Thursday, February 16, 2023

TANZANIA, ANGOLA ZASAINI HATI ZA MAKUBALIANO

Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola zimesaini Hati mbili za Makubaliano (MoU) kuanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) na Ushirikiano kati ya Chuo Cha Diplomasia cha Tanzania (CFR) na Chuo cha Venancio de Moura cha Angola.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Addis Ababa nchini Ethiopia.

Mara baada ya kusaini Hati hizo za Makubaliano, Dkt. Tax alisema Tanzania na Angola zimekuwa zikishirikiana kwa muda mrefu, na Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kuzisaidia nchi za Kusini mwa Bara la Afrika kujikomboa na tangu wakati huo imeendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali.

“Leo tumeona ni vyema turasimishe ushirikiano wetu kwa sababu dunia inakwenda mbele na kuna mambo mengi ya kufanya pamoja na hivyo tumesaini Hati mbili za Makubaliano ya kuanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja itakayotuwezesha kukutana na kujadili masuala mbalimbali yenye manufaa kwa pande zote mbili.

………lakini sisi kwa kuwa ni wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) tutaweza kujadili yanayojiri katika Kanda zetu na Kimataifa na kuona tunavyoweza kufanyia kazi kwa pamoja kwani umoja ni nguvu,” alisema Dkt. Tax

Kuhusu Makubaliano ya Ushirikiano wa Vyuo vya Diplomasia kati ya Tanzania na Angola, Waziri Tax alisema kupitia makubaliano hayo vyuo hivyo vitaweza kubadilishana uzoefu, utaalamu na wanafunzi ili kuboresha taasisi hizo za diplomasia.

“Kupitia makubaliano tuliyosaini leo, vyuo vyetu vya Dioplomasia vitabadilishana uzoefu, utaalamu na wanafunzi ili kuboresha zaidi taasisi zetu hizi za diplomasia,” alisema Waziri Tax.

Kwa Upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António amesema Angola imefurahishwa na uamuzi wa Serikali ya Tanzania kukubali kuanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) na kuelezea utayari wake wa kushirikiana katika nyanja mbalimbali kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Tanzania na Angola ni marafiki wa siku nyingi, kupiti makubaliano tuliyosaini leo tumefungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya mataifa yetu, tunayo mengi ya kushirikiana.

Kadhalika, kuhusu ushirikiano wa vyuo vyetu Waangola tumekuwa tukija kujifunza masuala mbalimbali ya kidiplomasia katika Chuo cha Diplomasia (CFR) na kuwa wanadiplomasia, hivyo kupitia makubaliano ya leo tutaweza kubadilishana uzoefu wa kidiplomasia na kuwanoa wanadiplomasia wengi zaidi,” alisema Balozi António.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakisaini Hati za Makubaliano (MoUs) za kuanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) na Hati ya Ushirikiano kati ya Chuo Cha Diplomasia cha Tanzania (CFR) na Chuo cha Venancio de Moura cha Angola. Hafla ya utiaji saini imefanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Addis Ababa nchini Ethiopia tarehe 16 Februari 2023.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakibadilishana Hati za Makubaliano (MoUs) za kuanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) na Hati ya Ushirikiano kati ya Chuo Cha Diplomasia cha Tanzania (CFR) na Chuo cha Venancio de Moura cha Angola baada ya kuzisaini katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Addis Ababa nchini Ethiopia tarehe 16 Februari 2023.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akieleza jambo baada ya kusaini Hati za Makubaliano (MoUs) za kuanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) na Hati ya Ushirikiano kati ya Chuo Cha Diplomasia cha Tanzania (CFR) na Chuo cha Venancio de Moura cha Angola katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Addis Ababa nchini Ethiopia tarehe 16 Februari 2023.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António baada ya kusaini Hati za Makubaliano (MoUs) katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Addis Ababa nchini Ethiopia tarehe 16 Februari 2023.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António kwenye picha ya pamoja na viongozi waandamizi wa serikali za Tanzania na Angola katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Addis Ababa nchini Ethiopia tarehe 16 Februari 2023


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.