Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maadhimisho ya Mwaka wa elimu wa Umoja wa Afrika wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha. |
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maadhimisho ya Mwaka wa elimu wa Umoja wa Afrika wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha. |
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi alipowasili katika Ukumbi wa AICC kufungua mkutano wa kwanza wa elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maadhimisho ya Mwaka wa elimu wa Umoja wa Afrika jijini Arusha. |
Akifungua mkutano huo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha Mhe. Dkt. Mpango amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwekeza zaidi katika elimu na afya ili kuweza kunufaika na idadi kubwa ya watu iliyopo hususani vijana ambao watakuwa wameelimika na kuwa na afya bora na hivyo kujiletea maendeleo.
Mhe. Dkt. Mpango amesema ongezeko la watu katika mataifa ya Afrika Mashariki linatoa ishara ya ulazima wa kuongeza uwekezaji wa rasilimali zaidi za kifedha, kiafya na kielimu ili kukidhi mahitaji ya upatikanaji wa elimu bora na afya bora kwa watu wake.
“Mwenendo wa idadi ya watu Afrika Mashariki unaweza kuwa baraka kubwa kama ukitumiwa vizuri kwani kuendelea kuwa na vijana wengi wenye ujuzi na umahiri wa kujenga uchumi imara hali ambayo itafikiwa ikiwa rasilimali watu hiyo itatumika kikamilifu”, alisisitiza Dkt. Mpango.
Amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuhakikisha mabadiliko ya dhati ya elimu yanafikiwa na hivyo kutoa matokeo chanya kwa vijana wengi ndani ya Jumuiya.
Amesema takwimu za Benki ya Dunia zinaonesha kuwa Bara la Afrika limekua likipata matokeo yenye faida katika elimu ukilinganisha na mabara mengine na kuongeza kuwa ukanda wa kusini mwa jangwa la sahara bado unakabiliwa ufadhili mdogo zaidi uliowekezwa katika sekta ya elimu ambao ukipatikana kwa kiwango kinachostahili utaleta tija na manufaa makubwa kwa nchi hizo.
Ametoa wito kwa hatua zaidi kuchukuliwa na juhudi zaidi kutumika ili kutambua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu barani Afrika ambazo kwa kiasi kikubwa zinatokana na uwekezaji mdogo unaofanywa katika sekta hiyo na kusababisha utoaji wa elimu bora yenye ujuzi unaohitajika kuawa mgumu na hivyo kushindwa kukabiliana na changamoto tatu zinazoikabili dunia kwa sasa ambazo ni ongezeko la idadi ya watu, utandawazi na maendeleo ya teknolojia.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ambapo ameeleza kuwa imefanya elimu ya lazima kutoka miaka saba hadi miaka kumi ifikapo mwaka 2027/2028. Aidha amesema Serikali imefanya mabadiliko ya mtaala wa elimu nchini ambayo yanalenga kuongeza ubora wa elimu pamoja na kuandaa rasilimali watu itakayoendana na mahitaji ya dunia kwa sasa ya aendeleo ya dijitali, teknolojia pamoja na kutumia vema fursa mbalimbali zilizopo.
Ametaja pia hatua za uboreshaji wa miundombinu ya elimu kama vile kujenga madarasa ya kufundishia, nyumba za walimu, kuboresha mazingira ya ufundishaji kwa kuhakikisha kuna walimu wa kutosha na nyenzo za kufundishia kama vile kompyuta na vitabu ili kutimiza lengo la kuongeza ubora wa elimu, kuongeza upatikanaji wake na kuhakikisha elimu inayotolewa inatosheleza mahitaji ya ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya teknolojia.
Makamu wa Rais amewashukuru washirika wa Kimataifa wanaoiunga mkono Tanzania katika mageuzi ya sekta ya elimu na kuukaribisha mpango mpya wa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (PEERS) ambao utasaidia uratibu wa mifumo ya elimu katika kanda.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo amesema Elimu ni jiwe la msingi ambalo tunajengea sio tu maendeleo ya kitaaluma na kijamii na kwa mtu mtu binafsi bali pia ni uwezeshaji wa kiuchumi ambao husaidia kupunguza umaskini na kuleta maendeleo kwa jamii.
Ameongeza kuwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zimepiga hatua kubwa hususan katika viwango vya usajili wa Watoto shuleni hali ambayo imetokana na juhudi za serikali kwa kushirikiana na washirika mbalimbali wa maendeleo na hivyo kufanikisha utekelezaji wa mipango ya kitaifa na kimataifa ya Elimu kwa Wote kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 26 cha Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948.