TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali kutoa viwanja kwa ajili Mabalozi
kujenga ofisi na makazi Dodoma
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda amewahakikishia Waheshimiwa Mabalozi na
Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa hapa nchini kuwa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuwapatia viwanja
vya ukubwa wa ekari 5 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na makazi ya Balozi mjini
Dodoma itatekelezwa kama ilivyoahidiwa.
Rais Magufuli alitoa
ahadi hiyo katika sherehe za kufungua mwaka wa 2018 ya wanadiplomasia
zilizofanyika Ikulu jijini Dar Es Salaam tarehe 09 Februari 2018.
Prof. Mkenda alitoa
kauli hiyo kwa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wakati wa
kuwasilisha mada kuhusu Mpango Mkuu wa Mji wa Serikali mjini Dodoma.
Mada hiyo ilitolewa
kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
na Manispaa ya Dodoma kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius
Nyerere (JNICC) leo Jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mada
hiyo, mji wa Serikali mjini Dodoma utajengwa pembeni ya Barabara ya Dar Es
Salaam hadi Dodoma, kilomita 17 kutoka katikati ya mji wa Dodoma na unakadiriwa
kugharimu Shilingi za Kitanzania trilioni 10 hadi unakamilika.
Mji huo ambao
umesanifiwa kwa asilimia 100 na wataalamu wa Kitanzania umezingatia mahitaji
yote muhimu ambayo mji wa kisasa unastahili kuwa nayo. Miongoni mwa mahitaji
hayo ni pamoja na miundombinu ya kutosha ikiwemo barabara, maji safi na maji
taka, nishati ya umeme, TEHAMA na dampo kwa ajili ya taka ngumu ambalo ujenzi
wake umeshakamilika na juhudi zinaendelea za kutafuta mwekezaji kwa ajili ya
kubadilisha taka kwa matumizi mengine (recycling).
Aidha, usanifu wa
mji huo umezingatia vigezo vya uendelezaji endelevu wa miji duniani ikiwa ni
pamoja na utunzaji wa mazingira na urithi wa asili, kuepuka uchafuzi wa hali ya
hewa na urahisi wa kufikika.
Wasanifu wa mji huo
wakisisitiza kuhusu uendelezaji endelevu wa miji, katika usanifu wao
wamezingatia hali ya hewa ya Dodoma ambayo ni ya joto na upepo mkali, hivyo,
wametenga maeneo kwa ajili ya upandaji miti itakayopunguza kasi ya upepo na
ujenzi wa vyanzo vya maji kwa ajili ya kupoza joto.
Mkurugenzi wa
Manispaa ya Dodoma, Bw. Godwin Kunambi alitumia fursa hiyo kuwakaribisha
wawekezaji kwenda kuwekeza katika mji wa Dodoma katika miradi mbalimbali
ikiwemo mashule, hospitali, mahoteli, maduka makubwa na miundombinu mingine.
“Tumetenga eneo kubwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda ambalo limegawanywa
katika ukubwa tofauti tofauti kutegemea na mahitaji ya mwekezaji, hivyo
wahimizeni wafanyabiashara kutoka katika nchi zenu waje kuwekeza Dodoma”. Bw.
Kunambi aliwaambia Mabalozi.
Bw. Kunambi alieleza
kuwa Mpango Mkuu wa mji wa Dodoma ulisanifiwa tangu mwaka 1976 na kufanyiwa
mapitio mwaka 2010 na sasa wataalamu hao ambao wamepata uzoefu kutoka nchi
mbalimbali zikiwemo Nigeria, Malaysia, China na Malawi ili kusanifu mji unaozingatia
mahitaji ya sasa.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 16 Februari
2018
|