Friday, October 4, 2024

MKUU WA MISHENI YA UANGALIZI WA UCHAGUZI YA SADC NCHINI MSUMBIJI AFANYA MAZUNGUMZO NA MGOMBEA URAIS WA CHAMA CHA FRELIMO

Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC –SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume ameendelea kukutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi mkuu wa Msumbiji ambapo leo tarehe 04 Oktoba, 2024 jijini Maputo amekutana na kufanya mazungumzo na Mgombea urais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Daniel Francisco Chapo.

 

Katika mazungumzo yao, Mhe. Chapo alimweleza Mhe. Dkt. Karume masuala mbalimbali kuhusu maandalizi ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa rais na wabunge unaotarajiwa kufanyika nchini humo tarehe 09 Oktoba 2024.


Kwa upande wake,  Mhe. Dkt. Karume alimshukuru Mhe. Chapo kwa taarifa yake na kumweleza lengo la Misheni anayoiongoza  kuwa ni kuangalia uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni na Miongozo  ya SADC inayoongoza Uchaguzi wa Kidemokrasia iliyorekebishwa mwaka 2021 na kuridhiwa na nchi wanachama. Pia alitumia nafasi hiyo kuwatakia  wananchi wa Msumbiji uchaguzi mwema wa amani na utulivu.

 

Wakati wa Mkutano huo, Mhe. Dkt. Karume aliambatana na Wajumbe wa Troika kutoka Tanzania, Zambia na Malawi, Sekretarieti ya SADC akiwemo Mkurugenzi wa Troika, Prof. Kula Ishmael Theletsane na  Wajumbe wa Baraza la Ushauri wa masuala ya Uchaguzi la SADC (SEAC). Wajumbe  wa Troika kutoka Tanzania walioshiriki ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushiriano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa na  Mshauri wa Rais masuala ya Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Sofia Mjema.

 

Mhe. Dkt. Karume kwa nafasi yake ya Mkuu wa Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC ameendelea  kukutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi ambapo hadi sasa amekutana na Mwenyekiti wa  Tume ya Uchaguzi ya Msumbiji (CNE), Mabalozi wa Nchi za SADC waliopo Msumbiji, Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji na Kamishna Msidizi wa Jeshi la Polisi la Msumbiji.

Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume akizungumza na Mgombea urais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Daniel Francisco Chapo.  Mazungumzo yao yamefanyika tarehe 04 Oktoba 2024 jijini Maputo. Uchaguzi wa Rais na Wabunge nchini Msumbiji utafanyika tarehe 09 Oktoba 2024.

Mazungumzo yakiendelea ambapo Mhe. Chapo amemweleza Mhe. Dkt. Karume kuhusu maandalizi ya uchaguzi ya Chama chake kuelekea uchaguzi tarehe 09 Oktoba 2024

Mhe. Chapo akizungumza

Wajumbe wa Troika kutoka Tanzania ambao walishiriki mazungumzo kati ya Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji, Mhe. Dkt Karume na mgombea urais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Chapo (hawapo pichani). Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa na Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania masuala ya Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Sofia Mjema

Wajumbe wa Troika kutoka Zambia nao wakishiriki mazungumzo kati ya Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji, Mhe. Dkt Karume na mgombea urais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Chapo (hawapo pichani). 
Wajumbe wakishiriki mazungumzo kati ya Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji, Mhe. Dkt Karume na mgombea urais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Chapo (hawapo pichani). 
Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji, Mhe. Dkt Karume akiagana na  mgombea urais wa Chama cha FRELIMO, Mhe. Chapo baada ya kumaliza mazungumzo yao 
Picha ya pamoja




















MISHENI YA UANGALIZI WA UCHAGUZI YA SADC NCHINI MSUMBIJI YAZINDULIWA RASMI

Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume amezindua rasmi Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi  leo tarehe 03 Oktoba 2024 katika hafla iliyofanyika jijini Maputo.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliowashirikisha wadau mbalimbali muhimu wakiwemo Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini Msumbiji, Wawakilishi kutoka Serikali ya Msumbiji, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Msumbiji (CNE), Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini, Jumuiya za Kiraia na waandishi wa habari, Mhe. Dkt. Karume ameishukuru Serikali ya Msumbiji kwa kuialika Misheni hiyo ambayo ina jukumu la kuangalia namna misingi ya demokrasia, taratibu na kanuni za uchaguzi za SADC zinavyotekelezwa.


Amesema Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC pamoja na mambo mengine itatathmini mwenendo wa uchaguzi kulingana na  Kanuni na Miongozo ya SADC inayoongoza Uchaguzi wa Kidemokrasia iliyorekebishwa mwaka 2021 na kuridhiwa na Nchi Wanachama.


Amesema pamoja na mambo mengine, Kanuni na Miongozo hiyo inazitaka nchi wanachama kushirikisha wananchi  katika mchakato wa demokrasia, kuwawezesha  wananchi kufurahia  haki za binadamu na kuwa huru katika kushirikiana, kukusanyika  na kujieleza. Kadhalika kanuni na miongozo hiyo imeweka mikakati ya kuzuia rushwa, upendeleo, migogoro ya kisiasa, kutovumiliana na kuhakikisha zinakuwepo fursa sawa  kwa vyama vyote vya siasa katika kutumia vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Serikali na kuhakikisha  uhuru wa wananchi kupata taarifa kuhusu masuala ya uchaguziunazingatiwa.

 

Mhe. Dkt. Karume pia alitumia fursa hiyo kupongeza kazi kubwa iliyofanywa  na Misheni ya Ulinzi wa Amani ya SADC nchini Msumbiji (SAMIM), ambayo ilifanikiwa kudhibiti  vikundi vya kigaidi vilivyoibka katika maeneo ya Kaskazini mwa Msumbiji na kuishukuru Serikali ya Msumbiji kwa kuahidi kuendelea kulinda mafanikio yaliyofikiwa na SAMIM katika eneo hilo.

 

Vilevile, Mhe. Dkt. Karume alilipongeza Jeshi la Ulinzi la Msumbiji na vyombo vingine vya Usalama vya nchi hiyo kwa jitihada zao zilizofanikisha Wananchi katika maeneo ya Kaskazini mwa nchi hiyo wanajiandikisha kwa ajii ya kupiga kura licha  ya changamoto za kiusalama.

 

Mhe. Dkt. Karume alitumia nafasi hiyo pia kuwatakia uchaguzi wa amani na utulivu wananchi wa Msumbiji na kutoa wito kwa wale wote waliojiandikisha kujitokeza  kwa wingi siku ya tarehe 09 Oktoba 2024 na kupiga kura. Pia alitoa rai kwa wadau wote wa siasa nchini Msumbiji kuheshimu maoni na mitazamo tofauti ya kisiasa miongoni mwao na kujua wajibu wao katika kipindi chote cha uchaguzi na baada ya uchaguzi.

 

Naye Mkurugenzi wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama, Prof. Kula Ishmael Theletsane alieleza umuhimu wa Misheni za Uangalizi kuwa zinalenga  kufikia malengo  mahsusi ya mafanikio hususan kwa mtangamano wa SADC kupitia kanuni ya ustahimilivu, utekelezaji wa demokrasia, utwala bora na amani.

 

Misheni  ya SADC, iliwasili nchini Msumbiji tarehe 24 Septemba, 2024 na itakuwepo nchini humo hadi tarehe 20 Oktoba, 2024 kwa lengo la kuangalia uchaguzi kwa mujibu  wa Kanuni na Miongozo ya SADC inayoongoza Uchaguzi  wa Kidemokrasia iliyorekebishwa mwaka 2021.

 

Misheni hiyo ya SADC ina jumala ya wajumbe 97 ambapo miongoni mwao 52 ni waangalizi wa uchaguzi ambao watasambazwa kwenye majimbo 11 ya uchaguzi nchini Msumbiji ambayo ni Cabo Delgado, Nampula, Niassa, Maputo City, Maputo, Tete, Gaza, Inhambane, Sofala, Manica na Zambezia.

Waangalizi hao wanatoka katika Nchi 10 ambazo ni wanachama wa SADC. Nchi hizo ni Tanzania, Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Eswatini, Malawi, Namibia, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe.


Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume akizindua rasmi Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi tarehe 03 Oktoba 2024 katika hafla iliyofanyika jijini Maputo. Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge nchini Msumbiji unatarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024

Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume akizindua rasmi Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi tarehe 03 Oktoba 2024 katika hafla iliyofanyika jijini Maputo. Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge nchini Msumbiji unatarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024

Mkurugenzi wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama , Prof. Kula Ishmael Theletsane akizungumza wakati wa uzinduzi wa  Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC nchini Msumbiji. Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge nchini humo unatarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024
Mjumbe wa Troika ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa akichangia jambo wakati wa uzinduzi wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC nchini Msumbiji. Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge nchini humo unatarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024

Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume akizungumza na na Waangalizi 52 wa SADC kwa lengo la kuwaaga kabla ya kusambazwa katika majimbo 11 ya uchaguzi nchini Msumbiji kwa ajili ya kuangalia uchaguzi. Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge nchini Msumbiji unatarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024

Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Mhe. Phaustine Kasike akishiriki hala ya uzinduzi wa 
Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC nchini Msumbiji. Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge nchini humo unatarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024
Mjumbe wa Troika ambaye pia ni Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala ya Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Sofia Mjema akishiriki hafla ya uzinduzi wa
Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC nchini Msumbiji. Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge nchini humo unatarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024
Mjumbe wa Troika ambaye ni Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri akifuatilia uzinduzi wa 
Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC nchini Msumbiji. Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge nchini humo unatarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024
Sehemu ya Waangalizi wa Uchaguzi wa SADC wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa
Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC nchini Msumbiji. Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge nchini humo unatarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024

Sehemu nyingine ya waangalizi
Waangalizi wa Uchaguzi wa SADC nchini Msumbiji wakishiriki uzinduzi wa 
Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC nchini Msumbiji. Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge nchini humo unatarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024
Sehemu nyingine ya waangalizi wa uchaguzi 
Meza kuu katika picha ya pamoj
Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Msumbiji walioshiriki hafla ya uzinduzi wa misheni hiyo
Picha ya pamoja ya kundi la waangalizi wa uchaguzi
Picha ya pamoja ya waangalizi wa uchaguzi

Wageni waalikwa wakifuatilia uzinduzi

Tuesday, October 1, 2024

NAIBU WAZIRI LONDO AWAPONGEZA NJE – SPORTS KWA KUFANYA VIZURI SHIMIWI


 NAIBU WAZIRI LONDO AWAPONGEZA NJE – SPORTS KWA KUFANYA VIZURI SHIMIWI

 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo amewapongeza wanamichezo wa timu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje - Sports), kwa kufanya vizuri katika michezo ya SHIMIWI inayoendelea mjini Morogoro.

Mhe. Londo amezipongeza Timu ya Mpira wa miguu wanaume kwa kuingia Nusu fainali , Timu ya Kamba wanawake na Timu ya Mpira wa pete kwa kuingia 16 Bora ya michuano ya SHIMIWI yanayoendelea Mkoani Morogoro

 Mhe. Londo ametoa pongezi hizo tarehe 30 Septemba, 2024 alipokutana na wachezaji wa Nje – Sports katika hafla ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa ajili yao mjini Morogoro. 

Hafla hiyo imefanyika maalum kuwapa hamasa wachezaji ili waendelee kufanya vizuri kwenye michuano hiyo. 

Katika hafla hiyo Mhe. Londo alifikisha salam za Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Thabit Kombo ambaye aliwataka wachezaji hao waendelee kupambana hadi mwisho.

 “Nilimweleza Mhe. Waziri kuwa naenda Mikumi lakini nitarudi jioni kwa ajili ya chakula cha jioni na Ninyi. amefurahia na ameniambia niwaletee salamu za upendo na kusema kwamba yupo pamoja na ninyi na muendelee kupambana hadi mwisho na anawatakia kila la kheri” Amesema Mhe. Londo

 Naye Mwenyekiti wa Michezo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Ismail Abdallah, ameupongeza na kuushukuru uongozi wa Wizara kwa namna wanavyo wapa miongozo na namna wanavyo wapa hamasa ambayo imekuwa chachu ya wao kufanya vizuri kwenye michezo hiyo.  

Pia amempongeza Naibu Waziri Mhe. Londo kwa kufika uwanjani kujionea pamoja na kuzungumza na wachezaji kitu kilichowapa hamasa kubwa wachezaji na kupelekea kufanya vizuri kwenye mchezo wao.

 “Mafanikio haya Mheshimiwa yamechagizwa sana na kitendo ulichokifanya juzi, kitendo cha kutenga muda wako na kuja kututembelea na hukuja kambini bali umekuja Uwanjani, kwakweli toka tumefika hapa sidhani kama kuna Timu Waziri wao amekuja kuwatembelea kama ulivyo fanya, kwakweli umetujengea hamasa kubwa, heshima kubwa mpaka tumeonekana Watoto pendwa sijui nitumie neno gani lakini tumeonekana wakipekee. Tunashukuru sana” Amesema Bwa. Ismail

 Nje – Sports inatarajia kuingia dimbani hapo kesho kwa Mchezo wa Nusu Fainal dhidi ya mpinzani Wake Wizard ya Maji.


Monday, September 30, 2024

NJE - SPORTS YAICHAPA MIFUGO KWA PENATI 6-5


.Yaifundisha mifugo diplomasia ya michezo 

. Yatinga nusu fainali 

Timu ya Soka ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje - Sports), yaichapa Timu ya Mifugo kwa penati 6-5 katika mchezo wa nusu fainali ya michezo ya Shimiwi inayofanyika mjini Morogoro.

Hadi dakika 90 zinakamilika timu hizo zilikuwa zimefungana goli    1 – 1 na kulazimika kupigiana mikwaju ya penati.

Katika kupigiana mikwaju ya penati, Nje Sports ilitumia umahiri wake wa Diplomasia ya Michezo kupachika kimiani mikwaju Sita bila kumjeruhi Mlinda Mlango wa timu ya Mifugo Bwana NKANA ambapo Mlinda Mlango wa Nje – Sports Bw. Deusi Benedictor alipangua mikwaju miwili ya penati kwa Ustadi wa hali ya juu na kuisukuma nje ya mashindano kwa kishindo Timu ya Mifugo.

 Mwenyeki wa Michezo wa Wizara na team ya Nje – Sports Bwa. Ismail  H.Abdallah alionekana kuwa na furaha  baada ya Timu ya Wizara ya Mambo ya Nje kuibuka na Ushindi huo.

 “Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata Ushindi ambao tulikuwa tunatamani,  nashukuru timu imepambana, ahadi tuliyo muahidi Katibu Mkuu tumeitimiza kwa kuingia Nusu fainali”, alisema Bw. Ismail.

Bw. Ismail ametoa rai kwa wanamichezo wa Nje Sports  kujituma na kujitoa kwani kupitia michezo hiyo wanaonesha Diplomasia ya Michezo pia kuionesha jamii kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Afrika Mashariki inafanya vizuri pia kwenye anga za michezo.

Aidha, Kocha  Maganga na wachezaji wake wametoa pongezi kwa Katibu Mkuu kwa namna alivyowapa hamasa iliyopelekea kufanya vizuri kwenye michezo hiyo ya Shimiwi.

Kocha huyo wa Nje sports amewaalika viongozi wa Wizara kwenda kuiona Timu yao itakaposhuka kwenye mchezo wa Nusu Fainali utakaofanyi baada ya ratiba kutolewa.

 

Friday, September 27, 2024

NJE – SPORTS YAONESHA DIPLOMASIA YA MICHEZO INAVYOTEKELEZWA KWA VITENDO DHIDI YA TAKUKURU

Leo tarehe 27 Septemba, 2024 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo amefika na kujionea Mtanange kati ya Timu ya Nje Sports wanaume na vijana wa kupambana na Kuzuia rushwa TAKUKURU, ambapo kandanda safi na lenye kuonesha namna Diplomasia ya Michezo inavyotekeleswa na Nje– Sports, inayoshiriki kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) inayoendelea Mkoani Morogoro.

Nje – Sports Wanaume pamoja na kuonyesha kabumbu safi mbele ya Mhe. Londo iliadhibu bila huruma Timu ya Takukuru kwa Mikwaju ya Penati baada ya dakika 90 kuisha bila kufungana. Nje – Sport ilifanikiwa kuweka kimiani Penati 7  dhidi ya 6 za Mpinzani wake Takukuru, Wazee wa Kupambana na Kuzuia Rushwa. Kwa matokea Hayo Nje – Sports wanaume wamesonga mbele na kuingia 8 Bora.

Matokeo mengine kwa Upande wa Nje - Sports Kamba wanawake iliyokuwa imekabiliwa na Majuruhi ya wachezaji wake muhimu haikuweza kufua Dafu dhidi ya Timu ya Uchukuzi Wanawake. 

Kunako Mpira wa Netiboli mchezo uliokuwa na mbwembwe zilizo vuta hisia za mashabiki na wapenzi wengi wa mchezo wa Netboli, Nje – Sports wanawake waliokuwa wakipasiana mpira kwa kasi kitu ambacho kiliwashtua wapinzani wake Timu ya Bunge kucheza kwa tahadhari kubwa kitu ambacho kiliwasaidia kuibuka na Ushindi. Nje – Sports walipoteza kwa kufungwa goli 49 – 35.     

Awali, Mhe. Londo alipata fursa ya kuzungumza na wanamichezo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, (Nje - Sports) na kuwaeleza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Thabit Kombo amemtuma kuwafikishia salamu zake na kueleza kuwa alitamani sana kuja kujionea namna wanavyo tekeleza Diplomasia ya Michezo kwa vitendo katika Mashindano ya SHIMIWI, hata hivyo anafurahishwa kwa namna Nje – sports inavyo fanya vizuri katika mashindano hayo ukizingatia na yeye pia ni mdau mzuri wa michezo. 

“Kwanza nimekuja kutoa salamu za Mhe. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Thabit Kombo, kwa vijana wake wa Wizara ya Mambo ya Nje wanaoshiriki michezo hapa yeye Waziri yupo Nje ya Nchi lakini amenituma kuja kuwasilisha Salamu zake za Upendo kwa Vijana wake, pia amewataka vijana wake wawakilishe Wizara katika Michezo hii na kuwa Mfano wa Kuigwa na Wizara na Taasisi nyingine za Serikali.” Amesema Mhe. Londo.

Aidha, Mhe. Londo ametoa rai kwa wanamichezo wote wanaoshiriki Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) kwa kutumia msemo wa walatini wenye maana ya “Akili safi inakaa kwenye Mwili Safi”, ambapo alieleza kuwa mwili safi ni pamoja kufanya mazoezi, pia mwili safi hutokana na michezo, hivyo ili mtu uwe na akili safi lazima uushughulishe mwili, na kushughulisha mwili kuna jenga Afya ya mtu na kujikinga na maradhi pamoja na kujenga mahusiano chanya kwa jamii nzima inayomzunguka.

Kwa Upande wa Mwenyekiti wa Michezo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Ismail Abdallah, alitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri Londo kwa kufika na kuzungumza na wachezaji. 

“Mhe. Naibu Waziri Tunashukuru sana kwa kutenga muda na kuweza kufika, tunatambua kuwa unaratiba ngumu za shughuli za kitaifa, ujio wako unawafanya wanamichezo kupata hamasa ya kufanya vizuri zaidi kwenye mashindano ya SHIMIWI” Amesema Bw. Ismail Abdallah

Pamoja na Mambo mengine, Mhe. Naibu Waziri Mhe. Denis Londo amepanga kukutana na Wanamichezo wote wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Nje – Sports kwa ajili ya kupata nao chakula cha pamoja na kubadilishana nao uzoefu kwenye maswala ya michezo katika kuimarisha Diplomasia ya Michezo.


Thursday, September 26, 2024

NAIBU WAZIRI CHUMI AKUTANA NA NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA OMAN JIJINI DODOMA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshulikia masuala ya Utawala na Fedha Mhe. Khalid Hashil Al Muslahi, yaliyofanyika jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi amekutana na kuzungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia Utawala na Fedha Mhe. Khalid Hashil Al Muslahi Ofisini kwake jijini Dodoma. 

Katika mazungumzo yao Mhe. Chumi amemhakikishia Mhe. Al Muslahi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Oman katika kukuza uhusiano wa kihistoria uliopo kwa manufaa na maslahi ya pamoja kati ya nchi hizo na watu wake.

Mhe. Chumi pia ameishukuru Serikali ya Oman kwa uamuzi wa kuiunga mkono Serikali ya Tanzania kwa kuamua kujenga Ubalozi na Kituo cha Utamaduni jijini Dodoma ambapo waliongozana na Naibu Waziri Chumi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi. Rosemary Senyamule kutembelea viwanja hivyo, ambavyo Tanzania iliipatia serikali ya Oman kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya ubalozi na makazi vilivyopo katika mji wa Serikali Mtumba, na mradi wa kihistoria wa ujenzi wa Kituo cha Utamaduni cha Oman jijini Dodoma.

Mhe. Chumi amemhakikishia Mhe. Al Muslahi kuwa Tanzania itashiriki Kongamano la Uwekezaji na Biashara la Oman litakalofanyika tarehe 26 hadi 28 Septemba 2024 Muscat, Oman ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji na Oman. Ameongeza kuwa Ujumbe wa Tanzania utaongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Sharriff Ali Shariff.

Tanzania na Oman zinashirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji na utalii ambapo Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Oman mwaka huu unatimiza miaka 54 tangu kuanzishwa kwake na kuufanya uhusiano huo wa muda mrefu wa karibu na kirafiki kuendelea kuimarika zaidi.

Kwa mujibu wa TIC kuanzia mwaka 1997 hadi 2023, miradi 66 yenye thamani ya jumla ya Dola za Kimarekani milioni 352.6 imesajiliwa Tanzania Bara, huku Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) inaonesha kuwa kuanzia mwaka 1999 hadi 2023, Oman imewekeza miradi 23 Zanzibar yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 1.2.

Aidha, Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaonyesha kuwa mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenda nchini Oman yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 14.6 mwaka 2022 hadi kufikia Dola milioni 16.4 mwaka 2023 na uagizaji wa bidhaa kutoka Oman umepungua kutoka Dola za Kimarekani milioni 207.9 mwaka 2022 hadi Dola milioni 100.1 mwaka 2023.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia masuala ya Utawala na Fedha Mhe. Khalid Hashil Al Muslahi akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi, jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Mhe. Khalid Hashil Al Muslahi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule na Balozi wa Oman nchini Tanzania Mhe. Saud Al Sidhani wakifurahia jambo walipotembelea eneo litakalojengwa Ubalozi wa Oman katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akelezea jambo kwenye ramani ya Mji wa Serikali Mtumba walipotembelea kiwanja cha Ubalozi wa Oman, jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Mhe. Khalid Hashil Al Muslahi na ujumbe wao wakiwa katika mazungumzo jijini Dodoma.

NJE – SPORTS YAPONGEZWA NA UONGOZI NA MENEJIMENTI YA WIZARA


Timu ya michezo ya Wizara ya Mambo ya. Je na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje Sports Club) imepongezwa kwa kuendelea kufanya vizuri katika michuano ya 38 Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) inayoendelea Mkoani Morogoro.

Pongezi hizo zimewasilishwa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu (ADA) Bw. Kawina Kawina alipotembelea na kuzungumza na wachezaji wa timu hiyo walioweka kambi kwenye milima ya Uluguru.

 Katika mazungumzo na wachezaji hao Bw. Kawina kwa niaba ya Uongozi na Menejimenti ya Wizara amewapongeza wachezaji kwa kuendelea kufanya vizuri katika michezo ya SHIMIWI na kuwahakikishia kuwa wizara ipo pamoja nao kwenye kila hatua wanayopiga katika michezo hiyo.

 “Uongozi na Menejimenti ya Wizara umekuwa ukipata taarifa kupitia Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali (GCU), kuwa Nje – Sports inafanya vizuri kwenye michezo ya SHIMIWI inayoendelea hapa Mkoani Morogoro,” alisema Bw. Kawina.

 Aliongeza kuwa, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo anamatumaini makubwa na na timu hiyo na matarajio ya Wizara ni kuwa wataibuka na ushindi na kurejea na Vikombe.

 Bw. Kawina pia amewapongeza wanamichezo wote kwa kuendelea kuwa waadilifu na kuonyesha nidhamu huku wakizingatia Kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma wakati huu wa Michezo ya SHIMIWI na kuwa chachu ya kuzifikisha Timu zote tatu za Nje Sports katika hatua ya 16 Bora.

Akizungumza katika kikao hicho na Mkurugenzi Kawina  Kapteni wa Mpira wa Miguu Bw. Mikidadi Magola ameishukuru Wizara kwa namna inavyokabiliana na changamoto zinazoikabili  timu ya Nje  na kuiwezesha Timu kupata vifaa vyote vya mühimu kwa timu hiyo  ambavyo vimekuwa chachu ya kufanya vizuri kwenye michezo ya SHIMIWI mwaka huu.


Wednesday, September 25, 2024

NAIBU WAZIRI CHUMI NA BALOZI WA JAPAN WAKUTANA JIJINI DODOMA


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisalimiana na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa walipo akutana kwa mazungumzo jijini Dodoma.

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi amekutana na Balozi wa Japan nchini Mhe. Yasushi Misawa aliyemtembelea ofisini kwake Jijini Dodoma. 

Katika mazungumzo yao viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Japan kwa manufaa ya pande zote.

Mhe. Chumi aliishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania kupitia sekta mbalimbali na hivyo kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mhe. Chumi pia amemhakikishia Mhe. Balozi Misawa kuwa Tanzania inajali na kuthamini uhusiano wake na Japan na kumuahidi kuwa Mamlaka ya Biashara Nje (Tantrade) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Japan wanaendelea na maandalizi ya kushiriki katika maonesho ya Kimataifa ya Biashara yatakayofanyika Osaka nchini Japan mwaka 2025.

Naye Balozi wa Japan Mhe. Misawa ameelezea utayari wa nchi yake kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa manufaa ya pande zote mbili.

Pia ameshukuru Ushirikiano anaoupata kutoka Serikali ya Tanzania na hivyo kumuwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Tanzania na Japan zinashirikiana kupitia sekta za biashara na uwekezaji, miundombinu, afya na masuala ya kodi.
Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi yaliyofanyika jijini Dodoma. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mazungumzo yakiendelea

Tuesday, September 24, 2024

NJE – SPORTS WANAUME YAFUZU HATUA YA MAKUNDI 16 BORA MICHEZO YA SHIMIWI


Timu ya Mpira wa Miguu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje– Sports) Wanaume imefuzu kuingia hatua ya makundi 16 Bora kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) baada ya kuifunga Timu ya Wizara ya Kilimo na kutoka Sare (0 - 0) na Timu ya Ujenzi.

Timu hiyo ikiwa imevalia jezi nadhifu zilizopendezeshwa kwa rangi ya njano na buluu, yenye kuvutia machoni mwa mashabiki waliojitokeza kuutazama mtanange wa kukata na shoka kati ya timu hiyo na Timu ya Ujenzi uliochezwa katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro (Mji kasoro Bahari) majira ya saa tatu asubuhi ya tarehe  24 Septemba 2024, ilijituma kikamilifu hadi kutoka sare ya 0-0 na timu hiyo hatua iliyofanikisha timu ya Nje kusonga mbele hatua ya makundi.

Akizungumza kwa njia ya simu ili kuwapa hamasa wachezaji hao, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Chiku Keguhe amewapongeza wachezaji wote wa Nje – Sports kwa kuingia 16 Bora, na kuwakumbusha kuwa Wizara ipo pamoja nao hatua kwa hatua. 

“Nawapongeza kwa kufuzu kuingia 16 bora, mmeiheshimisha Wizara na hii ndio maana sahihi ya Diplomasia ya Michezo. Pongezi kwenu wachezaji kwa kuendelea kupambana na kuhakikisha mnachukua ushindi. Tusisahau matarajio ya Viongozi na Menejimenti ya Wizara ni kupata Vikombe” amesema Bi. Chiku Keguhe.

Akizungumza mara baada ya kufuzu hatua hiyo,  Kocha wa Nje – Sports,  Bw. Shabani Maganga amewapongeza wachezaji wake kwa kuendelea kuonesha mchezo mzuri unaoakisi Diplomasia ya Michezo na kuwasihi kuendelea kupambana na kuhakikisha wanafika fainali.

Nje Sports wanaume imeendelea kupata matokeo mazuri na kuifanya kuwa nafasi ya pili kwenye kundi H, huku wachezaji wake wakiendelea kujifua kikamilifu kwq lengo la kuchukua ushindi wa SHIMIWI kwa mwaka 2024–2025.

Ikumbukwe kuwa, mbali na mpira wa miguu, Timu ya Nje–Sports pia inashiriki Mchezo wa Kamba kwa Wanawake na  Netiboli ambayo yote imeingia kwenye hatua ya makundi 16 bora.

Timu zote za Nje–Sports zitaendelea na mazoezi mepesi huku zikisubiri ratiba ya mchezo wa makundi unaotarajiwa kutolewa na viongozi wa Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI).


Waziri Kombo ashiriki kwenye Mkutano wa Nchi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth Foreign Affairs Ministers Meeting - CFAMM)



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Thabit Kombo (Mb.) ameshiriki kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth Foreign Affairs Ministers Meeting - CFAMM) uliofanyika pembezoni mwa Kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79) tarehe 23 Septemba, katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York. 

 

Kikao hicho kilicho hudhuriwa na Mawaziri kutoka nchi 56 za Jumuiya ya Madola kilijadili ajenda mbalimbali, zikiwemo taarifa ya utekelezaji wa maelekezo ya Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Nchi za Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliofanyika mwaka 2022, Kigali, Rwanda na taarifa ya maandalizi ya Mkutano ujao wa CHOGM, utakaofanyika mwezi Oktoba 2024, Apia, Samoa.
 

Monday, September 23, 2024

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshiriki Mkutano wa ngazi ya juu wa Wakuu wa Nchi na Serikali ‘Summit of the Future’



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Septemba 22, 2024 ameshiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa ngazi ya juu wa Wakuu wa Nchi na Serikali ‘Summit of the Future’ uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Umoja wa Mataifa New York nchini Marekani.

Mkutano huo unawakutanisha viongozi wa nchi na Serikali duniani ili kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo na namna wanaweza kuboresha hali ya sasa na kuzilinda siku zijazo.

Katika Mkutano huo, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliambatana na viongozi waandamizi wa Serikali wakiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Hussein Kattanga.

Mheshimiwa Majaliwa yupo nchini Marekani kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79).