Serikali ya Tanzania inaendelea kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kushirikiana
na nchi mbalimbali duniani ili kukuza uchumi
wa nchi kupitia fursa za biashara, uwekezaji na utalii zilizopo ndani na nje ya
nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Bungeni leo tarehe 09
Februari,2023 wakati akijibu swali la Mhe.
Felista Njau, Mbunge wa Viti Maalum kuhusu umuhimu
wa Serikali wa kuainisha nchi zenye fursa za biashara na uwekezaji ili kukuza
pato la Taifa.
Amesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa
kushirikiana na Wizara za kisekta na Balozi za Tanzania imeendelea kutangaza
fursa za biashara na uwekezaji zenye manufaa kwa Taifa na kwamba Wizara
inaandaa Mpango wa Kitaifa wa kutekeleza Diplomasia ya Uchumi utakaojumuisha
Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ili kufikia malengo tarajiwa.
Amesema Mpango huu ambao unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Desemba
2023, pamoja na mambo mengine unalenga kuhakikisha fursa za biashara, uwekezaji
na utalii zinakuwa na tija zaidi kwa wananchi wa Tanzania. Pia Mpango huo
utajumuisha Sekta zote husika ikiwa ni pamoja na kuainisha maeneo muhimu ya
kisekta yatakayo changia katika kukuza uchumi na pato la Taifa.
Akichangia hoja kuhusu mkakati wa utoaji elimu kwa wananchi kuhusu dhana ya Diplomasia ya Uchumi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, amesema Wizara inaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali na kufafanua kwamba Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi unaoandaliwa pia utajumuisha Mpango wa kutoa elimu kwa umma kuhusu dhana hiyo ili kuwawezesha wananchi kuielewa dhana hii na kuwawezesha kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali.
Kuhusu taarifa hasi zinazotolewa na vyombo vya kimataifa dhidi ya Tanzania, Mhe. Dkt. Tax amesema tayari Wizara imeanza kushirikiana na vyombo vya habari vya Nje hususan vile vinavyorusha matangazo yake kwa Kiswahili ili kupitia vyombo hivyo fursa na taarifa chanya kuhusu Tanzania zitangazwe duniani kote.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.