Thursday, May 10, 2018

Benki ya Exim ya India yaipatia Tanzania mkopo nafuu kusaidia sekta ya maji

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi Amina Kh. Shaaban kwa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Exim ya India, Bw. David Resquinha wakisaini kwa niaba ya Serikali zao Mkataba wa Mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika miji 23 ya Tanzania.
Bi. Shaaban na Bw. Resquinha wakibadilishana mkataba huo mara baada ya kusaini

Picha ya pamoja
=========================================================================

BENKI YA EXIM YA INDIA YAIPATIA SERIKALI YA TANZANIA MKOPO WA MASHARTI NAFUU KUSAIDIA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI KATIKA MIJI 23 YA TANZANIA

Serikali ya India kupitia Benki ya Exim imeipatia Serikali ya Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 500, sawa na shilingi Trilioni 1.14 za Tanzania, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika miji 23 ya Tanzania.

Hafla ya uwekaji saini wa mkataba huo imefanyika leo tarehe 10 Mei, 2018 mjini  New Delhi, India ambapo Bi. Amina Kh. Shaaban, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango na Bw. David Resquinha, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Exim walisaini kwa niaba  ya Serikali zao..

Miji  itakayonufaika na Fedha za mkopo huu ni Muheza, Makambako, Kayanga, Njombe, Manyoni, Songea, Sikonge, Chunya, Kasulu, Kilwa Masoko, Rujewa, Mugumu, Geita,  Makonde, Wangingómbe, Handeni , Singida mjini, Kiomboi, Mpanda, Chemba, Mafinga, Urambo-Kaliua pamoja na miji ya Zanzibar.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba, Naibu Katibu Mkuu, Bi. Amina Kh. Shaaban, amesema kuwa miradi hiyo ni muhimu kwa sababu itawezesha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika miji husika hivyo kusaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko yanayotokana na maji yasiyo salama.

Aidha, miradi itasaidia kufikiwa kwa malengo na mipango ya Taifa na Kimataifa ya Maendeleo ikiwemo: Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano awamu ya pili (FYDPII) , Mkakati wa Kukuza na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA III) na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDG’s).

Vilevile, amesema uamuzi wa Serikali wa kuboresha  huduma za maji umelenga kuwapunguzia Wananchi husususan Wanawake adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji, na hivyo kupata muda wa kutosha kufanya shughuli mbali mbali za maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.