Saturday, March 15, 2014

WAZIRI MEMBE AENDESHA KIKAO CHA MAWAZIRI WA NCHI ZA JUMUIYA YA MADOLA


Mhe. Bernard Membe akiendesha kikao cha 43 cha Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumiya ya Madola Jijini London Uingereza. 

Mawaziri wa Kikosi Kazi cha Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola wakiwa kwenye mazungumzo na Waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza Kikao cha 43 cha chombo hicho.




Kikao cha arobaini na tatu cha Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Jumuiya ya Madola kimeipunguzia adhabu nchi ya Fiji na hivyo kuiruhusu kushiriki kwenye baadhi ya matukio ikiwemo michezo ya Jumuiya ya Madola ya mwaka 2014.

Kikao hicho kilichofanyika Jijini London Uingereza chini ya uenyekiti wa  Mhe. Bernard Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania kilifikia uamuzi huo baada ya kupitia na kuridhishwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Fiji katika kujiandaa na uchaguzi mkuu ujao ikiwa ni jitihada za kutetea uanachama wake ndani ya jumuiya hiyo.

Akiongoza mjadala huo, Mhe. Membe alisifu hatua za makusudi zilizochukuliwa na nchi hiyo kama vile kushugulikia masuala ya haki za binadamu na utawala bora, kuanzisha daftari la kudumu la wapiga kura, kuandaa mazingira ya uwazi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Septemba 2014 ikiwemo kuandaa mazungumzo na wadau mbalimbali wa siasa na aliyekuwa Waziri Mkuu aliyeingia kijeshi kujiuzulu na kugombea kama raia.

Akiendesha kikao hicho cha kwanza kama mwenyekiti wa chombo hicho muhimu, Mhe. Membe alisisitiza umuhimu wa kikosi kazi hicho kutekeleza majukumu yake bila urasimu na ubaguzi bali kwa kutoa fursa sawa za ushiriki wa nchi wanachama na kuzingatia misingi ya haki kwa manufaa ya wanachama wote.

Mhe. Membe pia aliwasisitizia mawaziri wenzake wanaotumikia chombo hicho kuwa makini na kuheshimu mila na desturi za nchi wanachama hususan zile za Kiafrika na kuepuka kushinikiza ajenda ambazo zinagusa dini, tamaduni na mila za nchi nyingi za kiafrika, kama vile ndoa za jinsia moja. Alisema kwa kufanya hivyo Jumuiya ya Madola itahatarisha muungano na mshikamano uliopo sasa ndani ya jumuiya hiyo.

Aidha Mhe. Membe alisema hazina kubwa ya Jumuiya ni wingi wa nchi wanachama na tamaduni na desturi mbalimbali zinazowakilishwa na wanajumuiya. Hivyo kuheshimu tamaduni zote ndio kutajenga heshima ya Jumuiya ya Madola kimataifa.

Akiwashukuru wajumbe wa kikosi kazi kama mwenyekiti, Mhe. Membe alisema jukumu la uenyekiti wa chombo hicho si dogo, lakini wajumbe wa chombo hicho wakiungana kwa pamoja na kwa msaada wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola anahakika ndani ya miaka miwili ya uenyekiti wake Jumuiya hiyo itaendelea kusimamia misingi muhimu ya jumuiya hiyo bila kutetereka.

Mhe. Membe amewakilisha Tanzania kama Waziri mwenye dhamana kuanzia mwaka 2011 akiwa kama mjumbe, na mwaka 2013 Jijini Kolombo Sri Lanka alichaguliwa bila kupingwa kuwa mwenyekiti kwa miaka miwili. Waziri wa Mambo ya Nje wa New Zealand Mhe. Murray McCully alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti.

Ukiacha Tanzania na New Zealand, wajumbe wengine ni mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi saba ambazo ni Cyprus, Guyana, India, Pakistan, Sierra Leone, Visiwa vya Solomon na Sri Lanka ambao wanaingia kwa nafasi yao ya uenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Madola.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa

Wednesday, March 12, 2014

Katibu Mkuu amkabidhi Hati za kazi Mwakilishi wa Heshima wa Mauritius hapa nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John M. Haule kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akimkabidhi  Bw. Syed Nazre Abbas Rizvi Hati zinazomwezesha kufanya kazi kama Mwakilishi wa Heshima wa Mauritius nchini Tanzania. Makabidhiano hayo yalifanyika Ofisini kwa Katibu Mkuu tarehe 12 Machi, 2014. 
Bw. Syed Nazre Abbas Rizvi akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kupokea kibali cha kuwa Mwakilishi wa Heshima wa Mauritius hapa nchini
Katibu Mkuu,  Bw.  Haule akizungumza na  Bw. Syed Nazre Abbas Rizvi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bw. John Haule akiagana na Bw. Syed Nazre Abbas Rizvi mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.



Picha na Reginald Philip

Tuesday, March 11, 2014

Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC waendelea nchini Malawi



Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC, Mhe. Ephraim Chiume (kushoto) akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC ulioanza jana tarehe 10 Machi, 2014 jijini Lilongwe, Malawi.

Mhe. Chiume akiendelea na hotuba ya ufunguzi, kushoto ni Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Stergomena Tax

Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Salum (Mb) mwenye ushungi. Waziri wa Nchi wa Serikali ya Zanzibar anayeshughulikia masuala ya Utawala Bora, Mhe. Mwinyi Haji Makame (kushoto) na Mhe. Janeth Mbene (Mb), Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara wakiwa katika chumba cha mkutano.
Wajumbe wa mkutano.

Picha ya Pamoja ya Baraza la Mawazri  wa SADC. Waliokaa wa kwanza kutoka kushoto ni Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Salum

Mhe Tax Aainisha mafanikio ya SADC katika kipindi cha mwaka 2013/2014

Na Ally Kondo, Lilongwe

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Stergomena Tax aeleza mafanikio ya SADC katika kipindi cha utekelezaji wa bajeti na Mpango Kazi wa Jumuiya hiyo kwa mwaka 2013/2014. Mhe. Tax alitoa maelezo hayo mbele ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC ambao ni wa kwanza kushiriki tangu alipochaguliwa kushika wadhifa huo.  Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC unafanyika Lilongwe, Malawi na unatarajiwa kukamilika tarehe 11 Machi, 2014.

Mhe. Tax ambaye ni Mtanzania alisema kuwa SADC ilitekeleza kikamilifu na kwa mafanikio makubwa mpango kazi wa kusuluhisha mgogoro wa Madagascar. Hivyo alitumia fursa hiyo kuipongeza Madagascar, kurejeshewa uanachama wa SADC baada ya kufanya uchaguzi wa amani  kati ya mwezi Oktoba na Desemba, 2013 ambao umerejesha utawala wa Katiba katika nchi hiyo.
SADC pia katika kipindi hicho, ilituma timu za waangalizi wa uchaguzi katika chaguzi za Madagascar, Swaziland na Zimbabwe. Katika nchi zote hizo, waangalizi wa uchaguzi hao walikamilisha majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.

Sanjari na hayo, SADC imeendelea kujadiliana na COMESA na EAC kuhusu ushirikiano wa kuanzisha Soko Huru la Pamoja baina ya nchi za jumuiya hizo. Awamu ya kwanza ya majadiliano hayo yanatarajiwa kukamilika mwaka 2015.

Aidha, SADC inajivunia kuanza kwa utekelezaji wa Itifaki ya Jinsia na Maendeleo katika nchi wanachama. Itifaki hiyo imeanza kutekelezwa baada ya theluthi mbili ya nchi za SADC kuidhinisha Itifaki hiyo.
SADC pia inakamilisha Rasimu ya Itifaki kuhusu kuanzisha upya Mahakama ya SADC.  

Katika orodha hiyo ya mafanikio, SADC pia imeweza kuwa na chombo cha kuandaa miradi ya maendeleo, chombo ambacho kitasaidia kubuni miradi makini itakayoweza kupata fedha kutoka taasisi za fedha. Sambamba na hili, SADC imeandaa Mpango Mkuu wa miradi ya miundombinu.

Katika mkutano huo, Mhe. Tax alitaja pia maeneo yatakayopewa kipaumbele katika Mwaka wa Fedha 2014/2015. Maeneo hayo ni pamoja na: kuimarisha soko huru katika nchi za SADC; majadiliano ya utatu wa kuanzisha Soko huru la pamoja la nchi za EAC, COMESA na SADC;  maendeleo ya viwanda na maendeleo ya miundombinu katika ushirikiano wa utatu (EAC,SADC, COMESA) na utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Kikanda wa Maendeleo ya Miundombinu.

Vipaumbele vingine ni: utekelezaji wa mikakati ya kikanda ili kuboresha upatikanaji wa uhakika wa chakula (food security); kuhamasisha na kujenga amani pamoja na kuimarisha demokrasia na utawala bora katika Kanda ya SADC; na kutekeleza mikakati ya pamoja ya kukabiliana na ugonjwa wa UKIMWI. 



Monday, March 10, 2014

Tanzania na Malawi zasaini Mkataba wa kuanzisha Kituo cha Pamoja cha Uhamiaji na Ushuru wa Forodha




Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Salum (Mb), kushoto na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Malawi, Mhe. Sosten Gwengwe wakisaini Mkataba wa kuanzisha Kituo cha Pamoja cha Uhamiaji na Ushuru wa Forodha katika mpaka wa Songwe - Kasumulu. Hafla ya uwekaji saini imefanyika katika Ofisi ya Wizara ya Biashara na Viwanda, Lilongwe, Malawi tarehe 10 Machi, 2014.




Mhe. Salum, kulia akitoa neno baada ya shughuli za kusaini Mkataba kukamilika. Anayemsikiliza ni Waziri wa Biashara na Viwanda wa Malawi, Mhe. Gwengwe.



Maafisa wa Tanzania na Malawi wakifanya maandalizi kabla ya Mawaziri kuwasili kwa ajili ya shughuli ya uwekaji saini Mkataba

Waziri wa Nchi wa Serikali ya Zanzibar anayeshughulikia Masuala ya Utawala Bora, Mhe. Mwinyi Haji Makame naye alishuhudia hafla ya uwekaji saini. hapa Mhe. Makame akisaini Kitabu cha wageni alipowasili katika ofisi za Wizara ya Biashara na Viwanda nchini Malawi.

 
Maneno aliyosema Waziri wa Fedha baada ya uwekaji saini
 
Na Ally Kondo. Lilongwe
Nchi za Afrika zimehimizwa kufanya biashara baina yao ili kujiletea maendeleo, badala ya kusubiri misaada isiyokuwa na uhakika kutoka nchi wahisani. Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Salum (Mb) wakati wa hafla ya uwekaji saini Mkataba wa kuanzisha Kituo cha Pamoja cha Uhamiaji na Ushuru wa Forodha cha Songwe – Kasumulu kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Malawi.
 Uwekaji saini huo ulifanyika Lilongwe, Malawi siku ya Jumatatu tarehe 10 Machi, 2014 ambapo Mhe Salum aliwela saini kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, wakati Waziri wa Biashara na Viwanda, Mhe.  Sosten Gwengwe aliweka saini kwa niaba ya Serikali ya Malawi.
Mhe. Salum alieleza kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho, kutasaidia, sio tu kupunguza gharama za kufanya biashara kati ya Tanzania na Malawi bali pia kutaimarisha uhusiano baina ya watu wa nchi hizi mbili ambao kimsingi wana utamaduni unaofanana.
Mhe. Waziri aliwataka wataalamu wa pande zote mbili kuandaa mpango kazi wa kutekeleza Mkataba huo haraka iwezekanavyo ili wananchi na Serikali waone matunda yake badala ya kuishia katika makaratasi.
Alipoulizwa na wanahabari kutoa maoni kuhusu utekelezaji wa Mkataba huo, Mhe Wazri aliwahakikishia wananchi wa Malawi na Tanzania kwa ujumla kuwa kituo hicho kitafanya kazi kama ilivyokusudiwa na hakuna tishio lolote la kuvurugika kwa uhusiano kati ya nchi hizi mbili.
Kwa upande wake, Mhe. Gwengwe alifarijika na uanzishwaji wa kituo hicho, kwa kuwa kitarahisisha usafirishaji wa bidhaa kwa haraka kutoka Tanzania kuingia Malawi ambayo haina Bandari.
Uwekaji saini wa Mkataba huo umeenda sambamba na mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo Mhe. Salum anaongoza ujumbe wa Tanzania. Mkutano huo ulioanza na vikao vya Makatibu Wakuu unatarajiwa kukamilika tarehe 11 Machi, 2014.
 
 

Saturday, March 8, 2014

Wanawake Mambo ya Nje washiriki Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani

Wanawake wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wameungana na Wanawake wengine kote duniani katika kusheherekea Siku ya Wanawake Duniani, iliyofanyika katika Viwanja vya Mwembe Yanga Temeke, jijini Dar es Salaam. Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo alikuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Hawa Ghasia (Mb.). Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni "CHOCHEA MABADILIKO KULETA USAWA WA KIJINSIA"
Wanawake wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakiwa na nyuso za furaha wakati wa maadhimisho hayo.
Wanawake wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakiwa katika maandamano.
 Mhe. Ghasia (wa tatu kutoka kushoto) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Said Mecky Sadick pamoja na wageni waalikwa katika jukwaa wakiwashangilia Wanawake wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (hawapo pichani) walipokuwa wakipita mbele yao .
Wanawake wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakipita mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakiwa wamejawa na furaha.
Wanawake  kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakiwa katika Picha ya Pamoja
Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bibi Amisa Mwakawago akiwaongoza wanawake wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Kimataifa kutoka uwanjani mara baada ya maadhimisho.
Picha na Reginald Kisaka


Thursday, March 6, 2014

Balozi Mdogo wa Tanzania, Dubai atembelewa na Balozi Mdogo wa Ethiopia

Mhe. Mjenga akimkaribisha ofisini kwake Balozi Mdogo wa Ethiopia Mhe. Yibeltal Alemu.
Wakiwa katika mazungumzo, walipata fursa ya kuzungumzia njia muafaka na mbalimbali za kufanya kazi kwa karibu ili kuhakikisha wanavutia utalii na uwekezaji katika nchi zao hasa kwa kuwavutia wawekezaji wakubwa waliopo Dubai
Mhe. Mjenga alimuomba Mhe. Yibeltal kubadilishana uzoefu wa Ethiopia katika kuvutia wawekezaji kutoka Dubai katika sekta ya kilimo. Pia aliomba Maafisa wa Biashara kutoka Balozi zote mbili wakutane ili kubadilishana uzoefu huo ili Tanzania nayo iweze kuchukua mkondo huo kuwavutia wawejezaji kwenye kilimo.


 


Wednesday, March 5, 2014

Mhe. Rais Kikwete akutana kwa mazungumzo na Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Ufaransa


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Waziri wa Biashara za Kimataifa wa Ufaransa, Mhe. Nicole Bricq mara baada ya Waziri huyo kuwasili Ikulu. Mhe. Bricq ameitembelea Tanzania kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya nchini hizi mbili.
Mhe. Rais Kikwete katika mazungumzo na Mhe.Bricq
Mhe. Rais Kikwete akimsikiliza Mhe.Bricq wakati wa mazungumzo yao.

Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dora Msechu pamoja na Wajumbe wengine wakifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Rais Kikwete pamoja na Waziri wa Biashara za Kimataifa wa Ufaransa (hawapo pichani).
Balozi wa Ufaransa (katikati) nchini Tanzania pamoja na Ujumbe uliofuatana na Mhe. Bricq wakifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Rais Kikwete na Mgeni wake Mhe. Bricq hawapo pichani.
Mhe. Bricq akimkabidhi Mhe. Rais Kikwete ujumbe aliokuja nao.
Mhe. Rais Kikwete akiongozana na Mhe. Bricq mara baada ya mazungumzo
Mhe. Rais Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Bricq, na wajumbe wengine.

Picha na Reginald Kisaka



Tuesday, March 4, 2014

PRESS RELEASE


PRESS RELEASE

H.E Jakaya Mrisho Kikwete, President of the United Republic of Tanzania has sent a condolence message to H.E. Xi Jinping, President of the People’s Republic of China following a terrorist attack that killed 28 people and injuring more than 130 others. 
The message reads as follows;
“H.E. Xi JINPING,
President of the People´s Republic of China,
BEIJING.

Your Excellency and Dear Friend,
I have received with great shock and sadness, the devastating news on the terrorist attack that occurred on the 1st March, 2014, at the square and ticket hall of the Railway Station of Kunming, Capital of China´s South West Yunnan Province, killing at least 28 civilians and injuring more than 130 others.
In this tragic moment and ordeal, I wish, on behalf of the Government and People of the United Republic of Tanzania, and indeed on my own behalf, to convey our deepest condolences to Your Excellency, and through you, to the Government and People of China, especially the family of the victims who have lost their loved ones and who have been severely injured by the attacks.
My government strongly condemns the attacks and calls for the perpetrator to be brought to justice to face the crimes committed.
During this period of mourning, we share with you, your pain over this irreparable loss and pray to the Almighty God to comfort the bereaved families and grant the People of China courage and fortitude to carry on with their daily lives.
May God the Almighty rest the souls of the deceased in eternal peace.
Please accept your Excellency and Dear Friend, the assurances of my highest consideration”.

ISSUED BY: THE MINISTRY OF FOREIGN AFFAIRS AND INTERNATIONAL COOPERATION, DAR ES SALAAM
4TH MARCH, 2014

Monday, March 3, 2014

Mhe. Membe ashuhudia mpambano kati ya Yanga na Al Ahly ya Misri

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akifuatilia kwa makini pambano la mpira wa miguu kati ya Timu ya Yanga ya Tanzania na Al Ahly ya Misri (hawapo pichani) lilifanyika katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Mhe. Membe alikuwa mgeni rasmi wakati wa pambano hilo ambapo Timu ya Yanga ilijipatia ushindi wa goli 1-0.
Mhe. Membe aliposhindwa kujizuia kusimama wakati Timu ya Yanga (hawapo pichani) ikielekea kufunga goli. Pembeni yake ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Said Mecky Sadick.
Mhe. Membe kwa pamoja na Mhe. Mecky Sadick wakifurahia goli pekee lililofungwa na Timu ya Yanga  dhidi ya Al Ahly ya Misri.