Mhe. Bernard K. Membe (MB), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, akifafanua ombi lililotolewa na Tanzania la kuanzishwa kwa
Taasisi ya Kiafrika kuhusu Sheria za Kimataifa (African Institute of
International Law). Ombi hilo lilikubaliwa na Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Umoja wa Afrika (AU) na Taasisi hiyo itaanzishwa hivi karibuni mjini
Arusha. Waziri Membe alikuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini
kwake leo jijini Dar es Salaam.
Mhe. Bernard K. Membe (MB), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uchaguzi wa Mwenyekiti
wa Kamisheni wa Umoja wa Afrika (AU). Pichani ni Bi. Zuhura Bundala
(kulia), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika na Bw. Assah
Waziri Membe aongea kuhusu Kikao cha 18 cha AU
Kikao cha 18 cha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) kimemalizika hivi karibuni mjini Addis Ababa, Ethiopia ambapo kilihudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali wapatao 40, akiwemo Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wakuu hao walitoa msisitizo wa uimarishwaji wa biashara miongoni mwa nchi za Afrika na uhumimu wa uanzishwaji wa Soko Huru Barani Afrika (Continental Free Trade Area – CFTA) ifikapo mwaka 2017.
Hayo yalibainiwa leo na Mhe. Bernard K. Membe (MB), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alipokutana na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Katika mazungumzo yake, Mhe. Membe alisema kuwa Wakuu hao walijadili kwa kina kauli mbiu ya “Kukuza Biashara miongoni mwa Nchi za Afrika – (Boosting Intra-African Trade” na umuhimu wake kwa Bara la Afrika. Ilibainishwa kuwa biashara miongoni mwa nchi za Afrika ni kidogo mno ikilinganishwa na biashara kati ya Afrika na nchi nyingine za nje ya Bara la Afrika.
Aidha, Mhe. Membe alisema Wakuu hao walijadili umuhimu wa uanzishwaji wa Soko Huru Barani Afrika (Continental Free Trade Area- CFTA) ifikapo mwaka 2017, na kwamba uanzishwaji huo utakuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu na kuongeza nafasi za ajira Barani Afrika. Kadhalika, Kamati ya Ngazi ya Juu kuhusu Biashara ya Afrika (High Level African Trade Committee – HATC) ilipendekezwa iwe na jukumu la kuratibu suala hilo na kutanzua vikwazo vinavyoweza kujitokeza, pamoja na kuishirikisha Kamisheni ya Uchumi ya Afrika ya Umoja huo – UNECA na Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank - AfDB) kuisadia Afrika katika utekelezaji wake na hatua zilizokubalika katika kuanzisha CFTA.
Kikao hicho kilifunguliwa rasmi tarehe 29 Januari, 2012 chini ya unyekiti wa Mhe. Theodoro Obiang Nguema Mbasogo, Rais wa Jamhuri ya Equatorial Guinea na kufanyika katika jengo jipya ambalo AU imejengewa na Serikali ya China. Jengo hilo ni zawadi kutoka Serikali hiyo ikiwa ni ishara ya urafiki wa kweli na wa dhati kati ya Afrika na China na lilifunguliwa rasmi tarehe 28 January 2012 na Mhe. Jia Qinglin, Mwenyekiti wa CPPCC (Chinese People’s Political Consultative Conference). Ujenzi wa jengo hilo umegharimu kiasi cha US $200 milioni.
Awali, Kikao hicho kilitanguliwa na vikao viwili: kwanza, Kikao cha Kamati ya Mabalozi, ambacho kilifanyika tarehe 23 hadi 24 Januari, 2012 na; Pili, Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika tarehe 26 hadi 27 Januari, 2012.
Aidha, Wakuu hao wa Umoja wa Afrika walifanya uchaguzi wa nafasi mbalimbali katika Umoja huo na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu amani na usalama Barani Afrika. Katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa AU, Mhe. Boni Yayi, Rais wa Jamhuri ya Benin ndiye aliyechukua nafasi ya uenyekiti huo badala ya Mhe. Rais Mbasogo wa Equatorial Guinea.
Sambamba na uchaguzi wa Benin kuwa Mwenyekiti wa AU, nchi nyingine zilizochaguliwa (Members of the Bureau) kusaidiana na Benin, zilikuwa ni: Uganda kutoka kanda ya Mashariki mwa Afrika (Makamu wa Kwanza wa Mwenyekiti); Tunisia kutoka Kaskazini mwa Afrika (Makamu wa Pili wa Mwenyekiti); Afrika Kusini kutoka kanda ya Kusini mwa Afrika (Makamu wa Tatu wa Mwenyekiti); na Central African kutoka kanda ya Afrika ya Kati (Rappoteur). Nchi nyingine zilizoteuliwa kama wasaidizi katika Drafting Committee ni Burkina Faso, Nigeria, Senegal, Sierra Leone, Ethiopia, Rwanda, Tanzania, Algeria, Libya, Afrika Kusini, Lesotho, Zimbabwe, Cameroon, Gabon na Chad.
Aidha, Wakuu hao walifanya uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU tarehe 30, ambao wagombea wa nafasi hiyo walikuwa ni Mhe. Dkt. Jean Ping, raia wa Gabon, aliyekuwa akitetea nafasi yake, na Mhe. Dkt. Nkosazana Dlamini Zuma, raia wa Afrika Kusini. Jitihada za kupiga kura mara nne za kumchagua Mwenyekiti mpya wa Kamisheni hiyo zilishindikana kufuatana na taratibu za AU za mshindi kupata kura 36 (theluthi mbili ya Nchi Wanachama 53 zinazostahili kupiga kura) na hivyo kukosekana mshindi.
Hivyo, Wakuu wa Nchi na Serikali waliamua kusimamisha uchaguzi huo hadi Kikao kijacho cha Wakuu wa Nchi na Serikali kinachotarajiwa kufanyika mwezi Juni 2012. Aidha, Wakuu wa Nchi na Serikali waliamua kuunda Kamati (Ad-Hoc Committee of Heads of State and Government) ambayo itajumuisha nchi moja kutoka kila kanda chini ya Uenyekiti wa Benin. Katika kamati hiyo, nchi za Gabon na Afrika Kusini zitashiriki. Jukumu la kamati hiyo ni kushughulikia masuala yote yanayohusu uchaguzi unaokuja wa kujaza nafasi katika Kamisheni ya AU.
Aidha, Wakuu hao walifanya uteuzi wa wanachama 10 wa Baraza la Amani na Usalama (Peace and Security Council – PSC) la AU na kuziteua nchi za Cameroon, Congo, Djibouti, Tanzania, Misri, Angola, Lesotho, Cote d’Ivoire, Gambia, Guinea. Nchi hizo zitatumikia PSC kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwezi Machi 2012.
Katika mjadala wa suala la amani na usalama Barani Afrika, Kikao hicho pia kilijadili kwa kirefu juhudi zinazofanyika katika kutafuta suluhu za migogoro na maendeleo ya nchi mbalimbali zikiwemo Tunisia, Misri na Libya. Kuhusu nchi ya Madagascar, Wakuu hao walipongeza juhudi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa nchi za Afrika (SADC) kwa hatua ya kutafuta suluhu ya mgogoro na kuifikisha nchi hiyo kusaini mpangilio wa kumaliza mgogoro uliyofanyika tarehe 16 September, 2011.
Kuhusu Somalia, Wakuu wa Nchi na Serikali walielezea pia kuridhishwa kwao na hatua iliyofikiwa katika kutafuta suluhu nchini humo. Aidha, waliunga mkono hatua ya kuimarisha AMISOM pamoja na vikundi vya TFG. Vile vile, walihimiza wadau wa AU kuunga mkono juhudi zinazoendelea. Mwisho, walionyesha matumaini yao kwa Mkutano kuhusu Somalia unaotarajiwa kufanyika London tarehe 23 Februari, 2012.
Kadhalika, kuhusu Sudan, Wakuu hao waliisifu AU-UN Hybrid Operation in Darfur (UNAMID) kwa mchango wake katika kutafuta amani na usalama katika Darfur. Aidha, Wakuu wa Nchi na Serikali walilaani mapigano yanayoendelea katika maeneo ya Blue Nile na Kordofan.
Wakuu hao pia walielezea masikitiko yao ya hali inayoendelea ati ya nchi mbili za Sudan na Sudan Kusini. Hivyo, walizitaka nchi hizo mbili kuacha mara moja hatua binafsi wanazochukua kuhusiana na mafuta, ambayo inaweza kuleta athari katika mahusiano ya nchi hizo.
Nchi ya Tanzania ilikuwa ni mojawapo ya nchi zilizowasilisha agenda wakati wa Kikao cha 18 cha Wakuu wa Nchi na Serikali. Agenda ya kwanza ilihusu ombi la Tanzania kuwa mwenyeji wa Sekretarieti ya AU ya Bodi ya Ushauri dhidi ya Rushwa (AU Advisory Board on Corruption). Wakuu wa Nchi na Serikali kwa kutambua umuhimu wa Bodi hiyo kushirikiana na Koti ya Afrika inayohusu Haki za Binadamu na Watu (African Court on Human and People’s Rights), ambayo iko Arusha, Tanzania, katika kuimarisha njia za kuzuia, kupiga vita na kuondoa rushwa Barani Afrika, walikubaliana kwa kauli moja na kuiteua Tanzania iwe mwenyeji wa Bodi hiyo ikiwa na makazi mjini Arusha.
Agenda ya pili ilihusu ombi la Tanzania kuanzisha Taasisi ya Kiafrika kuhusu Sheria za Kimataifa (African Institute of Internatinal Law). Kwa kuzingatia umuhimu wa Taasisi hiyo siyo tu kwa Nchi Wanachama bali pia kwa Kamisheni ya AU, Wakuu wa Nchi na Serikali walikubali kuwa Taasisi hiyo pia ianzishwe mjini Arusha, Tanzania.
Kikao kifuatacho cha 19 kinatarajiwa kufanyika Lilongwe nchini Malawi, mwezi Juni 2012.