Wednesday, February 22, 2023

MAKATIBU WAKUU WAKAMILISHA MAANDALIZI YA MKUTANO WA 43 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA EAC

Mkutano wa Makatibu Wakuu kukamilisha maandalizi ya Mkutano wa 43 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika  jijini Bujumbura, Burundi.

 

Mkutano huo ambao umetanguliwa na mkutano wa Wataalam uliofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 21 Februari 2023 umepokea na kupitia taarifa, agenda na mapendekezo yaliyotokana na Mkutano wa wataalam hao kuhusu masuala mbalimbali ya Jumuiya ambazo hatimaye zitawasilishwa kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri tarehe 23 Februari 2023.

 

Taarifa zilizowasilishwa ni pamoja na  taarifa ya utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa kwenye vikao vilivyopita katika maeneo mbalimbali ya  biashara na forodha, miundombinu, ulinzi na usalama, sheria, utalii, ajira na utawala na fedha. Pia mkutano umepokea taarifa ya mwaka ya Ukaguzi wa Hesabu za Jumuiya kwa mwaka wa fedha ulioishia mwezi Juni 2022; Taarifa ya Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya; Taarifa kuhusu Taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kupitia na kupitisha ratiba ya shughuli za Jumuiya kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2023.

 

Kadhalika masuala mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na umuhimu wa kukitangaza Kiswahili kwa kuanzisha vituo vya utamaduni wa lugha hiyo katika Balozi za Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki; na kutoa mwelekeo wa kuanza kutumika kwa lugha ya Kifaransa na Kiswahili katika uendeshaji wa shughuli  rasmi za Jumuiya. 

 

Katika Mkutano huo ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine.

 

Viongozi wengine walioambatana naye ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi,  Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Khatibu Kazungu, Naibu  Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Yamungu Kayandabila na Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jilly Maleko.

 

Wengine waliombatana naye ni Balozi Stephen  Mbundi, Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama, Bw. Bernard Haule Mkurugenzi Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Bw. Haji Janabi wote wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Maafisa kutoka Wizara mbalimbali. 

 

Mkutano huo ambao umefanyika chini ya uenyekiti wa Burundi, umehudhuriwa na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki huku Sudan Kusini wakishiriki kwa njia ya mtandao

Mwenyekiti wa Mkutano wa Makatibu Wakuu ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Burundi, Bw. Severin Mbarubukeye (katikati) akiongoza Mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika jijini Bujumbura tarehe 22 Februari 2023 kwa ajili ya kuandaa Mkutano wa 43 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika jijini hapa tarehe 23 Februari 2023. Mkutano huo pamoja na mambo mengine umejadili na kupitisha agenda mbalimbali zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa Mawaziri. Kushoto ni Naibu katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine (kulia) akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika jijini Bujumbura tarehe 22 Februari 2023 kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri la  Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika jijini hapa tarehe 23 Fevruari 2023. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bibi. Amina Khamis Shaaban na katikati ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akichangia jambo wakati wa Mkutano wa makatibu Wakuu uliofanyika Bujumbura kuandaa Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mkutano ukiendelea
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akisaini Ripoti itakayowasilishwa kwenye Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mwenyekiti kutoka Burundi nae akisaini Ripoti hiyo
Mjumbe kutoka Rwanda nae akisaini Ripoti
Mjumbe kutoka Uganda akisaini Ripoti

Mjumbe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo akisaini ripoti

Mjumbe kutoka Kenya akisaini ripoti

Balozi Sokoine akibadilisha kwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Kenya, Bw. Abdi Dubat na Mjumbe kutoka Uganda wakibadilishana mawazo wakati wa mkutano wa Makatibu Wakuu

Awali Timu ya maandalizi ya Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Ngazi ya Wataalam wakisaini ripoti iliyowasilishwa kwenye Mkutano wa Makatibu Wakuu. Ujumbe  Tanzania uliongozwa na Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi (wa pili kushoto)

Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jilly Maleko (kushoto) akishiriki moja ya vikao vya maandalizi
Wajumbe wengine kutoka Tanzania katika vikao vya maandalizi

Wajumbe wakifuatilia mikutano ya maandalizi ya Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya  ya Afrika Mashariki

Mkutano ukiendelea


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.