Tuesday, March 11, 2014

Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC waendelea nchini Malawi



Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC, Mhe. Ephraim Chiume (kushoto) akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC ulioanza jana tarehe 10 Machi, 2014 jijini Lilongwe, Malawi.

Mhe. Chiume akiendelea na hotuba ya ufunguzi, kushoto ni Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Stergomena Tax

Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Salum (Mb) mwenye ushungi. Waziri wa Nchi wa Serikali ya Zanzibar anayeshughulikia masuala ya Utawala Bora, Mhe. Mwinyi Haji Makame (kushoto) na Mhe. Janeth Mbene (Mb), Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara wakiwa katika chumba cha mkutano.
Wajumbe wa mkutano.

Picha ya Pamoja ya Baraza la Mawazri  wa SADC. Waliokaa wa kwanza kutoka kushoto ni Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Salum

Mhe Tax Aainisha mafanikio ya SADC katika kipindi cha mwaka 2013/2014

Na Ally Kondo, Lilongwe

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Stergomena Tax aeleza mafanikio ya SADC katika kipindi cha utekelezaji wa bajeti na Mpango Kazi wa Jumuiya hiyo kwa mwaka 2013/2014. Mhe. Tax alitoa maelezo hayo mbele ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC ambao ni wa kwanza kushiriki tangu alipochaguliwa kushika wadhifa huo.  Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC unafanyika Lilongwe, Malawi na unatarajiwa kukamilika tarehe 11 Machi, 2014.

Mhe. Tax ambaye ni Mtanzania alisema kuwa SADC ilitekeleza kikamilifu na kwa mafanikio makubwa mpango kazi wa kusuluhisha mgogoro wa Madagascar. Hivyo alitumia fursa hiyo kuipongeza Madagascar, kurejeshewa uanachama wa SADC baada ya kufanya uchaguzi wa amani  kati ya mwezi Oktoba na Desemba, 2013 ambao umerejesha utawala wa Katiba katika nchi hiyo.
SADC pia katika kipindi hicho, ilituma timu za waangalizi wa uchaguzi katika chaguzi za Madagascar, Swaziland na Zimbabwe. Katika nchi zote hizo, waangalizi wa uchaguzi hao walikamilisha majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.

Sanjari na hayo, SADC imeendelea kujadiliana na COMESA na EAC kuhusu ushirikiano wa kuanzisha Soko Huru la Pamoja baina ya nchi za jumuiya hizo. Awamu ya kwanza ya majadiliano hayo yanatarajiwa kukamilika mwaka 2015.

Aidha, SADC inajivunia kuanza kwa utekelezaji wa Itifaki ya Jinsia na Maendeleo katika nchi wanachama. Itifaki hiyo imeanza kutekelezwa baada ya theluthi mbili ya nchi za SADC kuidhinisha Itifaki hiyo.
SADC pia inakamilisha Rasimu ya Itifaki kuhusu kuanzisha upya Mahakama ya SADC.  

Katika orodha hiyo ya mafanikio, SADC pia imeweza kuwa na chombo cha kuandaa miradi ya maendeleo, chombo ambacho kitasaidia kubuni miradi makini itakayoweza kupata fedha kutoka taasisi za fedha. Sambamba na hili, SADC imeandaa Mpango Mkuu wa miradi ya miundombinu.

Katika mkutano huo, Mhe. Tax alitaja pia maeneo yatakayopewa kipaumbele katika Mwaka wa Fedha 2014/2015. Maeneo hayo ni pamoja na: kuimarisha soko huru katika nchi za SADC; majadiliano ya utatu wa kuanzisha Soko huru la pamoja la nchi za EAC, COMESA na SADC;  maendeleo ya viwanda na maendeleo ya miundombinu katika ushirikiano wa utatu (EAC,SADC, COMESA) na utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Kikanda wa Maendeleo ya Miundombinu.

Vipaumbele vingine ni: utekelezaji wa mikakati ya kikanda ili kuboresha upatikanaji wa uhakika wa chakula (food security); kuhamasisha na kujenga amani pamoja na kuimarisha demokrasia na utawala bora katika Kanda ya SADC; na kutekeleza mikakati ya pamoja ya kukabiliana na ugonjwa wa UKIMWI. 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.