Thursday, October 26, 2017

Waziri Mahiga afungua Mkutano wa Mawaziri wa nchi wananchama wa Jumuiya ya Utatu wa COMESA-EAC-SADC (TRIPARTITE)

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akifungua Mkutano wa kwanza wa Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Miundombinu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Utatu wa COMESA-EAC-SADC (TRIPARTITE) uliofanyika katika Hotel ya Serena Jijini Dar es Salaam tarehe 26 Oktober 2017.
Viongozi na wajumbe kutoka Nchi Wanachama wakifuatilia Mkutano, wa tatu kutoka kushoto ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbalawa na wa nne kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima.

Sehemu nyingine ya Wajumbe kutoka nchi Wanachama wakifuatilia Mkutano.
Mkutano ukiendelea.

Picha ya pamoja.
============================================================


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MHE. WAZIRI MAHIGA AFUNGUA RASMI MKUTANO WA KWANZA WA MAWAZIRI WENYE DHAMANA YA MASUALA YA MIUNDOMBINU WA NCHI WANACHAMA WA JUMUIYA YA UTATU WA COMESA-EAC-SADC (TRIPARTITE) UNAOFANYIKA HAPA DAR ES SALAAM LEO TAREHE 26 OKTOBA 2017

Mkutano wa Kwanza wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Utatu wa COMESA-EAC-SADC umefanyika hapa Dar es Salaam, Serena Hoteli leo tarehe 26 Oktoba 2017. Mkutano huo unahusisha jumla ya nchi 26 Wanachama wa Umoja huo. Mkutano huu unafanyika hapa Tanzania kwa kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ndiyo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Utatu wa COMESA-EAC-SADC.

Mkutano huu umefunguliwa na Mhe. Dkt. Augustine Phillip Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Kufanyika kwa Mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Miundombinu kunatokana na maazimio ya Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa COMESA, EAC na SADC uliofanyika Johannesburg, Afrika Kusini tarehe 14 Juni, 2011 ambao ulipitisha maeneo matatu ya kutekelezwa kwenye ushirikiano wa Utatu wa COMESA – EAC – SADC. Maeneo hayo ni: 1) Kuunganisha Soko; 2) Kuendeleza Miundombinu ili kuunganisha Nchi Wanachama kwa miundombinu iliyo bora; na 3) Kukuza Viwanda.
Kwa upande wa Sekta za Miundombinu, huu ni Mkutano wa Kwanza wa Mawaziri  wa Nchi Wanachama wa Utatu wa COMESA, EAC na SADC. Mkutano huu katika Ngazi ya Wataalam ulijadili hatua zilizofikiwa na Nchi Wanachama katika uendelezaji wa miundombinu na kupendekeza maamuzi ya kisera kwenye sekta za miundombinu ya uchukuzi (barabara, reli, bandari, anga); teknolojia ya habari na mawasiliano; na nishati.

Kwa ujumla Mkutano wa Mawaziri umepita na kujadili programu kuu zifuatazo:
           i.          Programu ya Uendelezaji wa Sekta za Uchukuzi kwa njia ya Barabara kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Utatu wa COMESA-EAC-SADC (Tripartite Transport and Transit Facilitation Programme (TTTFP);

          ii.          Taarifa za utekelezaji wa miradi na programu kuhusiana na Sekta ya Miundombinu ya Uchukuzi (Anga, Barabara, Reli na Bandari); Sekta ya Mawasiliano na Sekta ya Nishati;

         iii.          Maendeleo ya Kanda za Uchukuzi (Corridor Development) za Jumuiya ya Utatu wa COMESA, EAC na SADC, ambapo hatua mbalimbali za Utekelezaji wa Vituo vya Kutoa Huduma kwa Pamoja Mipakani (OSBPs) kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya hizo zimejadiliwa;

        iv.          Utekelezaji wa Programu ya Kikanda wa Uendelezaji wa Miundombinu katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Ukanda wa Afrika Kusini na Ukanda wa Bahari ya Hindi (Regional Indicative Programme for Eastern Africa, Southern Africa and the Indian Ocean (2014 – 2020); na

         v.          Utekelezaji wa Miradi ya NEPAD Presidential Infrastructure Championship Initiative (PICI);
        vi.          Rasimu ya Mpangokazi wa shughuli za utatu wa COMESA- EAC- SADC hususan uratibu wa mikutano ya miundombinu;
       vii.          Utafutaji raslimali fedha za kuwezesha shughuli za utatu wa COMESA- EAC- SADC; na

     viii.          Uzinduzi rasmi wa Programu ya Uendelezaji wa Sekta za Uchukuzi kwa njia ya Barabara kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Utatu wa COMESA-EAC-SADC (Tripartite Transport and Transit Facilitation Programme (TTTFP).

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Waziri Mahiga, pamoja na kuwakaribisha Mawaziri nchini Tanzania na jijini Dar es Salaam, amesisitiza umuhimu wa kuwa na miradi ya pamoja ya kuendeleza sekta ya miundombinu baina ya Jumuiya za kikanda kama njia madhubuti ya kuwaletea maendeleo ya haraka wananchi. Mhe. Mahiga pia amesisitiza kwamba Tanzania inathamini ushirikiano wa kanda na hivyo itaendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za maendeleo za kikanda ikiwemo zile za Jumuiya ya Utatu (Tripartite) kama njia mojawapo wa utekelezaji wa Sera ya Tanzania ya Viwanda. Mwisho, Mhe. Mahiga amewatakia mkutano mzuri Mawaziri wa Miundombinu akiwaomba kuibua mikakati na mapendekezo madhubuti katika kuendeleza miundombinu katika eneo lote la UTATU.

Aidha, Mawaziri kwa pamoja, wakiongozwa na Mhe. Aggrey Henry Bagiire, Waziri wa Uchukuzi na Ujenzi wa Jamhuri ya Uganda na ambaye atakuwa ni Mwenyekiti wa Mkutano huo kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, watazindua rasmi Programu ya Uendelezaji wa Sekta za Uchukuzi kwa njia ya Barabara kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Utatu wa COMESA-EAC-SADC (Tripartite Transport and Transit Facilitation Programme (TTTFP).

Uzinduzi huu utafanyika leo tarehe 26 Oktoba, 2017 saa 9.00 Alasiri na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa Serikali na Sekta Binafsi.
I
Imetolewa na,
KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI,
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI,
TAREHE 26/10/2017







No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.