Friday, May 12, 2023

BALOZI SHELUKINDO AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA MABALOZI

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amekutana na kuzungumza na mabalozi wa China, Kenya, Denmark, Italia na Sudan kwa nyakati tofauti na kujadiliana nao masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na nchi zao.

Mabalozi waliokutana na Balozi Shelukindo ni Balozi wa China, Mhe. Chen Mingjian, Balozi wa Kenya, Mhe. Isaac Njenga, Balozi wa Denmark, Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet, Balozi wa Italia, Mhe. Marco Lombard na Kaimu Balozi wa Sudan, Mhe. Asim Mustafa Ali.

Dkt. Shelukindo amekutana na mabalozi hao katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili na kuahidi kuongeza ushirikiano katika sekta za elimu, michezo, biashara na uwekezaji.

“Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri na China, Kenya, Denmark, Italia na Sudan ambapo uhusiano huo umesaidia kuwa na misingi imara ya ushirikiano kwa maslahi mapana ya Taifa letu na nchi zao,” alisema Dkt. Shelukindo

“Vilevile nimepata fursa ya kukutana na balozi wa Sudan na amenijulisha juu ya uwezekano wa mapigano yanayoendelea nchini humo kufikia mwisho kwa njia ya makubaliano. Na amenihakikishia kuwa wanafunzi waliokuwa wanasoma nchini Sudan watapokelewa na kuendelea na masomo yao baada ya mapigano kumalizika.

Amesema tarehe 11 Mei, 2023 pande zinazopigana nchini humo zilisaini mkataba wa makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano,” alisema Dkt. Shelukindo 

Kwa upande wake Kaimu Balozi wa Sudan nchini, Mhe. Mustafa Ali amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kumalizika kwa mapigano yanayoendelea nchini humo kwa njia ya makubaliano ya amani. 

“Naomba nikuhakikishie kuwa Serikali ya Sudan itawapokea wanafunzi waliokuwa wanasoma nchini kwetu na kupata fursa ya kuendelea na masomo yao baada ya mapigano kumalizika,” alisema Mhe. Mustafa Ali

Naye Balozi wa China nchini, Mhe. ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono China na kuahidi kuendeleza harakati za kusaidia nchi zinazoendelea na kuongeza kuwa China itaendelea kuisadia Tanzania katika kufanikisha miradi mbalimbali ya kimkakati.

Kwa nyakati tofauti mabalozi hao  wameishukuru Tanzania kwa ushirikiano mzuri ambao wamekuwa wakiupata wakati wa utekelezaji wa majukumu yao na kuahidi kuwa nchi zao zitaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali kwa maslahi ya pande zote.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akisalimiana na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Isaac Njenga 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza na Balozi wa Denmark nchini, Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza na Balozi wa Italia, Mhe. Marco Lombard. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Shwahiba Mndeme pamoja na Afisa wa Idara hiyo, Bi. Kisa Mwaseba. 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza na Kaimu Balozi wa Sudan, Mhe. Asim Mustafa Ali katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



TANZANIA, UINGEREZA KUIMARISHA BIASHARA NA UWEKEZAJI

Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wake na Serikali ya Uingereza katika sekta za biashara pamoja na uwekezaji.

Dhamira hiyo imeelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) aliposhiriki hafla maalum ya kutawazwa kwa Mfalme Charles III na Malkia Camilla iliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi wa Uingereza Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Mei, 2023. 

 Dkt. Tax alisema kuwa Tanzania na Uingereza zinafurahia uhusiano mzuri wa kihistoria na kirafiki uliodumu kwa muda mrefu na kuongeza kuwa kupitia uhusiano huo, Tanzania na Uingereza zimekuwa zikifanya kazi kwa ukaribu katika sekta mbalimbali hususan biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote. 

“Uingereza ni miongoni mwa washirika wa kibiashara wa Tanzania wa siku nyingi na imesalia kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuwa na uwekezaji mkubwa wa Kigeni hapa nchini katika sekta mbalimbali. Tanzania inaahidi kuendelea kushirikiana na utawala wa Mtukufu Mfalme Charles III katika nyanja mbalimbali,” alisema Waziri Tax

Alisema Uingereza imeendelea kuwa mwekezaji mkuu wa pili nchini Tanzania, ikiwa na jumla ya miradi 956 yenye thamani ya pauni bilioni 4.6 na kuajiri zaidi ya watu 275,000 na hivyo kutoa mchango mkubwa katika maendeleo yetu ya kijamii na kiuchumi. 

“ Uingereza imeendelea kuwa mwekezaji mkuu wa pili nchini Tanzania, ikiwa na jumla ya miradi 956 yenye thamani ya pauni bilioni 4.6 na kuajiri zaidi ya watu 275,000 na hivyo kutoa mchango mkubwa katika maendeleo yetu ya kijamii na kiuchumi, Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Uingereza kwa manufaa mapana ya nchi na watu wake,” aliongeza Dkt. Tax. 

Dkt. Tax alitumia fursa hiyo kuwahakikishia Waingereza na wageni mbalimbali walioshiriki hafla hiyo kuwa, Tanzania ina mazingira salama ya uwekezaji na biashara kwa kuzingatia juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwemo kuweka sera imara na zinazotabirika pamoja na sheria na taratibu rafiki, kuboresha huduma za kijamii, kuimarisha demokrasia, usawa wa kijinsia na utawala wa sheria, kuendeleza miradi mikubwa ikiwemo ya nishati na miundombinu, uchukuzi na usafirishaji.

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concar alisema Uingereza na Tanzania zimeendelea kuwa na urafiki imara kwa muda mrefu kutokana na heshima, dhamira ya kukuza maendeleo na kuthaminiana kwa wananchi wa pande zote mbili.

“Uingereza imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika sekta ya biashara na uwekezaji ambapo wafanyabiashara wengi kutoka Uingereza wamewekeza nchini Tanzania, tutaendelea kuwaeleza kuwa Tanzania ni salama kwa uwekezaji na biashara ili wawekeze kwa wingi” alisema Balozi Concar.   

Balozi Concar aliongeza kuwa Ushirikiano wa Uingereza na Tanzania umekuwa ukistawishwa na juhudi za maendeleo katika sekta mbalimbali hususan za fedha zikiwemo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

“Uingereza na Tanzania hivi karibuni zitasaini mkataba wa ushirikiano katika sekta ya afya hususan Utafiti wa matibabu lengo likiwa ni kuimarisha sekta ya afya. Uingereza na Tanzania zimekuwa na ushirikiano wa maendeleo kwa lengo la kuendeleza malengo ya pamoja kwa maslahi ya pande zote mbili,” aliongeza Balozi Concar.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akihutubia katika hafla maalum ya kutawazwa kwa Mfalme Charles III na Malkia Camilla iliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi wa Uingereza Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Mei, 2023

Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concar akiwakaribisha wageni mbalimbali walioshiriki katika hafla maalum ya kutawazwa kwa Mfalme Charles III na Malkia Camilla iliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi wa Uingereza Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Mei, 2023

Sehemu ya wageni walioshiriki katika hafla maalum ya kutawazwa kwa Mfalme Charles III na Malkia Camilla iliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi wa Uingereza Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Mei, 2023

Sehemu ya wageni walioshiriki katika hafla maalum ya kutawazwa kwa Mfalme Charles III na Malkia Camilla iliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi wa Uingereza Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Mei, 2023


Thursday, May 11, 2023

TANZANIA YAMTEUA DKT. TULIA KUGOMBEA URAIS UMOJA WA MABUNGE DUNIANI

 




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akizungumza na Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini (Hawapo pichani), wakati alipokuwa akiwaomba kumnadi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Akson ambaye anagombea nafasi ya Urais katika Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Mhe. Tax amezungumza na Mabalozi hao Jijini Dar es Salaam.

Mbunge wa Singida Magharibi ambaye pia ni mbunge wa Bunge la IPU, Mhe. Elibariki Kingu akizungumza na Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini Jijini Dar es Salaam



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akizungumza na Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, wakati alipokuwa akiwaomba kumnadi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Akson ambaye anagombea nafasi ya Urais katika Umoja wa Mabunge Duniani (IPU)


Sehemu ya Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipokuwa akizungumza nao Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini

FURSA ZA UFADHILI WA MASOMO NCHINI JAPAN


 

Wednesday, May 10, 2023

TANZANIA, UGANDA ZAKUBALIANA KUONDOA VIKWAZO VYA BIASHARA

Tanzania na Uganda zimekubaliana kuondoa vikwazo vya biashara ili kuendeleza na kuboresha ushirikiano kati ya mataifa hayo kwenye nyanja mbalimbali.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika mkutano wa majadiliano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga uliofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano wao, viongozi hao wamekubaliana kukamilisha michakato ya kuendeleza miundombinu ili kukamilisha barabara zinazounganisha Uganda na Tanzania, usafiri katika ziwa Victoria ambao pia utaunganisha reli ya kisasa ya SGR kwenda Uganda. 

“Tumewekeana muda ili tuweze kukamilisha baadhi ya masuala kwa haraka lakini pia kuona jinsi gani pale panapo hitaji kila nchi itoe rasilimali iweze kujipanga na kuhakikisha rasilimali hizo zinapatikana kwa wakati,” alisema Dkt. Tax.

Katika mkutano huo viongozi hao wamekubaliana pia kukamilisha ujenzi wa kituo cha uokoaji Jijini Mwanza kitakachoshughulikia maafa yanayoweza kutokea katika ziwa Victoria.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga amesema mkutano huo umewawezesha kukamilisha baadhi ya mambo yaliyokuwa mezani na kujipa muda hadi mwishoni mwa mwezi Julai 2023 kukamilisha machache yaliyosalia.

Amesema wataendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili waweze kutatua vikwazo vilivyopo katika itifaki ya soko la pamoja la forodha. 

“Tuendelee kushirikiana kufanya kazi kwa pamoja ili tuweze kutatua vikwazo katika itifaki ya soko la pamoja la forodha,” alisema Mhe. Kadaga

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga (aliyevaa barakoa) katika mkutano wao uliofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga akiongoza ujumbe wa Uganda katika mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax uliofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mkutano baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga ukiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mkutano baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga ukiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Sehemu ya Ujumbe wa Uganga ukiongozwa na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga



Tuesday, May 9, 2023

NAIBU WAZIRI MKUU WA KWANZA WA UGANDA AWASILI NCHINI KIKAZI

Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Rebecca Kadaga amewasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere. Mhe. Kadaga anatarajia kuwa na mkutano wa majadiliano baina yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) tarehe 10 May, 2023, katika Ofisi Ndogo ya Wizara, Jijini Dar es Salaam.

Mara baada ya kuwasili nchini, Mhe. Kadaga alipokelewa na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz pamoja Balozi wa Uganda nchini, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye.

Pamoja na mambo mengine, mazungumzo ya viongozi hao yatahusu kuimarisha ushirikino kati ya Tanzania na Uganda, pamoja na ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Rebecca Kadaga amewasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Rebecca Kadaga amewasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Rebecca Kadaga akizungumza na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz (katikati) pamoja Balozi wa Uganda nchini, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye (kulia) baada ya kuwasili amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere


VACANCY ANNOUNCEMENT


 

Friday, May 5, 2023

BIASHARA KATI YA TANZANIA NA UFARANSA YAONGEZEKA

Ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na Ufaransa umeongezeka kutoka kiasi cha shilingi billioni 27.8 kwa mwaka 2015 hadi bilioni 94.5 kwa mwaka 2022. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amebainisha hayo alipofungua mkutano wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Ufaransa uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Mbali na kukua kwa biashara kati ya mataifa hayo mawili, pia kumekuwa na ongezeko la watalii kutoka Ufaransa ambapo kwa mwaka 2022 Tanzania ilipokea watalii 100,600 kutoka Ufaransa na kuwa nchi ya pili kuleta watalii nchini Tanzania.

“Biashara imeendelea kukua lakini pia katika uwekezaji tunashirikiana, katika utalii Ufaransa imekuwa nchi ya pili kwa kuleta watalii kwenye taifa letu, haya yanatokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Serikali imefanya kazi kubwa kuvutia wawekezaji na watalii hususan kupitia filamu ya ‘Royal Tour’ na ndiyo maana utalii umeongezeka,” alisema Dkt. Tax

Mhe. Dkt. Tax amesema madhumuni ya mkutano huu wa majadiliano ambao ni wa pili kati ya Tanzania na Ufaransa ni kuwawezesha Wafaransa kutambua fursa mbalimbali zinazopatikana nchini pamoja na Watanzania kuzijua fursa zinazopatikana nchini Ufaransa ili kuzitumia kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Tanzania na Ufaransa zimekuwa zikishirikiana katika sekta za elimu, nishati, utalii, usafirishaji, ulinzi na usalama (maritime security) …...Ufansa wamekuwa wadau wakubwa katika ujenzi wa bomba la mafuta linalojengwa kutoka Uganda hadi Tanzania mambo yote haya lazima tuendelee kuyadumisha lakini pia kufungua fursa nyingine zinazoweza kupatikana,” alisisitiza Dkt. Tax

Naye Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui amesema kufanyika kwa mkutano huo wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Ufaransa ni uthibitisho kuwa Tanzania na Ufaransa zimekuwa na ushirikiano mzuri na imara.

“Tumekuwa tukikutana mara kwa mara na kujadili masuala ya kikanda na kimataifa ili kuimarisha maendeleo ya miradi kati ya nchi zetu mbili katika sekta mbalimbali hususan mabadiliko ya tabianchi, uwekezaji, utalii, uchumi wa buluu, usalama wa baharini, na tumefanikiwa kujadili masuala yote vizuri kwa sababu uhusiano mzuri tulio nao. Itakumbukwa kuwa mwaka jana 2022 Marais wetu walipokutana na walikubaliana kushirikiana na kusonga mbele kwa maslahi ya pande zote mbili,” alisema Balozi Nabil.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Ulaya na Mambo ya Nje ya Ufaransa, Bw. Christophe Bigot amesema Ufaransa itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuimarisha sekta za biashara na uwekezaji, nishati, usalama wa baharini, uwekezaji, utalii, uchumi wa buluu, michezo na utamaduni.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Makatibu Wakuu na Manaibu makatibu Wakuu kutoka Wizara mbalimbali wakiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA). 

Mkutano wa kwanza wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Ufaransa ulifanyika mwezi Juni 2018 nchini Ufaransa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akihutubia mkutano wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Serikali ya Tanzania na Ufaransa Jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Ulaya na Mambo ya Nje ya Ufaransa, Bw. Christophe Bigot akichangia ajenda katika mkutano wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Serikali ya Tanzania na Ufaransa Jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza katika mkutano wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Serikali ya Tanzania na Ufaransa Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui akichangia ajenda katika mkutano wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Serikali ya Tanzania na Ufaransa Jijini Dar es Salaam

Mkutano wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Ufaransa ukiendelea Jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Idara ya Amerika na Ulaya katika Wizara ya Mambio ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme akiongoza mkutano wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Serikali ya Tanzania na Ufaransa Jijini Dar es Salaam



UJUMBE WA DRC WATEMBELEA BANDARI YA DAR ES SALAAM

Mkurugenzi wa Forodha na Ushuru wa bidhaa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayesimamia majimbo ya Haut Katanga, Lualaba, Tanganyika na Lomami, Bw. René Kalala Masimango na ujumbe wake upo nchini kwa ziara ya kikazi ambapo tarehe 04 Mei 2023 ulikutana na Uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) jijini Dar Es Salaam.

 

Akizungumzia kuhusu ziara hiyo, Balozi wa Tanzania nchini DRC, Mhe. Said Mshana alisema ubalozi wake umeiandaa kwa lengo la kuwakutanisha wadau wa Tanzania na DRC ili wajadili na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazokwamisha biashara kati ya nchi hizo mbili.

 

Wakati wa kikao na uongozi wa TPA, Bw. Masimango alisema Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu sana kwa mizigo ya Congo na inahudumia mizigo mingi, hivyo ziara yake ni kujionea utendaji kazi wa Bandari na ameridhika kuwa kazi zinazofanywa na mamlaka hiyo ni nzuri na zimepangiliwa vizuri.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Plasduce Mkeli Mbossa ameahidi kuwa Menejimenti yake ipo tayari kutatua changamoto zozote zitakazojitokeza katika kuhudumia shehena ya mizigo inayoenda na kutoka Congo kupitia Bandari za Tanzania kwa lengo la kulinda uhusiano mzuri na wa muda mrefu wa kidiplomasia na biashara kati ya nchi hizi mbili. 


“Menejimenti ya TPA itaendelea kuzifanyia kazi changamoto zozote katika kuhudumia shehena ya Congo na kuimarisha uhusiano ili shughuli zinazofanywa na TPA katika bandari zake ziwe na manufaa kwa DRC.” Alisema Bw. Mbossa. 


Naye Balozi wa DRC nchini Tanzania, Mhe. Jean Pierre Massala amesema ziara hiyo ni muhimu kwa uhusiano kati ya DRC na Tanzania na muhimu ni kufanya kazi kwa pamoja kwa faida ya nchi hizi mbili. 


Ujumbe huo wa DRC unaendelea na ziara yake nchini na leo tarehe 05 Mei 2023 umepanga kutembelea Bandari Kavu ya Kwala na Reli ya Kisasa ya SGR.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bw. Plasduce Mkeli Mbossa akitoa maelezo kwa ujumbe wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ukiongozwa na Mkurugenzi wa Forodha na Ushuru wa bidhaa  anayesimamia majimbo ya Haut Katanga, Lualaba, Tanganyika na Lomami, Bw. René Kalala Masimango ulipotembelea bandari ya Dar Es Salaam 


Balozi wa Tanzania nchini DRC, Mhe. Said Mshana (kushoto) akizungumza wakati wa kikao baina ya ujumbe wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ukiongozwa na Mkurugenzi wa Forodha na Ushuru wa bidhaa anayesimamia majimbo ya Haut Katanga, Lualaba, Tanganyika na Lomami, Bw. René Kalala Masimango na uongozi wa TPA. 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bw. Plasduce Mkeli Mbossa (wa nne kulia) na Balozi wa Tanzania nchini DRC, Mhe. Said Mshana (katikati) katika picha ya pamoja na ujumbe wa DRC uliotembelea Bandari ya Dar Es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bw. Plasduce Mkeli Mbossa akiwapitisha maeneo mbalimbali ya Bandari ya Dar Es Salaam  ujumbe wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ukiongozwa na Mkurugenzi wa Forodha na Ushuru wa bidhaa anayesimamia majimbo ya Haut Katanga, Lualaba, Tanganyika na Lomami, Bw. René Kalala Masimango ulipotembelea bandari hiyo


Tuesday, May 2, 2023

TUME HAKI JINAI YAKUTANA NA MABALOZI JIJINI DAR ES SALAAM

Tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini imekutana na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na kuwapa taarifa ya hatua iliyofikiwa na tume hiyo. 

Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohammed Othman Chande, amesema tume imekutana na mabalozi hao kwa lengo la kuwapa taarifa ya hatua iliyofikiwa na tume hiyo wakiwa ni sehemu ya wadau. 

"Taasisi za Kimataifa wakati mwingine zinafanya kazi na taasisi za haki jinai, tumeona tuwafahamishe kwa kuwa nao ni wadau. Pia tunawakaribisha watoe mapendekezo yao kwa sababu huu sio mwisho wa kupokea maoni," alisema Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Chande. 

“Kwa sasa tunamalizia uchambuzi wa maoni yaliyokusanywa, kazi ambayo inatarajiwa kufanyika kwa mwezi mmoja na baadaye itatolewa rasimu ya mapendekezo,” alisema Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Chande na kuongeza kuwa  rasimu ya mapendekezo itahusisha yanayopaswa kutekelezwa haraka, kwa muda wa kati na kwa muda mrefu. 

Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Chande, alisema kuwa shauku ya wananchi ni kuwa na imani na taasisi za haki jinai nchini na kinachofanywa na tume hiyo kinalenga kufanikisha hilo. 

"Shauku kubwa ya wananchi ni kuona mageuzi katika taasisi za haki jinai na tunatarajia mapendekezo yetu yafanikishe hilo," alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Chande. 

Kwa kipindi cha miezi mitatu takriban wananchi 10,000 wamesikilizwa, mikutano 25 ya hadhara, imefanyika katika Wilaya 53 na Mikoa 25 na tume imefanikiwa kuwasikiliza wadau mbalimbali. 

Akifungua mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab alisema tume hiyo iliundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuangalia njia bora ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini. 

Alisema tume hiyo ina jukumu la kuangalia changamoto zinazokabili taasisi za haki jinai na kupendekeza uboreshaji wa mfumo wa haki jinai nchini. 

Balozi Fatma Rajab alifafanua kuwa tume kama hiyo zimekuwa zikiundwa tangu uhuru wa Tanganyika na maboresho mbalimbali yamefanyika nchini ikiwa ni matokeo ya tume hizo. 

"Tume hii tunatarajia ije na mapendekezo yatakayoboresha mfumo wa haki jinai kulingana na mahitaji ya sasa," alisema Balozi Fatma. 

Pamoja na mambo mengine, Balozi Fatma ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mfumo wa haki jinai nchini unaboreshwa na kuwa imara zaidi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akiwasilisha hotuba yake wakati wa mkutano baina ya Tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini pamoja na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akiwasilisha hotuba yake wakati wa mkutano baina ya Tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini pamoja na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam

Mwenyekiti wa tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohammed Othman Chande akizungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akiongoza mkutano wa tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam
Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Mhe. Manfredo Fanti akichangia jambio wakati wa mkutano wa tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam
Balozi wa Norway Nchini Mhe. Elisabeth Jacobsen akichangia jambio wakati wa mkutano wa tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam

Baadhi ya Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wakifuatilia mkutano baina yao na tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini Jijini Dar es Salaam

Mwenyekiti wa tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohammed Othman Chande (kulia) pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab (kushoto) wakifuatilia mkutano

Mwenyekiti wa tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohammed Othman Chande pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab pamoja na wajumbe wa tume hiyo katika picha ya pamoja na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa 
 


 



Monday, May 1, 2023

WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI YASHIRIKI MAADHIMISHO YA MEI MOSI 2023


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Naibu Waziri Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouku (Mb.) wakijadili jambo muda mfupi baada ya kuhitimishwa ka Sherehe za Maadhimisho ya Mei Mosi 3023

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki terehe 1 Mei 2023 imeungana na maelfu ya Wafanyakazi nchini kusheherekea Maadhimisho ya Mei Mosi 2023 yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. 

Katika maadhimisho hayo ambayo mgeni Rasmi alikuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyoongozwa na kauli mbiu isemayo “Mishahara Bora na Ajira za Staha ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi”, mbali na Mheshimiwa Rais Samia kuzungumza na Wafanyakazi, sherehe za maadhimisho hayo ziliambatana na shughuli mbalimbali kama vile maandamano ya Wafanyakazi, burudani, na maandamano ya magari yaliyokuwa yakionesha huduma zinazotolewa na Taasisi mbalimbali. 

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika sherehe hizo iliwakilishwa na Waziri Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.), Naibu Waziri Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.), Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu Bi. Chiku Kiguhe na Wafanyakazi wengine wa Wizara.

Wakati huo huo Viongozi na Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wametoa pongezi wa Bi. Mary Peter kwa kuwa mfanyakazi Hodari wa Wizara kwa mwaka 2023. Pongezi hizo kwa Bi. Mary Peter zimeambatana na zawadi ya kiasi cha shilingi milioni 5.

Mheshimiwa Rais Samia mbali na kuahidi kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zilizo wasilishwa na Vyama vya Wafanyakazi na kuboresha maslahi ya Wafanyakazi, aliwahimiza Wafanyakazi wote nchini kuendelea kufanya kazi kwa kujituma zaidi kwa kuzingatia weledi, uaminifu na ubunifu ili kuendelea kuleta tija zaidi kwa Taifa. 
Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa na bango la Wizara kwenye Sherehe ya Maadhimisho ya Mei Mosi iliyofanyika Kitaifa mjini Morogoro.

Bw. Shaaban Maganga mfanyakazi wa Wizara akipokea cheti za ushiriki wa michezo ya Mei Mosi 2023


Sehemu ya wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa kwenye Sherehe ya Maadhimisho ya Mei Mosi iliyofanyika Kitaifa mjini Morogoro.