Thursday, January 25, 2024

RAIS SAMIA AFUNGUA KONGAMANO LA UWEKEZAJI NA BIASHARA KATI YA TANZANIA –INDONESIA

 












 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefungua Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Indonesia na kuwaambia wafanyabiashara na wawekezaji wa Indonesia sababu tano zinazowafanya waje Tanzania kuwekeza mitaji yao.

 

Akifungua Kongamano hilo, lililofanyika jijini Jakarta tarehe 25 Januari, 2025 Mhe. Rais Samia amewaeleza wawekezaji kutoka Indonesia sababu tano zinazoifanya Tanzania kuwa kituo bora cha kuwekeza mitaji yao.

Ametaja sababu ya kwanza kuwa ni amani na utulivu uliopo nchini na Serikali inayofuata utawala bora, sababu nyingine ni sehemu ilipo Tanzania kijiografia kwa kuzungukwa na nchi ambazo hazina bandari na hivyo kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma kwenda katika nchi hizo.

Ametaja sababu nyingine kuwa ni kuwepo kwa fursa za kutengeneza bidhaa na kupata masoko kutokana na Tanzania kuwa mwanachama wa Jumuiya za Kikanda kama EAC, SADC na Soko Huru la Pamoja la AfCFTA ambalo linahusisha watu zaidi ya bilioni 1.2 hali ambayo itawezesha wafanyabiashara wa Indonesia kuwafikia watu hao kupitia soko hilo.

 

Sababu nyingine ni Tanzania kuwa na mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuridhia sheria na mikataba ya kimataifa inayolinda mitaji na uwekezaji wa kigeni na nia thabiti ya kisiasa ya Serikali kutambua sekta binafsi kama injini ya maendeleo ya kiuchumi na kuweka msimamo wa kusaidia biashara na wafanyabiashara kukua.

 

“Uchumi mdogo na imara wa Tanzania ni himilivu, uchumi huo umeweza kuibuka baada ya janga la UVIKO 19. Uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kwa kasi baada ya kuisha kwa janga hilo, Tanzania ni miongoni mwa nchi 20 ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi baada ya kuisha kwa janga la UVIKO 19, hii inaifanya Tanzania kuwa mahali pazuri kwa uwekezaji, niwaambie majadiliano na nchi kama Indonesia yanadhihirisha azma ya Tanzania ya kujenga mazingira mazuri na bora kwa uwekezaji”, alisema Mhe. Rais Samia.

 

Katika kongamano Hati tatu za makaubaliano zilizosainiwa kati ya taasisi za Tanzania na taasisi za Indonesia zilitajwa. Hati hizo ni Makubaliano kati ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) na PT Perusahaan Perdagangan Indonesia yenye lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya Mamlaka zinazosimamia Biashara Tanzania na Indonesia hivyo, kutengeneza umahili katika masoko na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kati ya Tanzania na Indonesia.

 

Hati nyingine ni Makubaliano kati ya Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo ya Tanzania, Chemba ya Taifa ya Biashara ya Zanzibar na Chemba ya Biashara na Viwanda ya Indonesia ikilenga kukuza na kuwezesha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara ili kuondoa vikwazo vya kibiashara kati ya Tanzania na Indonesia.

 

Hati ya tatu ni Makubaliano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo cha Teknolojia cha Bangung yenye lengo la kuwezesha kufanyika kwa tafiti za pamoja za kitaaluma katika masuala mbalimbali, kutoa  fursa za kujengeana uwezo na fursa za masomo ya elimu ya juu kutoka Serikali ya Indonesia.

 

Rais Samia amesema kuwa kusainiwa kwa hati hizo kunalenga kuchochea kasi mpya katika sekta ya biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Indonesia kwani biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi bado ni muhimu.

MAKAMU WA RAIS WA CUBA AHITIMISHA ZIARA YAKE NCHINI


Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa amemaliza ziara ya kikazi ya siku tatu nchini aliyoifanya kuanzia tarehe 23 hadi 25 Januari, 2025.

 

Akiwa nchini, Mhe. Mesa alikutana kwa mazungumzo na Mwenyeji wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango.

 

Katika mazungumzo yao, Viongozi hao walikubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria baina ya Tanzania na Cuba hususan kwenye maeneo ya kimkakati ya kilimo, afya, teknolojia na elimu.

 

Vilevile viongozi hao walishuhudia utiaji saini wa Hati mbili za Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Chuo Kikuu cha Artimesa Diaz Gonzalez cha Cuba. 

 

Hati ya pili ya Makubaliano iliyosainiwa ilihusu ushirikiano  kati ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania(TMDA) na Kituo cha Afya cha Taifa cha Udhibiti na Vifaa Tiba (CECMED) cha Serikali ya Cuba kwa lengo la kupanua wigo na kuongeza matumizi ya teknolojia katika masuala ya dawa na vifaa tiba.

 

Mhe. Mesa pia alitembelea Taasisi ya Mwalimu Nyerere ya jijini Dar es Salaam pamoja na kutembelea Kiwanda cha Viuadudu cha Biotech kilichopo Kibaha, Pwani.

 

Mhe. Mesa pia alipata nafasi ya kumtembelea Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere kwenye makazi yake jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumsalimia na kumjulia hali.

Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa akiagana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki mara baada ya kukamilisha ziara yake ya siku tatu nchini aliyoianza tarehe 23 hadi 25 Januari, 2024. Akiwa nchini, pamoja na mambo mengine Mhe. Mesa alikutana kwa mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango pamoja na kutembelea taasisi mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Mwalimu Nyerere. Katikati anayeshuhudia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk
Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa akiagana na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole mara baada ya kukamilisha ziara yake ya siku tatu nchini aliyoianza tarehe 23 hadi 25 Januari, 2024. Wengine wanaoshuhudia ni Naibu Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa (wa kwanza kulia) akifuatiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme
Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa akiagana na Maafisa wa Ubalozi wa Cuba nchini  mara baada ya kukamilisha ziara yake ya siku tatu nchini aliyoianza tarehe 23 hadi 25 Januari, 2024.
Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa akiagana na wadau mbalimbali
Mhe. Kairuki akibadilishana mawazo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk wakati wa hafla ya kumuaga Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa 
Vikundi vya ngoma vikitumbuiza wakati wa hafla ya kumuaga Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa mara baada ya kukamilisha ziara yake ya siku tatu nchini aliyoianza tarehe 23 hadi 25 Januari, 2024.
Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu akiagana na Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa  mara baada ya kukamilisha ziara yake ya siku tatu nchini aliyoianza tarehe 23 hadi 25 Januari, 2024.
Mawaziri wakimpungia mkono wa kwaheri Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Mesa  mara baada ya kukamilisha ziara yake ya siku tatu nchini aliyoianza tarehe 23 hadi 25 Januari, 2024.

 

RAIS DKT. SAMIA APOKELEWA RASMI INDONESIA, HATI SABA ZASAINIWA












Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Samia Suluhu Hassan amepokelewa rasmi katika Ikulu ya Bogor jijini Jakarta na mwenyeji wake Mhe. Joko Widodo baada ya kuwasili nchini Indonesia kwa ziara ya siku tatu ya Kitaifa iliyoanza tarehe 24 hadi 26 Januari, 2024.

Akipokelewa katika Ikulu ya Bogor na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Indonesia Mhe. Joko Widodo,  Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alikagua gwaride maalum lililoandaliwa kwa heshima yake na kupigiwa mizinga 21.

Baada ya tukio hilo Mhe. Rais Samia na mwenyeji wake walielekea sehemu iliyoandaliwa katika viwanja vya Ikulu ya Bogor jijini Jakarta kwa ajili ya kupanda mti wa kumbukumbu ya ziara yake nchini humo.

Rais Samia Suluhu Hassan na mwenyeji wake Mhe. Joko Widodo walipata wasaa wa kuzungumza katika Ikulu hiyo na baadaye walizungumza na Waandishi wa Habari kuelezea mazungumzo yao kwa ufupi na mambo waliyokubaliana kuyatekeleza.

Ziara hiyo ya kitaifa imeshuhudia Indonesia na Tanzania zikisaini Hati SABA za makubaliano na barua ya kusudio moja. Hati hizo ni Makubaliano Kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Indonesia kuhusu Ushirikiano katika Nyanja ya Uchumi wa Buluu. Hati hii ina lengo la kukuza biashara zitokanazo na shughuli za majini kama kuwezesha masoko ya samaki.

Hati ya pili ni Makubaliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Indonesia kuhusu Ushirikiano katika Sekta ya Kilimo. Hati hii inalengo la kuongeza uwezo wa Taasisi za Kilimo hivyo kuimarisha ushirikiano  katika kutengeneza masoko ya bidhaa za kilimo.

Hati ya tatu ni Makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Indonesia kuhusu Ushirikiano katika Sekta ya Madini. Hati hii ina lengo la kuwezesha tafiti za madini na uchakataji wa uongezaji thamani ya madini ya vito.

Hati ya nne ni Makubaliano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje Indonesia kuhusu Ushirikiano wa Kujengeana Uwezo katika Masuala ya Kidiplomasia. Hati hii inatarajiwa kutekelezwa kupitia Vyuo vya Diplomasia vya nchi mbili hizi ikiwa na lengo la kuanzisha ushirikiano katika masuala ya Utafiti na kitaaluma, kubadilishana utaalamu katika mafunzo ya kidiplomasia na utafiti katika nyanja za uhusiano wa kimataifa na lugha.

Pia Barua ya Kusudio kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Indonesia kuhusu kukuza na kuwezesha Uwekezaji. 

 
Barua hiyo ina lengo la kuweka mazingira mazuri ya kiuwekezaji baina ya nchi mbili ili kuongeza kiwanjo cha uwekezaji kati ya Tanznaia na Indonesia. Barua hiyo imesainiwa kama sehemu ya kuonesha nia ya Serikali za nchi hizi mbili kuingia katika mkataba wa kukuza na kulinda Uwekezaji.

Mhe. Rais Samia yuko nchini Indonesia kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia tarehe 24-26 Januari 2024 kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake Rais wa Indonesia Mhe. Joko Widodo ambaye alitembelea Tanzania mwezi Agosti,2023.

Wednesday, January 24, 2024

MAKAMU WA RAIS WA CUBA ATEMBELEA KIWANDA CHA VIUADUDU CHA KIBAHA

Makamu  Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Valdes Mesa amesema Serikali ya Cuba itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha  kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha  mkoani Pwani ili kiendelee kuhudumia Watanzania na nchi nyingine za Afrika.


Mhe. Mesa ametoa kauli hiyo leo tarehe 24 Januari 2024 alipotembelea Kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 23 hadi 25 Januari 2024.


Amesema nchi yake itaendelea kutoa msaada wa kitaalam kwa mamlaka za Tanzania ili kukiwezesha kiwanda hicho kuzalisha bidhaa tofautitouti mbali na viuadudu vya malaria,  zikiwemo mbolea, viuatilifu na bidhaa nyingine za kilimo


Pia amesema kiwanda hicho kitaendelea kuwa mfano wa ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Cuba katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya.


“Nimepata bahati ya kukitembelea kiwanda hiki kwa mara ya pili sasa, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2016 wakati kinakamilishwa. Napongeza hatua iliyofikiwa kwenye uzalishaji” amesema Mhe. Mesa.



Amesema kiwanda hicho kinatakiwa kutunzwa kwani ni chanzo cha ajira kwa watanzania lakini pia kinakuza uchumi wa Tanzania pamoja na kuimarisha afya za watanzania.


Awali akizungumza kumkaribisha Mhe. Mesa katika kiwanda hicho, Mkuu wa Mkoa wa Pwani , Mhe. Abubakar Kunenge amesema kuwa anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhamasisha uwekezaji wa viwanda kwenye mkoa huo na kuwakaribisha wawekezaji zaidi kutoka Cuba kuja kuwekeza.


Miongoni mwa Viongozi wengine walioshiriki ziara ya Mhe. Mesa kwenye kiwanda hicho ni Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki, Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne Vera. 

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akimpokea Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa mara baada ya kuwasili katika kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani. Mhe. Mesa yupo nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 23 hadi 25 Januari 2024
Mhe. Mesa akiwa amepokelewa na Mhe. Dkt. Kijaji mara baada ya kuwasili kwenye kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Mhe. Dkt. Kijaji akitoa taarifa fupi kwa Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Mesa baada ya kuwasili kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Mhe. Meda akizungumza alipokitembelea kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani. Kiwanda hicho kimejengwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge akizungumza wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Mesa alipotembelea kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani.
Meza kuu
Waziri wa maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki akifuatilia hotuba ya Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Mesa alipotembelea kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani.


Viongozi na wageni waalikwa kutoka Mkoa wa Pwani walioshiriki ziara ya Makamu wa Rais wa Cuba alipotembelea kiwanda cha kuzalisha Viuadudu vya kuua Viluwiluwi vya Mbu wanaoeneza Malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Mkutano ukiendelea

 

WAZIRI MAKAMBA ATETA NA WATUMISHI UBALOZI WA JAKARTA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akikaribishwa na Mtumishi wa Ubalozi Bw. Suleiman ......alipowasili katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumishi .

Balozi wa Tanzania nchini Indonesia Mhe. Makocha Tembele akimuwekea Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba kitabu cha wageni alipotembelea  Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumishi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumishi

 

Balozi wa Tanzania nchini Indonesia Mhe. Makocha Tembele akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba alipotembelea  Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumish
Mwakilishi wa watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Indonesia Bw. Suleiman .........akizungumza neno mbele ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba  alipotembelea  Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumishi


 

Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Indonesia wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba  alipotembelea  Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumishi hao

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba ametembelea Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Jakarta na kuzungumza na watumishi Ubalozini.

Akizungumza Ubalozini hapo Mhe. Makamba amewapongeza watumishi hao kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kuiwakilisha vyema Tanzania.

Aidha, amewasihi watumishi hao kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kuchapa kazi na kutimiza azma ya kuanzishwa Ubalozi huo na kufikia matarajio ya serikali kutoka kwao.

“Nyinyi ni wawakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Indonesia mna wajibu wa kuchapa kazi , kushirikiana na kuwa wamoja katika kushirikiana na  Indonesia na kufanya mambo yaende”, na kuongeza “mnatakiwa msiende kinyume na matarajio ambayo nchi inayo, nyinyi ni wawakilishi wa nchi kwa hiyo hulka, maneno, muonekano na vitendo vyenu lazima viakisi nchi yenu, na mhakikishe mnalilinda hilo,” alisisitiza Mhe. Waziri Makamba.

Alisema Tanzania inawategemea watumishi hao kuleta manufaa nyumbani kwa kuvutia biashara na wawekezaji na wadau wengine ambao watasaidia juhudi za kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.

Amesema ziara ya Mhe. Rais nchini Indonesia ni bahati kubwa  kwa ubalozi huo kwakuwa mwaka jana ulimleta Rais wa Indonesia Tanzania na safari hiii umemleta Mhe. Rais Indonesia, “wenzenu wanamaliza muda wao bila kupata nafasi kama hii, hili ni jambo la kujivunia na mjipongeze kwa kazi nzuri.

Akiwa Ubalozini hapo Waziri Makamba amempongeza Balozi wa Tanzania nchini Indonesia Mhe. Makocha Tembele kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ubalozini hapo.

“Tunajivunia sana uwezo wako Jakarta, uendelee kuchapa kazi na hatutachoka kukusaidia itakapobidi kufanya hivyo,” alisema

Amesema ziara hizo za wakuu wa nchi ni jitihada za kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Indonesia ambao mwaka huu unatimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.

Ameongeza kuwa ziara hiyo pia inalenga kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika maeneo ya kımkakati ya biashara, uwekezaji, afya, elimu, uchumi wa buluu na kilimo na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kwa faida ya pande zote mbili.

Mhe. Makamba yuko nchini Indonesia kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya Ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itakayofanyika nchini humo tarehe 24-26 Januari, 2024.



 

MAKAMU WA RAIS WA CUBA ATEMBELEA TAASISI YA MWALIMU NYERERE NA KUMJULIA HALI MAMA MARIA NYERERE

Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa ametembelea Makao Makuu ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere yaliyopo jijini Dar es Salaam na kuzungumza na Wafanyakazi wa Taasisi hiyo pamoja na Wajumbe wa Umoja wa Urafiki wa Tanzania na Cuba.


Mara baada ya kuwasili, Mhe. Mesa alipokelewa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Bw. Joseph Butiku pamoja na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi hiyo, Mhe. Stephen Wasira.


Pamoja na mambo mengine Mhe. Mesa alipokea taarifa kuhusu utendaji wa Taasisi hiyo isiyo ya Serikali ambayo ilianzishwa mwaka 1996 kwa lengo la kuhamasisha  amani, umoja na maendeleo ya watu pamoja na kuenzi mchango wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika utu na maendeleo ya watu pamoja na kutunza kumbukumbu mbalimbali za kazi zake ikiwemo vitabu, majarida, machapisho na picha.



Wakati huohuo, Mhe. Mesa amemtembelea, Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere kwenye makazi yake jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumsalimia na kumjulia hali.



Katika mazungumzo yao, Mhe. Mesa amemweleza Mama Maria kuwa amewiwa kumtembelea kama ishara ya kuenzi urafiki wa Tanzania na Cuba ulioasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Fidel Castro na mchango mkubwa wa Mwalimu Nyerere katika kujenga amani, umoja na mshikamano na kuwa mstari wa mbele kwenye harakati za ukombozi kusini mwa Afrika. Kadhalika amemtakia afya njema na maisha marefu Mama Maria.


Kwa upande wake Mama Maria amemshukuru Mhe. Mesa kwa kutenga muda na kumtembelea.


Mazungumzo kati yao yalihudhuriwa pia na Watoto wa Hayati Baba wa Taifa akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Makongoro Nyerere.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku akimpokea Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa alipotembelea Taasisi hiyo tarehe 24 Januari 2024. Mhe. Mesa alifanya ziara ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 23 hadi 25 Januari 2024

Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa akizungumza alipotembelea Taasisi ya Mwalimu Nyerere wakati wa ziara yake nchini
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku akimzawadia Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa vitabu na machapisho mbalimbali ya Hayati Mwalimu Nyerere alipotembelea Taasisi hiyo tarehe 24 Januari 2024.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku akizungumza wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa (kushoto) alipotembelea Taasisi hiyo tarehe 24 Januari 2024. Wengine katika picha ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (wa pili kushoto) na Balozi wa Tanzania nchini Cuba. Mhe. Humphrey Polepole.
Mhe. Mesa akiwa katika meza kuu na Mhe. Kairuki na Mhe. Polepole
Mkutano ukiendelea
Mkutano ukiendelea. Kulia ni Mhe. Stephen Wasira, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere na kushoto ni Prof. Shivji
Sehemu ya wanafunzi
Wageni waalikwa wakimsikiliza Mhe. Mesa
Mkutano ukiendelea


...............ZIARA YA MHE. MESA KWA MAMA MARIA NYERERE

Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa akisalimiana na Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere alipomtembelea kwenye makazi yake jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumsalimia na kumjulia hali. Mhe. Mesa yupo nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 23 hadi 25 Januari 2024
Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Makongoro Nyerere ambaye pia ni mtoto wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere alipowatembelea kwenye makazi yao jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumsalimia na kumjulia hali Mama Maria Nyerere. Mhe. Mesa yupo nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 23 hadi 25 Januari 2024
Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Mesa akizungumza na Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere alipomtembelea kwenye makazi yake jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumsalimia na kumjulia hali. Mhe. Mesa yupo nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 23 hadi 25 Januari 2024
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole pamoja na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Vera
Mhe. Mesa akiwa katika picha ya pamja na Mama Maria Nyerer alipomtembelea nyumbani kwake jijini Dar es Salaam
Mhe. Makongoro akiwa na Wanafamilia wengine wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Mesa alipowatembelea
Mhe. Makongoro akizungumza 
Picha ya pamoja kati Mhe. Mesa, Mama Maria Nyerere na wanafamilia wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere