Saturday, October 21, 2023

RAIS SAMIA KUWA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA MIKA 59 YA UHURU WA ZAMBIA

 

            

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akizungumza na Waandishi wa Habari (hawako pichani) kuhusu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan  kuwa mgeni Rasmi katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 59 ya Uhuru wa Jamhuri ya Zambia zinazotarajiwa kufanyika tarehe 24 Oktoba 2023

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akizungumza na Waandishi wa Habari (hawako pichani) kuhusu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan  kuwa mgeni Rasmi katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 59 ya Uhuru wa Jamhuri ya Zambia zinazotarajiwa kufanyika tarehe 24 Oktoba 2023

kikao na waandishi kikiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akifafanua kitu alipozungumza na Waandishi wa Habari (hawako pichani) kuhusu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan  kuwa mgeni Rasmi katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 59 ya Uhuru wa Jamhuri ya Zambia zinazotarajiwa kufanyika tarehe 24 Oktoba 2023

 

 










 

 

 

 

 

 


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

RAIS SAMIA KUWA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA MIAKA 59 YA UHURU WA ZAMBIA

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni Rasmi katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 59 ya Uhuru wa Jamhuri ya Zambia zinazotarajiwa kufanyika tarehe 24 Oktoba 2023 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya bara la Afrika.

 

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amesema kuwa Mheshimiwa Rais Samia amealikwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mheshimiwa Hakainde Hichilema.

 

Mheshimiwa Dkt. Samia pia amealikwa kufanya Ziara ya Kitaifa nchini Zambia kuanzia tarehe 23 - 25 Oktoba 2023 ambapo pamoja na mambo mengine, atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Kongamano la Biashara kati ya wafanyabishara wa Tanzania na Zambia.

 

“Ziara hii ni ya kwanza ya Kitaifa ya Mheshimiwa Rais kufanya nchini Zambia tangu alipohudhuria uapisho wa Rais Haichilema mwaka 2022, itakumbukwa kuwa Tanzania na Zambia zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu ambao umejengwa na misingi ya kindugu,” alisema Waziri Makamba.

 

Mhe. Waziri Makamba amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia pia amepewa heshima ya kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Zambia tarehe 25 Oktoba, 2023 na anakuwa kiongozi mashuhuri wa wanne kuhutubia Bunge hilo.

 

“Mhe. Rais katika ziara hii amepewa heshima kubwa ya kuhutubua Bunge la Jamhuri ya Zambia, hii ni heshima kubwa na ya kipekee kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwani anakuwa mgeni mashuhuri wa nne kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Zambia tangu mwaka 2012,” Alisema Waziri Makamba

 

Waziri Makamba aliongeza kuwa ziara hiyo inalenga kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Zambia katika maeneo ya kimkakati ya sekta za uchukuzi, nishati, biashara na miundombinu na kuongeza kuwa katika ziara hiyo Mhesimiwa Rais Dkt. Samia na Mwenyeji wake watajadili namna ya kuboresha miundombinu inayomilikiwa kwa pamoja kati ya Tanzania na Zambia ikiwemo Bomba la Mafuta la TAZAMA, Reli ya TAZARA na barabara ya TANZAM.

 

Aidha, malengo mengine ya ziara hiyo ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wafanyabiasha na wasafirishaji ili waweze kuendesha shughuli zao kwa urahisi, kuibua fursa mpya za ushirikiano na kuieleza jumuiya ya wafanyabiashara Zambia kuhusu maboresho yaliyofanyika katika bandari ya Dar es Salaam.

 

Akielezea kuhusu urari wa biashara kati ya Tanzania na Zambia, Mhe. Waziri Makamba amesema mwenendo wa ukuaji wa Biashara kati ya Tanzania na Zambia umeendelea kuongezeka kwa miaka ya hivi karibuni ambapo mwaka 2016 Tanzania iliuza nchini Zambia bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 70,815.40 na kiasi hicho kimeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 183,648.5 kwa mwaka 2022.

 

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.

 

 






WAZIRI MAKAMBA APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO ZA MWAKILISHI MKAZI WA UNDP

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akipokea Hati za Utambulisho za mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bw. Shigeki Komatsubara katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akipeana mikono na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bw. Shigeki Komatsubara baada ya kupokea Hati za Utambulisho za mwakilishi huyo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akizungumza na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bw. Shigeki Komatsubara baada ya kupokea Hati za Utambulisho za mwakilishi huyo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

 

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bw. Shigeki Komatsubara akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) baada ya kukabidhi Hati zake za Utambulisho katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) katika picha na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bw. Shigeki Komatsubara baada ya kupokea Hati za Utambulisho za mwakilishi huyo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) na ujumbe wake (kulia) katika picha na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bw. Shigeki Komatsubara na ujumbe wake (kushoto) baada ya kupokea Hati za Utambulisho za mwakilishi huyo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.





 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amepokea Hati za Utambulisho za mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bw. Shigeki Komatsubara katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

 

Mara baada ya kupokea nakala za hati hizo, Mhe. Waziri Makamba amemhakikishia Bw. Komatsubara kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na UNDP ili kusogeza mbele agenda yake ya maendeleo na hivyo kuinua maisha ya watanzania kisiasa, kijamii na kiuchumi.

 

Mhe. Waziri amesema Tanzania na UNDP zimekuwa zikishirikiana kutekeleza mipango ya maendeleo kwa kuwa zina lengo la kuboresha maisha ya watu kupitia maeneo ya utawala wa demokrasia, ukuaji uchumi, maendeleo endelevu  mazingira endelevu na uhimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi.

 

Waziri Makamba ameongeza kuwa Tanzania inathmini na kutambua jitihada za UNDP katika kukabiliana na madhara yaliyotokana na janga la UVIKO 19

 

Kwa upande wake Mwakilishi wa UNDP nchini, Bw. Komatsubara ameahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuendeleza jitihada za UNDP nchini na kuongeza kuwa atakuwa sio tu Balozi mzuri wa Tanzania bali pia atakuwa mtangaza mazuri ya Tanzania kupitia kazi zake.

 

Bw. Komatsubara ameongeza kuwa ofisi yake ina nia ya kusaidia Tanzania kujenga uwezo kwa watu wake ili kutekeleza kwa ufanisi mipango ya maendeleo na kwamba atahakikisha UNDP inaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha kuwa ajenda ya maendeleo inafanikishwa.


Friday, October 20, 2023

RAIS DKT. MWINYI AFUNGUA KIKAO CHA 77 CHA TUME YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea na jitihada mbalimbali katika kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na kutekelezwa kwa mujibu wa mikataba ambayo Tanzania ni mwanachama.

 

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati akifungua Kikao cha 77 cha Kawaida cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kilichofanyika jijini Arusha tarehe 20 Oktoba 2023.

 

Mhe. Dkt. Mwinyi ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi  wa kikao hicho amesema kuwa jitihada za Serikali za kulinda na kuimarisha haki za binadamu zimewezesha kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya upatikanaji wa haki mbalimbali zikiwemo haki ya usawa mbele ya sheria, uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa kuabudu, haki ya kumiliki mali, na uhuru wa vyombo vya habari.

 

“Kwa taarifa ni kwamba kutokana na uhuru huo wa vyombo vya habari, hivi sasa Tanzania ina vyombo vya habari vingi ikiwemo Radio 210,Televisheni 56, Magazeti 288 pamoja na mitandao mbalimbali ya kijamii. Pia tumefikia hatua kubwa ya kuimarika kwa uhuru wa kidemokrasia, haki za wanawake, watoto na watu wenye ulemavu kwa kuzingatia usawa wa kijinsia,” amesema Mhe. Rais Dkt. Mwinyi.

 

Kadhalika ameongeza kusema,  Tanzania na Afrika kwa ujumla  inaheshimu haki za binadamu na watu kwa kuzingatia utamaduni, maadili na tunu kama waafrika ambapo katika kutekeleza jukumu hili Serikali ya Tanzania inasimamia haki za binadamu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia kanuni na taratibu zilizopo.

 

“Katika Katiba yetu, haki za binadamu zimeainishwa kuanzia Ibara ya 12 hadi 24 lakini pia Katiba yetu kuanzia Ibara ya 25 hadi 30 imeanisha wajibu wa kila raia” amesisitiza Mhe. Rais Dkt. Mwinyi.

 

Pia ameeleza kuwa katika kuhakikisha haki za binadamu na watu zinalindwa na kutetewa kikamilifu hapa nchini, Serikali ilianzisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambayo ni Taasisi ya Kitaifa yenye jukumu la kulinda, kutetea na kuhifadhi haki hizo.

 

Akizungumzia hali ya ulinzi wa haki za binadamu barani Afrika amesema bado jitihada za pamoja zinahitajika ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazorejesha nyuma jitihada hizo ikiwemo mapinduzi ya Serikali zilizo madarakani, vita vya wenyewe kwa wenyewe, mila na desturi zisizofaa, ukatili wa kijinsia, athari hasi za utandawazi na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu haki zao.

 

Mhe. Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo pia kuwahamasisha washiriki kutenga muda wao na kutembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana kote nchini pamoja na Zanzibar.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Prof. Remy Ngoy Lumbu ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuheshimu haki za binadamu na kuitaja  amani iliyopo kama alama na kielelezo cha ulinzi wa haki  hizo za binadamu.

“Nchi hii inaheshimu haki za binadamu na amani inatawala. Tanzania ina utamaduni wa kutatua changamoto zao kwa njia ya amani na katika hili tunapaswa kujifunza” alisisitiza Mhe. Lumbu.

 

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Mwinyi imeendelea kulinda na kuheshimu haki za binadamu kwa kuboresha mazingira na huduma za kijamii ikiwemo afya, maji, miundombinu na elimu.

 

Awali akimkaribisha Mhe. Dkt. Mwinyi kuzungumza, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kikao hicho muhimu kufanyika nchini na kwamba kikao hicho pamoja na mambo mengine kitajadili namna bora ya kuendelea kusimamia masuala ya haki za binadamu na watu barani Afrika.

 

Pia Mhe. Dkt. Chana amesema kikao hicho ambacho kilitanguliwa na vikao viwili vya Asasi za kiraia na Taasisi za Haki za Bianadamu, kimehudhuriwa na takribani wadau 1,000 kutoka Serikalini, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Asasi za Kiraia, waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akifungua rasmi Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha tarehe 20 Oktoba 2023. Mhe. ais Dkt. Mwinyi alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi huo. Kikao hicho kitafanyika kuanzia tarehe 20 Oktoba 2023 hadi 09 Novemba 2023
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kinachofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 20 Oktoba 2023 hadi 09 Novemba 2023.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu

Mwenyekiti wa Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Prof. Remy Ngoy Lumbu naye akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu
Sehemu ya Viongozi na wageni waalikwa wakishiriki Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu
Sehemu nyingine ya washiriki

Picha ya pamoja




 

Thursday, October 19, 2023

BALOZI ULANGA AKUTANA NA BALOZI WA UBELGIJI

 

 

Mkurugenzi wa Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi John Ulanga (kulia) akizungumza na Balozi wa Ubelgiji nchini Mhe. Peter Huyghebaert (kushoto) alipomtembelea katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salam.

Mazungumzo yakiendelea

 

Mkurugenzi wa Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi John Ulanga na ujumbe wake (kulia) akizungumza na Balozi wa Ubelgiji nchini Mhe. Peter Huyghebaert na ujumbe wake (kushoto) walipokutana katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salam.

 
Mkurugenzi wa Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi John Ulanga amekutana na kuzungumza na Balozi wa Ubelgiji nchini Mhe. Peter Huyghebaert katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salam.

Mazungumzo ya viongozi hao yamelenga kujadiliana na kuangalia uwezekano wa kuimarisha uwekezaji wa makampuni ya Tanzania nchini Ubelgiji na makampuni ya Ubelgiji hapa nchini.