Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini |
Tanzania na Uganda zimekubaliana kuondoa vikwazo vya biashara ili kuendeleza na kuboresha ushirikiano kati ya mataifa hayo kwenye nyanja mbalimbali.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika mkutano wa majadiliano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga uliofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano wao, viongozi hao wamekubaliana kukamilisha michakato ya kuendeleza miundombinu ili kukamilisha barabara zinazounganisha Uganda na Tanzania, usafiri katika ziwa Victoria ambao pia utaunganisha reli ya kisasa ya SGR kwenda Uganda.
“Tumewekeana muda ili tuweze kukamilisha baadhi ya masuala kwa haraka lakini pia kuona jinsi gani pale panapo hitaji kila nchi itoe rasilimali iweze kujipanga na kuhakikisha rasilimali hizo zinapatikana kwa wakati,” alisema Dkt. Tax.
Katika mkutano huo viongozi hao wamekubaliana pia kukamilisha ujenzi wa kituo cha uokoaji Jijini Mwanza kitakachoshughulikia maafa yanayoweza kutokea katika ziwa Victoria.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga amesema mkutano huo umewawezesha kukamilisha baadhi ya mambo yaliyokuwa mezani na kujipa muda hadi mwishoni mwa mwezi Julai 2023 kukamilisha machache yaliyosalia.
Amesema wataendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili waweze kutatua vikwazo vilivyopo katika itifaki ya soko la pamoja la forodha.
“Tuendelee kushirikiana kufanya kazi kwa pamoja ili tuweze kutatua vikwazo katika itifaki ya soko la pamoja la forodha,” alisema Mhe. Kadaga
Sehemu ya Ujumbe wa Uganga ukiongozwa na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga |
Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Rebecca Kadaga amewasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere. Mhe. Kadaga anatarajia kuwa na mkutano wa majadiliano baina yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) tarehe 10 May, 2023, katika Ofisi Ndogo ya Wizara, Jijini Dar es Salaam.
Mara baada ya kuwasili nchini, Mhe. Kadaga alipokelewa na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz pamoja Balozi wa Uganda nchini, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye.
Pamoja na mambo mengine, mazungumzo ya viongozi hao yatahusu kuimarisha ushirikino kati ya Tanzania na Uganda, pamoja na ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na Ufaransa umeongezeka kutoka kiasi cha shilingi billioni 27.8 kwa mwaka 2015 hadi bilioni 94.5 kwa mwaka 2022.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amebainisha hayo alipofungua mkutano wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Ufaransa uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Mbali na kukua kwa biashara kati ya mataifa hayo mawili, pia kumekuwa na ongezeko la watalii kutoka Ufaransa ambapo kwa mwaka 2022 Tanzania ilipokea watalii 100,600 kutoka Ufaransa na kuwa nchi ya pili kuleta watalii nchini Tanzania.
“Biashara imeendelea kukua lakini pia katika uwekezaji tunashirikiana, katika utalii Ufaransa imekuwa nchi ya pili kwa kuleta watalii kwenye taifa letu, haya yanatokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Serikali imefanya kazi kubwa kuvutia wawekezaji na watalii hususan kupitia filamu ya ‘Royal Tour’ na ndiyo maana utalii umeongezeka,” alisema Dkt. Tax
Mhe. Dkt. Tax amesema madhumuni ya mkutano huu wa majadiliano ambao ni wa pili kati ya Tanzania na Ufaransa ni kuwawezesha Wafaransa kutambua fursa mbalimbali zinazopatikana nchini pamoja na Watanzania kuzijua fursa zinazopatikana nchini Ufaransa ili kuzitumia kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Tanzania na Ufaransa zimekuwa zikishirikiana katika sekta za elimu, nishati, utalii, usafirishaji, ulinzi na usalama (maritime security) …...Ufansa wamekuwa wadau wakubwa katika ujenzi wa bomba la mafuta linalojengwa kutoka Uganda hadi Tanzania mambo yote haya lazima tuendelee kuyadumisha lakini pia kufungua fursa nyingine zinazoweza kupatikana,” alisisitiza Dkt. Tax
Naye Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui amesema kufanyika kwa mkutano huo wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Ufaransa ni uthibitisho kuwa Tanzania na Ufaransa zimekuwa na ushirikiano mzuri na imara.
“Tumekuwa tukikutana mara kwa mara na kujadili masuala ya kikanda na kimataifa ili kuimarisha maendeleo ya miradi kati ya nchi zetu mbili katika sekta mbalimbali hususan mabadiliko ya tabianchi, uwekezaji, utalii, uchumi wa buluu, usalama wa baharini, na tumefanikiwa kujadili masuala yote vizuri kwa sababu uhusiano mzuri tulio nao. Itakumbukwa kuwa mwaka jana 2022 Marais wetu walipokutana na walikubaliana kushirikiana na kusonga mbele kwa maslahi ya pande zote mbili,” alisema Balozi Nabil.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Ulaya na Mambo ya Nje ya Ufaransa, Bw. Christophe Bigot amesema Ufaransa itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuimarisha sekta za biashara na uwekezaji, nishati, usalama wa baharini, uwekezaji, utalii, uchumi wa buluu, michezo na utamaduni.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na Makatibu Wakuu na Manaibu makatibu Wakuu kutoka Wizara mbalimbali wakiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA).
Mkutano wa kwanza wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Ufaransa ulifanyika mwezi Juni 2018 nchini Ufaransa.
Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui akichangia ajenda katika mkutano wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Serikali ya Tanzania na Ufaransa Jijini Dar es Salaam |
Mkutano wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Ufaransa ukiendelea Jijini Dar es Salaam |
Mkurugenzi
wa Forodha na Ushuru wa bidhaa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayesimamia
majimbo ya Haut Katanga, Lualaba, Tanganyika na Lomami, Bw. René Kalala
Masimango na ujumbe wake upo nchini kwa ziara ya kikazi ambapo tarehe 04 Mei
2023 ulikutana na Uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) jijini Dar Es
Salaam.
Tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini imekutana na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na kuwapa taarifa ya hatua iliyofikiwa na tume hiyo.
Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohammed Othman Chande, amesema tume imekutana na mabalozi hao kwa lengo la kuwapa taarifa ya hatua iliyofikiwa na tume hiyo wakiwa ni sehemu ya wadau.
"Taasisi za Kimataifa wakati mwingine zinafanya kazi na taasisi za haki jinai, tumeona tuwafahamishe kwa kuwa nao ni wadau. Pia tunawakaribisha watoe mapendekezo yao kwa sababu huu sio mwisho wa kupokea maoni," alisema Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Chande.
“Kwa sasa tunamalizia uchambuzi wa maoni yaliyokusanywa, kazi ambayo inatarajiwa kufanyika kwa mwezi mmoja na baadaye itatolewa rasimu ya mapendekezo,” alisema Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Chande na kuongeza kuwa rasimu ya mapendekezo itahusisha yanayopaswa kutekelezwa haraka, kwa muda wa kati na kwa muda mrefu.
Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Chande, alisema kuwa shauku ya wananchi ni kuwa na imani na taasisi za haki jinai nchini na kinachofanywa na tume hiyo kinalenga kufanikisha hilo.
"Shauku kubwa ya wananchi ni kuona mageuzi katika taasisi za haki jinai na tunatarajia mapendekezo yetu yafanikishe hilo," alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Chande.
Kwa kipindi cha miezi mitatu takriban wananchi 10,000 wamesikilizwa, mikutano 25 ya hadhara, imefanyika katika Wilaya 53 na Mikoa 25 na tume imefanikiwa kuwasikiliza wadau mbalimbali.
Akifungua mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab alisema tume hiyo iliundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuangalia njia bora ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini.
Alisema tume hiyo ina jukumu la kuangalia changamoto zinazokabili taasisi za haki jinai na kupendekeza uboreshaji wa mfumo wa haki jinai nchini.
Balozi Fatma Rajab alifafanua kuwa tume kama hiyo zimekuwa zikiundwa tangu uhuru wa Tanganyika na maboresho mbalimbali yamefanyika nchini ikiwa ni matokeo ya tume hizo.
"Tume hii tunatarajia ije na mapendekezo yatakayoboresha mfumo wa haki jinai kulingana na mahitaji ya sasa," alisema Balozi Fatma.
Pamoja na mambo mengine, Balozi Fatma ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mfumo wa haki jinai nchini unaboreshwa na kuwa imara zaidi.
Baadhi ya Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wakifuatilia mkutano baina yao na tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini Jijini Dar es Salaam |
|
Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa na bango la Wizara kwenye Sherehe ya Maadhimisho ya Mei Mosi iliyofanyika Kitaifa mjini Morogoro. |
Bw. Shaaban Maganga mfanyakazi wa Wizara akipokea cheti za ushiriki wa michezo ya Mei Mosi 2023 |
Sehemu ya wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa kwenye Sherehe ya Maadhimisho ya Mei Mosi iliyofanyika Kitaifa mjini Morogoro. |
Baadhi ya wageni waliohudhuria hafla ya maadhimisho
ya miaka 29 ya Uhuru wa Jamhuri ya
Afrika Kusini iliyofanyika jijini Dar es Salaam wakifuatilia hafla hiyo |
Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) ameshiriki hafla ya maadhimisho ya miaka 29 ya Uhuru wa Jamhuri ya Afrika Kusini iliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuwaita wawekezaji wengi zaidi waje kuwekeza nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Balozi Mbarouk amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Afrika Kusini kuendelea kuuenzi uhusiano wa kidugu na wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizo ambao uliasisiwa na viongozi waasisi wa mataifa hayo.
“Tanzania itaendelea kutumia fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Afrika Kusini na nitoe wito kwa wawekezaji wengi zaidi wa Afrika Kusini waje Tanzabia kuwekeza hasa ikizingatia kuna fursa katika maeneo ya kilimo, uzalishaji, mifugo, viwanda vya dawa, usafiri, utalii, madini na viwanda vya kusindika mazao ya chakula,”alisema.
Amesema wakati Taifa la Afrika Kusini likiadhimisha siku ya uhuru wake Tanzania itaendelea kushirikiana na Afrika Kusini ili kuhakikisha nchi zote zinanufaika na uwepo wa uhusiano huo.
Amesema ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Afrika Kusini umeoneshwa zaidi na ziara ya kitaifa aliyoifanya nchini Afrika Kusini Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kufanyika kwa mikutano ya pamoja kati ya nchi hizi.
Akizungumza katika hafla hiyo Balozi wa Afrika Kusini nchini Mhe. Noluthando Mayende- Malepe amesema Afrika Kusini inajali na kuthamini mchango mkubwa ambao Tanzania imetoa katika harakati za ukombozi wa nchi hiyo na kuifanya Tanzania kuwa nyumbani kwa wapigania uhuru wa Afrika Kusini.
“Tunaishukuru sana serikali na wananchi wa Tanzania kwa mambo yote ambayo Tanzania imeifanyia Afrika Kusini wakati wote hadi kufikia kupata uhuru wetu, kwakweli sisi tunawashukuru sana, niwahakikishie kuwa Afrika Kusini itaendelea kuuthamini mchango wenu katika uhuru wetu na tutaendelea kuuenz uhusiano wa kidugu na wa kihistoria uliopo kati ya nchi zetu mbili hizi, alisema.
Ameahidi kuwa Tanzania na Afrika Kusini zitaendelea kushirikiana katika mambo mengi ambayo nchi mbili hizi zimekuwa zikiyafanya.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na waheshimiwa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amemuaga Balozi wa Jamhuri ya Rwanda nchini Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba, baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini.
Akiongea wakati wa hafla ya kumuaga Balozi Karamba iliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, Dkt. Tax amempongeza Balozi Karamba kwa kumaliza muda wake wa uwakilishi salama na kumpongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kukuza na kudumisha uhusiano mzuri na wa kindugu baina ya Tanzania na Rwanda katika kipindi chake cha uwakilishi nchini.
Aidha, Mhe. Tax ameeleza kwamba, wakati wa Uwakilishi wake, Balozi Karamba amechangia Kwa kiasi kikubwa kukuza ushirikiano wa Tanzania na Rwanda katika maeneo mbalimbali ikiwemo, biashara na Uwekezaji, Nishati, uchukuzi na ujenzi, na yapo maeneo ambayo nchi hizi mbili zitaendelea kushirikiana kwa ukaribu na maeneo mengine Tanzania itaendelea kubadilishana uzoefu na Rwanda.
Naye, Mhe. Balozi Karamba ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumpa ushirikiano wa kutosha wakati wa kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini.
Mhe. Balozi ameelezea kufurahishwa na uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi hizi mbili na kupongeza hatua mbalimbali ambazo Tanzania imeendelea kuzichukua katika kuimarisha mahusiano hayo.