Friday, May 11, 2018

Katibu Mkuu afanya mazungumzo na Balozi wa Ufaransa nchini

 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Balozi wa Ufaransa nchini Mhe. Frederic Clavier, alipomtembelea Wizarani tarehe 10 Mei,2018, Jijini Dar es Salaam,  mazungumzo hayo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ufaransa.

Akiongea katika mazungumzo hayo Katibu Mkuu alimshukuru Mhe. Clavier kwa ushirikiano huo hasa kwa kuwezesha ziara ya wafanyabiashara kutoka Ufaransa hapa nchini na kuendelea kusaidia miradi mbalimbali. 
Naye kwa upande wake Mhe. Clavier alisema anafurahishwa sana na kasi ya Maendeleo hapa nchini na wataendelea kumuunga mkono  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli katika juhudi zake za kujenga uchumi wa Viwanda,pia alisema ataendelea kushawishi wawekezaji wengi kuja hapa nchini na pia kuendelea kusaidia miradi mbalimbali hapa nchini.

 Mkutano ukiendelea, wanaofuatilia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ni Balozi Celestine Mushy(wa tatu kutoka kulia), anayefuata ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ulaya na Amerika, Bw. Jestus Nyamanga na wengine ni Maafisa kutoka Wizarani na Ubalozi wa Ufaransa.
Picha ya Pamoja baada ya mazungumzo

Thursday, May 10, 2018

Dkt, Mahiga akutana na Waziri Mkuu wa Israel

Waziri Mkuu wa Israel, Mhe. Benjamin Netanyahu (kulia) akimkaribisha ofisini kwake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga kwa ajili ya kufanya mazungumzo jijini Jerusalem, Israel leo.  Wawili hao walikubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, elimu, afya, utalii na uwekezaji.


Waziri Mkuu wa Israel, Mhe. Benjamin Netanyahu akiwa tayari kuanza mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga 

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ukiwa katika mazungumzo rasmi na Mhe. Netanyahu.
Pande mbili zikiwa katika mazungumzo.



Benki ya Exim ya India yaipatia Tanzania mkopo nafuu kusaidia sekta ya maji

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi Amina Kh. Shaaban kwa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Exim ya India, Bw. David Resquinha wakisaini kwa niaba ya Serikali zao Mkataba wa Mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika miji 23 ya Tanzania.
Bi. Shaaban na Bw. Resquinha wakibadilishana mkataba huo mara baada ya kusaini

Picha ya pamoja
=========================================================================

BENKI YA EXIM YA INDIA YAIPATIA SERIKALI YA TANZANIA MKOPO WA MASHARTI NAFUU KUSAIDIA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI KATIKA MIJI 23 YA TANZANIA

Serikali ya India kupitia Benki ya Exim imeipatia Serikali ya Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 500, sawa na shilingi Trilioni 1.14 za Tanzania, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika miji 23 ya Tanzania.

Hafla ya uwekaji saini wa mkataba huo imefanyika leo tarehe 10 Mei, 2018 mjini  New Delhi, India ambapo Bi. Amina Kh. Shaaban, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango na Bw. David Resquinha, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Exim walisaini kwa niaba  ya Serikali zao..

Miji  itakayonufaika na Fedha za mkopo huu ni Muheza, Makambako, Kayanga, Njombe, Manyoni, Songea, Sikonge, Chunya, Kasulu, Kilwa Masoko, Rujewa, Mugumu, Geita,  Makonde, Wangingómbe, Handeni , Singida mjini, Kiomboi, Mpanda, Chemba, Mafinga, Urambo-Kaliua pamoja na miji ya Zanzibar.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba, Naibu Katibu Mkuu, Bi. Amina Kh. Shaaban, amesema kuwa miradi hiyo ni muhimu kwa sababu itawezesha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika miji husika hivyo kusaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko yanayotokana na maji yasiyo salama.

Aidha, miradi itasaidia kufikiwa kwa malengo na mipango ya Taifa na Kimataifa ya Maendeleo ikiwemo: Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano awamu ya pili (FYDPII) , Mkakati wa Kukuza na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA III) na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDG’s).

Vilevile, amesema uamuzi wa Serikali wa kuboresha  huduma za maji umelenga kuwapunguzia Wananchi husususan Wanawake adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji, na hivyo kupata muda wa kutosha kufanya shughuli mbali mbali za maendeleo.

Katibu Mkuu afanya mazungumzo na Balozi wa Japan nchini

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Aldof Mkenda akisisitiza jambo katika mazungumzo na Balozi wa Japan nchini Mhe.Masaharn Yoshida alipomtembelea na ujumbe wake Wizarani tarehe 10 May,2018, Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine mazungumzo hayo yalijikita katika kuendelea kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na Japan. Aidha, alimsisitiza Balozi kwa nafasi yake kuendelea kuhamasisha wawekezaji kutoka Japan kuendelea kuwekeza hapa nchini, alimhakikishia ushirikiano kutoka Serikalini iwapo watakuja kuwekeza hapa nchini.

Mkurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan Idara inayosimamia masuala ya Afrika, Bi. Mariko Kaneko akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu katika mazungumzo hayo. Bi. Kaneko alisema Japan inafurahishwa na ukuaji wa haraka wa uchumi wa Tanzania hivyo nchi yake itaendelea kuiunga mkono Tanzania hasa kwa upande wa maendeleo ya Viwanda na miradi mbalimbali.


Mazungumzo yakiendelea


Dkt. Mahiga afanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Israel

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga akipeana mkono na Waziri wa Ulinzi wa Israel, Mhe. Avigdor Liberman walipokutana jijini Tel Aviv leo asubuhi kwa ajili ya kufanya mazungumzo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga na ujumbe wake (kulia) na Waziri wa Ulinzi wa Israel, Mhe. Avigdor Liberman na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo ambapo walijadili masuala mbalimbali ikiwemo kushirikiana katika masuala ya ulinzi na usalama.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga wa kwanza kulia na akifuatiwa na Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Job Masima na Afisa Dawati wa Israel, Bi Kisa Mwaseba wakiwa katika mazungumzo na ujumbe wa Israel.



Waziri wa Ulinzi wa Israel, Mhe. Avigdor Liberman wa kwanza kulia akisisitiza jambo kwenye mazungumzo hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (kulia) akikabidhi zawadi kwa Waziri wa Ulinzi wa Israel, Mhe. Avigdor Liberman walipokutana jijini Tel Aviv leo asubuhi.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga naye akipokea zawadi kutoka kwa Waziri wa Ulinzi wa Israel, Mhe. Avigdor Liberman jijini Tel Aviv leo asubuhi.

Kaimu Mkurugenzi wa Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Suleiman Salehe akisalimiana na Waziri wa Ulinzi wa Israaele, Mhe. Avigdor Liberman.

Waheshimiwa Mawaziri wakiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Job Masima wa kwanza kushoto  na Balozi wa Israel nchini Kenya ambaye anawakilisha pia Tanzania.

Yanayojiri katika ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje nchini Israel

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Dkt, Mahiga atembelea taasisi ya Save the Children Haert ya Israel

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ameshukuru Ushirikiano kati ya Taasisi ya Moyo ya Save the Children Heart ya Israel na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kuokoa maisha ya watu wengi nchini, hususan watoto.

Waziri Mahiga alitoa shukrani hizo leo alipoitembelea taasisi hiyo jijini Tel Aviv, Israel akiwa anaendelea na ziara yake ya siku tatu aliyoianza jana. "Zamani nilijua kuwa mtu akizaliwa na maradhi ya kurithi, mtu huyo hawezi kuishi lazima atakufa, lakini uwepo wa taasisi yenu kumenifanya niondoe itikadi hiyo" Dkt. Mahiga alisema.

Taasisi ya Moyo ya Save the Children Heart imeisifu Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kuwa ni moja ya Taasi bora kusini mwa Jangwa la Sahara na kwamba ina uwezo na wataalam wa kufanya upasuaji bila ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi. "Serikali inachotakiwa kufanya ni kuiboresha taasisi hiyo kwa kujenga majengo mapya na kuipatia vifaa zaidi na itakapofanya hivyo itaokoa maisha ya watu na fedha nyingi ambazo zingelitumika kugharamia matibabu nje ya nchi".  Mkurugenzi wa taasisi hiyo alishauri.

Mkurugenzi wa Taasisi hiyo alimweleza Dkt. Mahiga kuwa taasisi ilianzishwa miaka ya 90  kwa madhumuni ya kuokoa maisha ya watoto wenye maradhi ya moyo duniani kote, hususan katika nchi zinazoendelea. Hadi sasa imeshatoa matibabu kwa zaidi ya watoto 460,000 wenye maradhi ya moyo kutoka Afrika, Amerika, Asia na kwingineko.

Shughuli za taasisi hiyo inajumuisha kutibu wagonjwa, kutoa mafunzo kwa madaktari na wakufunzi na kusambaza madaktari katika nchi mbalimbali kuendesha upasuaji kwa kipindi maalum. Madaktari waliopewa mafunzo na taasisi hiyo wanaendelea kupata miongozo ya taasisi wanaporejea katika nchi zao kwa ajili ya kufanya matibabu.

Mhe. Waziri alipokuwa katika taasisi hiyo alipata fursa ya kuonana na Watanzania wanaosoma na wengine wanaopata matibabu ya maradhi ya moyo katika taasisi hiyo. Aidha, alioneshwa watoto wawili wanaougua maradhi ya moyo kutoka Nymmar na Romania ambao kwa mujibu wa Mkurugenzi alisema ndio wa kwanza kupokelewa kutoka nchi hizo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Israel
10 Mei 2017


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe, Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akiongea na wawakilishi wa Taasisi ya Moyo ya Save the Children Heart ya Israel mara baada ya kuwasili katika taasisi hiyo kujionea namna inavyoendesha shughuli zao. 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe, Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akimjulia hali mmoja wa watoto kutoka Tanzania anayepata tiba ya maradhi ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Save the Children Heart ya Israel

Kutoka kulia, mtu wa kwanza na wa pili ni Watanzania wanaosomea fani za tiba za maradhi ya moyo katika taasisi ya Save the Children Haert wakiongea na Mhe. Waziri wakati alipoitembelea taasisi hiyo jijini Tel Aviv, Israel leo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Save the Children Heart ya Israel akitoa maelezo kwa Mhe. Waziri hayupo pichani namna taasisi hiyo inavyofanya kazi.

Wanne kutoka kushoto ni wanafunzi kutoka Tanzania wanaosomea fani ya tiba ya maradhi ya Moyo wakimsikiliza Mkurugenzi wao hayupo pichani.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe, Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akimkabidhi zawadi Mkurugenzi wa Taasisi ya Save the Children Heart/

Kaimu Mkurugenzi wa Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Suleiman Salehe akibadilishana mawasiliano na wanafunzi wanaosomea fani ya tiba ya maradhi ya moyo kutoka Tanzania.


Ulinzi wa Mpaka kwenye Ukanda wa Ghaza
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe, Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akisalimiana na Afisa Usalama kutoka Kitengo cha Protection Unit alipowasili katika eneo la Netiv Haasara lililopo Ghaza ambapo ni mpakani na eneo la Palestina linalotawaliwa na Hamas.
Mkazi wa eneo la Netiv Haasara, Ghaza, Bibi Hila Fenton akitoa maelezo kwa Mhe. Waziri na wajumbe wengine kuhusu madhila wanayokutana nayo wananchi wa Israel wanaoishi karibu na mpaka wa Ghaza.



Bibi Hila Fenton akionesha mabaki ya gruneti la kwanza kabisa kurushwa kutoka Palestina na kuangukia kwenye eneo wanaloishi mwaka 2001/

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe, Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akipokea maelekezo alipowasili eneo la mpaka katika ukanda wa Ghaza lililojengwa ukuta/
Wageni wanaofika katika eneo la mpaka huu wanaombwa kuandika ujumbe wa matumaini katika mawe yaliyotengenezwa kwa sanaa ya aina yake na kuyabandika kwenye ukuta unaozuia maguruneti kupita. Hapo Mhe, Waziri na Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Job Masima wakibandika vijiwe vyenye ujumbe wa kuleta matumaini kwenye ukanda wa Ghaza.

Bi. Kisa Mwaseba naye akibandika ujumbe wake

Sehemu ya ukuta wa sengenge unaotenganisha mpaka wa Israel na Palestina katika Ukanda wa Ghaza.

Sehemu ya ukuta uliojengwa imara kuzuia vijiji vya Israel vilivyo mipakani visifikiwe na mashumbulizi ya magruneti.


Eneo la Ukaguzi wa Malori ya mizigo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akipata maeleozo kutoka kwa Meneja wa Usalama wa ukaguzi wa malori ya mizigo yanayokwenda Palestina kutoka Israel na kinyume chake.

Meneja wa Usalama anatoa maelezo namna kazi ya kukagua malori ya mizigo inavyofanywa kwa uangalifu mkubwa ili kuzuia uwezekano wowote wa kupitisha vilipuzi au vifaa vya kuundia vilipuzi.

Baadhi ya Malori ya mizigoAdd caption

baadhi ya mizigo ambayo imekamilika kukaguliwa inasubiri kusafirishwa/Add caption

Eneo la ukaguzi wa maslori ya mizigo ambalo pia limejengewa ukuta kwa ajili ya kuzuia mashambulizi ya maguruneti.

Scanner inayotumika kukagua malori ya mizigo ambayo ina nguvu kubwa ya kubaini vifaa vilivyobebwa katika lori kimoja baada ya kingine. kutokana na nguvu ya scanner hiyo harusiwi mtu kukaa karibu inapofanya kazi. 

Waziri Mahiga akionesha moja ya mitambo iliyofungwa kwa ajili ya kuzuia bomu lisilipuke kabla halijasababisha madhara.



Wednesday, May 9, 2018

Katibu Mkuu akutana kwa mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Bi. Inmi Patterson alipofika Wizarani kwa ajili ya mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani.
Mazungumzo yakiendelea

Katibu Mkuu afanya mazungumzo na Balozi wa Vietnam nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Vietnam nchini Mhe. Nguyen Doanh, tarehe 09 Mei,2018, Jijini Dar es Salaam.

Balozi Doanh alitumia fursa hii kujitambulisha na kumpongeza Prof. Mkenda kwa kuteuliwa kuwa Katibu mkuu wa Wizara. Aidha,  mazungumzo hayo pia yalilenga kuboresha mahusiano yaliyokuwepo kati ya Tanzania na Vietnam, pia Prof.Mkenda amemhakikishia Balozi  ushirikiano  kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu yake hapa nchini.
Balozi Doanh naye akifafanua jambo katika mazungumzo hayo.
Mazungumzo yakiendelea