Friday, July 31, 2015

Marais wastaafu wajadili uongozi wa Afrika

Rais Yoweri Museveni na Mhe. Rais Mstaafu, Benjamin William Mkapa wakiwa na baadhi ya  marais wastaafu wa Afrika waliohudhuria mkutano huo akiwemo Mhe. Festus Mogae (wa kwanza kushoto), Rais Mstaafu wa Botswana, Mhe, Olusegun Obasanjo (wa pili kushoto), Rais Mstaafu wa Nigeria,  Mhe. Jerry Rawlings (wa tatu kutoka kulia), Rais Mstaafu wa Ghana, Mhe. Bakili Muluzi (wa pili kulia), Rais mstaafu wa Malawi na Mhe. Hifikepunye Pohamba (wa kwanza kulia), Rais Mstaafu wa Namibia
===========================================
MARAIS WASTAAFU WAJADILI UONGOZI WA AFRIKA

Marais wastaafu wa nchi sita za Afrika wamekutana Jijini Dar es Salaam jana kutafakari mustakabali wa Bara lao wakizingatia mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia ulimwenguni. Mjadala huo ulioitishwa na Rais Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Benjamin Mkapa, ulifunguliwa rasmi na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Museveni.

Ulihudhuriwa na Marais Wastaafu wa Nigeria, Mhe. Olusegun Obasanjo, Ghana, Mhe Jerry Rawlings, Malawi, Mhe. Bakili Muluzi; Botswana, Mhe. Festus Mogae, na Namibia, Mhe. Hifikepunye Pohamba.

Marais wastaafu pamoja na wanazuoni na watu mashuhuri wa Afrika walisisitiza muhimu wa kujenga mtangamano wa bara hilo ili kuleta maendeleo ya haraka ya kiuchumi. Washiriki walikubaliana kuwa juhudi za pamoja zifanywe kudhibiti vikwazo dhidi ya mtangamano, ikiwa ni pamoja na historia ya tawala tofauti za kikoloni; elimu na teknolojia duni, na ukosefu wa utashi wa kisiasa.

Pamoja na kusifia hatua zilizofikiwa kuboresha demokrasia barani Afrika, washiriki walisema maendeleo ya uchumi yanahitaji kasi kubwa zaidi ili wananchi wafaidike na rasilimali nyingi zilizopo.

Uongozi wa nchi za Afrika ulikosolewa kwa kushindwa kutoa kipaumbele kwa maendeleo ya kiuchumi na kuzembea utekelezaji wa maamuzi yanayochukuliwa kwenye majukwaa mbalimbali ya pamoja, kama vile Umoja wa Afrika na Jumuiya za Maendeleo za kikanda.

Ilishauriwa jumuiya za kikanda ziimarishwe kwa kutengewa rasilimali za kutosha na kupewa uwezo zaidi wa kufanya maamuzi ili ziwe misingi ya kujenga umoja wa kiuchumi.

Washiriki walisifia Mpango Mkakati wa Umoja wa Afrika wa kulifanya bara hilo liongoze  duniani kiuchumi na kiteknolojia ifikapo mwaka 2063, lakini wakasisitiza uwekwe mpango madhubuti wa utekelezaji ili kufikia azma hiyo.

Katika hotuba yake, Rais Museveni alisema Afrika inayo misingi imara ya umoja. Alitupilia mbali madai kuwa bara hilo lina mgawanyiko mkubwa wa kijamii. "Bara hili lina makundi manne tu ya kilugha," alisema.
Kiongozi huyo wa Afrika Mashariki alihimiza juhudi zaidi kuleta mtangamano wa kiuchumi na kisiasa Afrika. "Lazima tujenge mtangamano wa kiuchumi. Pale inapowezekana, tuungane kisiasa pia."

Alisema Afrika ilitawaliwa na wakoloni kwa sababu haikuwa na mtangamano, kitu kinacholifanya bara hilo liendelee kubaki nyuma kimaendeleo. Alitaka hatua za pamoja zichukuliwe kuendeleza viwanda na maliasili za Afrika, ikiwapo madini, mafuta na gesi.
Jana usiku, Mhe. Mkapa aliwaandalia wageni wake hafla ya  chakula cha jioni ambapo pia Jukwaa la Uongozi Afrika lilikabidhi zawadi kwa washidi wa shindano la kuandika insha lililoshirikisha vijana 522 kutoka nchi 11 za bara hilo.

Mshindi wa kwanza ni Munyaradzi Shifetete kutoka Zimbabwe, ambaye alikabidhiwa cheti na fedha taslim. Wengine waliokabidhiwa zawadi na Rais Mstaafu wa Botswana, Mhe. Mogae, ni Vicky Mbabaazi kutoka Uganda, Sholopelo Sholopelo kutoka Botswana, Joseph Wanga kutoka Kenya na Omolo Juema kutoka Uganda

(mwisho)

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.