Ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Diaspora, wakiwemo Washiriki Wakuu kutoka Tanzania. Kutoka kushoto walioketi ni Bw. Michael Kmba,Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Balozi Bertha Semu-Somi (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora - Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Ali Saleh (wa tatu kushoto), Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Oman, na Balozi Simba Yahya (wa nne kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Wengine katika picha ni Bw. Olal Kungu (wa pili kulia), Kamishna wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, na Bw. Shariff Sharrif (kulia), Mkurugenzi-ZIPA kutoka Zanzibar.
Baadhi ya Watanzania waishio nchini Oman wakisikiliza kwa makini wakati wa Ufunguzi wa Mkutano unaoghusia masuala ya Diaspora yakiwemo uwekezaji katika sekta mbalimbali za kuinua maendeleo ya uchumi nchini Tanzania.
Balozi Simba Yahya (kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akipokea maoni kutoka kwa Watanzania wenye asili ya Oman kuhusu ushiriki wao kwenye maendeleo ya kuinua uchumi nchini Tanzania.
Bi. Patricia Nguma (kulia), kutoka Benki ya Afrika (BOA), akijadiliana na Mdau wa Diaspora kuhusu mikopo ya nyumba inayotolewa na BOA.
Bw. Hassan Hafidh (katikati) kutoka Ofisi ya Rais-Diaspora Zanzibar, akizungumza na wadau wa Diapsora juu ya mipango ya Serikali ya Mapinduzi wa Zanzibar kwa Watanzania wenye asili ya Zanzibar waishio nje.
Bw. Boniface Ngowi wa Wizara ya Viwanda na Biashara akitoa maelezo kwa Watanzania waishio Oman kuhusu Sera za Biashara nchini Tanzania.
Mkutano Kati ya Ujumbe kutoka Tanzania na Watanzania waishio Oman (Diaspora)Wafana Jijini Muscat.
Na RAINMAN,
Muscat, Oman
Mkutano wa Diaspora kati ya Watanzania waishio nchini Oman na Ujumbe wa Serikali, Taasisi za Serikali na zile Binafsi kutoka Tanzania na Zanzibar umemalizika kwa mafanikio makubwa jana mjini Muscat. Mkutano huo ulianza rasmi tarehe 20 na kumalizika tarehe 22 Desemba 2012.
Mkutano huo uliitishwa kufuatia maazimio yaliyofikiwa katika Mkutano uliopita kati ya Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania waishio Oman. Katika Mkutano huo, Rais Kikwete aliwashawishi Watanzania hao kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi nchini Tanzania.
Aidha, Mhe. Rais aliwaahidi Watanzania hao kuwa atatuma timu ya wataalamu kutoka sekta mbalimbali nchini Tanzania kukutana nao mapema iwezekanavyo, ili wapate fursa ya kuelimika na kupatiwa maelezo mbalimbali kuhusu fursa zilizoko nyumbani.
Vilevile, Mhe. Rais Kikwete aliwaambia Watanzania hao waitumie fursa hiyo kueleza ni changamoto zipi zinazowakwamisha kutoa mchango wao wa kujenga na kuinua maendeleo ya uchumi nchini Tanzania.
Katika Mkutano huo uliomalizika jana mjini Muscat, Watanzania hao walipata fursa ya kukutanishwa na Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Balozi Bertha Semu-Somi, Mkurugenzi wa Masuala ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, pamoja na wadau kutoka Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Rais - Menejimenti na Utumishi wa Umma, Wizara ya Miundombinu na Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni.
Ujumbe kutoka Tanzania ulijumuisha wadau kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Ofisi ya Rais inayoshughulikia masuala ya Diaspora Zanzibar na Tume ya Mipango Zanzibar. Vilevile Taasisi za Serikali za TBC,TIC,TCRA, EPZA, ZIPA, UHAMIAJI, TTB,TANAPA na Dar es Salaam Maritime Institute. Sekta binafsi zilijumuisha TPSF, BOA, Azania Bank, CRDB, PBZ, Uhuru One, Zanzibar Insurance Corporation na Zanzibar Chamber of Commerce.
Aidha, Watanzania wa Diaspora nchini Oman walipewa maelezo na ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo namna ya kuanzisha mawasiliano yenye lengo la kukuza ushirikiano wa kibiashara.
Masuala muhimu yaliyojitokeza katika Mkutano huo ni pamoja na haja ya kuanzishwa kwa Chama cha Watanzania waishio nchini Oman.
Oman ni nchi ambayo wananchi wake wengi wana asili ya Tanzania kutokana na uhusiano wa kihistoria baina ya nchi hizi mbili. Inakadiriwa kuwa familia 780 za Watanzania wanaishi nchini Oman na kuendesha shughuli zao katika sekta binafsi na Serikali.
Mwisho.