Mkutano wa Makatibu Wakuu kukamilisha maandalizi ya Mkutano wa 43 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika jijini Bujumbura, Burundi.
Mkutano huo ambao umetanguliwa na mkutano wa Wataalam uliofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 21 Februari 2023 umepokea na kupitia taarifa, agenda na mapendekezo yaliyotokana na Mkutano wa wataalam hao kuhusu masuala mbalimbali ya Jumuiya ambazo hatimaye zitawasilishwa kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri tarehe 23 Februari 2023.
Taarifa zilizowasilishwa ni pamoja na taarifa ya utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa kwenye vikao vilivyopita katika maeneo mbalimbali ya biashara na forodha, miundombinu, ulinzi na usalama, sheria, utalii, ajira na utawala na fedha. Pia mkutano umepokea taarifa ya mwaka ya Ukaguzi wa Hesabu za Jumuiya kwa mwaka wa fedha ulioishia mwezi Juni 2022; Taarifa ya Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya; Taarifa kuhusu Taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kupitia na kupitisha ratiba ya shughuli za Jumuiya kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2023.
Kadhalika masuala mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na umuhimu wa kukitangaza Kiswahili kwa kuanzisha vituo vya utamaduni wa lugha hiyo katika Balozi za Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki; na kutoa mwelekeo wa kuanza kutumika kwa lugha ya Kifaransa na Kiswahili katika uendeshaji wa shughuli rasmi za Jumuiya.
Katika Mkutano huo ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine.
Viongozi
wengine walioambatana naye ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti
ya Utumishi Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria,
Dkt. Khatibu Kazungu, Naibu Gavana wa
Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Yamungu Kayandabila na Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jilly Maleko.
Wengine waliombatana naye ni Balozi Stephen Mbundi, Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama, Bw. Bernard Haule Mkurugenzi Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Bw. Haji Janabi wote wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Maafisa kutoka Wizara mbalimbali.
Mkutano huo ambao umefanyika chini ya uenyekiti wa Burundi, umehudhuriwa na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki huku Sudan Kusini wakishiriki kwa njia ya mtandao
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine (kulia) akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika jijini Bujumbura tarehe 22 Februari 2023 kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika jijini hapa tarehe 23 Fevruari 2023. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bibi. Amina Khamis Shaaban na katikati ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi. |
Mkutano ukiendelea |
Mwenyekiti kutoka Burundi nae akisaini Ripoti hiyo |
Mjumbe kutoka Rwanda nae akisaini Ripoti |
Mjumbe kutoka Kenya akisaini ripoti |