Thursday, October 19, 2017

Watanzania wahimizwa kudumisha na kuuenzi utamaduni wao

Mgeni rasmi, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamis Kigwangalla (Kushoto) akikaribishwa na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Mhe. Dkt. Mohammed Hamad Al Rumhy (kulia) mara baada ya kuwasili katika Viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki katika sherehe za utamaduni wa muziki wa Oman zilizofanyika tarehe 18 Oktoba 2017.

Kikundi cha ngoma kutoka nchini Oman ambacho ni sehemu ya ujumbe wa Mfalme wa Oman uliopo nchini kwa ziara kikitumbuiza jukwaani.

Mhe. Dkt. Kigwangalla na Mhe. Dkt.Mohammed wakijadiliana jambo.
Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Kilima akifuatilia buruduni iliyokuwa ikitolewa na kikundi cha ngoma kutoka Oman. Wengine ni sehemu ya ujumbe wa Serikali ya Tanzania na Oman.
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Oman ikifuatilia burudani.
Bendi ya Jeshi kutoka nchini Oman ambayo pia ni sehemu ya ujumbe huo ilitoa burudani kwa wananchi waliohudhuria hafla hiyo.


=======================================================================


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Hamis Kigwangalla amewataka Watanzania kuwa mabalozi wazuri katika kuzitangaza na kuzidumisha mila, tamaduni na desturi zao kwakua ndio nguzo na utambulisho wa Mtanzania popote Duniani.

Waziri Kigwangala aliyasema hayo katika sherehe za muziki wa utamaduni wa Oman zilizofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Oktoba 2017.

Sherehe hizo ambazo Mgeni rasmi alikuwa Mhe. Dkt. Kigwangalla, ziliandaliwa na ujumbe wa Mfalme wa Oman uliokuja na Meli ya Mfalme huyo nchini kwa ziara ya siku sita inayotarajiwa kumalizika siku ya Jumamosi tarehe 21 November 2017.

Mhe. Kigwangala alisema kupitia tamasha hilo la muziki na ziara nzima kwa ujumla, Oman inapata fursa ya kujitangaza na kuutumia utamaduni wao  kama sehemu ya utalii na kwamba hii ni nafasi ya pekee kwa Watanzania kujifunza namna gani watu wa mataifa mengine wameweza kutumia utamaduni wao kwa tija na kuongeza pato la Taifa. 

Aidha, alisisitiza ni wakati sasa makundi yote ya utalii  yaliyopo nchini kama utalii wa kwenye maji, utalii wa misitu hususan kwa kutumia upekee wa mazingira yetu, fukwe na hata historia ya binadamu vikaendelea kuhifadhiwa na kupatiwa ubunifu zaidi wa namna ya kuvitangaza na kupata mfumo wa kisasa kwa ajili ya kuwezesha watalii wengi kuingia na kutoka nchini kwa namna bora zaidi.

Halikadhalika akaongeza kwa kusema “Nchi yetu imebarikiwa sana kwa kuwa na idadi kubwa ya vivutio vya utalii ukilinganisha na Oman, katika fursa niliyopata ya kukutana na Naibu Waziri wa Utalii wa Oman ambaye ameambatana na ujumbe huu nimeweza kuzungumza naye mengi ambayo tutayaweka katika utekelezaji ili sekta ya utalii iweze kuongeza fedha za kigeni zaidi.”

Kwa upande wake Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Bw. Mohammed bin Hamad Al-Rumhy ameahidi kuwa Serikali ya Oman itaendeleza undugu huo kwa kufanya biashara  na kuongeza uwekezaji katika sekta mbalimbali ili kuweza kuingia katika soko la ushindani duniani.

Lengo kuu la ziara ya ujumbe huo ni kutangaza amani katika ukanda wa Afrika Mashariki sambamba na kudumisha undugu uliopo baina ya Tanzania na Oman ambapo utamaduni wa mataifa haya mawili umekuwa ukifanana hususan katika ukanda wa pwani kufuatia historia na muingiliano wa wananchi wake katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.