Friday, February 24, 2023

DKT. TAX AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA 43 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA EAC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa  43 wa Kawaida wa  Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 23 Februari 2023.

 

Mhe. Dkt. Tax ambaye ameshiriki Mkutano huo kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwake kwenye wadhifa huo, ameungana na Mawaziri wenzake wanaosimamia masuala ya Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda katika Jumuiya hiyo kupitia, kujadili na kupitisha mapendekezo ya agenda mbalimbali zinazolenga kuboresha utendaji wa Jumuiya kwa manufaa ya Nchi Wanachama.

 

Miongoni mwa agenda zilizojadiliwa na kupitishwa na Baraza hilo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maazimio mbalimbali yaliyofikiwa na Baraza hilo kwenye vikao vilivyopita; taarifa kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, taarifa ya utekelezaji wa program mbalimbali katika sekta za miundombinu, forodha na biashara, utalii na ajira;  taarifa ya mwaka ya ukaguzi wa hesabu za jumuiya kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2022 na ripoti ya kamati ya utawala na fedha.pamoja na kupitia na kupitisha ratiba ya shughuli za Jumuiya kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2023.

 

Kadhalika masuala mengine yaliyojadiliwa ni umuhimu wa kukitangaza Kiswahili  duniani kwa kuanzisha vituo vya utamaduni wa lugha hiyo katika Balozi za Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki; na kutoa mwelekeo wa kuanza kutumika kwa lugha ya Kifaransa na Kiswahili katika uendeshaji wa shughuli  rasmi za Jumuiya. 

 

Awali akizungumza na Waandishi wa Habari Mwenyekiti kutoka Jamhuri ya Burundi ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Ezekiel Nibigira amesema kuwa Burundi kama mwenyekiti inaona fahari kuandaa Mkutano wa aina hiyo ambapo pia aliwakaribisha Mawaziri wenzake na washiriki wa Mkutano  huo nchini humo na kueleza kuwa nchi hiyo imeendelea kuwa na amani na utulivu wakati wote.

                                                                                           

Mkutano huo ambao umefanyika kwa siku tano , ulitanguliwa na vikao vya Wataalam na Makatibu Wakuu kutoka nchi wanachama viilivyofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 22 Februari 2023.

 

Mbali na Mhe. Dkt. Tax ujumbe wa Tanzania pia uliwajumuisha Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda,  Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Jilly Maleko,  Naibu Makatibu Wakuu akiwemo Bibi.  Amina Khamis Shaaban   Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.

 

Miongoni mwa majukumu ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya ni kutunga sera za Jumuiya, kufuatilia na kufanya mapitio ya mara kwa mara juu ya utekelezaji wa program mbalimbali za Jumuiya kwa maslahi mapana ya Nchi Wanachama.

 

Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inaundwa na nchi saba za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeendelea kuhakikisha wananchi katika nchi hizo wananufaika na Jumuiya hiyo hususan katika nyanja za biashara, ulinzi na usalama, viwanda, kilimo, miundombinu na huduma za kijamii.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (katikati) akichangia jambo wakati wa Mkutano wa 43 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliomalizika hivi karibuni jijini Bujumbura, Burundi. Mhe. Dkt. Tax aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo.

Mhe. Dkt. Tax akiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (kushoto)na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya (kulia) wakati wa Mkutano wa 43 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
 


Mwenyekiti wa Mkutano wa 43 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye pia ni Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki nchini Burundi, Mhe. Balozi Ezekiel Nibigira akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano huo. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Peter Mathuki.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda (kulia) akishiriki Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bibi Amina Khamis Shaaban
Sehemu ya ujumbe wa Burundi wakishiriki mkutano
Ujumbe wa Uganda na Sudan Kusin katika mkutano
Ujumbe wa Kenya katika mkutano
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakishiriki Mkutano

Ujumbe wa Rwanda katika Mkutano
Mkutano ukiendelea
Awali Mhe. Dkt. Tax aliongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya nchi kuhusu Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri. Pichani Mhe. Dkt. Tax akizungumza wakati wa kikao hicho kilichomshirikisha pia Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushiriano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine (kushoto)
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda akichangia jambo wakati wa kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya nchi kuhusu Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri. Pichani Mawaziri. Kulia ni Balozi Sokoine
Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jilly Maleko akishiriki kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya nchi kilichofanyika kabla ya kuanza Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri.
Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi akifafanua jambo kuhusu agenda za Mkutano kwa Waheshimiwa Mawaziri (hawapo pichani) wakati wa kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya nchi kuhusu Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri. Kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya na katikati ni Mhe. Balozi Maleko
Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Japhary Kachenje akishiriki kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya nchi kabla ya Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri.

Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Haji Janabi akishiriki kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya nchi kuhusu Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri.

Kikao kikiendelea

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.