Wednesday, October 19, 2022

DKT. STERGOMENA TAX AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUTOKA POLAND KUJA NCHINI

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Poland waje nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ya uchumi wa bluu na madini.

 

Waziri Tax ameyasema hayo, wakati akihutubia mkutano uliowakutanisha wawakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Taasisi za Kiuchumi za Poland. Mkutano huo ambao uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Poland na Ubalozi wa Tanzania nchini humo umefanyika katika Ofisi za Taasisi ya Uwekezaji na Biashara ya Poland zilizopo jijini Warsaw.

 

Mhe. Dkt. Tax amesema Serikali chini ya uongozi imara wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili kuvutia wawekezaji wengi wenye tija na mitaji waje kuwekeza nchini.

 

Ameyataja maeneo ambayo yanahitaji wawekezaji kutoka Poland na sehemu nyingine duniani kuwa ni pamoja  uchimbaji madini, uchumi wa bluu, teknolojia ya habari na mawasiliano, viwanda vya sukari na nguo na miundombinu.

 

Amesema ili kuhakikisha wawekezaji wanaofika nchini wanafikia malengo yao, Serikali inaendelea kuboresha mifumo mbalimbali ikiwemo,  kuboresha upatikanaji wa viza na vibali mbalimbali lakini pia Serikali inaboresha mikataba mbalimbali ili kuondokana na urasimu wote kwenye sekta hiyo muhimu ya uwekezaji. Pia Serikali imeendelea kuboresha miundombinu yake ikiwemo Bandari ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wawekezaji. Huduma zingine zinazoboreshwa ni kuwa na umeme wa uhakika ambapo hadi sasa ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) wa megawati 2,115  na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaendelea nchini.

 

Amesema ziara yake nchini Poland pamoja na mambo mengine inalenga kukuza baiashara na uwekezaji kati ya nchini hizi mbili.

 

“Ninawakaribisha wafanyabaiasha na wawekezaji kutoka Poland kuja Tanzania. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia imejipanga kikamilifu kuwahudumia. Tunaendelea siku hadi siku kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini” alisema Dkt. Tax.

 

Amesema mbali na maboresho hayo, Tanzania ni nchi sahihi kwa wawekezaji kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo amani, miundombinu ya kisasa ya barabara, reli, bandari na soko la uhakika kupitia uanachama wa Tanzania kwenye Jumuiya za kikanda za Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Soko Huru la Biashara Barani Afrika (CFTA)

 

“Serikali imeendelea kuondoa  vikwazo vya  kuanzisha na kuendesha  biashara  kwa kupitia upya   sheria, kanuni na taratibu za biashara  na kuzifuta zile  ambazo zimethibitika  kuwa zinayafanya mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kuwa magumu.”

 

Mhe. Waziri  amesema kwa kuwa nchi ya Poland imepiga hatua kubwa katika masuala mengi ikiwemo teknolojia ya usimamizi wa maji, Tanzania ingefurahi kuona wawekezaji kutoka nchi hiyo wanawekeza kwenye sekta hiyo kwa wingi.

 

Amesema kuwa uchimbaji wa madini kama vile Tanzanite na mengine mengi, ni fursa nyingine ya kibiashara ambayo wafanyabiashara wa Poland wanakaribishwa kuichangamkia hapa nchini.

 

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Taasisi hiyo,  Bw. Zbigniew Sokal alitumia fursa hiyo kumweleza utayari wa Taasisi yake kushirikiana na Taasisi za Uwekezaji nchini ikiwemo TIC na ZIPA ili kujiimarisha zaidi. Alisema tayari makampuni kadhaa ya Poland yapo tayari kuwekeza nchini Tanzania.

 

Wakati wa Mkutano huo Wawakilishi kutoka Kampuni 10 za Poland zinazojishughulisha na masuala mbalimbali  ikiwemo utengenezaji wa mitambo ya kilimo, uchimbaji visima virefu, usimamizi wa maji na utunzaji wa mazingira, teknolojia mpya ya uchomeleaji vyuma na  umeme wa jua waliwasilisha mada kuhusu Kampuni zao.

                                                       

Wakati huhuo, Mhe. Waziri Dkt. Tax alipata fursa ya kutembelea Mradi mkubwa wa Usimamizi wa Majitaka wa Hydrosfera uliopo  katika mji wa Jozefow. Mradi huo wa aina yake pamoja na mambo mengine hususanya majitaka kutoka majumbani na kuyatibu kwa matumizi mbalimbali ikiwemo umwagiliaji miti na maua katika mji huo. Kadhalika takangumu zingine hutayarishwa kitaalam na kuwa mbolea ya samadi kwa ajili ya mazao hayo ya miti na maua.

 

Akizungumza kuhusu mradi huo, Rais wa Kampuni hiyo, Bw. Stanslaw Zdanowicz amesema mradi huo ambao unaendeshwa kisasa, pamoja na mambo mengine umesaidia kuwapunguzia wananchi gharama za uondoshaji majitaka majumbani kwao.

 

Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Tax alishukuru kupata fursa ya kutembelea Kampuni hiyo na kujionea teknolojia ya hali ya juu ya usimamizi wa kisasa wa majitaka na alitumia fursa hiyo kuwakaribisha nchini kuja kuwekeza pamoja na kutembelea vivutio vya utalii vya nchini ikiwemo Zanzibar, Mlima Kilimanjaro na Hifadhi za Ngorongoro na Serengeti.

 

Mhe. Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba, 2022, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.

 

Katika ziara hiyo Mhe. Waziri Tax amefuatana na Wajumbe kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mambo ya  Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),  Mamlaka ya Ukuzaji  Biashara na Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Wakala wa Taifa wa Hifadi ya Chakula (NFRA), Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana na Makamu wa Rais wa Taasisi ya Biashara na Uwekezaji ya Poland Bw. Zbigniew Sokal alipowasili kwenye  Ofisi za Taasisi hiyo jijini Warsaw, Poland kwa ajili ya kushiriki Mkutano uliowakutanisha wawakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Taasisi za Kiuchumi za Poland wenye nia ya kuwekeza nchini. Wakati wa Mkutano huo Kampuni 10 ziliwasilisha mada. Mhe. Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Poland. 

Mhe. Dkt. Tax akizungumza wakati wa Mkutano uliowakutanisha wawakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Taasisi za Kiuchumi za Poland wenye nia ya kuwekeza nchini. Pamoja na mambo mengine aliwaeleza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini ikiwemo uchimbaji madini, uchumi wa bluu kilimo na  miundombinu,
 
Wajumbe kutoka Tanzania na Poland walifuatilia mkutano. Walioketi upande wa kushoto ni Balozi wa Poland nchini Tanzania, (kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (katikati) na Brigedia Jenerali, Mkeremy
Mhe. Dkt. Tax akimsikiliza Bw. Sokal akizungumza. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Poland, Mhe. Abdallah Possi
Sehemu ya wajumbe kutoka Poland na Tanzania wakifuatilia mkutano
Sehemu nyingine ya wajumbe
Sehemu nyingine ya wajumbe
Sehemu nyingine ya wajumbe
Mkutano ukiendelea
Mkutano ukiendelea
 
   


 
  

.......Ziara ya Mhe. Dkt. Tax kwenye Mradi  wa Usimamizi wa Majitaka wa Hydrosfera

Mhe. Dkt. Tax na ujumbe wake wakifuatilia mada kuhusu Mradi wa Usimamizi wa Majitaka wa Hydrosfora kutoka kwa Rais wa Kampuni hiyo Bw. Stanisław Zdanowicz
Mhe. Dkt. Tax na ujumbe wake wakifuatilia mada

Mkutano ukiendelea
Mhe. Dkt Tax akipata maelezo ya namna wanavyobadilisha taka ngumu kuwa mboleaM
Mhe. Dkt. Tax akiwa kwenye moja ya maabara kwenye kampuni hiyo




Mhe. Dkt. Tax akipokea zawadi ya mchoro wa jengo hilo

Mhe. Dkt Tax akimpatia zawadi Rais wa Kampuni hiyo



  

Come to invest in Tanzania, Dr. Bana tells Nigerian investors

Ambassador Dr. Benson Alfred Bana, High Commissioner of the United Republic of Tanzania to the Federal Republic of Nigeria was special guest at the 50th AGM of the Manufacturers Association of Nigeria in Lagos. Alhaji Aliko Dangote, GCON, President/CE Dangote Industries Ltd, delivered a lecture on *”Agenda Setting for Industrializing Nigeria the Next Decade.”* The High Commissioner seized the opportunity to invite captains of industries in Nigeria and West African countries to invest in Tanzania, illuminating opportunities and incentives provided by the Government of the United Republic of Tanzania and the Revolutionary Government of Zanzibar.

Tanzanian Ambassador to Nigeria, H.E Dr. Benson Bana (c) in attendance to the 50th AGM of the Manufacturers Association of Nigeria in Lagos held  on 18th October 2022.

Tanzanian Ambassador to Nigeria, H.E Dr. Benson Bana is in group photo with other dignitaries who attended the
50th AGM of the Manufacturers Association of Nigeria in Lagos held on 18th October 2022.


 

Tuesday, October 18, 2022

TANZANIA NA POLAND ZAKUBALIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO

Serikali ya Tanzania na Poland zimekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano kwenye sekta mbalimbali zenye manufaa kwa nchi hizi mbili ikiwemo kilimo, elimu,  nishati, utalii, biashara na uwekezaji.


Makubaliano hayo yamefikiwa leo tarehe 18 Oktoba 2022 jijini Warsaw,  Poland wakati wa mazungumzo rasmi  yaliyofanyika kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Mhe. Zbigniew Rau.


Wakizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mazungumzo hayo,  Mawaziri hao  wamesema Tanzania na Poland ambazo zinaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano, zina fursa nyingi zenye manufaa kwa pande zote mbili na kwamba  wamekubaliana kuweka mikakati madhubuti ya utekelezaji wa makubaliano hayo ikiwa ni pamoja na kuanzisha ushirikiano kwenye maeneo mapya ya ulinzi na usalama pamoja na nishati.


Akizungumza,  Mhe. Dkt. Tax amesema Poland imeandelea kuwa mshirika muhimu wa kimkakati kwa Tanzania katika kipindi chote cha miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia, na kwamba wamekubaliana kuendelea kushirikiana kwenye sekta ambazo zimekuwa na tija kubwa kwenye ushirikiano huo ikiwemo kilimo, elimu, utalii, biashara na uwekezaji.

 

"Katika majadiliano yetu leo, tumetathmini ushirikiano wetu katika maeneo ambayo tayari tunashirikina na Poland kama kilimo, elimu, biashara na uwekezaji na utalii. Pia tumekubaliana kuongeza maeneo ya  ushirikiano katika masuala ya nishati na ulinzi na usalama ambayo ni muhimu katika kukuza ushirikiano wetu” amesema Dkt. Tax.

 

Kadhalika Mhe. Dkt. Tax ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kuja nchini kuwekeza kwani Tanzania bado inazo fursa nyingi za uwekezaji. Aidha, Mhe. Dkt. Tax ameipongeza Serikali ya Poland na Wananchi wake kwa kuendelea kuichagua Tanzania kama kituo chao muhimu cha utalii ambapo nchi hiyo ni miongoni mwa nchi tano  za juu zenye idadi kubwa ya  watalii waliotembelea nchini mwaka 2022.

 

“Ni imani yangu kuwa, baada ya ziara yangu hii biashara, uwekezaji, utalii na ushirikiano wa kisiasa kati ya Tanzania na Poland utaimarika zaidi. Pia kipekee nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Poland kwa upendo wao kwa Tanzania. Kwani kwa mwaka huu 2022, Poland ni miongoni mwa nchi tano zilizoshika nafasi ya juu kwa wananchi wake kutembelea nchini kwetu nawashukuru sana na karibuni tena, alisisitiza Dkt. Tax.

 

 Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Mhe. Zbigniew Rau amesema kuwa nchi yake inathamini ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Tanzania na kwamba maeneo muhimu yaliyojadiliwa na kukubaliwa wakati wa mkutano wao yatatekelezwa na Serikali ya nchi hiyo.

 

“Tanzania ni mshirika muhimu sana kwa Poland na miongoni mwa nchi zinazopewa kipaumbele katika program za muda mrefu za maendeleo ikiwemo uwekezaji kwenye sekta ya kilimo,” amesema Mhe. Rau.

 

Pia alitumia fursa hiyo kumshukuru Mhe. Dkt. Tax kwa kukubali mwaliko wake na kuitembelea Poland ambapo alisema hatua hiyo ni muhimu katika kukuza ushirikiano kati ya nchi mbili kwani utaharakisha utekelezaji wa makubalino mbalimbali ambayo tayari yapo na mapya.

 

“Tumekuwa na mazungumzo yenye tija na Mhe. Waziri Dkt. Tax. Kupitia mazungumzo hayo ushirikiano wetu utaimarika zaidi. Nitumie fursa hii kumshukuru Mhe. Waziri na ujumbe wake kwa kukubali mwaliko wangu na kututembelea”, amesema Mhe. Rau.

 

Wakati huohuo,  Mhe. Dkt. Tax ametembelea na kuweka shada la maua kwenye kaburi la askari mashujaa wa nchi hiyo lililopo jijini Warsaw.

 

Mhe. Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba, 2022, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.

Katika ziara hiyo Mhe. Waziri Tax amefuatana na Wajumbe kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Wizara ya Mambo ya  Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),  Mamlaka ya Ukuzaji  Biashara na Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Wakala wa Taifa wa Hifadi ya Chakula (NFRA), Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipokelewa rasmi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Mhe. Zbiniew Rau mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje za nchi hiyo tarehe 18 Oktoba 2022. Akiwa Wizarani hapo, Mhe. Waziri Dkt. Tax na Mhe. Rau walikutana kwa mazungumzo rasmi na kukubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za kilimo, nishati, elimu, biashara na uwekezaji. Mhe. Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba 2022.

Mhe. Dkt. Tax akiwa katika picha ya pamoja namwenyeji wake Mhe. Rau mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Mambo ya Nje zilizopo Warsaw nchini Poland

Mhe. Dkt. Tax na ujumbe wake akiwa kwenye mazungumzo rasmi na Mhe. Rau na ujumbe wake.
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ulioshiriki mazungumzo kati ya Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Rau. Kulia ni balozi wa Tanzania nchini Ujerumani na Poalnd, Mhe. Abdallah Possi

Sehemu ya ujumbe wa Poland wakati wa mazungumzo hayo
Mhe. Waziri Dkt. Tax na mwenyeji wake, Mhe. Rau wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbali mbali ya ushirikiano waliyojadili na kukubaliana

Sehemu ya Ujumbe wa Tanzania akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikisno wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (Kushoto)

Mhe. Waziri akisindikizwa  na Naibu Mkuu wa Itifaki wa Poland, Bw. Artur Harazim kwenye kaburi la askari mashujaa wa Poland kwa ajili ya kuweka shada la maua kwa lengo la kuwaenzi na kuwakumbuka

Gwaride la heshima liloandaliwa rasmi kwa ajili ya Mhe. Dkt. Tax alipofika eneo hilo kwa ajili kuwakumbuka mashujaa wa Poland


Mhe. Dkt. Tax akisaini kitabu cha wageni alipowasili kwenye eneo hilo la makumbusho ya mashujaa

Mhe. Waziri Dkt. Tax akiwa na ujumbe wa Tanzania na Poland mara baada ya kukamilisha shughuli ya uwekaji shada la maua kuwakumbuka askari mashujaa wa Poland




 

MALKIA MAXIMA AWASILI DAR ES SALAAM KWA ZIARA YA KIKAZI

Malkia wa Uholanzi, Malkia Maxima amewasili Jijini Dar es Salaam akitokea mkoani Kilimanjaro ambapo alianzia ziara yake jana tarehe 17 Oktoba 2022 baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 – 19 Oktoba, 2022.

Mara baada ya Malkia Maxima kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam, alipokelewa na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Robert Kahendaguza.

Malkia Maxima ambaye pia ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Mfumo Jumuishi wa Fedha katika Maendeleo anatarajia kukutana kwa mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 19 Oktoba 2022.

Mbali na kukutana na Mhe. Rais Samia pia Malkia Maxima kabla ya kuhitimisha ziara yake hapa nchini, anatarajia pia kukutana na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali.

Malkia wa Uholanzi, Malkia Maxima akipokelewa na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Robert Kahendaguza baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam

Malkia wa Uholanzi, Malkia Maxima akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam. Pembeni yake mwenye suti ya kijivu ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Robert Kahendaguza

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Robert Kahendaguza akiteta jambo na Malkia wa Uholanzi, Malkia Maxima baada ya Malkia kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam

Malkia wa Uholanzi, Malkia Maxima akimueleza jambo Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Robert Kahendaguza baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam