Thursday, July 7, 2022

DKT. MWINYI AZISIHI NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI KUBUNI MBINU ZA KUENEZA KISWAHILI

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezisihi nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kubuni mbinu bora za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili katika ukanda huo na duniani kwa ujumla.

Dkt. Mwinyi ametoa wito huo wakati akifunga Kongamano la Kiswahili Duniani lililoanza jana na kuhitimishwa leo Zanzibar ambapo amezisihi nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kuhakikisha kuwa zinashirikiana na Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoa mafunzo ya Isimu na Fasishi katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa mikakati madhubuti ya kuendeleza lugha ya Kiswahili Duniani.

“Natoa wito pia kwa taasisi za elimu ya juu kushirikiana na Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutumia lugha ya Kiswahili kama fursa kwa vijana wetu kwani lugha hii ni kama bidhaa,” amesema Dkt. Mwinyi.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Mwinyi ameihakikishia Kamisheni ya Kiswahili na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa zitaendelea kuunga mkono jitihada za kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili duniani kote.

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kushirikiana na wadau wa Lugha ya Kiswahili ili kuweza kuanzisha mabaraza ya Kiswahili ikiwa ni njia moja wapo mahsusi ya kukuza na kuendeleza lugha hiyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine amesema kuwa ni lugha ya Kiswahili ni lugha ya kwanza kutumika katika shughuli rasmi za Umoja wa Afrika, pia ni lugha ya kwanza Afrika na ya nane duniani kuwa na siku maalum ya kuadhimishwa

“Kutumia lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki  kutasaidia kuongeza umoja baina ya wananchi wa ukanda huo kuliko ilivyokuwa awali na kuongeza maelewano na baina ya nchi na nchi” amesema balozi Sokoine

Balozi Sokoine ameongeza kuwa, lugha ya Kiswahili ikitumika vizuri itasaidia kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika masuala mbalimbali yakiwemo masuala ya kisiasa, biashara, uchumi, elimu utamaduni na ustawi wa jamii.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Sokoine amezisisi nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Masahriki kuongeza kasi ya kutangaza na kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika shughuli zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki” 

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Dkt. Mwanahija Ali Juma amezisihi nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhakikisha kuwa wanakuza na kuendeleza matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa kuanzisha mabaraza ya Kiswahili

Dkt. Mwanahija ameongeza kuwa njia nyingine ya kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili ni pamoja na nchi wanachama kuungana pamoja na Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya tafiti za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.

Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani limehudhuriwa na nchi wanachama sita kutoka ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Kenya, Jamhuri ya Rwanda, Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Rwanda na Jamhuri ya Sudani kusini.

Novemba 23, 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) lilitangazwa rasmi kuwa tarehe 7 Julai ya kila mwaka ni siku maalumu ya kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani. Vilevile, Februari 2022, Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika katika Mkutano wake wa kawaida wa 35 walipitisha Kiswahili kama Lugha ya Kazi na mawasiliano mapana Barani Afrika.

Aidha, Mwezi Septemba, 2022 Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa  ulianza kuitangaza na kuisamba lugha ya Kiswahili, nchini Ufaransa kwa kushirikiana na Chama cha Watanzania Ufaransa (CCWU), ambapo ulianza kutoa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa mwaka wa masomo 2021/22, ambayo yaliendeshwa na Kituo cha Utamaduni na Lugha cha Kitanzania (CCLT).

Washiriki wa matembezi kutoka ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakionesha baadhi ya Bendera za nchi wananchama wa Jumuiya hiyo wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika leo Zanzibar




Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akipokelewa na viongozi mbalimbali alipowalisi kuhitimisha Kongamano la Kiswahili Duniani leo Zanzibar

   
Washiriki wa Kongamano la Kiswahili Duniani wakifuatilia Hotuba ya Rais wa Zanzibaar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati wa kufunga kongamano hilo leo Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwasilisha Hotuba yake wakati wa kuhitimisha Kongamano la Kiswahili Duniani leo Zanzibar

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote akitoa hotuba yake katika Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililohitimishwa leo Zanzibar



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali waliohudhuria Kongamano la Kiswahili Duniani leo Zanzibar




SERIKALI YA TANZANIA NA ETHIOPIA ZAKUTANA KWA KIKAO CHA PAMOJA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Mhandisi Hamad Masauni wamefanya kikao cha pamoja na Balozi wa  Ethiopia nchini, Mhe. Shibru Kedida tarehe 06 Julai 2022 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine kikao hicho kimejadili juu ya kuimarisha ushirikiano imara na wa kihistoria baina ya Tanzania na Ethiopia pamoja na changamoto za uhamiaji haramu nchini.

Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Mhandisi Hamad Masauni akifafanua jambo wakati wa kikao hicho.

Kulia ni Kamishna wa Udhibiti na Usimamizi wa Mipaka wa Idara ya Uhamiaji, Samwel Mahirane akifafanua jambo juu ya masuala ya  usimamizi wa mipaka wakati wa majadiliano ya kikao hicho, pembeni yake ni Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza nchini, ACP George Wambura.

Aliyesimama ni Naibu Kamishna Msaidizi wa Udhibiti na Usimamizi wa Mipaka wa Idara ya Uhamiaji,Phabian Philo akifafanua jambo katika majadiliano ya kikao hicho.

Majadiliano yakiendelea.

Kutoka Kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara hiyo wakaijadiliana jambo na Kamishna Mahirane na Kamishna Philo wa Idara ya Uhamiaji baada ya kumalizika kwa mazungumzo. 

Picha ya Pamoja Waheshimiwa Mawaziri, Mhe. Balozi na Ujumbe walioambatana nao katika kikao hicho.

Waziri Mulamula akiagana na Mhe. Balozi Shibru Kedida baada ya mazungumzo.

 

WAZIRI MULAMULA AFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI MTENDAJI WA TAASISI YA TWAWEZA NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akipokea jarida kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza nchini, Bw. Aidan Eyakuze alipomtembelea tarehe 6 Julai 2022 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Waziri Mulamula akizungumza na Bw. Eyakuza ambapo pamoja na mambo mengine, Bw. Eyakuze alienda kujitambulisha kwa Mhe. Waziri pamoja na kueleza majukumu yanayotekelezwa na Taasisi ya TWAWEZA nchini.

Picha ya pamoja Mhe. Waziri Mulamula, Bw. Eyakuze pamoja na ujumbe ulioambatana nao katika mazungumzo hayo. 

 

Wednesday, July 6, 2022

TANZANIA NA ALGERIA KUFUNGUA MAENEO MAPYA YA USHIRIKIANO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) akipokea barua kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Algeria iliyowasilishwa na Balozi wa Algeria nchini, Mhe.Ahmed DJELAL leo tarehe 6 Julai 2022 jijini Dar es Salaam.

Mhe. Balozi Ahmed DJELAL akifafanua jambo kwa Mhe. Waziri Mulamula.
Mhe. Waziri  Mulamula akizungumza na Mhe. Balozi Ahmed DJELAL, katika mazungumzo yao viongozi hao wamejadili juu ya kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali zao hususan katika sekta za afya, nishati, elimu,miundombinu, usimamizi wa majanga, zimamoto na uokoaji.
Pia wamekubaliana kuanzishwa kwa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria ili maeneo hayo ya ushirikiano yasimamiwe kwa tija ya mataifa yao.

Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini, Algeria, Mhe. Maj. Gen. Jacob Kingu akitoa ufafanuzi wakati wa mazungumzo hayo, kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga .

Mhe. Waziri Mulamula akiagana na Balozi Ahmed DJELAL baada ya mazungumzo.

 

VACANCY ANNOUNCEMENT


 

BALOZI MULAMULA: SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA WEZESHI KWA SEKTA BINAFSI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya mazungumzo na Wawakilishi wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) katika ofisi ndogo za Wizara leo tarehe 6 Julai 2022 jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo Waziri Mulamula amewahakikishia Wawakilishi hao kuwa Serikali inaendelea kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili kukuza sekta za uzalishaji kwa maslahi mapana ya Taifa.

‘’ Wizara kupitia Balozi zetu nje imeendelea kuhakikisha fursa mbalimbali zinazopatikana nchini zinatangazwa katika maeneo ya uwakilishi ili kuzihakikishia sekta hizo mageuzi makubwa ya  kiuchumi” alisema Balozi Mulamula.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TPSF, Bi. Angelina Ngalula pamoja na wajumbe alioambatana nao wameipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mkazo wa kuinua sekta binafsi.

Akifafanua Bi. Ngalula ameeleza juu ya uwepo wa mafanikio katika sekta za biashara, Utalii, uwekezaji, kilimo, madini, huduma, uchukuzi na usafirishaji na ujenzi.

“Sisi sekta binafsi tunaishukuru Serikali yetu kwa kuboresha mazingira ya biashara, sasa tunashuhudia mipaka inafunguka sambamba na ongezeko la watalii kupitia jitihada za makusudi zinazofanyika katika kuitangaza filamu ya “Tanzania the Royal Tour” alisema Bi. Ngalula

Aidha, akafafanua matokeo yaliyopatikana kupitia ziara za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwamba kupitia ziara hizo mikutano na makongamano ya biashara yalifanyika katika nchi mbalimbali na yamesaidia kupatikana kwa washirika wa kibiashara kutoka mataifa hayo.

Kupitia mazungumzo hayo Waziri Mulamula na Wawakilishi wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi, wamekubaliana kuanzisha timu maalum ya uratibu na ufuatiliaji wa masuala mbalimbali ya kimkakati kitaifa, kwa lengo la kuimarisha na kukuza diplomasia ya uchumi nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (kati) akizungumza na Wawakilishi wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) leo tarehe 6 Julai 2022 katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya TPSF, Bi. Angelina Ngalula.


Waziri Mulamula akizungumza na Wawakilishi wa Bodi ya TPSF kutoka katika Sekta za Huduma, Sekta Umma, Sekta ya Wenye Viwanda Vidogo,Sekta ya Wafanyabiashara Wanawake, Sekta ya Uhandisi na Ujenzi, na ulioambatana, Uongozi wa TPSF uliokuwa umeambatana na Bi. Ngalula.

Kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Balozi Mindi Kasiga akifafanua jambo katika mazungumzo hayo.


Balozi Mulamula akimkabidhi  Mwenyekiti wa Bodi ya TPSF, Bi. Ngalula vitabu vya Diplomasia ya Uchumi.

Picha ya Pamoja.



VACANCY ANNOUNCEMENT


 

VACANCY ANNOUNCEMENT









 

NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI ZATAKIWA KUKUZA, KUENZI KISWAHILI

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

Nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimetakiwa kuweka mikakati ya muda mrefu ili kukuza, kuendeleza na kueneza lugha ya Kiswahili duniani.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Bw. Khamis Abdalla Saidi aliyemwakilisha Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe.Tabia Maulid Mwita katika Kongamano la kwanza la Siku ya Kiswahili Duniani lililoanza leo tarehe 6 Julai, 2022 Zanzibar. 

Kongamano hilo linalongozwa na Kauli Mbiu: “Kiswahili kwa Amani, Ustawi na Utangamano wa Kikanda” litahitimishwa kwenye siku ya Kilele cha Siku ya Kiswahili duniani tarehe 7 Julai 2022.

Katika hotuba yake, Bw. Saidi amesema kuenea kwa Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki na Mataifa mengine ni bidhaa ya bishara, hivyo umuhimu wa Kiswahili ni mkubwa katika kupiga hatua ya kimaendeleo. 

“Ni jukumu la kila mmoja wetu kukifuatilia Kiswahili katika kila hatua na kutafuta na kubuni njia na mikakati ya muda mrefu na ya kisasa ya kuikuza lugha hii adhimu ya Kiswahili,” amesema Bw. Saidi.

Bw. Saidi aliongeza Lugha ya Kiswahili inatakiwa itumike kama bidhaa inayouzwa na kupata tija. Kuna haja kubwa ya kuwekeza kuwasomesha wataalamu wa lugha kuwa na stadi na uwezo unaotakiwa katika kutoa huduma ya kufundisha, ukalimani, kutafrisi na kuandaa machapisho mbali mbali kwa Kiswahili.

“Ni jukumu la vyuo vikuu vya Afrika Mashariki kutilia mkazo mikakati ya muda mrefu ya uwekezaji wa kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa kufanya tafiti mbalimbali za lugha,” ameongeza Bw. Saidi. 

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote amesema kuwa jumuiya ya Afrika Mashariki inapaswa kushirikiana kwa pamoja na wadau wa Lugha ya Kiswahili ili kuweza kupata uzoefu wa matumizi ya Kiswahili pamoja na kujadili changamoto za lugha hiyo ili kuimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili yataimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa lugha hii ni lugha ya biashara hivyo tunapaswa kujivunia lugha hii adhimu kwa maslahi mapana ya jumuiya yetu,” amesema Mhandisi Mlote.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (MS TCDC), Bi. Yusta Mganga amesema licha ya kuimarika kwa matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ukanda huo unapaswa kuchukua hatua madhubuti zaidi kwa ajili ya kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakuzwa na kuendelezwa miongoni mwa nchi ambazo bado hazijaimarika katika matumizi ya Kiswahili. 

“Kuna njia mbalimbali za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kama vile kufanya tafiti, uandaaji wa makongamano na semina mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya Kiswahili…….katika kuandhimisha siku hii muhimu ni vyema tukatafakari mafanikio ya Kiswahili katika ukanda wa Jumuiya yetu ili kuimarisha amani na utangamano wa kikanda,” amesema Bb. Mganga

Novemba 23, 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) lilitangazwa rasmi kuwa tarehe 7 Julai ya kila mwaka ni siku maalumu ya kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani. 

Februari 2022, Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika katika mkutano wake wa kawaida wa 35 walipitisha Kiswahili kama Lugha ya Kazi na mawasiliano mapana Barani Afrika.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, Bw. Khamis Abdalla Saidi akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani linalofanyika Zanzibar kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote akitoa hotuba yake katika Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar

Kaimu Katibu Mtendaji Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. James Jowi akizungumza na washiriki wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar 

Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Dkt. Mwanahija Ali Juma akielezea mchango wa BAKIZA katika Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar 

Meza Kuu wakifuatilia kikundi cha ngoma za asili kutoka Zanzibar wakati wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar 

Washiriki wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani wakifuatilia kikundi cha ngoma za asili kutoka Zanzibar  

Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota akitoa mchango wake katika Kongamano la Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar

Washiriki wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani wakiimba wimbo wa Taifa  

Washiriki wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani wakifuatilia Kongamano hilo lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar 

Meza Kuu katika picha ya pamoja na wawakilishi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar 



WATANZANIA WAASWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MASOKO YA KIMATAIFA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amewasihi Watanzania kuchangamkia fursa za masoko ya bidhaa mbalimbali nje ya nchi.

Balozi Fatma ametoa rai hiyo leo alipotembelea Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam.

Balozi Fatma ameeleza Wizara ya Mambo ya Nje kupitia Balozi zake nje imekuwa ikitatafuta fursa za uwekezaji, masoko ya bidhaa na kutangaza vivutio vya utalii kupitia majukwaa na mikutano mbalimbali inayofanyika katika vituo vya uwakilishi nje ya nchi.

“Fursa za masoko zinazopatikana kwa sasa ni pamoja na; Soko la zao la ufuta, mihogo na soya nchini China; Soko la nyama na wanyama kama mbuzi na kondoo nchini Saud Arabia; Soko la nafaka kama maharage na mbaazi nchini Oman na Umoja wa Falme za kiarabu (U.A.E);  Soko la parachichi nchini Ufaransa, India na Uholanzi; na Soko la asali katika nchi za Scandnavia na Mashariki ya Kati.

Balozi Fatma pia ameeleza uwepo wa soko la uyoga katika masoko ya kimataifa kufuatia umuhimu wa zao hilo na kutoa rai kwa watanzania kuchangamkia kilimo kwa ajili ya biashara badala ya kuzalisha kwa chakula pekee.

Aidha, aliongeza kusema jitihada hizi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zinafanywa kwa kushirikiana na Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Mamlaka ya Usimamizi wa Biashara Tanzania (TANTRADE) pamoja na Wizara ya Kilimo kwa lengo la kuhamasisha wakulima na wafanyabiashara kuchangamkia fursa mbalimbali za masoko ili kujitangaza kimataifa na kukuza mitaji ya biashara zao.

Wakati huo huo Balozi Fatma amezungumzia jitihada zinazofanywa na Balozi zetu katika kutangaza filamu ya “Tanzania the Roya Tour” kwa lengo la kuongeza watalii sambamba na kuitangaza Tanzania Nje ya mipaka kupitia mandhari na mazingira ya asili yanayo onekana katika filamu hiyo.

Kadhalika, ameeleza fursa zinazopatikana kutokana na jitihada za wizara kupitia Balozi zake katika kukuza lugha ya Kiswahili duniani hususan wakati huu tunapoelekea tarehe 7 Julai 2022 kwenye maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yatakayoadhimishwa kitaifa Jijini Dar es Salaam.

Balozi Fatma akiwa katika viwanja vya Maonesho ya Sabasaba pia ametembelea banda la Kituo cha Mikutano cha Kitamataifa cha Arusha (AICC), Kenya, Zanzibar, pamoja na Shirika la Madini (Stamico).

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akipokea maelezo kutoka kwa maafisa wa Wizara hiyo wakati wa maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba tarehe 5 Julai 2022 jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akipokea maelezo kutoka kwa maafisa wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha wakati wa maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba tarehe 5 Julai 2022 jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akipokea maelezo kutoka kwa mjasiliamali anayeshiriki maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba  tarehe 5 Julai 2022 jijini Dar es Salaam.


BALOZI MUSHY AITAFUTIA MSHIRIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA

Balozi wa Tanzania nchini Austria, Mhe. Celestine Mushy akiwa katika kikao na uongozi wa Hospitali na Chuo Kikuu cha Tiba cha Vienna ambapo wamekubaliana kuandaa Hati ya Makubaliano (MoU) ya kuanzisha ushirikino na Hospitali ya Benjamin Mkapa ya jijini Dodoma.

Balozi wa Tanzania nchini Austria, Mhe. Celestine Mushy
akiwa na baadhi ya viongozi wa Hospitali na Chuo Kikuu cha Tiba cha Vienna baada ya kikao chao walichokubaliana kuandaa Hati ya Makubaliano (MoU) ya kuanzisha ushirikino na Hospitali ya Benjamin Mkapa ya jijini Dodoma.

Balozi wa Tanzania nchini Austria, Mhe. Celestine Mushy akiwa na baadhi ya madaktari wa
Hospitali na Chuo Kikuu cha Tiba cha Vienna. Hospitali hiyo imekubali kuanzisha ushirikino na Hospitali ya Benjamin Mkapa ya jijini Dodoma.

Balozi wa Tanzania nchini Austria, Mhe. Celestine Mushy akiwa katika picha ya pamoja na Watanzania wanaoishi nchini Ausrtia baada ya kufanya nao mkutano wa kujadili mustakabali wao. katika mkutano huo Watanzania hao walianzisha umoja wao na kuchagua viongozi wa umoja huo  utakaoitwa Tanzania Diaspora in Austria (TADA)

Balozi wa Tanzania nchini Austria, Mhe. Celestine Mushy (tai nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Umoja wa Watanzania wanaoishi Austria mara baada ya kuanzisha umoja huo na kuchagua viongozi wake.





 

TANZANIA NA AFRIKA KUSINI KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA ELIMU

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini, Mhe. Matsie Angelina Motshekga ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi.

Wakati wa kikao chao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam leo tarehe 5 Julai 2022, Mawaziri hao walijadili pamoja na mambo mengine, namna nchi zao zitakavyoweza kushirikiana katika sekta ya elimu.

Mhe. Motshekga anayetarajiwa kusaini Hati ya Makubaliano na Waziri wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda kuhusu Tanzania kushirikiana na Afrika Kusini kufundisha Kiswahili katika nchi hiyo, alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuainisha maeneo ya kipaumbele ya aina ya elimu tunayoihitaji ili tuweze kubadilishana uzoefu katika maeneo hayo.

Maeneo mengine ambayo viongozi hao waliyadili ni pamoja na programu za kubadilishana wanafunzi na walimu na changamoto zinazoikabili sekta za elimu za nchi hizo ambazo ni pamoja na uhaba wa miundombinu, mimba za mapema, kuacha shule na uhaba wa vitabu.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberrata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini Mhe. Matsie Angelina jijini Dar Es Salaam.

Ujumbe ulioambatana na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini Mhe. Matsie Angelina ukifuatilia kwa makini mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberrata Mulamula na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini Mhe. Matsie Angelina jijini Dar Es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberrata Mulamula na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini Mhe. Matsie Angelina wakiendelea kujadili masuala ya elimu kuhusu nchi zao huku ujumbe wa Tanzania ukifuatilia kwa makini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberrata Mulamula akiwa na mgeni wake, Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini Mhe. Matsie Angelina baada ya mazungumzo yao.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberrata Mulamula  na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini, Mhe. Matsie Angelina wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe walioambatana nao kwenye mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam.