Monday, May 22, 2023

SERIKALI YAZINDUA RASMI MFUMO WA KIDIGITALI KUSAJILI DIASPORA WENYE ASILI YA TANZANIA

 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Mashariki, Mhe. Dkt Stergomena Tax (Mb.) akihutubia katika hafla ya uzinduzi rasmi wa mfumo wa kuwasajili Diaspora wenye asili ya Tanzania Kidigitali (Diaspora Digital Hub) Jijini Dar es Salaam  
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Mashariki, Mhe. Dkt Stergomena Tax akizinduzi rasmi mfumo wa kuwasajili Diaspora wenye asili ya Tanzania Kidigitali (Diaspora Digital Hub) Jijini Dar es Salaam. Wengine pichani ni Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Bw. Abdulmajid Nsekela (kulia), Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini Dkt.Anna Makakala (kushoto) na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge – Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa (Mb).  
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akiwasilisha salamu za Wizara kwa Diaspora kabla ya uzinduzi rasmi wa DDH
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Bw. Abdulmajid Nsekela akielezea faida za mfgumo wa kuwasajili Diaspora wenye asili ya Tanzania Kidigitali (Diaspora Digital Hub)
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba akieleza faida za Wanadiaspora kuchangia katika mifuko ya hifadhi ya jamii
Mwakilishi wa Mkuregenzi Mkuu wa Benki ya NMB, Bw. Philbert Mponzi akiwaeleza washiriki fursa ambazo Diaspora watazipata kupitia Benki ya NMB watakapo jiunga na mfumo wa DDH 















KUKUA KWA KISWAHILI DUNIANI NI FURSA KWA TANZANIA

Wizara imelieleza Bunge kuwa imekuwa ikizitumia Ofisi za Balozi zilizoenea duniani kukuza Kiswahili na kuchangia ongezeko la fursa za ajira kwa Watanzania.

Kauli hiyo imetolewa Bungeni leo tarehe 22 Aprili 2023 wakati wa kujibu swali la Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Mhe.  Ameir Abdallah Ameir aliyetaka kujua namna Balozi zinavyotumia fursa ya kukua kwa Kiswahili duniani kutafuta ajira kwa Watanzania.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Geofrey Pinda kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alisema kuwa Ofisi za Balozi zimeanzisha programu za kufundisha, kutafsiri na kufanya ukalimani wa Kiswahili duniani, hatua ambayo inatoa ajira kwa watanzania. Jumla ya balozi 13 zimeanzisha madarasa, vituo na club za Kiswahili. Kupitia programu hizo, zaidi ya watanzania 95 wamepata ajira katika maeneo hayo.

Vilevile, vyuo na vituo binafsi zaidi ya 150 vinafundisha Kiswahili duniani. Kwa sasa, Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) limepewa kazi ya kufundisha walimu kumi (10) wa Diaspora katika Ubalozi wetu wa Abu Dhabi ambao ulihitaji walimu wa kwenda kufundisha Kiswahili katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mhe. Naibu Waziri aliendelea kueleza kuwa Ofisi za Balozi zipo katika mazungumzo na vyuo vikuu kwenye maeneo yao ya uwakilishi ili Lugha ya Kiswahili iweze kujumuishwa katika mitaala ya vyuo hivyo ikiwa ni pamoja na kupata wahadhiri wa Kiswahili kutoka Tanzania.  Vyuo hivyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Kuwait, Chuo Kikuu cha Holon Institute of Technology nchini Israel na Chuo Kikuu cha Buraimi nchini Oman.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Geofrey Pinda akijibu Swali Bungeni kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhusu Lugha ya Kiswahili inavyotoa fursa za ajira kwa Watanzania.



 

Saturday, May 20, 2023

ZAMANA: KUTOKA IRENTE HADI KASRI LA BUCKINGHAM


Bi. Zamana (kulia) na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro wakiwa na tuzo iliyotolewa na Mfalme Charles III
Bi. Zamana (wa kwanza kushoto) katika picha ya pamoja na Mfalme Charles III (wa kwanza kulia) wakati wa hafla ya kuwapongeza waliopata tuzo iliyoandaliwa na Mfalme huyo

Bi. Zamana (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro (wa pili kushoto) na maafisa wengine wa Ubalozi huo



Friday, May 19, 2023

DKT SAMIA AZINDUA MAANDALIZI YA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI AFRIKA KUHUSU RASILIMALI WATU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali watu (Africa Heads of State Human Capital Summit) utakaofanyika nchini tarehe 25 - 26 Julai, 2023. 

Mhe. Dkt. Samia ametoa wito kwa viongozi wa Afrika kuendelea kuchukua hatua kwa kuwekeza kwa watu na kutoa kipaumbele kwa vijana na wanawake.

Mhe. Rais pia amewataka viongozi wa Afrika kuchukua hatua zaidi ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili watu wengi kwa kuwekeza zaidi katika kuboresha afya za watu, maji safi na salama, elimu bora na ujuzi muhimu kwa maendeleo ya rasilimali watu.

“Viongozi wa Afrika lazima tuendelee kuchukua hatua kwa kuwekeza kwa watu na kutoa kipaumbele kwa vijana na wanawake. Nitoe wito kwa viongozi wa Afrika kuchukua hatua zaidi ili kukabiliana na changamoto zinazokabili rasilimali watu kwa kuwekeza zaidi katika kuboresha afya za watu, kuwaletea maji safi na salama, kutoa elimu bora na ujuzi muhimu kwa maendeleo ya rasilimali watu,” alisema Mhe. Samia 

Rais Samia amesema taarifa za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa nchi nyingi za Afrika ukitoa za Afrika Kaskazini zinakabiliwa na changamoto katika utekelezaji wa malengo ya milenia ya uendelezaji rasilimali watu hali ikiwa chini ya wastani hasa katika maeneo ya elimu, afya na ulinzi wa jamii. 

“Hali ya afya ya uzazi, uwepo wa maji safi na salama na usimamizi wa maji taka bado ni changamoto kwa nchi nyingi huku ujumuishi wa kijinsia ukiwa na kasi ndogo na utekelezaji wa sheria za kulinda wanawake na watoto wa kike dhidi ya ubaguzi, unyanyasaji wa kijinsia, ndoa za utotoni na ukeketaji ukiwa mdogo na kuongeza kuwa kuwa hali ya ukamilishaji wa malengo ya milenia namba , 4, 5, 6 na 8 kwa nchi za Afrika hairidhishi na inaonesha hatari ya kutokamilika kwa malengo hayo kufikia mwaka 2030,” alisema Dkt. Samia.

Akizungumza katika uzinduzi wa Mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax (Mb.) alisema kuwa kufanyika kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Rasilimali Watu mwezi Julai 2023, kunatokana na jitihada za Serikali kuboresha ushirikiano na kuzingatia umuhimu wa rasilimali watu katika kukuza uchumi na umuhimu wa kuwekeza kwa watu.

 “Kufanyika kwa mkutano huo hapa nchini, kunatokana na jitihada za serikali katika kuboresha ushirikiano na kuzingatia umuhimu wa rasilimali watu katika kukuza uchumi wa na kuona umuhimu wa kuwekeza kwa watu,” 

Alisema kufanyika kwa mkutano huo kutatoa fursa kwa wakuu wa nchi kubadilishana ujuzi na uzoefu kuhusu rasilimali watu na kutoka na maazimio madhubuti kuhusu cha kufanya kuendeleza rasilimali watu.

Dkt. Tax aliongeza kuwa Azma ya agenda 2063 inalenga kuzibadilisha nchi za Afrika na kuwa na nguvu za kiuchumi lakini azma hiyo inahitaji uwekezaji wa makusudi katika ujuzi na uwezo ili kutumia fursa za kijamii na kiuchumi katika bara la Afrika.

Naye Waziri wa Fedha na Mipango  Dk. Mwigulu Nchemba (Mb.) alisema Tanzania imekuwa mwenyeji wa mkutano huo kutokana na vipaumbele vya Rais Dkt. Samia alivyoweka katika maeneo ya afya na  makundi mbalimbali ya vijana na wanawake.

Alisema mbali ya Rais kufanya mabadiliko mbali mbali yaliyofanyika nchini lakini pia tumeshuhudia uwekezaji mkubwa wa fedha ukielekezwa katika eneo la elimu ili watoto wengi zaidi wanufaike kwa kupata elimu.

Awali Mkurugenzi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, Bw. Nathan Belete alisema Bara la Afrika lina nguvu kazi kubwa ambapo zaidi ya asilimia 75 ya watu wake wanafanya kazi katika sekta rasmi na kwamba nchi za Afrika zinapaswa kuungana na kufanya kazi kwa pamoja ili kumaliza changamoto zinazokabili rasilimali watu.

“Bara la Afrika lina nguvu kazi kubwa, tunaona kuwa asilimia 75 ya watu katika bara hili wanafanya kazi katika sekta rasmi, hivyo Nchi  zinapaswa kuungana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuzimaliza changamoto zinazokabili rasilimali watu kwa urahisi katika ukanda huo,” alisema. 

Alisema nchi za Afrika lazima zifanyie kazi suala la unyanyasaji wa kijinsia kwa kuwekeza katika elimu, afya na kuwawezesha wananchi wake kupata maarifa, ujuzi na afya bora.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia Viongozi, Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kabla ya kuzindua Mkutano wa Maandalizi kwa ajili ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali watu (Africa Heads of State Human Capital Summit), Jijini Dar es Salaam. Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu unatarajiwa kufanyika tarehe 25-26 Julai, 2023 Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza wakati wa Mkutano wa Maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali watu (Africa Heads of State Human Capital Summit), Jijini Dar es Salaam

Sehemu ya Viongozi, Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wakifuatilia Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa Mkutano wa Maandalizi kwa ajili ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali watu (Africa Heads of State Human Capital Summit), Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Balozi wa Canada nchini, Mhe. Kyle Nunas kabla ya uzinduzzi wa Mkutano wa Maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali watu (Africa Heads of State Human Capital Summit), Jijini Dar es Salaam


VACANCY ANNOUNCEMENT


 

Thursday, May 18, 2023

MAMBO YA NJE YAAINISHA FURSA ZINAZOPATIKANA KATIKA MIKUTANO YA KIMATAIFA

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akijibu swali bungeni jijini Dodoma lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Neema Kichiki Lugangira tarehe 18 Mei 2023. 
=================================


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amefafanua fursa mbalimbali zinazopatikana nchini kupitia ushiriki wa Tanzania katika mikutano ya kimataifa.

Ufafanuzi huo umetolewa Bungeni jijini Dodoma leo tarehe 18 Mei 2023 wakati Mhe. Balozi Mbarouk akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Neema Kichiki Lugangira aliyetaka kujua ni kwa kiasi gani ushiriki wa Tanzania katika Mikutano ya Kimataifa unazingatia upatikanaji wa fursa za kiuchumi na utekelezaji wake.

Mhe. Balozi Mabarouk amesema kuwa, ushiriki wa Tanzania katika Mikutano ya Kimataifa unalenga kupata na kutumia fursa za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kupata mitaji, uwekezaji, masoko ya bidhaa na huduma, kukuza utalii, miradi ya kisekta, mikopo ya masharti nafuu na misaada, kujengewa uwezo wa kitaalamu, na upatikanaji wa teknolojia.

Mafanikio mengine ni pamoja na kupata masoko ya bidhaa mbalimbali kama vile mbogamboga, matunda, korosho, nafaka, nguo na mavazi, utalii, malumalu, na bidhaa za kioo. Vilevile, nchi yetu inanufaika kwa kupata wawekezaji katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utalii, viwanda, kilimo, uvuvi, mifugo, madini, na nishati jadidifu. 

Wednesday, May 17, 2023

MAJALIWA, DKT. KIKWETE WAONGOZA WAOMBOLEZAJI MAZISHI YA MEMBE


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete wameongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi ya aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe yaliyofanyika kijijini kweke Rondo, mkoani Lindi yaliyofanyika jana Jumanne tarehe 16 Mei 2023.

Akitoa salamu za Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Mhe. Majaliwa amesema kifo cha Bernard Membe kimewacha Watanzania na wana Lindi na simanzi, majonzi na huzuni isiyo na kifani.

"Kipekee Mhe. Rais Samia anawashukuru wananchi wote wa Lindi kwa utulivu mliouonesha wakati huu wa msiba wa Mzee Membe wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwa kuhakikisha shughuli ya mazishi inaenda vizuri kama ilivyokusudiwa, tunawashukuru na Mwenyezi Mungu aendelee kuwajaalia faraja na uvumilivu katika kipindi hiki cha majonzi mnachopitia," alisema Mhe. Waziri Mkuu.

Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango naye ameungana na Rais Samia kutoa pole kwa wana Lindi na wana Mtama na amewasihi kuendelea kuyaenzi mazuri yote aliyofanya enzi za uhai wake.

Marehemu Membe atakumbukwa kwa mengi hususani utumishi wake uliotukuka na hasa katika taasisi za Kimataifa alizohudumu wakati wa uhai wake ambapo pia ametumikia Watanzania katika nafasi mbalimbali na kuleta maendeleo. 

“Mchango wa marehemu Membe ni mkubwa hasa katika Jimbo la Mtama," alisema Mhe. Majaliwa.

Mhe. Waziri Mkuu aliongeza kuwa CCM imeelezea kazi nzuri aliyoifanya kwa nafasi mbalimbali alizoshika wakati wa utumishi wake, umahiri na weledi, alikuwa pia na siasa za kistaarabu hakika Chama kimempoteza kiongozi makini na hodari na utumishi uliotikuka, hakika alikuwa kiongozi wa kuigwa.

Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete alisema alifahamiana na Marehemu Membe muda mrefu na tangu wakati huo wamekuwa wakisaidiana mambo mengi katika kazi na nje ya kazi.

"Alikuwa msaada mkubwa kwangu wakati wote wa utumishi. Alifanya mambo makubwa na alileta medali za kimataifa kutokana na uchapa kazi wake wa kujitoa kwa moyo wake wote," alisema Dkt. Kikwete.

Mhe. Dkt. Kikwete aliongeza kuwa Marehemu alikuwa mwanadiplomasia mahiri na aliyekuwa na mikakati mizuri iliyokuwa na mafanikio makubwa kwa taifa.......na alikuwa msomi mzuri lakini pia alikuwa mcha Mungu," alisisitiza Dkt. Kikwete.

Dkt. Kikwete aliongeza kuwa Marehemu Membe aliweka maslahi ya Tanzania mbele na hakutaka mchezo na maslahi ya taifa lake, alikuwa jasiri, hakika taifa limepoteza moja kati ya watu muhimu.

Akitoa salamu za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) alisema Marehemu Membe alitoa mchango mkubwa katika Wizara ya Mambo ya Nje na mchango huo utakumbukwa daima.

"Marehemu alikuwa mchapa kazi, mpenda watumishi wake, kiongozi mahiri na mwanadiplomasia nguli....na Kipindi cha uongozi wake, Serikali ilipata medali nyingi za Kimataifa kutokana na uchapa kazi wake," alisema Balozi Mbarouk.

Balozi Mbarouk aliongeza kuwa Marehemu Membe alikuwa ni Mwalimu na mfano bora wa kuigwa, hivyo kwa niaba ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki waliopo nchini na Nje ya nchi, Wizara inatoa pole kwa familia, Mungu awajalie uvumilivu wakati huu mgumu wa msiba.

Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa (NEC), CCM Taifa, ndgu Sophia Mjema alisema Marehemu Membe aliyeshika nafasi mbalimbali kwenye Chama za Ubunge, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Mjumbe wa Sektrtariet ya Halmashauri Kuu ya Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa Ali fanya kazi y’a kukitetea Chama chake na daima watamkumbuka kwa hilo. 

"Membe alifanya kazi ya kutetea Chama chake CCM, alikuwa kiongozi makini na hodari, alikuwa mwana CCM kweli kweli, CCM itamkumbuka ndgu Membe kwa uanachama wake na uongozi wake mahiri...aliweza kukitetea Chama chake na kuiunganisha CCM na vyama rafiki katika Dunia," alisema ndugu. Mjema

Ndgu Mjema alisema kuwa CCM itaendelea kumkumbuka kwa kazi nzuri aliyoifanya.

Ibada ya mazishi ya Marehemu Membe ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainabu Telack, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Mstaafu Ahmed Abbas; Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Batilda Buriani; Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka.

Wengine ni Waziri wa TAMISEMI Mhe. Angela Kairuki, Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwan Kikwete, Mhe. William Lukuvi, Mbunge Isimani; Wakuu wa Wilaya mbalimbali na wakuu wa taasisi za Serikali na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb.) akiwasili nyumbani kwa Marehemu Bernard Membe kijiji cha Rondo, Lindi ambapo aliongoza mamia ya waombolezaji kwenye  mazishi ya Mwanadiplomasia huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete akiwasili nyumbani kwa Marehemu Bernard Membe kijiji cha Rondo, Lindi ambapo aliongoza mamia ya waombolezaji kwenye  mazishi ya Mwanadiplomasia huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akitoa salamu za pole kwa familia na waombolezaji muda mfupi baada  ya Ibada ya kumwombea Marehemu Bernard Membe iliyofanyika nyumbani kwake Rondo, Lindi
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete na Mke wake Mhe. Salma Kikwete (Mb) wakiweka shada la maua kwenye kaburi la Marehemu Bernard Membe
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akiweka udongo kwenye kaburi la Marehemu Bernard Membe
Mwili wa Marehemu Bernard Membe ukiwa katika eneo la ibada maalumu ya kumwombea muda mfupi kabla ya kupunzishwa kwenye nyumba yake ya milele. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akisalimiana  na baadhi ya waombolezaji alipowasili nyumbani kwa Marehemu Bernard Membe Rondo, Lindi kwenye  mazishi ya Mwanadiplomasia huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Mwili wa Marehemu Bernard Membe ukiwa kwenye ibada maalumu ya kumwombea muda mfupi kabla ya kupunzishwa kwenye nyumba yake ya milele. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (wa kwanza kushoto) akishiriki Ibada ya kumwombea Marehemu Bernard Membe


Ibada maalumu ya kumwombea Marehemu Bernard Membe ikiendelea nyumbani kwake kijiji cha Rondo, Lindi
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb.) akitoa salamu za pole kwa familia na waombolezaji muda mfupi baada  ya Ibada ya kumwombea Marehemu Bernard Membe iliyofanyika nyumbani kwake Rondo, Lindi
Naibu Waziri Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi James Bwana wakiweka shada la maua kwenye kaburi la Marehemu Bernard Membe
Sehemu ya waombolezaji walioshiriki kwenye mazishi ya Marehemu Bernard Membe
Sehemu ya Viongozi wakiweka mataji ya maua kwenye kaburi la Marehemu Bernard Membe
Waziri wa TAMISEMI Mhe. Anjela Kairuki (Kulia) na Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Mbelwa Kairuki (katika) wakiwasili nyumbani kwa Marehemu Bernard Membe Kijiji cha Rondo, Lindi kushiriki kwenye  mazishi ya Mwanadiplomasia huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa

Tuesday, May 16, 2023

MCHANGO WA TANZANIA KATIKA MEDANI ZA KIKANDA NA KIMATAIFA UTUNZWE: DKT TAX


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ametoa wito kwa Taasisi mbalimbali nchini kuendelea kutunza kumbukumbu za historia ya Tanzania na mchango wake katika medani za kikanda na kimataifa ili kuvirithisha vizazi vya sasa na vijavyo.


Kauli hiyo ameitoa jijini Dodoma tarehe 16 Mei 2023 wakati wa hafla fupi ya kikabidhi Machapisho ya Hashim Mbita kwa Taasisi 18 zikiwemo za elimu.


Mhe. Dkt. Tax amesema kuwa, Tanzania ina historia kubwa na nzuri katika medani za kikanda na kimataifa ikiwemo mchango wake katika harakati za ukombozi kusini mwa Afrika hivyo ni jukumu la wadau mbalimbali kuunganisha nguvu ya kutunza kumbukumbu ya historia hiyo nzuri na kuvirithisha vizazi vya sasa na vijavyo.


Ameeleza kuwa, Wizara imeamua kuyakabidhi machapisho hayo kwa Taasisi hizo ili yasaidie kurithisha historia iliyomo kwa vizazi vijavyo, na kujenga hamasa ya uzalendo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


“Wizara inawakabidhi nyinyi machapisho haya kama wawakilishi wa wengi. Tunaamini kupitia Vyuo na Taasisi zenu machapisho haya yatawafikia na kusomwa na Watanzania wengi. Vilevile kupitia machapisho haya historia kuhusu mchango uliotolewa na Tanzania katika harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika na Afrika kwa ujumla itatunzwa na kukumbukwa daima” amesisitiza Mhe. Dkt. Tax.


Pia ameziomba taasisi hizo kuwa chachu katika kueneza historia adhimu iliyomo kwenye chapisho hilo kwa kuhakikisha linasomwa. “Pamoja na kulitumia chapisho hili kama rejea, na kuhamasisha lisomwe, niwaombe wadau mbalimbali nchini kuona uwezekano wa kuandaa simulizi au filamu ya chapisho ili kuweza kuwafikia watu wengi hususan vijana” alisisitiza Mhe. Dkt. Tax.


Aidha, amefafanua kuwa, Chapisho hilo ambalo pamoja na mambo mengine linaeleza harakati za ukombozi katika nchi za Angola, Namibia, Afrika ya Kusini, Zimbabwe na Msumbiji na mchango wan chi za Tanzania, Zambia, Botswana, Lesotho, Malawi na Swaziland, lilipewa jina la Hashim Mbita kutoka na mchango thabiti na uongozi mahiri wa Hayati Brigedia Generali Hashim Mbita  alioutoa akiwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Kupigania Uhuru Afrika kuanzia mwaka 1972 hadi 1994.


Mhe. Dkt. Tax pia ameshukuru na kupongeza  mchango uliotolewa na Viongozi mbalimbali wa Tanzania akiwemo  Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kamabarage Nyerere kwenye harakati za ukombozi kusini mwa Afrika kwani fikra na mtazamo wake kuhusu umuhimu wa uhuru kwa nchi za Afrika zilifanikisha nchi zote za Afrika kujikomboa dhidi ya ukoloni.


Pia Mhe. Dkt. Tax alitumia fursa hiyo kuipongeza Kampuni ya Kitanzania ya Uchapishaji ya Mkuki na Nyota kwa kuchapisha chapisho hilo kwa umahiri.


“Nawashukuru wadau wote waliofanikisha uchapishaji wa Chapisho la Hashim Mbita ikiwemo Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa  kuandaa Chapisho hilo lenye Volume 9 na kwa kutambua mchango wa Tanzania katika harakati za Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika. Pia kipekee  namshukuru Rais Mstaafu wa wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa kwa kuniagiza nikiwa Katibu Mtendaji wa SADC na kunisisitiza kuhakikisha chapisho hili linakamilika baada mchakato wa awali kusimama ambapo mwaka 2014 kufuatia maagizo hayo, mchakato ulitekelezwa katika  awamu tatu na kukamilika mwaka 2020” alifafanua Dkt. Tax.


Awali akimkaribisha Mhe. Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amesema kwamba, Wizara imepokea makasha 28 ya Chapisho la Hashim Mbita lenye Volume 9.


Pia aliongeza kusema Sektretarieti ya SADC inaendelea na mchakato wa kutafsiri Chapisho la Hashim Mbita kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha watanzania wengi zaidi kulisoma na kuijua historia ya nchi yao hususan mchango wa Tanznaia katika Harakati za Ukombozi Kusini mwa Afrika.


Hafa hiyo ilihudhuriwa na viongozi na wawakilishi kutoka Taasisi mbalimbali zikiwemo Ofisi ya Rais, Bunge, Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Maktaba ya Taifa, Chuo Kikuu cha Dodoma na Taasisi ya Mwalimu Nyerere. 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi Machapisho Hashim Mbita kwa Taasisi mbalimbali za hapa nchini. Hafla hiyo ambayo ilizishirikisha Taasisi 18 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ilifanyika jijini Dodoma tarehe 16 Mei 2023

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi machapisho ya Hashim Mbita kwa Taasisi mbalimbali nchini. Katikati ni Mhe. Dkt. Tax na kulia ni Mhe. Vincent Mbogo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Sehemu ya wageni waalikwa walioshiriki hafla hiyo wakiwemo Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama

Sehemu nyingine ya washiriki

Wawakilishi wa Taasisi zilizoshiriki hafla ya kukabidhi machapisho ya Hashim Mbita wakifuatailia tukio. kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi machapisho ya Hashim Mbita kwa Taasisi mbalimbali.


Mhe. Dkt. Tax akimkabidhi Bw. Mbwana Msingwa kutoka Ofisi ya Rais Kasha lenye Volume 9 za Machapisho ya Hashim Mbita

Mhe. Dkt. Tax akiwakabidha Kasha lenye Volume 9 za Machapisho ya Hashim Mbita Wawakilishi kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwemo Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mabo ya Nje, Ulinzi na Usalama wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Mbogo (kulia)

Makabidhiano yakiendelea kwa wawakilishi wa taasisi mbalimbali ikiwemo Maktaba ya Taifa.

Makabidhiano ya Machapisho ya Hashim Mbita yakiendelea

Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) naye akikabidhiwa amachapisho ya Hashim Mbita