Friday, August 16, 2024

WAZIRI KOMBO ASISITIZA AMANI NA USALAMA KATIKA KANDA YA SADC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha amani na usalama katika kanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).


Balozi Kombo ametoa Msisitizo huo wakati wa Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama (MCO) wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)  uliofanyika Harare, Zimbabwe tarehe 16 Agosti, 2024.


Mkutano huo ulitanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 15 Agosti, 2024 ambapo, mikutano hii miwili ni mikutano ya awali ya maandalizi ya agenda na nyaraka kwa ajili ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika leo tarehe 16 Agosti, 2024.


Akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi hiyo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe amewakaribisha wajumbe wa mkutano huo kujadili ajenda zilizojikita katika kutafuta amani na usalama wa Jumuiya hiyo na umuhimu wa nguvu ya pamoja katika kufanikisha jitihada za suala hilo.


Agenda zilizojadiliwa na mkutano huu ni pamoja na Hali ya Ulinzi na Usalama katika Kanda, Uimarishwaji wa Demokrasia katika Kanda, Mfumo wa Kuwaenzi Viongozi Waasisi wa SADC na Wagombea wa Nafasi mbalimbali wa Kanda katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa.


Akichangia katika mkutano huo Waziri Kombo amesema kuwa Tanzania inalipa kipaumbele suala la kuimarisha ulinzi na usalama katika kanda na katika kufanikisha hili Tanzania inashiriki kikamilifu katika juhudi za kutafuta amani ndani ya kanda, barani Afrika na duniani ikiwa ni pamoja na kuchangia gharama zake.


“Tuna nia ya dhati ya kuunga mkono juhudi za kikanda na kimataifa katika masuala ya amani na usalama. Tunaamini uzoefu wetu utatuwezesha kuchangia kwa ufanisi katika jukumu la Baraza la Usalama” alisema waziri Kombo.


Aidha, Waziri Kombo amewasilisha ombi la kuendelea kuungwa mkono na nchi za SADC katika nafasi mbalimbali zinazowaniwa na Watanzania ikiwemo nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) – Afrika inayowaniwa na Dkt. Faustine Ndugulile.


Pia, ameomba kuungwa mkono katika nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka 2026 – 2028 na Ujumbe usio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka 2029 na 2030.


Mkutano huo pia umehudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW) na Maafisa Waandamizi kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali.

======================================= 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akishiriki Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) uliofanyika Harare, Zimbabwe tarehe 16 Agosti, 2024.

Kushoto ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW) wakifuatilia Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) uliofanyika tarehe 16 Agosti, 2024.

Kushoto ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW) wakifuatilia Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) uliofanyika tarehe 16 Agosti, 2024.



Kulia ni Mhe. Dkt. Ndugulia anayewania nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika. 
Kulia ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Jacob Mkunda akifuatilia Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) uliofanyika Harare, Zimbabwe tarehe 16 Agosti, 2024.

Ujumbe wa Tanzania ukiwa umesisiamam wakati wimbo wa SADC uliokuwa ukiimbwa kabla ya kuanza kwa mkutano.

Ujumbe wa Zambia

Sehemu nyingine ya Ujumbe wa Tanzania


KATIBU MKUU MAMBO YA NJE AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA KIKAO CHA KAMATI YA MAKATIBU WAKUU WA SADC ORGAN TROIKA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ameongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao cha Kamati ya Makatibu Wakuu cha Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 15 Agosti, 2024.

Mkutano huo pamoja na masuala mengine umejadili Hali ya Siasa, na Usalama katika kanda.
Nchi zilizoshiriki kikao hicho cha utatu ni pamoja na Tanzania, Zambia na Namibia.


Thursday, August 15, 2024

TANZANIA KUSHIRIKIANA NA IOM KUWEZESHA VIJANA

Tanzania imesisitiza kuendelea kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa lilanoshughulikia Wahamiaji (IOM) kuwawezesha vijana kiuchumi ili kutengeneza ajira zitakazojenga ustawi wao na kuleta maendeleo kwa taifa.

Msisitizo huo umetolewa leo tarehe 15 Agosti, 2024 wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo alipokutana na Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamiaji (IOM) Bw. Mohammed ABDIKER jijini Harare, Zimbabwe.

Aidha, katika mazungungumzo hayo Waziri Kombo ameeleza changamoto ya uhamiaji huwaathiri zaidi vijana wanaotoka katika mataifa yanayoendelea hususan mataifa ya Afrika ambapo wamekuwa wakihama kwenda kutafuta maisha bora kwa ajili yao na familia zao.

"Binafsi ningependa tatizo la uhamiaji lipate suluhisho kwa kufanyia kazi chanzo cha tatizo badala ya kufanyia kazi matokeo au matatizo yanayotokea baada ya watu kuhama na kupata changamoto wakiwa katika harakati za kuvuka mipaka" alisema Waziri Kombo.

Pia ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua changamoto hiyo imetafuta suluhisho la ajira kwa vijana wa kitanzania kwa kuwawezesha kiuchumi kupitia mradi wa kilimo ujulikanao kama “Building Better Tomorrow (BBT)’’ ambao, utawawezesha vijana kujiajiri na kuwaajiri wengine, pamoja na kufanya kilimo biashara kwa lengo la kukuza kipato.

Kwa upande wa Bw. ABDIKER ameipongeza Tanzania kwa kuwahudumia wahamiaji ambao sehemu kubwa ni wakimbizi na wale wanaopita kutoka Pembe ya Afrika kuelekea kusini mwa Afrika kutafuta maisha bora na kwamba IOM inaendelea kutoa ushirikiano katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza.

Pia amepongeza kwa uwepo wa chuo cha uhamiaji nchini ambacho kimekuwa kikitoa elimu ya uhamiaji kwa watanzania na kwa mataifa mengine na pia amesema kuwa IOM ina mpango wa kuanzisha chuo kikubwa cha uhamiaji kitakachochukua wanafunzi ulimwenguni kote, hivyo uwepo wa chuo hicho utaongeza ushirikiano na kujenga uwezo wa kitaaluma katika masuala ya uhamiaji.

Vilevile, viongozi hao wamejadili changamoto mbalimbali zinazowakabili wahamiaji ikiwemo, mabadiliko ya tabia nchi ambayo husababisha ajali kwenye safari za majini na kupelekea watu kupoteza maisha wakati wa kuhama sambamba na ajira zisizo na staha wanazozipata baada ya kufika uhamishoni pasipo kupata taratibu rasmi za kuhama.

Hivyo, IOM ina matumaini ya kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania hasa wakati huu ambapo inaenda kukabidhiwa nafasi ya Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security).

================================

Habari katika picha za mazungumzo ya Mhe. Waziri Kombo na Bw. Mohammed ABDIKER

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamiaji (IOM) Bw. Mohammed ABDIKER (hayupo pichani) jijini Harare, Zimbabwe tarehe 15 Agosti, 2024.

Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamiaji (IOM) Bw. Mohammed ABDIKER akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (hayupo pichani) jijini Harare, Zimbabwe tarehe 15 Agosti, 2024.

Mazungumzo yakiendelea.


NAIBU WAZIRI CHUMI AFUNGUA KONGAMANO LA KISWAHILI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisisitiza jambo alipokuwa akifungua Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb.) amefungua Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma, akimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo. 

Kongamano hilo linaloongozwa na mada kuu isemayo "Lugha ya Kiswahili kwa Maendeleo Barani Afrika" linajumuisha Wataalam, Watafiti na wadau wa Kiswahili kutoka Nchi za Afrika Mashariki na sehemu mbalimbali duniani. 

Akifungua Kongamano hilo Waziri Chumi ameeleza kuwa kiswahili kimekuwa miongoni mwa lugha inayotuunganisha Waafrika hususan waliopo Kusini mwa Jangwa la Sahara, na hasa kutokana na mchango wake wakati wa harakati za kupigania uhuru. 

Akizungumzia nafasi ya Wizara katika kueneza lugha ya Kiswahili ulimwenguni Mhe. Chumi ameeleza Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje Nchi ilitoa mchango mkubwa katika kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza Afrika kutambuliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO). 

Vilevile ameongeza kusema kuwa licha ya mchango huo, Wizara ya Mambo ya Nje inaendelea kukipa kipaumbele cha kipekee Kiswahili kupitia Sera Mpya ya Mambo ya Nje inayofanyiwa mapitio, hatua ambayo itachangia kubidhaisha lugha hiyo adhimu duniani hivyo kuongeza matumizi ya Kiswahili nje ya mipaka yetu. 

"Kwa sasa Wizara yetu ipo kwenye hatua za mwisho za mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya Taifa letu. Kutokana na tathmini tuliyoifanya kwenye mapitio hayo, tumekubaliana kuongeza mawanda ya Diplomasia ya Uchumi kwa kujumuisha maeneo ambayo siyo ya jadi (traditional) ikiwemo masuala ya kubidhaisha Kiswahili" Alieleza Mhe. Chumi.

Aliongeza kusema kuwa Wizara kwa siku za usoni inatarajia kuongeza wigo wa upatikanaji wa fursa kwa waalimu wa Kiswahili na wakalimani sehemu mbalimbali duniani pamoja na uuzaji wa vitabu vya kiswahili.

Kwa upande wake, mratibu wa kongamano hilo Dkt. Zainabu Idd ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuenzi na kukuza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya nchi. 

Aidha, Dkt. Zainabu pamoja na kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali, ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kutoa msukumo wa matumizi ya Kiswahili katika majukwaa na matukio mbalimbali ya kimataifa ikiwemo katika matamasha makubwa ya michezo kama vile AFCON, ili kukiongezea thamani na kuwavutia watu wengi zaidi duniani kutumia lugha hiyo adhimu.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanikisha kuongeza wigo wa matumizi ya Lugha ya Kiswahili hususan katika Jumuiya za Kikanda ambapo tayari Jumuiya za SADC, EAC na AU zinatumia lugha hiyo katika kuendesha vikao mbalimbali. 

Vilevile Wizara inaendelea na mikakati ya kukuza na kubidhaisha Kiswahili ikiwemo kufungua madarasa ya kufundishia Kiswahili katika Balozi za Tanzania zilizopo sehemu mbalimbali duniani. 

CHAKAMA ni chama kinachoundwa na wahadhiri wanaofundisha Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki kikilenga kuunganisha wadau wa Kiswahili Kikanda na Kimataifa kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo utafiti na kufanya mijadala fikirishi kuhusu lugha ya Kiswahili
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akitia saini kwenye kitabu cha wageni muda mfupi kabla ya ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb.) akisalimiana na Prof. Albino John Tenge Mkuu wa Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii, alipowasili katika Chuo Kikuu cha Dodoma kufungua Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika chuoni hapo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisisitiza jambo alipokuwa akifungua Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb.) akikabidhiwa cheti cha kutambua mchango wa Wizara katika kufanikisha kufanyika kwa Kongamano hilo na kukuza lugha Kiswahili.
Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki likiendelea
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akifuatilia  hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodom
Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki likiendelea
Mkuu wa Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii Prof. Albino John Tenge akizungumza kwenye ufunguzi Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa CHAKAMA linalofanyika jijini Dodoma
Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki likiendelea

PROF MKENDA AFUNGA MKUTANO WA ELIMU WA EAC JIJINI ARUSHA

 

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa Umoja Afrika uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti, 2024.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa Umoja Afrika uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti, 2024.

Mwenyekiti wa Baraza la Kisekta na Waziri wa Elimu na Mafunzo wa Sudan Kusini Mhe. Awut Deng Achuil akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti,2024.



 

washiriki wakifuatilia ufungaji wa  Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti,2024.


washiriki wakifuatilia ufungaji wa  Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti,2024.


washiriki wakifuatilia ufungaji wa  Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti,2024.


Picha ya pamoja na Meza Kuu wakati wa ufungaji wa  Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti,2024.

Picha ya pamoja na Meza Kuu wakati wa ufungaji wa  Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU uliofanyika jijini Arusha tarehe 12-15 Agosti,2024.

 

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amefunga rasmi Mkutano wa kwanza wa Elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa elimu wa Umoja Afrika uliofanyika jijini Arusha. 

Akizungumza katika hafla hiyo Prof. Mkenda amezitaka nchi wanachama kuandaa mpango kazi utakaoonesha namna bora ya kutekeleza maazimio yaliyotokana na mkutano huo ili kuhakikisha yanafanyiwa kazi kwa ukamilifu.

Pia ametaka kuhakikisha mafanikio yote yaliyopatikana katika maadhimisho ya mwaka wa elimu wa AU yanasherehekewa na kutafakari jinsi ya kuwa na mifumo bora zaidi ya utoaji elimu kwa vijana na hivyo baada ya miaka miwili mkutano ujao uone matunda ya mkutano huo. 

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Kisekta na Waziri wa Elimu na Mafunzo wa Sudan Kusini Mhe. Awut Deng Achuil alıtoa wito wa kuchukua hatua na kujitoa zaidi ili kuhakikisha malengo na maazimio ya mkutano yanatekelezwa kwa vitendo na ameipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji pamoja na Sekretarieti ya EAC na nchi wanachama kwa kuandaa mkutano huo kwa mafanikio makubwa. 

Mkutano huo wa kwanza na wa aina yake kufanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki ulijumuisha wadau mbalimbali wa elimu kutoka Serikalini na sekta binafsi umejadili na kuweka mikakati mipya ya kukabiliana na fursa na changamoto zilizopo katika sekta ya elimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Bara la Afrika kwa ujumla. Kufanyika kwa mkutano huo ni utekekezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Jumuiya ya Afrika Mashariki la Elimu, Sayansi na Teknolojia, Utamaduni na Michezo; na Umoja wa Afrika. 

Mkutano huo wa elimu na Maadhimisho uliwakutanisha Mawaziri wa Elimu kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wageni mashuhuri wakiwemo Wawakilishi wa Nchi mbalimbali kama Jamhuri ya Watu wa China; Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Kikanda na Kimataifa zinazojihusisha na agenda ya kuendeleza sekta ya elimu kama vile Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Afrika (AU), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Taasisi ya Maendeleo ya Elimu Afrika (ADEA), Taasisi ya Haki Elimu, na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ). 

Mkutano huo pia uliwakutanisha Wadau wa elimu zaidi ya 600 kutoka Nchi Wanachama, Taasisi za elimu, Mashirika yasiyo ya kiserikali, Sekta binafsi, Mashirika ya kimataifa, Asasi za kiraia waliokutana kutathmini, kubadilishana uzoefu wa mbinu bora za uendelezaji wa sekta ya elimu. Mkutano huo uliandaliwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Nchi wanachama, taasisi zisizo za kiserikali , wadau wa maendeleo na bhana vya elimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ulianza tarehe 12 hadi 15 Agosti 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan awasili Zimbabwe

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili Zimbabwe kwa ajilli ya kushiriki Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika tarehe 17 Agosti, 2024.


WAZIRI KOMBO AFANYA MAZUNGUMZO NA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA AFRIKA KUSINI NA MADAGASCAR


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Mhe. Ronald Lamola na Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Mhe. Dkt. Rasata Rafaravavitafika pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) leo tarehe 14 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe.

 

Akizungumza na Mhe. Lamola, Waziri Kombo ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kudumisha ushirikiano wa kihistoria na kindugu uliopo baina ya Tanzania na Afrika kusini ili kukuza sekta za kiuchumi ikiwemo biashara, utalii, uwekezaji, elimu, afya na maeneo mengine ya kimkakati kwa maslahi ya pande zote mbili.

 

Naye Mhe. Lamola ameeleza kuwa Afrika Kusini inaendelea kuthamini mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Taifa hilo hivyo, ina nia ya dhati ya kuuenzi mchango huo kwa kukuza ushirikiano katika shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa ustawi wa wananchi wa mataifa hayo mawili.

 

 

Aidha, katika mazungumzo ya Mhe. Kombo na Mhe. Dkt. Rafaravavitafika wamejadili juu ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi na taifa hilo hususan katika sekta ya uchumi wa blue ambao Tanzania imeuwekea mkazo ili kukuza uchumi kupitia rasilimali za bahari zinazopatikana na kukuza biashara yake kimataifa.

HABARI KATIKA PICHA: Waziri Kombo alipokutana kwa mazungumzo na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Mhe. Ronald Lamola.







HABARI KATIKA PICHA: Waziri Kombo alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Mhe. Dkt. Rasata Rafaravavitafika










Wednesday, August 14, 2024

WAZIRI KOMBO AFANYA KIKAO NA WATUMISHI WA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI ZIMBABWE

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amefanya kikao na watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe tarehe 14 Agosti, 2024.

 

Kikao hicho kilichofanyika pembezoni mwa mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kimejadili juu ya utekelezaji wa majukumu ya kidiplomasia yanayoendelea kutekelezwa na watumishi wa ubalozi huo.


“ Serikali ina imani nanyi ndio maana ikawaleta kutekeleza majukumu katika  kituo hiki, hivyo, ni vema mkajituma na kufanya kazi kwa tija ili kuweza kuleta matokeo makubwa kwa maslahi ya Taifa letu” alisema Waziri Kombo.


Pia, ameeleza kuwa Wizara inahitaji kuona Balozi za Tanzania nje zinatekeleza diplomasia ya uchumi kwa vitendo na kuwasilisha taarifa zenye matokeo hususan katika sekta za biashara, uwekezaji, na utalii. 


Aidha, Waziri Kombo ametembelea miradi mbalimbali ya maendeleo yenye umiliki wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zimbabwe ikiwemo, nyumba za makazi za watumishi wa Ubalozi, nyumba za makazi za kibiashara, jengo la ofisi la ubalozi na kiwanja cha ubalozi huo chenye ukubwa wa ekari  saba (7).


Waziri Kombo amemueleza Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe kuwa ziara yake katika miradi hiyo imekuwa ya mafanikio kwa kuwa amejionea namna Ubalozi unavyojituma katika kutekeleza majukumu yake pamoja na jitihada za kukuza ushirikiano na nchi hiyo rafiki.


Vilevile, miradi hiyo kwa upande mwingine imeuwezesha ubalozi kupata nyumba kwa ajili ya watumishi wake na hivyo kuipunguzia Serikali gharama ya kupangisha nyumba na za uendeshaji kwa ujumla.


Hivyo, Waziri Kombo amesisitiza kuwa miongoni mwa masuala ambayo atayatilia mkazo katika utekelezaji majukumu yake ni pamoja na kuona Balozi za Tanzania nje zinaendeshwa kwa tija ili kuongeza pato la taifa.

====================================

HABARI KATIKA PICHA: Waziri Kombo akitembelea miradi ya maendeleo katika Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.