kuwa Balozi Mteule atahakikisha kuwa ahadi na makubaliano yaliyofikiwa baina
ya pande mbili hizo yanatekelezwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa
ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga
unatekelezwa kama ulivyopangwa.
Mhe. Waziri alimalizia
kwa kumuhakikishia Balozi huyo kuwa Wizara na Serikali kwa ujumla itampa
ushirikiano wa kutosha ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Balozi
Mwesigye aliahidi kuwa atatumia ujuzi na maarifa aliyopewa kwa kushirikiana na
wenzake balozini kuhakikisha kuwa makubaliano na maelekezo yaliyotolewa wakati
wa ziara za viongozi wa kitaifa na majukwaa mengine yanatekelezwa ipasavyo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiendelea na mazungumzo na Balozi Mteule wa Uganda nchini Tanzania, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye. |
Monday, July 4, 2022
BALOZI MULAMULA: WIZARA KUENDELEA KUHAMASISHA WAWEKEZAJI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema Wizara itaendelea kuhakikisha kuwa sekta za uwekezaji, biashara na utalii zinazidi kuimarika.
Balozi Mulamula alitoa kauli hiyo wakati alipotembelea banda la Wizara katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam.
Akiwa katika banda la Wizara, Waziri Mulamula amewapongeza watumishi wanaoiwakilisha Wizara katika maonesho hayo na kuongeza kwamba Wizara imekuwa ikijivunia kuwa sehemu ya kutafuta wawekezaji na wafanyabiashara ili kuja kuwekeza nchini kama ambavyo kauli mbiu ya maonesho hayo inavyosema ‘Tanzania: Mahali sahihi pa Biashara na Uwekezaji’
“Wizara kupitia Balozi zake Nje ya nchi inaendelea kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali katika kuhakikisha kuwa tunapata wawekezaji wa kutosha kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan imejitahidi kuboresha mazingira ya biashara na uwekeza” alisema Balozi Mulamula
Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri aliwasihi watumishi wa Wizara kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, juhudi na bidii na kuendelea kuzitangaza fursa za biashara, uwekezaji pamoja na vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini.
Katika tukio jingine Balozi Mulamula alishiriki katika hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 46 ya Biashara ya Sabasaba yaliyofunguliwa na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) Mhe. Wamkele Mene tarehe 03 Juni, 2022 Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda na Wizara inayoiongoza katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na watumishi wa Wizara katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na watumishi wa Wizara alipotembelea banda la wizara katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Watumishi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AlCC) katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam |
Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) Mhe. Wamkele Mene akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula wakati wa hafla ya ufunguzi wa maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam |
Friday, July 1, 2022
TANZANIA YASHIRIKI KONGANANO LA MIJI DUNIANI
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshiriki Kongamano la Kumi na Moja la Miji Duniani, lililofanyika jijini Katowice, Poland tarehe 26 hadi 30 Juni 2022.
Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Kenya na Mwakilishi katika Shirika la UN Habitat Mhe. John Simbachawene
Katika kongamano hilo, Balozi Simbachawene alieleza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuleta maendeleo endelevu ya miji kwa kutengeneza sera ya maendeleo ya miji, kuwekeza kwenye miundombinu, kuwezesha sekta binafsi na kuhamasisha utunzaji wa mazingira katika miji.
Kupitia konganabo hilo, Balozi Simbachawene alipata nafasi ya kuzungumza na wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo UN Habitat, AfDB, UNECA, UNDP, Islamic Fund, Saudi Fund, European Commission ambao aliwaelezea kuhusu mipango ya Serikali ya kuendeleza miji na kuwaomba kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa mipango hiyo ili kutimiza lengo Namba 11 la Umoja wa Mataifa la Maendeleo Endelevu linalohusu maendeleo makazi na miji na (SDG 11).
Mbali na Balozi Simbachawene, Balozi wa Ujerumani anayewakilisha pia nchini Poland Mhe. Dkt. Abdalah Possi pia alishiriki kongamano hilo.
Taasisi nyingine zilizoshiriki ni pamoja na Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, Manispaa ya Jiji la Dodoma, TARURA na DART.
Thursday, June 30, 2022
WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA CUBA AFANYA MAZUNGUMZO NA MHE. DKT. ASHATU KIJAJI
Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amekutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Mhe. Bruno Parrilla kwenye ofisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) tarehe 30 Juni 2022 jijini Dar es Salaam. Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa yao kwa lengo la kukuza biashara na uwekezaji mathalan, viwanda vya dawa za binadamu, pembejeo na mifugo, tafiti katika masuala ya afya na kujenga uwezo wa upatikaji wa chanjo nchini. Vilevile, wamejadili juu ya kukuza thamani ya mazao ya kilimo na kuwawezesha wananchi kufanya kilimo cha biashara katika soko la kimataifa. Aidha, Serikali ya Cuba imewekeza nchini katika kiwanda cha viuadudu ambacho kinatarajiwa pia kuzalisha mbolea baada ya kukamilika kwa taratibu za uwekezaji zilizoafikiwa na pande zote mbili. Kupitia mazungumzo haya Serikali ya Cuba imeridhia kuendelea kutoa msaada wa kiufundi katika sekta za ushirikiano ili ziweze kuwanufaisha wananchi wa Tanzania na Cuba na kujenga mahusiano ya kimkakati baina yao. |
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) akimkaribisha Mhe. Bruno Parrilla. |
Kutoka kushoto Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Valentino Mlowola, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme na mwisho ni Afisa Mambo ya Nje, Bi Salma Rajab wakifuatilia mazungumzo. |