Tuesday, February 2, 2021

MKUTANO WA 38 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA UMOJA WA AFRIKA KUFANYIKA KWA NJIA YA MTANDAO

 


Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika unatarajiwa kufanyika tarehe 3 na 4 Februari, 2021 kwa njia mtandao (video conference).

 Katika Mkutano huo Tanzania itawakilishwa na Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye atashiriki Mkutano huo kutokea makao makuu ya nchi jijini Dodoma. Mkutano huo unafanyika baada ya kukamilika kwa Mkutano wa 41 wa Kawaida wa Kamati ya Uwakilishi ya Kudumu uliofanyika tarehe 20 hadi 26 Januari, 2021.

 Mkutano huo wa kawaida wa siku mbili utaongozwa na kufunguliwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo Mhe. Dr. Naledi Pandor Waziri wa Ushirikiano na Uhusiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini. 

Mkutano huo pamoja na mambo mengine utaandaa rasimu ya agenda za Mkutano wa 34 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika utakaofanyika tarehe 6 na 7 Februari, 2021.

Mkutano huo utajadili na kupitisha mapendekezo ya taarifa ya Mkutano wa 41 wa Kamati ya Kudumu ya Uwakilishi (Permanent Representatives Committee –PRC),taarifa ya hali ya ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID-19) Barani Afrika na taarifa ya Mkutano wa Pamoja wa Kamati ya Baraza la Mawaziri ya Tathimini na Kamati ya Mawaziri 15 wa Fedha.

Mkutano pia utafanya uchaguzi na Uteuzi wa Wajumbe Sita (6) wa Bodi ya Ushauri ya Masuala ya Rushwa ya Afrika, Makamishna wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Majaji wanne (4) wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.

 

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.