Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amepokea zawadi ya tende zilizotolewa na Serikali ya Saudi Arabia katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Tende hizo, tani 25 zimetolewa na Mfalme wa Saudi Arabia, Mtukufu Salman bin Abdulaziz Al Saud kupitia Kituo cha Hisani cha Mfalme wa Saudi Arabia na kuwasilishwa nchini na wajumbe maalum wa Taasisi hiyo ya Mfalme Bw. Alrazani Abdulaziz Abdulahman na Alqunur Fahad Abdulahman.
Akipokea zawadi hiyo Balozi Fatma amemshukuru Mtukufu Mfalme Salman kwa kuendelea kutambua urafiki na ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Saudia Arabia.
"Zawadi hii ya tende imetolewa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya Watanzania wote, hii inaonesha uhusiano uliopo kati ya nchi zetu kupitia ujumbe mahsusi uliowasili nchini kwa ajili ya kuwasilisha tende hizi” alisema Balozi Fatma.
Vilevile, Balozi Fatma ameeleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia unaendelezwa kwa vitendo ambapo Serikali ya Saudi Arabia imekuwa na ziara mbalimbali za wataalam nchini katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, afya ambapo wataalamu wa matibabu wamekuwa wakija kufanya huduma za pamoja za upasuaji nchini na katika sekta ya anga Saudi Arabia imeanzisha safari za ndege za moja kwa moja kuja nchini.
Naye Kaimu Balozi Bw. Fahad Alharbi alieleza kuwa Saudi Arabia inatambua umuhimu wa ushirikiano wake na Tanzania katika kukuza uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi na akaahidi kuwa Ofisi ya Ubalozi itaendelea kuhakikisha inadumisha uhusiano huo.
Alisema kuwa kituo cha hisani cha Mfalme Salman ambacho kimekuja na ujumbe wa Mfalme huyo kukabidhi salamu pamoja na tende, kimekuwa kikitoa misaada mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo usaidizi wa chakula, dawa na malazi kwa jamii zilizopatwa na majanga.
“Katika nyakati tofauti kituo hicho kimewezesha ziara za madaktari kutoka nchini Saudia Arabia ambao huweka kambi za huduma za matibabu ya upasuaji wa watoto wenye matatizo ya moyo” alisema Bw. Fahad.
Pia akaeleza kuwa huduma hiyo ya madakatari itaendelea kutolewa na kwamba hivi karibuni madaktari wengine wanatarajia kuja nchini kuendelea kutoa huduma ya matibabu katika hospitali mbalimbali.
Wakati huohuo Serikali ya Saudi Arabia imekabidhi msaada wa kifedha wenye thamani ya Dola 66, 532 ambazo ni zaidi ya Shilingi milioni 159 kwa lengo la kuimarisha huduma za TEHAMA katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Tanzania na Saudi Arabia zinashirikiana katika sekta za uvuvi, kilimo, mifugo, ujenzi wa miundombinu na masuala ya anga na utalii.
Tuesday, May 16, 2023
BALOZI FATMA RAJAB APOKEA ZAWADI YA TENDE KUTOKA SAUDI ARABIA
SERIKALI YA TANZANIA IMEJIPANGA KUENDELEA KUNUFAIKA NA FURSA ZA MTANGAMANO WA KIKANDA
Serikali ya Tanzania imejipanga kuendelea kunufaika na fursa zinazotokana na Mtangamano wa Kikanda ili kuwawezesha watanzania kufaidika na uanachama wa Tanzania katika Jumuiya mbalimbali za kikanda.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.
Stergomena Tax wakati wa ufunguzi wa semina kuhusu “Nafasi ya Tanzania katika
Mtangamano wa Kikanda” iliyotolewa na Wizara jijini Dodoma kwa Wajumbe
wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa lengo la kukuza uelewa
kuhusu masuala ya mtangamano wa kikanda.
Mhe. Dkt. Tax amesema kuwa, mtangamano wa kikanda ni dhana
muhimu katika kukuza uchumi, kuimarisha uhusiano wa kisiasa, amani na usalama
katika mataifa na kwamba Kamati hiyo ni
miongoni mwa wadau muhimu wanaotakiwa kuwa na uelewa mkubwa kuhusu mtangamano
wa kikanda ili kushirikiana na Wizara kueleza fursa na faida zake kwa wananchi.
Ameongeza kusema kwamba kwa Tanzania mtangamano wa kikanda ni
sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje hivyo uelewa wa pamoja kuhusu
dhana hii hususan fursa, faida na changamoto na namna ya kuzitatua unahitajika
ili kufikia malengo kusudiwa.
Vilevile ameeleza kuwa, Tanzania inao mchango mkubwa katika
Mtangamano wa kikanda na inategemewa ambapo pia imeendelea kunufaika na fursa
mbalimbali zinazotokana na uanachama wake katika Jumuiya za Kikanda hususan,
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
ikiwemo ajira, biashara, teknolojia, elimu na uwekezaji.
Mhe. Dkt. Tax pia alitumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa kila
Jumuiya kwa kusisitiza kuwa kila Jumuiya ina umuhimu na mchango mkubwa kwa
Tanzania kulingana na lengo la kuanzishwa kwake.
“Naomba niweke hoja hii sawa. Kumekuwa na ulinganifu wa
utendaji wa Jumuiya hizi ambapo baadhi ya watu wanaona jumuiya moja ni bora
kuliko nyingine pasipo kujua kwamba kila moja ina umuhimu wake kulingana na
lengo la kuanzishwa,” amesema Dkt. Tax.
Akitoa mfano amesema SADC ilianzishwa kwa lengo la kupigania
ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika. Hivyo kwa kiasi kikubwa Jumuiya hii imejikita kwenye masuala ya amani, ulinzi
na usalama na kwamba ni kutokana na lengo hilo nchi za kusini zilikombolewa
katika ukoloni lakini pia nchi wanachama kama Madagascar na Lesotho zilizokuwa
na migogoro zimerejea katika hali ya amani na utulivu.
Kuhusu EAC amesema lengo la kuanzishwa kwake lilikuwa ni
kuimarisha uchumi na biashara, hivyo kila jumuiya ni muhimu kulingana na
majukumu yake.
Pia amesema anaishukuru kamati hiyo kwa kuendelea
kushirikiana na Wizara kwenye masuala mbalimbali yenye maslahi kwa nchi na
kuahidi kuendelea kushirikiana nayo katika masuala mbalimbali yanayohusu
utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje.
Akiwasilisha mada hiyo, Mkufunzi kutoka Chuo cha
Diplomasia cha jijini Dar es Salaam, Bw. Charles Mtakwa amesema zipo faida
nyingi kwa Tanzania kuwa mwanachama katika EAC na SADC ikiwemo ajira, biashara,
elimu, teknolojia na uendelezaji miundombinu ya kikanda.
“Mtangamano wa Kikanda ni dhana muhimu kwa Tanzania na hususan
katika kukuza uchumi kupitia biashara, uwekezaji lakini pia kuboresha ufanisi
wa soko la bidhaa mbalimbali kwani ni muhimu kwa nchi za Afrika kuendelea
kukuza biashara miongoni mwake ambayo bado ipo katika kiwango cha chini cha
asilimia 13 ukilinganisha na nchi za Bara la Asia asilimia 61 na Amerika
asilimia 47” amesema Bw. Mtakwa.
Amesema kupitia Mtangangamano wa kikanda nchi wanachama
huweza kufanya maamuzi ya pamoja ya kisera na kuchochea mageuzi ikiwemo yale ya kiuchumi. Pia kupitia
mtangamano wa kikanda nchi wanachama hushirikiana kuchangia gharama za miradi
mikubwa na miundombinu kama miradi ya umeme na miradi ya barabara na reli.
Ameeleza kuwa, Mtangamano wa Kikanda ambao unalenga katika
kuziwezesha nchi wanachama kushirikiana katika masuala mbalimbali unazo hatua tano ambazo ni biashara huria;
muungano wa forodha;soko la pamoja;muungano wa kifedha na muungano wa kisiasa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya
Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa amesema kuwa anaipongeza na kuishukuru
Wizara kwa kuendelea kutoa semina kuhusu mada mbalimbali za umuhimu na kwamba
Kamati hiyo itaendelea kutoa ushirikiano na ushauri unaohitajika kwa Wizara.
Kwa upande wao, Wajumbe wa Kamati hiyo wameishauri Wizara kushirikiana na wadau mbalimbali kuendelea kutangaza fursa zinazopatikana katika mtangamano wa kikanda na kuendelea kusimamia makubaliano na mikataba iliyokwisha sainiwa katika kanda hizo ili itekelezwe kama ilivyopangwa.
Semina ikiendelea |
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama wakifuatilia semina kuhusu Mtangamano wa Kikanda |
Semina ikiendelea |
Washiriki wakifuatilia semina |
Mkutano ukiendelea |
Monday, May 15, 2023
MWILI WA MEMBE WAWASILI RONDO, LINDI
Helikopta ya Jeshi iliyobeba mwili wa aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Marehemu Bernard Membe ikiwasili kijijini kwake Rondo |
Mwili wa Marehemu Bernard Membe ukiwa umebebwa na wananchi ulipowasili kijijini kwake Rondo |
Wananchi wa Rondo na kutoka maeneo mbalimbali nchini wakiwa wamejipanga kupokea mwili wa Marehemu Bernard Membe ulipowasili nyumbani kwake kijiji cha Rondo, Lindi. |
Sehemu ya waombolezaji wakiwa katika hali ya huzuni na majonzi kwenye msiba wa Marehemu Bernard Membe kijijini kwake Rondo, Lindi |
Sunday, May 14, 2023
RAIS SAMIA ASHIRIKI KUUAGA MWILI WA BERNARD MEMBE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameungana na waombelezaji mbalimbali kuuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuanzia mwaka 2007 hadi 2015, Ndugu Bernard Kamilius Membe katika viwanja kwa Karimjee jijini Dar Es Salaam tarehe 14 Mei, 2023.
Akitoa salamu za rambirambi, Mhe. Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa kuondoka kwa Ndugu Membe kumeleta masikitiko kwake binafsi, familia yake, Serikali, wadau mbalimbali, familia ya marehemu, wana Lindi na wananchi kwa ujumla.
“Msiba huu umewagusa watu wengi ndani na nje ya nchi, kutokana na uhodari wake katika masuala ya siasa na diplomasia, hivyo nguzo kuu imeondoka Mwenyezi Mungu awape wanafamilia subira katika kipindi hiki cha majonzi”
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ambaye pia ni mwenyeji wa tukio hilo la kuaga mwili, katika salamu zake za pole alieleza kuwa Wizara imempoteza kiongozi mahiri na hodari ambaye alijenga misingi mizuri katika kusimamia utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje.
“Marehemu Membe pamoja na kusimamaia maslahi ya nchi alitumia umahiri wake kuwajenga watumishi wa Wizara ambao kwa sasa wengine wanahudumu katika nafasi za Balozi”.
Aidha, Ndugu Membe alikuwa mcheshi, mwenye upendo na hodari hivyo Wizara itaendelea kuyaenzi mafanikio yaliyofanywa naye wakati wa utumishi wake.
Tukio hilo la kuaga mwili wa Marehemu Bernard Membe lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ambao ni pamoja na: Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango; Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa; Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma; Naibu Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azan Zungu; Mawaziri, Manaibu Waziri, Wakuu wa Taasisi na Viongozi wengine wa Serikali, Taasisi binafsi na za dini na vyama vya siasa.
Wengine waliotoa salamu za rambirambi ni pamoja na: Mwakilishi wa kundi la wake wa Viongozi (Millenium group) Bi. Arafa Kikwete; Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Bw. Zitto Kabwe; Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Daniel Chongolo; Mkuu wa Mabalozi na Balozi wa Comoro nchini Tanzania, Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih; Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Amos Makala; Mtendaji Mkuu wa Mahakama (kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania), Prof. Elisante Ole Gabriel; na Naibu Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azan Zungu.
=============================================
Pichani, sehemu ya Waombolezaji walioshiriki kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,, Marehemu Bernard Membe. |
Gari lililobeba mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Marehemu Bernard Membe likiwasili katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. |
VIONGOZI MBALIMBALI WAMUAGA MHE. MEMBE KARIMJEE
Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki umeungana na waombolezaji wengine kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Mhe. Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa (Mb.) akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akisaini kitabu cha maombelezo wakati wa kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. |
Waombolezaji waliofika kwa ajili ya kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. |
Baadhi ya waombolezaji waliofika kwa ajili ya kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. |
Baadhi ya waombolezaji waliofika kwa ajili ya kumuaga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2007-2015) Ndugu Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. |
Saturday, May 13, 2023
SALAAM ZA RAMBIRAMBI
Friday, May 12, 2023
BALOZI SHELUKINDO AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA MABALOZI
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amekutana na kuzungumza na mabalozi wa China, Kenya, Denmark, Italia na Sudan kwa nyakati tofauti na kujadiliana nao masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na nchi zao.
Mabalozi waliokutana na Balozi Shelukindo ni Balozi wa China, Mhe. Chen Mingjian, Balozi wa Kenya, Mhe. Isaac Njenga, Balozi wa Denmark, Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet, Balozi wa Italia, Mhe. Marco Lombard na Kaimu Balozi wa Sudan, Mhe. Asim Mustafa Ali.
Dkt. Shelukindo amekutana na mabalozi hao katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili na kuahidi kuongeza ushirikiano katika sekta za elimu, michezo, biashara na uwekezaji.
“Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri na China, Kenya, Denmark, Italia na Sudan ambapo uhusiano huo umesaidia kuwa na misingi imara ya ushirikiano kwa maslahi mapana ya Taifa letu na nchi zao,” alisema Dkt. Shelukindo
“Vilevile nimepata fursa ya kukutana na balozi wa Sudan na amenijulisha juu ya uwezekano wa mapigano yanayoendelea nchini humo kufikia mwisho kwa njia ya makubaliano. Na amenihakikishia kuwa wanafunzi waliokuwa wanasoma nchini Sudan watapokelewa na kuendelea na masomo yao baada ya mapigano kumalizika.
Amesema tarehe 11 Mei, 2023 pande zinazopigana nchini humo zilisaini mkataba wa makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano,” alisema Dkt. Shelukindo
Kwa upande wake Kaimu Balozi wa Sudan nchini, Mhe. Mustafa Ali amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kumalizika kwa mapigano yanayoendelea nchini humo kwa njia ya makubaliano ya amani.
“Naomba nikuhakikishie kuwa Serikali ya Sudan itawapokea wanafunzi waliokuwa wanasoma nchini kwetu na kupata fursa ya kuendelea na masomo yao baada ya mapigano kumalizika,” alisema Mhe. Mustafa Ali
Naye Balozi wa China nchini, Mhe. ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono China na kuahidi kuendeleza harakati za kusaidia nchi zinazoendelea na kuongeza kuwa China itaendelea kuisadia Tanzania katika kufanikisha miradi mbalimbali ya kimkakati.
Kwa nyakati tofauti mabalozi hao wameishukuru Tanzania kwa ushirikiano mzuri ambao wamekuwa wakiupata wakati wa utekelezaji wa majukumu yao na kuahidi kuwa nchi zao zitaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali kwa maslahi ya pande zote.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akisalimiana na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Isaac Njenga |
TANZANIA, UINGEREZA KUIMARISHA BIASHARA NA UWEKEZAJI
Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wake na Serikali ya Uingereza katika sekta za biashara pamoja na uwekezaji.
Dhamira hiyo imeelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) aliposhiriki hafla maalum ya kutawazwa kwa Mfalme Charles III na Malkia Camilla iliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi wa Uingereza Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Mei, 2023.
Dkt. Tax alisema kuwa Tanzania na Uingereza zinafurahia uhusiano mzuri wa kihistoria na kirafiki uliodumu kwa muda mrefu na kuongeza kuwa kupitia uhusiano huo, Tanzania na Uingereza zimekuwa zikifanya kazi kwa ukaribu katika sekta mbalimbali hususan biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote.
“Uingereza ni miongoni mwa washirika wa kibiashara wa Tanzania wa siku nyingi na imesalia kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuwa na uwekezaji mkubwa wa Kigeni hapa nchini katika sekta mbalimbali. Tanzania inaahidi kuendelea kushirikiana na utawala wa Mtukufu Mfalme Charles III katika nyanja mbalimbali,” alisema Waziri Tax
Alisema Uingereza imeendelea kuwa mwekezaji mkuu wa pili nchini Tanzania, ikiwa na jumla ya miradi 956 yenye thamani ya pauni bilioni 4.6 na kuajiri zaidi ya watu 275,000 na hivyo kutoa mchango mkubwa katika maendeleo yetu ya kijamii na kiuchumi.
“ Uingereza imeendelea kuwa mwekezaji mkuu wa pili nchini Tanzania, ikiwa na jumla ya miradi 956 yenye thamani ya pauni bilioni 4.6 na kuajiri zaidi ya watu 275,000 na hivyo kutoa mchango mkubwa katika maendeleo yetu ya kijamii na kiuchumi, Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Uingereza kwa manufaa mapana ya nchi na watu wake,” aliongeza Dkt. Tax.
Dkt. Tax alitumia fursa hiyo kuwahakikishia Waingereza na wageni mbalimbali walioshiriki hafla hiyo kuwa, Tanzania ina mazingira salama ya uwekezaji na biashara kwa kuzingatia juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwemo kuweka sera imara na zinazotabirika pamoja na sheria na taratibu rafiki, kuboresha huduma za kijamii, kuimarisha demokrasia, usawa wa kijinsia na utawala wa sheria, kuendeleza miradi mikubwa ikiwemo ya nishati na miundombinu, uchukuzi na usafirishaji.
Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concar alisema Uingereza na Tanzania zimeendelea kuwa na urafiki imara kwa muda mrefu kutokana na heshima, dhamira ya kukuza maendeleo na kuthaminiana kwa wananchi wa pande zote mbili.
“Uingereza imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika sekta ya biashara na uwekezaji ambapo wafanyabiashara wengi kutoka Uingereza wamewekeza nchini Tanzania, tutaendelea kuwaeleza kuwa Tanzania ni salama kwa uwekezaji na biashara ili wawekeze kwa wingi” alisema Balozi Concar.
Balozi Concar aliongeza kuwa Ushirikiano wa Uingereza na Tanzania umekuwa ukistawishwa na juhudi za maendeleo katika sekta mbalimbali hususan za fedha zikiwemo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
“Uingereza na Tanzania hivi karibuni zitasaini mkataba wa ushirikiano katika sekta ya afya hususan Utafiti wa matibabu lengo likiwa ni kuimarisha sekta ya afya. Uingereza na Tanzania zimekuwa na ushirikiano wa maendeleo kwa lengo la kuendeleza malengo ya pamoja kwa maslahi ya pande zote mbili,” aliongeza Balozi Concar.
Sehemu ya wageni walioshiriki katika hafla maalum ya kutawazwa kwa Mfalme Charles III na Malkia Camilla iliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi wa Uingereza Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Mei, 2023 |
Sehemu ya wageni walioshiriki katika hafla maalum ya kutawazwa kwa Mfalme Charles III na Malkia Camilla iliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi wa Uingereza Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Mei, 2023 |