Thursday, July 2, 2015

Wizara ya Mambo ya Nje kujenga jengo jipya

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Hassan Simba Yahya kulia na Mwakilishi wa Kampuni itakayojenga jengo la Wizara ya Mambo ya Nje wakiweka saini Makubaliano ya mchoro wa jengo hilo.
Balozi Yahya akibadilishana nyaraka za makubaliano ya michoro ya jengo la Wizara na Mwakilishi wa Kampuni itakayojenga jengo hilo.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imeidhinisha michoro ya Jengo jipya la wizara hiyo, litakalojengwa jirani na Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar Es Salaam.
Makubaliano kuhusu michoro hiyo ya jengo la ghorofa sita, litakalogharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, yametiwa saini jana baina ya wizara na mwakilishi wa mkandarasi wa ujenzi.
Akiongea baada ya kutia saini makubaliano hayo kwa niaba ya wizara, Naibu Katibu Mkuu, Balozi Hassan Simba Yahya, alisema hatua hiyo inatoa fursa kwa matayarisho ya ujenzi kuanza, na kuwa kazi ya ujenzi inatarajiwa kuanza kabla ya mwisho wa muhula wa Serikali ya Awamu ya Nne.
"Tumekamilisha hatua muhimu katika matayarisho ya ujenzi wa Jengo la Wizara," alisema, na kuongeza kuwa mradi huu ulianzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete.
Utiaji saini wa makubaliano ya michoro hiyo ulishuhudiwa na wawakilishi wa Wakala wa Majengo (TBA).

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.