Nchi Wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC) zimehimizwa kuendelea kuunga mkono jitihada za kujikwamua
kiuchumi zinazofanywa na wajasiriamali wadogo na wa kati ili kupunguza
changamoto ya ajira kwa vijana na wanawake na kukuza uchumi wa nchi hizo.
Rai hiyo imetolewa na
Makamu wa Rais wa Burundi, Mhe. Prosper Bazombaza leo tarehe 08 Desemba 2023
jijini Bujumbura, Burundi wakati akifungua rasmi Maonesho ya 23 ya
Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayoendelea
jijini hapa kuanzia tarehe 05 hadi 15 Desemba 2023.
Amesema Nchi Wanachama za
Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaweza kujikwamua katika changamoto ya ajira kwa vijana na wanawake
kwa kuandaa mazingira yanawezesha makundi hayo kujiajiri ikiwa ni pamoja na
kuendelea kuimarisha na kuboresha Maonesho ya Wajasiriamali wadogo na wakati
maarufu kama Nguvu Kazi/Jua Kali ili kuwa na tija zaidi kwa maslahi mapana ya wananchi
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ameongeza kusema kuwa maonesho hayo ambayo yalianza kufanyika mwaka 1999 pamoja na
mambo mengine yanalenga kupunguza umaskini kwa kutengeneza ajira kwa vijana na
wanawake pamoja na kukuza uchumi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki kwa kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wakati kutumia jukwaa hilo
kukutana, kubadilishana uzoefu, kuuza bidhaa zao na kukuza ujuzi na teknolojia.
Awali akizungumza wakati
wa ufunguzi wa Maoenesho hayo, Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania ambaye pia ni Katibu
Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye
Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha Wajasiriamali 259
kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania kushiriki Maonesho hayo ambayo
yamewawezesha kutambulika kimataifa na kupata soko kwa bidhaa na huduma
mbalimbali walizo nazo.
Ameongeza kuwa, Serikali
ya Tanzania itaendelea kuwawezesha Wajasiriamali wadogo kuendelea kushiriki
katika fursa maonesho ya aina hiyo ili kuwa sehemu ya kuboresha mazingira yao
ya biashara na kuongeza ajira.
“Nimezungumza na
wajasiriamali wengi wa Tanzania waliopo hapa Burundi na wengi wao wamenieleza
kuwa wamepata kazi ya kuuza bidhaa zao katika baadhi ya Nchi za Afrika
Mashariki ikiwemo kina mama kutoka Kigoma wanaotengeza Chaki wamepata zabuni ya
kupeleka Chaki hizo nchini Congo na Uganda. Hivyo kupitia maonesho haya
tunawaonesha Watanzania wenzetu kwamba fursa ni nyingi na wazichangamkie amesema
Mhandisi Luhemeja.
Naye Balozi wa Tanzania
nchini Burundi, Mhe. Gelasius Byakanwa amewapongeza na kuwashukuru
Wajasiriamali walioshiriki maonesho hayo na kutoka wito kwa wajasiriamali
wengine kuendelea kushiriki maonesho
hayo kwani ni fursa ya kuyafikia masoko na kupata uzoefu na kujifunza ubunifu
kutoka kwa wajasiriamali wengine wanaoshiriki.
Kwa upande wake, Naibu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Fedha na
Biashara, Bi. Annette Mutaawe ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo
kwenye ufunguzi wa maonesho hayo amesema kuwa Sekretarieti ya Jumuiya hiyo
itaendelea kuboresha maonesho hayo ambapo wajasiriamali hao wanachangia
kupunguza changamoto ya ajira kwa asilimia 65 na pato la kanda kwa asilimia 15.
Akizungumza kwa niaba ya
Wajasiriamali hao, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali Wadogo
na wa Kati Afrika Mashariki, Bw.
Josephat Rweyemamu amezishukuru Serikali zinazounda Nchi Wanachama kwa
kuwewawezesha kushiriki na kusisitiza umuhimu wa nchi hizo wanachama kufanyia kazi changamoto chache
zilizopo ili kuboresha biashara miongoni mwa watu wake ikiwemo kuwa na sarafu
moja ili kurahisisha biashara pamoja na kuendelea kukuza lugha ya Kiswahili kwa
kukifanya kuwa lugha ya biashara.
Wakati wa ufunguzi huo,
washiriki walishuhudia uzinduzi rasmi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Kutoa
taarifa na kufuatilia uondoaji wa Vikwazo Visivyo vya Forodha ambao pamoja na
mambo mengine unalenga kurahisisha ufanyaji biashara baina ya nchi wanachama
hususan kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.
Maonesho ya 23 ya
Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo yamebeba
Kaulimbiu isemayo “Kuunganisha Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika
Mashariki kufanya biashara katika Eneo la Afrika Mashariki” yamehudhuriwa na
zaidi ya wajasiriamali 1,000 kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
|
Makamu wa Rais wa Burundi,
Mhe. Prosper Bazombaza akitoa hotuba tarehe 08 Desemba 2023 wakati wa ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Bujumbura tarehe 08 Desemba 2023. Maonesho hayo ambayo yamewashirikisha wajasiriamali zaidi ya 1,000 kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yanafanyika kuanzia tarehe 05 hadi 15
Desemba 2023.
|
|
Kiongozi
wa Ujumbe wa Tanzania kwenye ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali wadodgo na wa kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye pia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian
Luhemeja akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonesho hayo yanayofanyika jijini Bujumbura, Burundi kuanzia tarehe 05 hadi 15 Desemba 2023
|
|
Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Gelasius Byakanwa akishiriki hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati yanayofanyika jijini Bujumbura
|
|
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania wakishiriki hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati yanayofanyika jijini Bujumbura |
|
Makamu wa Rais wa Burundi,
Mhe. Prosper Bazombaza akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kutembelea banda la Tanzania mara baada ya kufungua rasmi Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayofanyika ijini Bujumbur. Wanaoshuhudia ni Mhandisi Luhemeja (kushoto) na Mhe. Balozi Byakanwa |
|
Makamu wa Rais wa Burundi, Mhe. Prosper Bazombaza akiwa kwenye picha ya pamoja na Mhe. Mhandisi Luhemeja, Mhe. Balozi Byakanwa na wageni wengine walioshiriki ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
|
|
Mhe. Mhandisi Luhemeja akisalimiana na Mwenyekiti
wa Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati Afrika Mashariki, Bw. Josephat Rweyemamu alipotembelea Banda la Tanzania
|
|
Mhe. Balozi Byakanwa akiteta jambo na Mhe. Mhandisi Luhemeja
|
|
Mhe. Mhandisi Luhemeja akizungumza na mmoja wa wajasiriamali kutoka Tanzania anayeshiriki Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali wadogo na wa kati maarfu kama Nguvu Kazi/Jua Kali alipotembelea mabanda ya wajasiriamali hao jijini Bujumbura
|
|
Mhe. Mhandisi Luhemeja akiwa na Mhe. Balozi Byakanwa wakizungumza na mmoja wa wajasiriamali anayeshiriki Maonesho ya 23 ya ajasiriamali wadogo na wa kati yanayoendelea jijini Bujumbura
|
|
Mhe. Balozi Byakanwa akisaini kitabu cha wageni alipotembelea Banda la Maonesho la Mfuko wa Taifa wa Jamii (NSSF). Mfuko huo unashiriki ili kuhamasisha Diaspora wa Tanzania waliopo Burundi kujiunga na huduma mbalimbali zinazotolewa kwao na mfuko huo
|
|
Picha ya pamoja
|