|
Rais Yoweri Museveni na Mhe. Rais Mstaafu, Benjamin William Mkapa wakiwa na baadhi ya marais wastaafu wa Afrika waliohudhuria mkutano huo akiwemo Mhe. Festus Mogae (wa kwanza kushoto), Rais Mstaafu wa Botswana, Mhe, Olusegun Obasanjo (wa pili kushoto), Rais Mstaafu wa Nigeria, Mhe. Jerry Rawlings (wa tatu kutoka kulia), Rais Mstaafu wa Ghana, Mhe. Bakili Muluzi (wa pili kulia), Rais mstaafu wa Malawi na Mhe. Hifikepunye Pohamba (wa kwanza kulia), Rais Mstaafu wa Namibia =========================================== |
MARAIS WASTAAFU
WAJADILI UONGOZI WA AFRIKA
Marais wastaafu wa nchi sita za Afrika wamekutana Jijini Dar es
Salaam jana kutafakari mustakabali wa Bara lao wakizingatia mabadiliko ya
kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia ulimwenguni. Mjadala huo ulioitishwa na Rais
Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Benjamin Mkapa, ulifunguliwa rasmi na Rais wa Uganda,
Mhe. Yoweri Museveni.
Ulihudhuriwa na Marais Wastaafu wa Nigeria, Mhe. Olusegun
Obasanjo, Ghana, Mhe Jerry Rawlings, Malawi, Mhe. Bakili Muluzi; Botswana, Mhe.
Festus Mogae, na Namibia, Mhe. Hifikepunye Pohamba.
Marais wastaafu pamoja na wanazuoni na watu mashuhuri wa Afrika walisisitiza
muhimu wa kujenga mtangamano wa bara hilo ili kuleta maendeleo ya haraka ya
kiuchumi. Washiriki walikubaliana kuwa juhudi za pamoja zifanywe kudhibiti
vikwazo dhidi ya mtangamano, ikiwa ni pamoja na historia ya tawala tofauti za
kikoloni; elimu na teknolojia duni, na ukosefu wa utashi wa kisiasa.
Pamoja na kusifia hatua zilizofikiwa kuboresha demokrasia
barani Afrika, washiriki walisema maendeleo ya uchumi yanahitaji kasi kubwa
zaidi ili wananchi wafaidike na rasilimali nyingi zilizopo.
Uongozi wa nchi za Afrika ulikosolewa kwa kushindwa kutoa
kipaumbele kwa maendeleo ya kiuchumi na kuzembea utekelezaji wa maamuzi
yanayochukuliwa kwenye majukwaa mbalimbali ya pamoja, kama vile Umoja wa Afrika
na Jumuiya za Maendeleo za kikanda.
Ilishauriwa jumuiya za kikanda ziimarishwe kwa kutengewa
rasilimali za kutosha na kupewa uwezo zaidi wa kufanya maamuzi ili
ziwe misingi ya kujenga umoja wa kiuchumi.
Washiriki walisifia Mpango Mkakati wa Umoja wa Afrika wa kulifanya
bara hilo liongoze duniani kiuchumi na kiteknolojia ifikapo mwaka 2063,
lakini wakasisitiza uwekwe mpango madhubuti wa utekelezaji ili kufikia azma
hiyo.
Katika hotuba yake, Rais Museveni alisema Afrika inayo misingi imara
ya umoja. Alitupilia mbali madai kuwa bara hilo lina mgawanyiko mkubwa wa
kijamii. "Bara hili lina makundi manne tu ya kilugha," alisema.
Kiongozi huyo wa Afrika Mashariki alihimiza juhudi zaidi kuleta
mtangamano wa kiuchumi na kisiasa Afrika. "Lazima tujenge mtangamano wa
kiuchumi. Pale inapowezekana, tuungane kisiasa pia."
Alisema Afrika ilitawaliwa na wakoloni kwa sababu haikuwa na
mtangamano, kitu kinacholifanya bara hilo liendelee kubaki nyuma kimaendeleo.
Alitaka hatua za pamoja zichukuliwe kuendeleza viwanda na maliasili za Afrika,
ikiwapo madini, mafuta na gesi.
Jana usiku, Mhe. Mkapa aliwaandalia wageni wake hafla ya chakula cha jioni ambapo pia Jukwaa la Uongozi
Afrika lilikabidhi zawadi kwa washidi wa shindano la kuandika insha lililoshirikisha
vijana 522 kutoka nchi 11 za bara hilo.
Mshindi wa kwanza ni Munyaradzi Shifetete kutoka Zimbabwe, ambaye
alikabidhiwa cheti na fedha taslim. Wengine waliokabidhiwa zawadi na Rais
Mstaafu wa Botswana, Mhe. Mogae, ni Vicky Mbabaazi kutoka Uganda, Sholopelo
Sholopelo kutoka Botswana, Joseph Wanga kutoka Kenya na Omolo Juema kutoka
Uganda.
(mwisho)