Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa
maadhimisho ya miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (PSC-AU)
yatakayofanyika tarehe 25 Mei, 2024 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha
Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amefafanua kuwa, uenyeji
huu umekuja kufuatia maamuzi ya Mkutano wa 37 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Umoja wa Afrika uliofanyika mwezi Februari 2024 jijini Addis Ababa, Ethiopia.
“Ikumbukwe kuwa, mwezi Machi 2022 Tanzania
ilichaguliwa kuhudumu kwenye nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la
Umoja wa Afrika kwa miaka miwili hadi mwezi Machi 2024 ambapo muda wa kuhudumu
ulifikia kikomo. Hivyo Tanzania imechaguliwa tena kuhudumu kwenye Baraza hilo
kwa muhula mwingine wa miaka miwili hadi mwaka 2026,” alisema Mhe Waziri.
Amesema Baraza la Amani na Usalama ni chombo
cha juu cha maamuzi kuhusu masuala ya amani na usalama kwenye Umoja wa Afrika
likiwa na jukumu la kuzuia kutokea kwa migogoro, kusuluhisha au kukabiliana
nayo pale inapojitokeza.
Amesema Nchi 15 tu kati ya nchi 55 wanachama wa
Umoja wa Afrika ndio wajumbe wa Baraza hilo na kuongeza kuwa wajumbe wa sasa ni pamoja na; Tanzania, Uganda
na Djibout (Ukanda wa Afrika Mashariki); Cameroon, DRC na Equatorial Guinea
(Kanda ya Kati); Afrika Kusini, Angola na Botswana (Kanda ya Kusini); Cote
d’Ivoire , Gambia, Nigeria, na Sierra Leone (magharibi) na Misri na Morocco
(Ukanda wa Kaskazini).
‘’Hivyo, Tanzania kuwa Mjumbe kwenye Baraza
hili ni ishara ya kuheshimika na kuaminika kwa nchi yetu, ambapo heshima hiyo
inaifanya nchi yetu kupewa jukumu jingine kubwa zaidi la kuwa mwenyekiti wa
Baraza hilo kwa mwezi Mei. Katika nafasi ya Uenyekiti Tanzania inajukumu la
kusimamia shughuli zote zinazohusu Baraza, ikiwemo kufuatilia kwa karibu hali
ya ulinzi na usalama kwenye Bara la Afrika, kutoa miongozo ya kushughulikia na
masuala ya kiusalama pale inapobidi na pia kuandaa ratiba na kuongoza vikao vya
Baraza,’’ alisema Waziri Makamba.
Pia Mhe. Makamba ametumia fursa hiyo kumshukuru
na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya ya kuimarisha
Diplomasia ya Tanzania katika kutoa kipaumbele kwenye masuala ya ulinzi na
usalama barani Afrika na dunia kwa ujumla.
Katika maadhimisho hayo Tanzania kwa
kushirikiana na Sekretarieti ya Baraza imeandaa ratiba ya shughuli mbalimbali kwa
kuifanya kila wiki katika mwezi Mei kubeba dhima mahsusi ambazo ni: Usuluhishi
na majadiliano; masuala ya mahitaji ya kibinadamu,amani na usalama; ulinzi kwa
Watoto na kusaidia misheni za amani.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ya Miaka 20 ya
Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika ni; ‘’Miaka 20 ya Baraza la Amani na
Usalama la Umoja wa Afrika ikiwa chombo cha Maamuzi: Miongo miwili ya Afrika ya
Amani na Usalama tunayoitaka (20 years
of the AU PSC as a Standing Decision-Making Organ: The Next Decades of the
Peace and Security We Want in Africa)’’
Maadhimisho haya, yanatoa fursa kwa Waafrika
wote wenye kuitakia mema Afrika kutoa maoni yao ya kuliimarisha Baraza ili
liweze kushughulikia changamoto za kiusalama barani Afrika. Hivyo, wageni
takriban 120 kutoka nchi mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria.
Kadhalika, Miongoni mwa watu mashuhuri
watakaoshiriki ni pamoja na; Mhe. Jesca Alupo, Makamu wa Rais Uganda, Mhe.
Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Rais Mstaafu
wa Nigeria, Mhe. Olesegun Obasanjo, Rais Mstaafu wa Burundi, Mhe. Domitien
Ndayizeye, Rais Mstaafu wa Msumbiji, Mhe. Joachim Chissano na Rais wetu
Mstaafu, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.
Mhe. Waziri Mkamba ametoa rai kwa watanzania kushiriki
kwa wingi katika siku ya tarehe 24 Mei, 2024 ambako kutakuwa na mjadala wa wazi
utakaofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na siku ya kilele cha maadhimisho
hayo ili kumuunga mkono Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa heshima kubwa aliyopewa na Umoja wa Afrika.
Maadhimisho ya miaka 20 ya Baraza
yatahitimishwa kwa kutolewa kwa Tamko la Dar es Salaam.
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akiongea na waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam tarehe 22 Mei, 2024.
|
|
Kutoka kushoto Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Afrika Addis Ababa, Ethiopia Mhe. Balozi Innocent Shiyo pamoja na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.
|
|
Mkutano ukiendelea.
|