Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujadili hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umefanyika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 29 Mei 2023.
Akifungua Mkutano huo, Waziri wa Ulinzi wa Burundi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Alain Tribert Mutabaze, amesema jitihada za pamoja ikiwemo mikakati mipya ya namna ya kukabiliana na vikundi vya waasi katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo bado zinahitajika ili kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana katika eneo hilo.
Amesema pamoja na kupongeza jitihada nyingi zinazofanywa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo kupeleka Kikosi cha Kulinda amani cha Jumuiya (EACRF), bado ipo haja ya kufanya tathmini ya mara kwa mara ya mikakati iliyopo kama inaleta tija na kuandaa mikakati mipya ikiwa ni pamoja na kuviwezesha Vikosi hivyo ili viweze kutekeleza kikamilifu jukumu la kulinda amani katika eneo hilo.
“Changamoto katika eneo la Mashariki mwa Congo bado zipo. Tunatakiwa kuboresha mikakati yetu na kufanya tathmini za mara kwa mara ya maendeleo ya jitihada hizi, kwani hali inayoendelea Mashariki mwa Congo inatuathiri sote kama jumuiya kwa namna moja au nyingine. Hivyo niwaombe Waheshimiwa Mawaziri tuje na mapendekezo yenye tija tutakayoyawasilisha kwa Wakuu wetu wa Nchi kwa mustakabali wa eneo hilo la Mashariki mwa Congo na sisi sote” amesema Mhe. Mutabaze.
Mhe. Mutabaze pia alitumia fursa hiyo kuwakaribisha Mawaziri hao nchini Burundi na kuwaomba kutumia muda wao kujadili na kuandaa mapendekezo yatakayoleta suluhu ya kudumu nchini DRC hususan eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki amesema Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kufanya kazi bega kwa bega na Nchi Wanachama ili kuhakikisha amani na utulivu wa kudumu unapatikana katika eneo la Mashariki mwa Congo.
Mkutano huo umewahusisha Mawaziri wa Ulinzi kutoka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Makatibu Wakuu na Wakuu wa Majeshi.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb.) na kumshirikisha pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Jilly Maleko, Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi pamoja na Maafisa wengine waandamizi kutoka Serikalini.
Ujumbe wa Burundi katika Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo |
Ujumbe wa Sudan Kusini ukishiriki Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo |
Ujumbe wa Kenya ukishiriki Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo |
ehemu ya ujumbe wa Tanzania wakishiriki Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo |