Tuesday, February 23, 2016

Matangazo ya moja kwa moja kutokea Ngorongoro Crater yarushwa nchiniMarekani

Mwakilishi wa Serikali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori katika Wizara hiyo, Bw. Herman Keraryo akizungumza na  Waandishi wa Habari kuelezea umuhimu  wa matangazo ya moja kwa moja yaliyorushwa na Shirika la Utangazaji la ABC News la nchini Marekani kutokea Bonde la Ngorongoro katika kuitangaza Tanzania.  Shirika la ABC News kupitia kipindi chake mashuhuri cha Good Morning America kimerusha matangazo yake ya moja kwa moja kutokea Bonde la Ngorongoro tarehe 23 Februari, 2016.
Mkurugenzi  wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bi Devotha Mdachi naye akifafanua jambo kwa waandishi

Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dkt. Freddy Manongi naye akifafanua kwa waandishi wa habari namna Tanzania na Mamlaka hiyo itakavyofaidika na matangazo hayo ya moja kwa moja yaliyorushwa na ABC News.
Bi. Mindi Kasiga,  Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa naye akizungumza na waandishi wa habari
Mhandisi Mkuu wa mawasiliano na matangazo  wa Shirika la  ABC News, Bi Farhoun akiwaeleza Wakurugenzi na Waandishi wa Habari namna matangazo hayo yatakavyorushwa kwa kutumia Teknolojia ya hali ya juu na kwamba wamejipanga kuwaonesha Wamarekani Wanyama  na  Jamii za Wamasai wanaoishi katika Bonde hilo. 
Bi. Farhoun akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwa Wakurugenzi
Bi. Farhoun akielezea namna baadhi ya vifaa na mitambo inavyofanya kazi
Wakurugenzi na Waandishi wa Habari wakiangalia namna matangazo yanavyorushwa moja kwa moja. Picha ya chini anayeonekana kwa mbali kwenye screen za  televisheni ni mtangazaji mashuhuri wa kipindi cha Good Morning America, Bi. Amy Robach akizungumza wakati wa matangazo hayo
Wakurugenzi wakisalimiana na sehemu nyingine ya Wataalam wa matangazo (crew) waliokuwa wamepiga kambi katikati ya Ngorongoro.
Baadhi ya Wanyama walioonekana katika kipindi cha moja kwa moja cha "Good Morning America"
Bi. Kasiga na Bw. Asante Melita kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wakiwa katika picha ya pamoja na Mtangazaji maarufu wa kipindi cha Good Morning America Bi. Amy Robach.
 ===================================================


Shirika la Utangazaji la ABC News la nchini Marekani limefanikiwa kurusha matangazo yake ya  moja kwa moja (live) kutokea Ngorongoro Crater kupitia kipindi chake maarufu cha “Good Morning America.”
Matangazo hayo ambayo yamerushwa tarehe 23 Februari, 2016 yanatarajiwa kutazamwa na watu milioni 5 Jijini New York na zaidi ya watu milioni 50 katika Marekani yote yanalenga kutangaza vivutio vya Utalii hapa nchini hususan Bonde la Ngorongoro pamoja na kuelezea jitihada za Serikali ya Tanzania katika uhifadhi wa mazingira na maliasili.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kutokea Bonde la Ngorongoro mara baada ya matangazo hayo kurushwa, Mwakilishi wa Serikali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Herman Keraryo alisema kuwa kuna  faida kubwa kwa matangazo hayo kurushwa nchini Marekani kwani ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuleta Watalii hapa nchini. Pia matangazo hayo ni moja ya jitihada za Serikali katika kukabiliana na changamoto  za kutangaza utalii ambapo njia hii iliyotumiwa na Shirika la ABC News ni nzuri kwani imefanikiwa kuwafikia watu wengi na kwa muda mfupi.
Bw. Keraryo ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutunza mazingira na Wanyamapori ambao wameendelea kuwa kivutio kikubwa cha utalii nchini.
“Kama mnavyojua utalii wa Tanzania bado unategemea wanyamapori kwa kiasi kikubwa pamoja na kuwa na vivutio vingine Kama vile  mambo ya kale lakini bado wanyamapori wanatangaza zaidi utalii wetu hivyo ni wajibu wetu kuendelea kuwatunza” alisema Bw. Keraryo.
Mbali na Bw. Keraryo wajumbe wengine kutoka Serikalini walioshuhudia urushwaji wa matangazo hayo ni  Bi. Devotha Mdachi, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dkt. Freddy Manongi, Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Bi. Mindi Kasiga,  Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu, Dkt. Manongi alisema kuwa anaishukuru na kuipongeza Wizara ya Mambo ya Nje kupitia Ubalozi wake wa New York, Marekani kwa jitihada za kulishawishi na kufanikisha shirika hilo la utangazaji kuja nchini na kwamba ana imani utalii utaongezeka kufuatia  matangazo hayo. Alisema kuwa Tanzania imepata fursa nzuri ya kujitangaza bure kwa vile imekuwa ikutumia fedha nyingi kwa ajili ya kazi hiyo.
“Kitendo cha kuleta shirika la ABC News nchini kwa ajili ya kutangaza utalii ni cha kujivunia na pia ni fursa kubwa sana kwetu Watanzania. Hivyo napenda kuushukuru Ubalozi wetu New York kwani ninaamini kupitia matangazo haya tutafaidika sana na tunatarajia baada ya miezi michache kupata watalii wengi hususan hapa Ngorongoro” alieleza Dkt. Manongi.
Naye Bi. Kasiga, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje alieleza  jitihada zilizofanywa na Wizara kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania, New York pamoja na Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali katika kufanikisha matangazo hayo ya moja kwa moja. Aliongeza kwamba jitihada hizo  zitaendelea ikiwemo kuzitumia Balozi zetu zilizopo nje katika kuhakikisha vivutio vya utalii vya hapa nchini vinatangazwa duniani kote. Pia alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa    Mashirika mengine makubwa ya utangazaji duniani kuja nchini kutangaza vivutio hivyo.
Kwa upande wake Bi. Mdachi kutoka Bodi ya Utalii aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Tanzania ina Mabalozi wa hiari wa utalii watano nchini Marekani na kwamba matangazo hayo ya ABC News yatakuwa ni nyenzo mojawapo itakayotumiwa na mabalozi hao kuendelea kuitangaza Tanzania.
Naye Mwakilishi wa Shirika la ABC News  Bi. Farhoun aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwawezesha kufanikisha matangazo hayo ambayo kwa namna moja au nyingine yataongeza watazamaji wa kituo chao kwa vile walihakikisha ni wanyama pekee wanaooneshwa kwenye matangazo hayo tangu mwanzo hadi mwisho.
Pia alisema kwamba wamevutiwa na hifadhi hiyo ya kipekee duniani na kuipongeza Tanzania kwa jitihada  za utunzaji wa mazingira hususan Bonde la Ngorongoro na hawajutii uamuzi wao wa kuichagua Ngorongoro kwa matangazo hayo.
-MWISHO-



Rais John Magufuli awapokea Mabalozi kutoka DRC na Namibia.

Video hii imeandaliwa na kutengenezwa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma, Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.

MHE. RAIS DKT. JOHN POMBE MAGUFULI APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO


Mhe. Balozi Jean Pierre Tshampanga Mutamba akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili Ikulu kwa ajili ya kuwasilisha Hati za Utambulisho.
Mhe. Balozi Mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hapa nchini, Mhe. Balozi Jean Pierre Tshampanga Mutamba akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu tarehe 22 February, 2016. 
Rais Magufuli akiwa katika mazungumzo na Balozi wa DRC mara baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho.




Mhe. Balozi Mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hapa nchini, Mhe. Jean Pierre Tshampanga Mutamba (katikati) akisikiliza nyimbo za Taifa mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam katika hafla fupi ya kukabidhi Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli iliyofanyika tarehe 22 February,2016.
Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Mhe. Balozi Mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)  hapa nchini wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Naibu Waziri Dkt. Susan Kolimba (watatu kulia) Mhe. Katibu Mkuu Balozi Aziz Mlima (wa pili kulia) na Balozi Samuel Shelukindo, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, kushoto ni maofisa kutoka Ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hapa nchini. 
Wakati huo huo Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipokea pia Hati za Utambulisho za Mhe. Balozi Mteule wa Namibia hapa nchini. 


Mhe. Balozi Mteule wa Namibia hapa nchini, Mhe. Theresia Samaria  akisaini Kitabu cha wageni Ikulu mara baada ya kuwasili kwa ajili ya kuwasilisha Hati za Utambulisho.


Mhe. Balozi Mteule wa Namibia hapa nchini, Mhe. Theresia Samaria akikabidhi Hati za Utambulisho kwa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu tarehe 22 February, 2016.
Mhe. Balozi Mteule akisalimiana na Mhe. Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dkt. Suzan Kolimba.

Mhe. Balozi akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Balozi Azizi Mlima. 
Rais Magufuli akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Namibia mara baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho.
 Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Mhe. Balozi Mteule wa Namibia wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa na maafisa wa Ubalozi wa Namibia hapa Nchini.
==============
Picha na Reuben Mchome.

Monday, February 22, 2016

Kituo maarufu cha Televisheni cha Marekani kuitangaza Ngorongoro moja kwa moja

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje , Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga akizungumza na Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Bw. Julius Kibebe alipowasili Ofisini kwake kwa ajili ya  kuratibu  urushwaji wa matangazo ya moja kwa moja na Kituo maarufu cha Televisheni cha Marekani ABC News kutokea Bonde la Ngorongoro yatakayofanyika tarehe 23 Februari, 2016. Matangazo hayo ambayo yatatazamwa na watu milioni tano wa Jijini New York na takribani watu milioni 52 nchini Marekani yanakusudia kutangaza Hifadhi hiyo ya kipekee duniani pamoja na kuelezea jitihada za Serikali ya Tanzania kwenye uhifadhi wa mazingira. Bi. Kasiga anaiwakilisha Wizara kwenye uratibu wa tukio hilo kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali.
Bi. Kasiga akifafanua jambo huku Bw. Kibebe (kulia) na Bw. Asante Melita (kushoto), Mhifadhi na Mratibu wa Tukio hilo wakimsikiliza



Bi. Kasiga akioneshwa namna matangazo hayo yatakavyorushwa na Fundi Mitambo Mkuu wa ABC News, Bw. John.


Friday, February 19, 2016

MHE.WAZIRI AREJEA KUTOKA ZIARA YA KIKAZI NCHINI RWANDA


WAZIRI MAHIGA AKUTANA NA RAIS WA RWANDA

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga amefanya ziara ya Kikazi Nchi Rwanda na kuonana na Rais wanchi hiyo Mhe. Paul Kagame. Waziri Mahiga alifanya ziara hiyo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Waziri Mahiga akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere mara baada ya kuwasili, amesema ziara hiyo ya kikazi nchini Rwanda ililenga kuonana na Rais wanchi hiyo Mhe. Paul Kagame kwakuwa ni jirani na ni mmoja wa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo pia walitumia fursa hiyo kujadili masuala mbambali kuhusu Jumuiya.

Aidha katika mazungumzo hayo walijadili suala la mgogoro wa kisiasa wa nchini Burundi na kwa pomoja kuangalia namna bora zaidi ya kurejesha amani ya kudumu katika nchi hiyo.
 Pia Mhe. Waziri alipata fursa ya kuzungumza na wafanyabishara wa Nchini Rwanda ambapo wamesifu utendaji wa Serikali ya awamu ya tano chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli. Wafanyabiashara hao wamesifu utendaji wa Serikali kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kuboresha utendaji wa taasisi zake ikiwamo Bandari. “Nimepewa salamu za pongezi na wafanyabiashara wa Rwanda nizilete kwa Serikali ya Tanzania kwa kazi nzuri iliyofanywa na Serikali na wameahidi kuongeza ushirikiano wa kibishara baina ya nchi hizi mbili” alisema Waziri Mahiga.
 
Vilevile Rais Mhe. Paul Kagame katika mazungumzo hayo amesisitiza ujenzi wa mradi wa reli ya ukanda wa kati ambayo itasaidia kukuza biashara zaidi baina ya nchi hizi mbili na kuongeza fursa za uwekezaji.
Mhe. Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga, akiwasili uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere akitokea Nchini Rwanda ambako alienda kumuwakilisha Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Mhe. Waziri akijadili jambo na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na msemaji wa Wizara Bi. Mindi Kasiga.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na msemaji wa Wizara Bi. Mindi Kasiga akimkaribisha Mhe. Waziri kuongea na waandishi wa habari juu ya lengo la safari ya kwenda nchini Rwanda na manufaa yake kwa Taifa, kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Mhe. Balozi Samuel Shelukindo.
Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano.
Mhe. Waziri akiongea na waandishi wa habari na kuwaeleza safari ilikuwa na lengo la kuonana na Mhe. Rais Paul Kagame kama jirani na mwanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki na kufanya mazungumzo naye juu ya hali ya kisiasa nchini Burundi pia aliweza kuzungumza na wafanyabiashara nchini Rwanda ambao walieleza kuridhishwa na utendaji wa Serikali ya awamu ya tano. 

Wakizungumza mara baada ya kumaliza Mkutano na vyombo vya habari.




Dkt. Kolimba akutana na Ujumbe wa Bunge la Sweden


Mhe. Naibu Waziri  wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb) akiukaribisha ujumbe wa wabunge wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje ya Bunge la Sweden walipomtembelea leo ofisini kwake.Wabunge hao wapo nchini kwa madhumuni ya kutathmini na kukagua miradi inayofadhiliwa na Serikali ya Sweden kwa Tanzania ili kubaini utaratibu bora zaidi wa kusaidia Tanzania katika kipindi kijacho.
Mhe. Naibu Waziri (kulia) akizungumza na kiongozi wa ujumbe huo, Mhe. Kenneth G. Forslund ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje ya Sweden. Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kolimba alishukuru Serikali ya Sweden kwa misaada yake katika sekta ya elimu ya juu na Bajeti ya Maendeleo. Aidha, Mhe. Naibu Waziri alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden hususan katika masuala ya kiuchumi na biashara.


Naafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje wakifuatilia mazungumzo hayo. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Balozi Joseph Sokoine, Bi. Tunsume Mwangolombe, Bw. Adam Issara na Bw. Ally Kondo.


Baadhi ya Waheshimiwa. Wabunge kutoka Sweden wakifuatilia mazungumzo hayo.

Sehemu nyingine ya Waheshimiwa Wabunge kutoka Sweden.

Mhe. Naibu Waziri, Dkt. Kolimba wa pili kutoka kulia akiwa katika picha ya pamoja na wabunge wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje ya Bunge la Sweden.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje azungumza na Mkurugenzi wa Shirika la Trade Mark East Africa

Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa
Dkt. Susan Kolimba (Mb.) akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la "Trade Mark East Africa", Bw. David Stanton aliyekuja kujitambulisha na kuutambulisha mradi wa maendeleo wa awamu ya pili wa Shirika hilo pamoja na kumweleza Mhe. Naibu Waziri mafanikio ya mradi wa awamu ya kwanza uliokwishamalizika kwa mwaka wa fedha 2015/2016.


Mkurugenzi wa Miundombinu katika Ushoroba wa Kati (central corridor) katika Bandari ya Dar es salaam Bw. Severine Kaombwe (kushoto), pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la "Trade Mark East Africa" wakishiriki katika mazungumzo hayo.
Shirika la "Trade Mark East Africa" ni shirika lisilo la kiserikali ambalo limekuwa likifanya kazi na Serikali ya Tanzania katika miradi ya kuendeleza na kuboresha Bandari ya Dar es Salaam, pamoja na miundombinu katika maeneo ya mipakani ili kuwezesha kukuza shughuli  za kiuchumi na kuongeza ajira kwa wananchi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bi. Graceana  Shirima akiwa na maafisa wa Wizara wakifuatilia mazungumzo ya viongozi hao na Mhe. Naibu Waziri.
Mhe. Naibu Waziri Kolimba akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa East Africa Trade Mark  pamoja na Wakurugenzi aliofuatana nao.