Saturday, March 15, 2014

WAZIRI MEMBE AKUTANA NA MABALOZI WA NCHI ZA KIAFRIKA WANACHAMA WA JUMUIYA YA MADOLA


Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania kwenye mazungumzo na Mabalozi wa Nchi za Kiafrika Wanachama wa Jumuiya ya Madola Jijini London, Uingereza. 



Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Mhe. Peter Kallaghe akimkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola Mhe.Bernard Membe kwenye mazungumzo mjini London, Uingereza.


Mhe. Bernard Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ametoa wito kwa Nchi za Kiafrika Wanachama wa Jumuiya ya Madola kuunganisha nguvu na kuwa na sauti moja itakayotetea maslahi ya nchi za kiafrika kwenye jumuiya hiyo.

Mhe. Membe aliyasema hayo alipokutana na Mabalozi wa Nchi 12 za Kiafrika wanaowakilisha nchi zao kwenye Jumuiya ya Madola pembezoni mwa Mkutano wa Kikosi Kazi cha Mawaziri cha jumuiya hiyo kilichofanyika Jijini London Uingereza tarehe 13-14 Machi 2014.

Kwenye mazungumzo yao Mhe. Membe aliwakumbusha Mabalozi hao chimbuko la jumuiya hiyo na ushiriki wa nchi za kiafrika ili kutetea maslahi ya Waafrika na hatimaye kuvuna matunda ya ushiriki wa Waafrika kwenye Jumuiya ya Madola.

“Kama wanachama kutoka Bara la Afrika, ni wajibu wetu kushikamana na hata pale mwanachama mmoja anapotolewa au anapowekewa vikwazo vya ushiriki, tuungane na kuhakikisha mwanachama huyo anaondolewa vikwazo na hatimaye kurudi kwenye jumuiya. Tusipofanya hivyo hata sisi tutakuwa na tatizo” alisema Mhe. Membe.

Aliwaasa kuwa na sauti moja katika kutetea haki za ushiriki wa nchi za Kiafrika ndani ya jumuiya hiyo. Alisema namba ya nchi za Afrika kwenye jumuiya hiyo ni kubwa na hivyo ushiriki wa Waafrika lazima uwe wa kushindo.

Alisisitiza kuwa na sauti moja ya Waafrika kutakemea masuala yanayokuja kama shinikizo kutoka wanachama wa Nchi za Magharibi kama vile ndoa za jinsia moja, ambayo yanagusa dini, tamaduni, mila na desturi za Kiafrika. Alisema upepo wa shinikizo hilo unavuma kwa kasi kana kwamba kukubaliana na masuala hayo kutaondoa umaskini barani Afrika. Nchi za Kiafrika kwenye Jumuiya hiyo zina wajibu wa kushiriki kikamilifu kwa kusimamia agenda zitakazoleta maendeleo barani Afrika.

Ili kufanikisha wajibu huo, Mhe. Membe aliwahimiza Mabalozi hao kushiriki  kwenye chaguzi mbalimbali za jumuiya, kutoa taarifa kwa Wakuu wa Nchi na Serikali zao kutoka Makao Makuu ya Sekretarieti ya Jumuiya hiyo yaliyopo London Uingereza na mwisho kuhakikisha wanashiriki kikamilifu na kutoa sauti ya pamoja kwenye shuguli mbalimbali za Jumuiya badala ya kusubiri wengine wafanye maamuzi kwa niaba yao.

Kwa upande wao, mabalozi hao walimpongeza Mhe. Membe kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Mawaziri cha jumuiya hiyo kwa kipindi cha miaka miwili. Aidha walisifu jitihada za Tanzania kutetea maslahi ya nchi za Kiafrika wanachama wa jumuiya hiyo. 

Kwa upande mwingine walilalamikia uongozi wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola kwa kutoshirikiana na mabalozi hao hususan kwenye maandalizi ya Vikao vya Wakuu wa Nchi na Serikali wanachama au baada ya vikao hivyo. Waliongeza kuwa kero za kiutendaji zinafanyiwa kazi juu juu tu na badala yake zinazua kero kubwa zaidi. Hivyo walimuomba Mhe. Membe kuwasaidia kwa kupitia Vikao vya Kikosi Kazi cha Mawaziri kuondoa changamoto hizo.

Ndani ya Jumuiya ya Madola kuna nchi za Kiafrika 18 ambapo 12 kati ya hizo zilizoshiriki kwenye mkutano huo ni; Mauritius, Cameroon, Seychelles, Namibia, South Africa, Uganda, Kenya, Mozambique, Ghana, Lesotho, Zambia na Tanzania. Jumuiya ya Madola ina jumla ya nchi 53.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.