Friday, February 24, 2023

SERIKALI YAWAHAKIKISHIA WAFANYABIASHARA MAZINGIRA SALAMA YA BIASHARA

Serikali imewahakikishia wafanyabiashara kutoka Nchi za Umoja wa Ulaya (EU) kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ni salama, bora na rafiki.

Rai hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi alipofunga Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya lililofanyika jijini Dar es salaam kuanzia tarehe 23 – 24 Februari 2023. 

Dkt. Mwinyi alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekusudia kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza nchini.

“EU imekuwa mwekezaji mkubwa nchini Tanzania na imechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la ufanyaji biashara kati yake na Tanzania, lengo la serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania ni kukuza na kuendeleza sekta binafsi yenye nguvu, hivyo natoa rai kwenu kuwekeza kwa wingi kwani mazingira ni bora na salama,” alisisitiza Dkt. Mwinyi

Rais Mwinyi aliongeza kuwa Serikali imejikita katika kukuza uwekezaji kupitia sekta za kilimo, uchumi wa buluu, madini, usafirishaji, miundombinu, utalii na nyingine nyingi na kuwasihi wafanyabiashara wapatao 400 kutoka EU kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana nchini. 

“Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali imejidhatiti kuweka mazingira yenye ushindani ya biashara na uwekezaji ikiwa ni mkakati wa kuendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara na kuhakikisha yanakuwa rafiki kwa wawekezaji,” aliongeza Rais Mwinyi.

Awali Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Mhe. Manfredo Fanti alisema Tanzania imejitahidi kuboresha mazingira, kuimarisha mahusiano ya nje na kuondoa vikwazo mbalimbali hivyo ni wakati muafaka kwa EU kufanya biashara na Tanzania kwakuwa mazingira ni mazuri na yanaridhisha.

“Mfano kitendo cha Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya (EIB) kurejea Tanzania na kufanya uwekezaji mkubwa wenye thamani ya Euro milioni zaidi ya 500 ni kutokana na Serikali kuboresha mazingira ya bishara na uwekezaji,” alisema Balozi Fanti   

Balozi Fanti amewasihi wafanyabiashara wa Tanzania kupenda kukuza ujuzi ili waweze kuendeleza na kukuza biashara zao pamoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

“EU kwa umoja wetu tutaendelea kuimarisha nguvu zetu kwa pamoja ili kuhakikisha tunaendelea kuwekeza na kukuza biashara kati yetu na Tanzania kwa maslahi ya mataifa yote,” alisema Balozi Fanti.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga amesema Tanzania na Nchi za Umoja wa Ulaya zimekuwa na ushirikiano imara na wa muda mrefu na kwamba ushirikiano huo umesaidia kuendelea kushirikiana katika sekta mbalimbali za maendeleo kwa maslahi ya mataifa yote mawili.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akihutubia wakati wa kufunga rasmi Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya lililofanyika jijini Dar es salaam kuanzia tarehe 23 – 24 Februari 2023  

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akifuatilia Hotuba ya ufunguzi wa Jukwaa  la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya lililofanyika Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde.   

Sehemu ya viongozi mbalimbali wakifuatilia Hotuba ya ufunguzi wa Jukwaa  la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya lililofanyika Jijini Dar es Salaam

Baadhi ya Mabalozi wa Tanzania katika nchi za Umoja wa Ulaya  wakifuatilia Hotuba ya ufunguzi wa Jukwaa  la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya lililofungwa Jijini Dar es Salaam


Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Grace Martin akichangia jambo wakati wa Jukwaa  la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya lililofungwa leo Jijini Dar es Salaam 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.