Wednesday, October 11, 2017

Tanzania na Cuba kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Suzan Kolimba (Mb.) akutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Prof. Lucas Domingo Hernandez Polledo,alipomtembelea leo katika ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Mkutano ukiendelea
Dkt. Kolimba akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe.Prof. Polledo, wa pili kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Amerika na Ulaya Bi. Mary Matare, na wa kwanza kulia ni Afisa Mambo ya Nje, Bi. Lilian Kimaro na kushoto ni afisa wa Ubalozi wa Cuba hapa nchini.

=======================================



Serikali ya Tanzania na Cuba zimeahidi kuendelea kuweka mikakati madhubuti kwaajili ya kuimarisha ushirikiano wa siku nyingi ulioasisiwa na viongozi wakuu wa Mataifa hayo Hayati Baba wa Taifa  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Fidel Castor.

Hayo yamesemwa leo katika mazungumzo baina ya Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba na Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Prof. Lucas Domingo Hernandez Polledo walipokutana katika ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wa Mhe. Kolimba alieleza Cuba imekuwa mdau wa Maendeleo nchini tangu enzi za ukoloni ambapo ilishiriki katika kupigania Ukombozi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla na hivyo kuleta undugu baina ya watu wa mataifa hayo mawili.

Aidha, aliongeza kwa kusema “Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua jitihada na mchango wa Serikali ya  Cuba katika Sekta  ya Afya kwa kuleta madakatari kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Hospitali ya Taifa Muhimbili, Pia ujenzi wa kiwanda cha viuadudu kilichopo Kibaha ni sehemu ya jitihada za kuwasaidia Watanzania katika kuhakikisha wanakuwa na Afya bora ili kuweza kumudu majukumu yao ya kila siku katika kuliletea Taifa maendeleo” alisema Dkt. Kolimba.

Halikadhalika Mhe. Prof. Polledo alisisitiza kuwa Cuba itaendeleza ushirikiano na Tanzania na kuzidi kuangalia maeneo mengine ya ushirikiano hususani upande wa michezo ambapo nchi hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika mchezo wa ngumi pamoja na walimu stadi wa mchezo huo ambao wamekuwa wakitoa mafunzo katika mataifa mengine ya Afrika.

Pia alieleza kutambua mchango wa Tanzania katika Kikao cha 72 cha Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kwa msimamo wake wa kutaka Cuba kuondolewe vikwazo vya kiuchumi ambavyo vimekuwa vikikwamisha na kurudisha nyuma jitihada za maendeleo ya Taifa hilo. “ ni wakati sasa Cuba na Tanzania zikaimarisha ushirikiano wake kwa kuhakikisha unakuwa na mafanikio  kiuchumi kwa manufaa ya mataifa hayo” alisema Prof. Polledo

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.