Monday, March 10, 2014

Tanzania na Malawi zasaini Mkataba wa kuanzisha Kituo cha Pamoja cha Uhamiaji na Ushuru wa Forodha




Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Salum (Mb), kushoto na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Malawi, Mhe. Sosten Gwengwe wakisaini Mkataba wa kuanzisha Kituo cha Pamoja cha Uhamiaji na Ushuru wa Forodha katika mpaka wa Songwe - Kasumulu. Hafla ya uwekaji saini imefanyika katika Ofisi ya Wizara ya Biashara na Viwanda, Lilongwe, Malawi tarehe 10 Machi, 2014.




Mhe. Salum, kulia akitoa neno baada ya shughuli za kusaini Mkataba kukamilika. Anayemsikiliza ni Waziri wa Biashara na Viwanda wa Malawi, Mhe. Gwengwe.



Maafisa wa Tanzania na Malawi wakifanya maandalizi kabla ya Mawaziri kuwasili kwa ajili ya shughuli ya uwekaji saini Mkataba

Waziri wa Nchi wa Serikali ya Zanzibar anayeshughulikia Masuala ya Utawala Bora, Mhe. Mwinyi Haji Makame naye alishuhudia hafla ya uwekaji saini. hapa Mhe. Makame akisaini Kitabu cha wageni alipowasili katika ofisi za Wizara ya Biashara na Viwanda nchini Malawi.

 
Maneno aliyosema Waziri wa Fedha baada ya uwekaji saini
 
Na Ally Kondo. Lilongwe
Nchi za Afrika zimehimizwa kufanya biashara baina yao ili kujiletea maendeleo, badala ya kusubiri misaada isiyokuwa na uhakika kutoka nchi wahisani. Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Salum (Mb) wakati wa hafla ya uwekaji saini Mkataba wa kuanzisha Kituo cha Pamoja cha Uhamiaji na Ushuru wa Forodha cha Songwe – Kasumulu kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Malawi.
 Uwekaji saini huo ulifanyika Lilongwe, Malawi siku ya Jumatatu tarehe 10 Machi, 2014 ambapo Mhe Salum aliwela saini kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, wakati Waziri wa Biashara na Viwanda, Mhe.  Sosten Gwengwe aliweka saini kwa niaba ya Serikali ya Malawi.
Mhe. Salum alieleza kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho, kutasaidia, sio tu kupunguza gharama za kufanya biashara kati ya Tanzania na Malawi bali pia kutaimarisha uhusiano baina ya watu wa nchi hizi mbili ambao kimsingi wana utamaduni unaofanana.
Mhe. Waziri aliwataka wataalamu wa pande zote mbili kuandaa mpango kazi wa kutekeleza Mkataba huo haraka iwezekanavyo ili wananchi na Serikali waone matunda yake badala ya kuishia katika makaratasi.
Alipoulizwa na wanahabari kutoa maoni kuhusu utekelezaji wa Mkataba huo, Mhe Wazri aliwahakikishia wananchi wa Malawi na Tanzania kwa ujumla kuwa kituo hicho kitafanya kazi kama ilivyokusudiwa na hakuna tishio lolote la kuvurugika kwa uhusiano kati ya nchi hizi mbili.
Kwa upande wake, Mhe. Gwengwe alifarijika na uanzishwaji wa kituo hicho, kwa kuwa kitarahisisha usafirishaji wa bidhaa kwa haraka kutoka Tanzania kuingia Malawi ambayo haina Bandari.
Uwekaji saini wa Mkataba huo umeenda sambamba na mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo Mhe. Salum anaongoza ujumbe wa Tanzania. Mkutano huo ulioanza na vikao vya Makatibu Wakuu unatarajiwa kukamilika tarehe 11 Machi, 2014.
 
 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.