Sunday, October 23, 2022
TANZANIA YAJIVUNIA USHIRIKIANO IMARA NA UMOJA WA MATAIFA
Tanzania imesema inajivunia ushirikiano kati yake na Umoja wa Mataifa (UN) na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo katika kuendeleza programu mbalimbali za maendeleo endelevu.
Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.), alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa Duniani katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo maadhimisho hayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 24 Oktoba.
“Tanzania inanufaika na uanachama wake kwenye Umoja wa Mataifa katika maendeleo. Kwa mfano, kupitia Mpango wa Malengo ya Milenia na Malengo ya Maendeleo Endelevu. Umoja wa Mataifa unaendelea kusaidia nchi wanachama kutekeleza malengo hayo ili kukuza amani, utawala wa sheria, haki za binadamu na maendeleo kwenye sekta mbalimbali. Tanzania imekuwa mnufaika wa mikakati hiyo na mwezi Mei, 2022, Umoja wa Mataifa ulizindua mpango wake mpya wa ushirikiano unaojulikana kwa jina la United Nations Sustainable Development Cooperation Framework baina ya Tanzania na Umoja huo, unaolenga kuleta maendeleo kwenye maeneo mbalimbali nchini,” alisema Balozi Mbarouk.
Pamoja na mambo mengine, Balozi Mbarouk aliongeza kuwa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini inasaidia kuhamasisha wadau mbalimbali kama vile taasisi za Serikali, asasi za kiraia, wanataaluma na kadhalika kupitia programu zake ili kuleta maendeleo ya Watanzania kama vile kuboresha huduma za afya, kutokomeza umaskini, njaa, kuhuisha sekta ya elimu, kupambana na mabadiliko ya tabianchi, na kukuza sayansi na teknolojia.
“Manufaa mengine ni ajira kwa Watanzania kwenye taasisi mbalimbali za Umoja wa Mataifa pamoja na misheni za kulinda amani za Umoja huo, suala linalonufaisha maisha ya Mtanzania mmoja mmoja lakini pia Taifa kwa ujumla,” Aliongeza Balozi Mbarouk.
Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bw. Zlatan Milišić amesema Umoja wa Mataifa umelenga kusaidia watu, ustawi, dunia na mazingira ili kuwawezesha wananchi kufikia vipaumbele vya maendeleo ya taifa na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
“Tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wake kwa kuweka mazingira wezeshi kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa unaahidi kuendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kuunga mkono jitihada za maendeleo za Serikali ili kuiwezesha kufikia vipaumbele vyake vya maendeleo na SDGs,” amesema Bw. Milišić.
Mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa Duniani anatarajia kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.)
Maadhimisho rasmi ya Siku ya Umoja wa Mataifa yatafanyika rasmi tarehe 24 Oktoba 2022 katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya madhimisho ya mwaka huu ni “Maendeleo yanayozingatia ujumuishwaji wa makundi yote”.
Saturday, October 22, 2022
TANZANIA NA URENO ZASAINI HATI KUIMARISHA USHIRIKIANO
Hati hiyo, imesainiwa
tarehe 21 Oktoba 2022 jijini Lisbon kati
ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.
Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ureno, Mhe. João Gomes Cravinho.
Akizungumza wakati
wa mazungumzo rasmi kati yao, Mhe. Dkt. Tax amesema anaishukuru Serikali ya
Ureno na Serikali yake kwa hatua hii muhimu katika ushirikiano wa kidiplomasia na
kwamba kusainiwa kwa hati hiyo kunalenga kuupeleka ushirikiano huo katika hatua
nyingine ya juu ambapo nchi hizi mbili zitaongeza zaidi ushirikiano katika
maeneo mbalimbali yenye maslahi kwao ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, uchumi wa
buluu, usafirishaji na elimu.
Vilevile amesema kwamba
hii ni ishara kwamba nchi hizi mbili zina nia ya ya dhati ya kushirikiana kwenye
masuala mbalimbali ya manufaa kwa pande zote mbili.
“Ziara yangu nchini
Ureno imekuwa ni ya manufaa makubwa kwani kwa mara ya kwanza katika historia ya
ushirikiano baina ya Tanzania na nchi hii tumesaini Hati ya Makubaliano ya
kuanzisha majadiliano ya kisiasa baina yetu. Hii ni hatua ya juu katika
ushirikiano wa kidiplomasia kwani sasa masuala mengi ya ushirikiano kati yetu ikiwemo
biashara, uwekezaji, utalii, yataimarika na kwenda viwango vingine vya juu kwa manufaa
ya pande zote mbili”, alisema Dkt. Tax.
Ameongeza kusema
kuwa, wamekubaliana na Waziri mwenzake kuweka mikakati thabiti ya pamoja ya ufuatiliaji
wa utekelezaji wa maeneo mbalimbali ya
ushirikiano waliyokubaliana ambapo pia Mhe. Dkt. Tax amewataka Watanzania kutumia
hatua ya kusainiwa kwa mkataba huo kama chachu ya kuanza kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo Ureno ikiwemo
biashara kwa bidhaa za kahawa, chai, samaki, viungo vya chakula na mbao.
Pia, wakati wa mazungumzo yao, Tanzania imesisitiza
umuhimu wa nchi hiyo kushirikiana nayo katika medani za kimataifa hususan
kuendelea kupaza sauti ili nchi za Ulaya ziendelee kuisadia Tanzania na nchi za Afrika katika kukabiliana na
changamoto zinazotokana na mabadiliko ya
Tabianchi.
Kwa upande wake, Mhe.
João Gomes Cravinho amemshukuru Mhe. Dkt. Tax kwa kukubali
mwaliko wake na kutembelea nchini humo na kwamba Ureno inathamini mchango wa
Tanzania kupitia ushirikiano uliopo kati yao ikiwa ni pamoja na ushirikiano katika
medani za Kimataifa.
Amesema ana imani kuwa kusainiwa kwa Hati hiyo
muhimu ni mwanzo mpya wa ushirikiano huo ambapo nchi hizi mbili sasa
zitazingatia na kujitoa zaidi katika kuhakikisha ushirikiano uliopo unaimarika
zaidi.
“Hatua ya kusainiwa kwa Hati hii ni ya
kihistoria.. Kilichobaki sasa ni kuhakikisha yale tuliyokubaliana leo na
kupitia hati hiyo yanatekelezwa” alisema Mhe. Gomez.
Akizungumzia maeneo ambayo nchi hiyo imepiga
hatua na ipo tayari kushirikiana na Tanzania kuwa ni pamoja na eneo la Nishati
Mbadala. Alisema nchi hiyo hadi sasa imefikia asilimia 62 ya matumizi ya
Nishati hiyo na kwamba malengo yao ni kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2026.
Wakati wa mazungumzo
yao viongozi hao pia walikubaliana kuimarisha ushirikiano katika masuala ya
biashara, elimu, utalii, sanaa na michezo pamoja na kukuza Lugha ya Kiswahili
kwa upande wa Ureno na Kireno kwa upande wa Tanzania.
Ziara ya Mhe. Waziri Tax nchini Ureno ni matokeo ya majadiliano kati ya Rais wa Ureno, Mhe. Rebelo De Sousa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Isdor Mpango walipokutana mwezi Juni 2022 pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari ambapo walizungumza kuhusu umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.
Mhe. Dkt. Tax amehitimisha ziara yake ya siku mbili aliyoifanya nchini humo kuanzia tarehe 20 hadi 22 Oktoba 2022 kwa mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mhe. João Gomes Cravinho. Itakumbukwa kuwa, Mhe. Waziri Tax alianza ziara yake nchini Poland kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba 2022 kabla ya kutembelea Ureno.
Waheshimiwa Mawaziri wakibadilisha Hati hiyo muhimu mara baada ya kusaini |
Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Gomes wakionesha Hati hiyo mara baada ya kusaini |
Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Gomes wakiwa katika mazungumza rasmi kuhusu namna ya kuimarisha na kuboresha ushirikiano kati ya Tanzania na Ureno |
Maafisa kutoaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakinukuu mazungumzo kati ya Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Gomes. Kushoto ni Bi. Liliani Kimaro na Bi. Sekela Mwambegele. |
Mhe. Gomes akimkabidhi zawadi Mhe. Dkt. Tax mara baada ya kukamilisha mazungumzo rasmi |
Mhe. Dkt. Tax naye akimpatia zawadi Mhe. Gomes. Zawadi hiyo ni bidhaa za Tanzania ikiwemo Korosho, Kahawa, Asali, Batiki na Viungo vya Chakula |
Mhe. Gomes akimtambulisha Mhe. Dkt. Tax kwa wasaidizi wake |
Ujumbe wa Tanzania |
Mkuu wa Itifaki wa Ureno akisoma Hati ya Makubaliano kwa Mawaziri kabla ya kusainiwa |
Mhe. Dkt. Tax na mwenyeji wake Mhe. Gomes wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukamilisha mazungumzo kati yao |
Mhe. Dkt. Tax akiagana na Mhe. Gomes mara baada ya kukamilisha mazungumzo na kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano |
Picha ya pamoja |
Friday, October 21, 2022
TANZANIA YANADI FURSA ZA UWEKEZAJI NCHINI URENO
Mhe.
Dkt. Stergomena ametoa kauli hiyo jijini
Lisbon wakati akifungua rasmi Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya
Tanzania na Ureno lililoloandaliwa kwa
ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini Ureno na Taasisi ya Biashara na
Uwekezaji ya Ureno na kuishirikisha
Jumuiya yaWafanyabiashara wa Ureno.
Mhe.
Dkt. Tax amesema dhamira kuu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa
Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuweka
mazingira wezeshi ya uwekezaji na ufanyaji biashara hususan kwa kuishirikisha
ipasavyo sekta binafsi. Amesema tayari Serikali imefanya majadiliano ya mara
kwa mara na sekta biafsi ili kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Amesema
katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini masuala
mbalimbali yanaboreshwa zikiwemo huduma, sheria, miundombinu pamoja na
kuishirikisha kikamilifu sekta binafsi ambayo ni muhimu katika kuchangia uchumi
wa nchini.
“Tupo
hapa leo ili kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ureno hususan katika
masuala ya biashara na uwekezaji. Tanzania inaendelea kuhamasisha uwekezaji
kutoka ndani na nje ya nchi kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji. Katika
maboresho hayo ni pamoja na Serikali kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi ili kuiwezesha sekta hii kuwa na
ufanisi na kuchangia uchumi ipasavyo” amesema Dkt. Tax.
Amesema
Serikali inaendelea kuboresha miundombinu kama barabara, bandari, reli, viwanja
vya ndege na upatikanaji wa maji na umeme ili kuwawezesha wawekezaji kutopata
changamoto zozote pale wanapokuja nchini kuwekeza.
“Serikali imefanya jitihada za makusudi za
kuhakikisha miundombinu yote ya msingi kama maji, umeme, barabara, reli,
usafiri wa anga na mawasiliano ya simu vinapatikana kwa ngazi tofauti tofauti.
Kupitia maboresho haya ni imani yetu wawekezeji watapata ujasiri wa kuwekeza Tanzania
na si mahali pengine popote”, amesisitiza Dkt. Tax.
Amesema
masuala mengine yanayohamasisha uwekezaji, biashara na utalii nchini ni pamoja
na ushiriki wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuri ya Muungano wa Tanzania
kwenye Filamu ya kutangaza Utalii nchini ya The
Royal Tour, Sera ya Mambo ya Nje yenye msisitizo katika Diplomasia ya
Uchumi ambayo imekuwa chachu katika kuwajengea ujasiri wawekezaji nchini pamoja
na ushiriki wa Tanzania kwenye majukwaa mbalimbali ya kimataifa ya biashara na
uwekezaji kama Maonesho ya Biashara ya Dubai ya mwaka 2020. Vyote hivi vimeipaisha zaidi Tanzania duniani na
kuchangia ongezeko la watalii na wawekezaji nchini.
Dkt.
Tax alitumia fursa hiyo pia kuwakaribisha wawekezaji na wananchi wa Ureno kwa
ujumla kutembelea Tanzania ili kujionea vivutio mbalimbali vya utalii huku
akiwahamasisha kuangalia Filamu ya Utalii ya Royal Tour ambayo ameilezea kuwa ni ya aina yake kwani mhusika mkuu
katika Filamu hiyo ni Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Kwa
upande wake, Waziri anayeshughulikia Biashara na Uwekezaji wa Ureno, Mhe.
Bernardo Ivo Cruz amepongeza ziara ya Mhe. Dkt. Tax nchini humo akisema imekuja
wakati mwafaka ambao wakati dunia ikiendelea kushuhudia changamoto mbalimbali za
kiuchumi, Tanzania na Ureno zinaangalia
namna ya kushirikiana katika biashara na uwekezaji ili kujikwamua
kiuchumi.
“Tanzania
ni mshirika wetu muhimu katika biashara na uwekezaji na tupo tayari kuimarisha
ushirikiano huu. Nakupongeza Mhe. Waziri kwa kufanya ziara katika kipindi hiki
na tunaahidi kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji
ikiwemo Kilimobiashara, Uchumi wa Bluu, Miundombinu na Sekta zingine za
uwekezaji” alisema Mhe. Cruz.
Pia
aliongeza kusema nchi yake inao Mpango wa miaka sita wa ushirikiano katika
biashara na uwekezaji kuanzia mwaka 2021-2027 ambapo Tanzania ni miongoni mwa
nchi zitakazonufaika na mpango huo.
Akiwasilisha
mada kuhusu Fursa za Uwekezaji zilizopo nchini kwa washiriki wa Jukwaa hilo,
Mkurugenzi wa Biashara na Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),
Bw. Revocatus Rasheli amewahamasisha wawekezaji na wafanyabiasha kutoka Ureno
kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji nchini huku akisema
tayari anayo mkononi miradi 100 chini ya Sekta ya Umma na miradi 36 chini ya
Sekta Binafsi ambayo ipo tayari na kwamba ni kiasi cha wawekezaji hao kuchagua
na kuwekeza.
Aliongeza
kusema Tanzania katika kuhamasisha uwekezaji imetenga ardhi yenye ukubwa wa Hekta
milioni 1.6 kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo ambapo tayari Hekta 6,000 zipo
Mkoani Morogoro kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo.
Pia
alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji hao kuwekeza kwenye sekta ya
utalii ikiwa ni pamoja na kujenga Hoteli, Nyumba za Makazi na Kumbi za Mikutano.
“Serikali
ya Tanzani ainazo fursa nyingi za uwekezaji. Nawakaribisha kuwekeza kwenye
kilimo, uvuvi, madini, miundombinu lakini pia ujenzi wa hoteli, nyumba za
makazi na kumbi za mikutano hususan katika miji mikuu ikiwemo Dar es Salaana na
Makao Makuu ya Nchi yetu Dodoma ambako mahitaji ni makubwa zaidi” alisisitiza
Bw. Rasheli.
Kadhalika,
Mkurugenzi huyo amesema Ureno ni mdau muhimu katika ushirikiano na Tanzania na
kwamba ipo haja ya kuongeza biashara
kati ya nchi hizi mbili ambapo amesema hadi
sasa Ureno imesajili miradi 13 nchini yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni
Tisa ambayo imetoa fursa za ajira 325 kwa watanzania.
“Ziara
hii ni muhimu sana kwetu Tanzania na Ureno, ni imani yetu kuwa ziara hii itaongeza
wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Ureno kuja nchini ili kwa pamoja nchi hizi
zinufaike kupitia ushirikiano mzuri uliopo” alisisitiza Bw. Rasheli.
Naye
Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango wa Mamlaka ya
Kukuza Uwekezaji Zanziabar (ZIPA) Bw. Emmanuel Mashimba amesema Serikali ya
Zanzibar inaendelea kuweka mazingira wezeshi katika kuvutia wawekezaji na
wafanyabiashara na kwamba Ureno ni miongoni mwa nchi muhimu ambazo Zanzibar ipo
tayari kushirikiana nazo katika sekta za uchumi wa bluu, utalii na miundombinu.
Mhe. Dkt. Tax yupo nchini Portugal kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 20 hadi 22 Oktoba, 2022. Akiwa nchini humo, Mhe. Dkt. Tax pamoja na mambo mengine atakutana kwa mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Joao Gomez Cravinho pamoja na kusaini Hati ya Makubaliano ya kuanzisha Majadiliano ya Kisiasa kati ya Tanzania na Ureno.
Waziri wa Nchi wa Ureno anayeshughulikia masuala ya Biashara na Uwekezaji, Mhe. Bernardo Ivo Cruz naye akizungumza wakati wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Ureno |
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Baiashara na Uwekezaji ya Ureno, Bw.Kuis Castro Henriques naye akiwakaribisha kwenye Ofisi za Taasisi yake washiriki wa Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno |
Mkurugenzi wa Uwekezaji na Biashara kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Revocatus Rasheli akinadi fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zilizopo nchini kwa washiriki wa Jukwaa |
Balozi wa Tanzania nchini Ureno mwenye makazi yake nchini Ufaransa, Mhe. Samwel Shelukindo (kulia) akishiriki Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno. |
Washiriki wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno wakifuatilia mada zilizowasilishwa kwao |
Washiriki wengine wakifuatilia matukio |
Washiriki wengine kutoka Tanzania wakifuatilia mada wakati wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno lililofanyika Lisbon |
Mhe. Dkt. Tax akimpatia zawadi kutoka Tanzania Mhe. Cruz. Zawadi hiyo ni mchanganyiko wa bidhaa za Tanzania kama vile Kahawa, Korosho, Batiki, Asali na Viungo vya Chakula |
Mhe. Dkt. Tax akiagana na Mhe. Cruz mara baada ya ufunguzi wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno |
Picha ya pamoja |
Thursday, October 20, 2022
TANZANIA YAHAMASISHA WAWEKEZAJI SEKTA YA TEHAMA ILI KUKUZA UCHUMI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini ikiwemo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kunufaika kiuchumi kupitia sekta hiyo.
Waziri Dkt. Tax amesema hayo alipokutana kwa mazungumzo na Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya ASSECO ya Poland Bw. Adam Goral, inayojishughulisha na masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yenye nia ya kuwekeza nchini.
Akizungumza na Rais huyo, Mhe. Dkt. Tax amemweleza nia ya Serikali ya Tanzania ya kutaka kujiimarisha kwenye masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kupitia teknolojia hiyo nchi iweze kunufaika kiuchumi.
Mhe. Waziri amesema kuwa, katika ulimwengu wa sasa mifumo mingi ya utendaji imebadilika ambapo kazi nyingi hukamilishwa kwa kutumia vifaa vya kisasa kama simu, kompyuta na mtandao. Hivyo unahitajika uwekezaji wenye tija hususan kwenye eneo la usalama wa taarifa za watumiaji.
Ameongeza kuwa matumizi ya tehama nchini yameendelea kukua siku hadi siku ambapo taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali, za Fedha, Shule, Hospitali na nyingine hutegemea teknolojia ya uhakika na salama ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na tija.
Amesema mbali na mchango mkubwa wa tehama katika ukuaji wa uchumi nchini pia imeendelea kuchangia uzalishaji wa ajira kwa watanzania hususan vijana.
"Tanzania inayo nia ya dhati ya kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza na kunufaika kiuchumi kupitia matumizi ya tehama. Hata hivyo jambo muhimu katika teknolojia hii ni usalama wa taarifa katika matumizi ya teknolojia hiyo. Hivyo, tungependa wawekezaji kulipa kipaumbele suala hili pale wanapokuja kuwekeza”, alisema Dkt. Tax.
Aidha, Mhe. Dkt. Tax ameahidi kuiunganisha taasisi hiyo na mamlaka husika nchini, ikiwemo Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhusu nia yao ya kutaka kuwekeza nchini ili mazungumzo yaanze.
Kwa upande wake Rais wa Kampuni hiyo, Bw. Goral amemshukuru Mhe. Waziri kwa kutembelea Kampuni hiyo na kusema kampuni yake inatengeneza software zake yenyewe na kuongoza kwa teknolojia kwa upande wa Ulaya mashariki ina nia ya dhati ya kuwekeza nchini na ipo tayari kushirikiana na Serikali katika kuboresha mifumo mbalimbali ya tehama.
“Kampuni yetu ina nia ya dhati ya kuwekeza Tanzania na usalama wa matumizi ya mtandao ni kipaumbele chetu. Tayari tunayoo Program maalum ilianza mwaka 2020 inayoshughulikia usalama wa mitandao. Tupo tayari kubadilishana uzoefu na ujuzi na Tanzania” alisema Bw. Goral
Awali akitoa mada kwenye mkutano huo kuhusu hali ya matumizi ya teknolojia ya habari nchini, Mtaalam wa Tehama kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Brigedia Generali Mbaraka Mkeremy amesema Tanzania imepiga hatua katika matumizi ya tehama ambapo kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari hadi sasa watanzania wanaomiliki simu ni milioni 28 na muamala ya simu imeingiza mapato ya zaidi Shilingi Trilion 20 kwa mwaka 2021 pekee.
Kampuni ya Asseco iliyoanzishwa mwaka 1991 hutoa mafunzo na ushauri kuhusu masuala ya tehama na kutengeneza software zake yenyewe. Tayari imewekeza katika Mabara sita na nchi 60 ulimwenguni zikiwemo Ethiopia, Nigeria, Togo na Botswana kwa upande wa Bara la Afrika.
Mhe. Dkt. Tax alikuwa nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine alitumia ziara hiyo kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo wawekezaji na wafanyabiashara kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji nchini.
Rais wa Kampuni ya ASSECO, Dkt. Goral akizungumza wakati wa mkutano na Mhe. Dkt. Tax |
Mkutano ukiendelea |
Wajumbe kutoka Tanzania wakati wa mkutano huo |
Wajumbe wengine wa Tanzania |
Brigedia Generali Mbaraka Mkeremy akiwasilisha mada kuhusu matumizi na changamoto za mtandao |
Ujumbe wa Serikali ya Poland akiwemo Balozi wa Poland nchini Tanzania (kushoto) |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiagana na Rais wa Kampuni ya ASSECO, Dkt. Goral |