TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA KUHUSU KUZINGATIA SHERIA KATIKA KUINGIZA
AU KUTOA MIFUGO NCHINI KWA AJILI YA
MALISHO NA MAJI
Hivi karibuni, tumeshuhudia kuibuka kwa wimbi kubwa
la uungizaji wa mifugo kutoka nchi jirani kuingia nchini kwa ajili ya malisho
na maji bila kufuata sheria za nchi. Uingizaji wa mifugo kutoka nchi moja
kwenda nyingine una madhara mengi, ikiwemo kiusalama, uharibifu wa mazingira na
kueneza magonjwa ya mifugo.
Ikumbukwe kuwa tarehe 13 Oktoba, 2017, Wizara ya
Mifugo na Uvuvi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa agizo la kuondoa
mifugo yote iliyo nchini kinyume cha sheria ndani ya siku saba (7). Kutofanya hivyo kutapelekea
mifugo hiyo kutaifishwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Kufuatia agizo hilo, Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki inatoa
wito kwa Watanzania wote wenye mifugo nchi jirani wafuate taratibu za kisheria
na kama kuna mifugo kwenye malisho nje ya Tanzania waiondoe mara moja ili
kuepusha hasara na usumbufu.
Aidha,
wizara inatoa wito kwa Watanzania hususan wanaoishi Mikoa iliyopakana na
nchi jirani kuwa wazalendo kwa kutokushirikiana na raia wa nchi za kigeni
kuvunja sheria mbalimbali za nchi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje Na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
17 Oktoba, 2017