Serikali imewasihi wafanyabiashara na wawekezaji nchini kutumia fursa ya Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya kujifunza, kubadilishana uzoefu na mawazo ya kibiashara ili kukuza na kuchochea maendeleo ya uchumi.
Rai hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango alipofungua Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) linalofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 23 – 24 Februari, 2023 Jijini Dar es Salaam.
“Nawasihi wafanyabiashara wa Tanzania, kutumia fursa hii adhimu kujifunza, kubadilishana uzoefu na mawazo ya kibiashara ili kupiga hatua kama wenzetu na muweze kukuza na kuchangia katika uchumi wa taifa letu,” alisema Dkt. Mpango
Dkt. Mpango alisema Serikali ya Tanzania inatoa kipaumbele katika sekta kilimo kwa kuwa ni moja ya sekta ambazo zina mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa.
“Serikali imetoa msukumo wa kipekee katika kujenga uchumi wa nchi kwa kuwekeza kwenye kilimo biashara ili kuifanya sekta ya kilimo kukua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030,” alisema Dkt. Mpango
“Serikali imechagua kilimo cha mashamba makubwa ya pamoja kwa vijana ambacho kinahitaji uwekezaji wa kisasa, tunalenga uwekezaji mkubwa wa kibiashara kwenye kilimo cha miwa, ngano, alizeti, mahindi, zabibu, matunda, mbogamboga, uvuvi wa bahari kuu, ufugaji na ufugaji wa Samaki,”alisema Dk Mpango
Amesema Serikali ya Tanzania inatambua na kuthamini mchango wa muda mrefu wa EU kwa Tanzania ambapo imenufaika na msaada kwa programu mbalimbali za ushirikiano wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni tatu ikiwemo msaada wa kukabiliana na janga la Uviko -19.
Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji alisema Jukwaa hilo ni muhimu kwa Tanzania kwakuwa linatoa fursa ya wafanyabiashara kutoka pande zote kujadili fursa za biashara na uwekezaji wenye tija kwa pande zote mbili.
“Jukwa hii ni muhimu kwa sababu linatoa fursa kwa wafanyabiashara kujadili na kubadilishana mawazo ya kibiashara hususan katika sekta za kilimo, utalii, nishati, na madini, tehama, miundombinu, fedha na nyinginezo, na kuwawezesha wafanyabiashara kuchochea maendeo yao na mataifa yao kwa ujumla" alisema Dkt. Kijaji
Jukwaa hilo limehudhuriwa na wafanyabiashara zaidi ya 700 kutoka Tanzania na Umoja wa Ulaya. Umoja wa Ulaya unaongoza kwa uwekezaji hapa nchini katika sekta mbalimbali ambapo imewekeza kiasi cha Euro milioni 344.23.
Jukwaa hilo pia limehudhuriwa na Mabalozi wa Tanzania katika nchi za Umoja wa Ulaya ambao ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestus Nyamanga, balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Dkt. Samwel Shelukindo, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi na Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Balozi Caroline Chipeta.
Sehemu ya washiriki wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) linalofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 23 – 24 Februari, 2023 Jijini Dar es Salaam |
Sehemu ya washiriki wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) linalofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 23 – 24 Februari, 2023 Jijini Dar es Salaam |
Viongozi mbalimbali wakifuatilia jukwaa la biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) (EU) linalofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 23 – 24 Februari, 2023 Jijini Dar es Salaam |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.