Saturday, March 15, 2014

WAZIRI MEMBE AENDESHA KIKAO CHA MAWAZIRI WA NCHI ZA JUMUIYA YA MADOLA


Mhe. Bernard Membe akiendesha kikao cha 43 cha Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumiya ya Madola Jijini London Uingereza. 

Mawaziri wa Kikosi Kazi cha Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola wakiwa kwenye mazungumzo na Waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza Kikao cha 43 cha chombo hicho.




Kikao cha arobaini na tatu cha Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Jumuiya ya Madola kimeipunguzia adhabu nchi ya Fiji na hivyo kuiruhusu kushiriki kwenye baadhi ya matukio ikiwemo michezo ya Jumuiya ya Madola ya mwaka 2014.

Kikao hicho kilichofanyika Jijini London Uingereza chini ya uenyekiti wa  Mhe. Bernard Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania kilifikia uamuzi huo baada ya kupitia na kuridhishwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Fiji katika kujiandaa na uchaguzi mkuu ujao ikiwa ni jitihada za kutetea uanachama wake ndani ya jumuiya hiyo.

Akiongoza mjadala huo, Mhe. Membe alisifu hatua za makusudi zilizochukuliwa na nchi hiyo kama vile kushugulikia masuala ya haki za binadamu na utawala bora, kuanzisha daftari la kudumu la wapiga kura, kuandaa mazingira ya uwazi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Septemba 2014 ikiwemo kuandaa mazungumzo na wadau mbalimbali wa siasa na aliyekuwa Waziri Mkuu aliyeingia kijeshi kujiuzulu na kugombea kama raia.

Akiendesha kikao hicho cha kwanza kama mwenyekiti wa chombo hicho muhimu, Mhe. Membe alisisitiza umuhimu wa kikosi kazi hicho kutekeleza majukumu yake bila urasimu na ubaguzi bali kwa kutoa fursa sawa za ushiriki wa nchi wanachama na kuzingatia misingi ya haki kwa manufaa ya wanachama wote.

Mhe. Membe pia aliwasisitizia mawaziri wenzake wanaotumikia chombo hicho kuwa makini na kuheshimu mila na desturi za nchi wanachama hususan zile za Kiafrika na kuepuka kushinikiza ajenda ambazo zinagusa dini, tamaduni na mila za nchi nyingi za kiafrika, kama vile ndoa za jinsia moja. Alisema kwa kufanya hivyo Jumuiya ya Madola itahatarisha muungano na mshikamano uliopo sasa ndani ya jumuiya hiyo.

Aidha Mhe. Membe alisema hazina kubwa ya Jumuiya ni wingi wa nchi wanachama na tamaduni na desturi mbalimbali zinazowakilishwa na wanajumuiya. Hivyo kuheshimu tamaduni zote ndio kutajenga heshima ya Jumuiya ya Madola kimataifa.

Akiwashukuru wajumbe wa kikosi kazi kama mwenyekiti, Mhe. Membe alisema jukumu la uenyekiti wa chombo hicho si dogo, lakini wajumbe wa chombo hicho wakiungana kwa pamoja na kwa msaada wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola anahakika ndani ya miaka miwili ya uenyekiti wake Jumuiya hiyo itaendelea kusimamia misingi muhimu ya jumuiya hiyo bila kutetereka.

Mhe. Membe amewakilisha Tanzania kama Waziri mwenye dhamana kuanzia mwaka 2011 akiwa kama mjumbe, na mwaka 2013 Jijini Kolombo Sri Lanka alichaguliwa bila kupingwa kuwa mwenyekiti kwa miaka miwili. Waziri wa Mambo ya Nje wa New Zealand Mhe. Murray McCully alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti.

Ukiacha Tanzania na New Zealand, wajumbe wengine ni mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi saba ambazo ni Cyprus, Guyana, India, Pakistan, Sierra Leone, Visiwa vya Solomon na Sri Lanka ambao wanaingia kwa nafasi yao ya uenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Madola.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.