Sunday, January 27, 2019

Ziara ya Kampuni kubwa za uwekezaji kutoka Austria na India


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ziara ya Kampuni kubwa za uwekezaji kutoka Austria na India
Ujumbe wa Makampuni 16 makubwa ya uwekezaji kutoka Austria utafanya ziara ya kikazi hapa nchini kuanzia tarehe 28 hadi 30 Januari, 2019.

Ziara ya ujumbe huo nchini ni mwendelezo wa jitihada za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani ambao unawakilisha pia nchini Austria na wadau mbalimbali katika kutekeleza diplomasia ya uchumi.  Pamoja na mambo mengine, diplomasia ya uchumi inalenga kwenye kutafuta na kuleta wawekezaji wenye nia ili wawekeze katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kukuza uchumi na kuinua kipato cha wananchi.

Makampuni hayo ya Austria yana nia ya kuangalia fursa za uwekezaji hapa nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, mawasiliano ya simu, umeme wa kutumia maji na usafirishaji.

Ukiwa nchini, ujumbe wa Kampuni 8 umeomba kuonana na kufanya majadiliano na viongozi wa Wizara mbalimbali tarehe 29 Januari, 2019 jijini Dodoma akiwemo Mhe. Japhet Ngailonga Hasunga (Mb.), Waziri wa Kilimo; Mhe. Dkt. Medard Kalemani (Mb.), Waziri wa Nishati; Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb.), Waziri wa Fedha na Mipango; Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto na Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Lengo la ujumbe huo kukutana na Mawaziri hao ni kutaka kufahamu kuhusu kazi na miradi mbalimbali inayosimamiwa na kutekelezwa na wizara hizo ili waone namna ya kuwekeza katika maeneo hayo.


Aidha, ujumbe huo utashiriki kwenye Kongamano la Biashara lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Chama cha Wafanyabiashara, Wakulima na Wenyeviwanda Tanzania (TCCIA) na Ubalozi wa Austria. Kongamano hilo litafanyika kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam tarehe 28 Januari 2019.

Serikali ya Tanzania na Austria zina mahusiano ya kidiplomasia ya muda mrefu tangu uhuru ambapo Austria imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) hapa nchini hususan katika sekta ya kilimo, afya na kuwajengea uwezo wanawake. Ziara ya ujumbe wa makampuni hayo ni dalili njema za kuanza kuimarika zaidi kwa mahusiano kati ya Tanzania na Austria.

Wakati huohuo, Ujumbe wa wawekezaji kutoka Kampuni ya Bureau Facility Services Pvt Ltd (CISB) ya India utafanya ziara hapa nchini kuanzia tarehe 29 Januari hadi 05 Februari 2019. Ziara hiyo ina lengo la kukamilisha utaratibu wa kuwekeza katika maeneo kadhaa ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha madawa, kutafuta fursa ya kuwekeza kwenye miundombinu kama vile barabara na madaraja na ujenzi wa nyumba na hoteli. Wajumbe hao wanatarajia kukutana na kufanya mazungumzo na Mawaziri na Viongozi Wakuu Waandamizi wa sekta husika.

Ujumbe huo wa watu watatu utaongozwa na Bw. Alban Rodricks kutoka CISB ambaye alishafanya ziara hapa nchini mara kadhaa. Aidha, Ujumbe huo unatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Hamisi Kigwangala (Mb.), Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb.), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto na Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe (Mb.), Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Mhe. Angellah Kairuki (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji.

Katika ziara yao hiyo fursa mbalimbali za kiuwekezaji zinatarajia kuibuliwa pamoja na kujadiliana namna bora ya kushirikiana kati ya Tanzania na India.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
27 Januari 2019

Kuwahudumia Wakimbizi ni jukumu la Wote sio la Nchi moja

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kuwahudumia Wakimbizi ni jukumu la Wote sio la Nchi moja

Kazi ya kuwahudumia wakimbizi ni Ubinadamu na ni jukumu la kimataifa na ni kitu cha kushangaza kuona nchi zilizoendelea zinaziachia nchi masikini kubeba mzigo wa kugharamia wakimbizi.
Kauli hiyo ilitolewa na Rais Mstaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa Baraza la Wakimbizi Duniani (World Refugees Council-WRC), Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa kuwasilisha ripoti ya Baraza hilo kwenye Umoja wa Mataifa New York, Marekani tarehe 24 Januari 2019.
Rais Mstaafu alitanabainisha kwamba Baraza lao lilipokea msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kukataa mpango wa kukopa Benki ya Dunia ili kuwahudumia wakimbizi wakati yenyewe inadaiwa mikopo ya kimaendeleo iliyonayo. Serikali inaamini kazi ya kuhudumia wakimbizi ni ya kibinadamu kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa badala ya kuibebesha nchi moja mzigo wa madeni.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa tatizo la wakimbizi limekuwa kubwa sana duniani wakati huu kuliko wakati wowote ule tangu vita vya Pili vya Dunia.  Mathalan, kuna idadi ya watu milioni 68.5 waliopoteza makwao (Internally displaced persons) mwaka 2017 na kati yao, milioni tatu wamepoteza makwao kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa na uchafuzi wa mazingira.
Ripoti inaeleza kuwa, kumekuwa na ongezeko kubwa la wakimbizi na wanaopoteza makwao kusini mwa jangwa la Sahara ambao walifikia milioni 18.4 mwaka 2017 ukilinganisha na idadi ya milioni 14.1 mwaka 2015.
Ripoti inabainisha kuwa ongezeko hilo limetokana na sababu mbalimbali zikwemo upvotevu wa amani katika nchi zao.
 Ripoti inazidi kubainisha kuwa asilimia 30 ya watu wote duniani mwaka 2017 walikuwa wakimbizi na waliopoteza makwao ukilinganisha na asilimia 23 ya mwaka 2015. Kati ya idadi hiyo, wanaotoka Afrika, asilimia 79% wanatoka katika nchi za Somalia, Nigeria, Sudan kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati. 
Ripoti imeeleza nchi zinazopokea wakimbizi wengi kuwa ni pamoja na Uganda, wakimbizi milioni moja na laki nne; Ethiopia, laki Tisa; Tanzania laki tatu na ishirini na Sita elfu; na Rwanda elfu 84.  Baadhi ya nchi zimechukua wakimbizi hao ikiwemo Marekani, Canada, Australia na Finland ingawa idadi yao ni ndogo mno. 
Katika ripoti hiyo, baraza limetoa mependekezo mbalimbali ya kukabiliana na tatizo la wakimbizi duniani.  Mapendekezo makubwa ni pamoja na kudhibiti nchi ambazo zinachochea au kuanzisha migogoro kwa kuweka mfumo thabiti wa kimataifa, kuongeza usuluhishi wa migogoro, kutowanyanyapaa wakimbizi kwa kujenga ukuta na kusaidia juhudi za kutafuta amani katika maeneo yenye migogoro. 
Baraza la Wakimbizi duniani ni chombo kilichoundwa na wataalamu mbalimbali wakiwemo wanasiasa, watafiti na watunga sera kwa lengo la kufanya utafiti wa kina utakaosaidia kubuni njia na mbinu za kitaalamu na za ubunifu zitakazosaidia kukabiliana na kumaliza kabisa tatizo la wakimbizi duniani.
  
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma
27 Januari 2019

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Wakimbizi Duniani (World Refugees Council, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete (mstari wa mbele wa kwanza kushoto) akiwa na viongozi mbalimbali jijini New York baada ya Baraza hilo kuwasilisha ripoti kwenye Umoja wa Mataifa ya namna ya kukabiliana na tatizo la wakimbizi duniani. Picha inaonesha kitabu cha ripoti iliyowasilishwa.

Mheshimiwa Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Balozi Modest J. Mero (kushoto) na viongozi wengine wa Baraza la Wakimbizi Duniani.

Saturday, January 26, 2019

Dkt. Mahiga amwakilisha Rais katika Jukwaa la Uchumi Duniani

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Dkt. Mahiga amwakilisha Rais katika Jukwaa la Uchumi Duniani

Tanzania imesisitiza umuhimu wa kukabili uhaba wa chakula kwa kuzalisha mazao kwa kutumia utalaamu wa kisasa kwa kuwpatia wakulima pembejeo na masoko ya uhakika ya chakula cha ziada.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) wakati wa kuchangia mjadala unaohusu uhakika wa chakula na changamoto za uhaba wa chakula duniani katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum-WEF) unaofanyika Davos, Uswisi kuanzia tarehe 22 hadi 25 Januari 2019.

Mhe. Mahiga alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika jukwaa hilo ambalo kaulimbiu ya mwaka huu ni Kutengeneza Mazingira ya Utandawazi wa Dunia kwa ajili ya Mapinduzi ya Kisasa ya Nne ya Viwanda “Shaping a Global Architecture in the Age of the Fourth Industrial Revolution”.

Katika mkutano huo, ajenda kuu zilizojadiliwa ni pamoja na Mapinduzi ya Nne ya Viwanda, Agenda ya Afrika ya Maendeleo, Hali ya Ulinzi na Usalama Pembe ya Afrika, changamoto za biashara ya kimataifa, ushirikiano wa Bara la Ulaya na Afrika katika ajenda mpya ya maendeleo.

Tanzania ilialikwa kuchangia mjadala unaohusu uhakika wa chakula na changamoto za uhaba wa chakula duniani pamoja na ajenda ya uwezeshaji wa mawasiliano ya simu za mkononi. Katika ajenda hiyo, Tanzania ilitoa wito wa umuhimu wa teknolojia katika kuboresha utaalamu katika sekta ya kilimo kwa ajili ya kuwawezesha wakulima wadogo waliopo vijijini.

Hili ni Jukwaa la pekee ambalo linakutanisha kwa pamoja Viongozi wa Serikali kutoka mabara yote duniani, Taasisi na Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa Makampuni Makubwa ya Kibiashara kwa ajili ya kujadili maendeleo na mwelekeo wa uchumi duniani.

Kando ya Mkutano huo, Mhe. Dkt. Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa mashirika na makampuni ambayo yapo Tanzania na yanayohitaji kupanua wigo kama vile Tigo na General Electric na makampuni yanayotafuta fursa za kuwekeza Tanzania. Aidha, alikutana na Rais wa WEF, Mhe. Borge Brende ambapo aliahidi kushawishi wawekezaji kuwekeza Tanzania na kuandaa Jukwaa la wawekezaji wa kimataifa la Tanzania ili waweze kuwekeza Tanzania.

Viongozi wengine waliokutana na Waziri Mahiga ni pamoja na; Bw. Scott Strazik, Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Gesi yenye Makao makuu yake Atlanta, Georgia- Marekani; Bw. Richard Hatchett, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kupambana na magonjwa ya Mlipuko (Coalition for Epidermic Preparedness Innovations); Bi. Rachel Samren, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Millicom ambayo TIGO ni Tawi la Kampuni hiyo, na Bw. Mohamed Al-Beity, Mtanzania aliyetambuliwa na Jukwaa la Uchumi Duniani kwa mradi wa kutangaza Utalii wa Tanzania kwa njia ya Mtandao (Tanzania Digital Tourism).


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma
 26 Januari 2019
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Kulia) akichangia Mjadala wa Changamoto za Usalama na uhaba wa Chakula Duniani tarehe 24 Januari 2019 Davos, Uswisi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine akizungumza na Rais wa WEF, Mhe. Borge Brende tarehe 25 Januari 2019 Davos, Uswisi
Mhe. Waziri Mahiga akifanya mazungumzo na  Bi. Rachel Samren, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Millicom (Millicom International Cellular S.A) tarehe 25 Januari 2019 Davos, Uswisi.


Mawaziri wa Tanzania na Uganda wajadili Ujenzi wa Bomba la Mafuta

Ujumbe wa Tanzania uliokwenda nchini Uganda kwa ajili ya ya mkutano wa majadiliano ya ujenzi wa Bomba la kusafirisha mafuta ghfi kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga, ujumbe huo kutoka kulia ni Mhe. January Makamba (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira); Mhe. William Lukuvi(Mb), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mhe. Dkt. Medard Kalemani (Mb), Waziri wa Nishati; Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria na Mhe. Dkt. Aziz Mlima, Balozi wa Tanzania nchini Uganda. 
Mkutano wa Bomba la Mafuta ghafi ulifanyika Kampala Uganda kuanzia tarehe 21 hadi 25 Januari 2019. Mkutano huo ulianza kwa ngazi za Wataalam, Makatibu Wakuu na kuhitimishwa kwa ngazi ya Mawaziri. Mkutano ulienda vizuri na upo katika hatua nzuri ya majadiliano ili kuanza utekelezaji. Pande zote mbili zimekubaliana mambo mbalimbali ya msingi ambayo.yanafungua na kuandaa njia za utekelezaji wa Mradi.

Mhe. Dkt. Aziz Mlima, Balozi wa Tanzania nchini Uganda (kushoto) akiwa katika kikao cha wataalamu cha kujadili utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Mhe. January Makamba (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) akichangia jambo katika mkutano huo.

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya mkutano huo kumalizika. kushoto kwake ni Waziri wa Nishati na Maendeleo ya adini wa Uganda, Mhe. Irene Muloni.

Tanzania na Bosnia na Herzegovina Kuanzisha Mahusiano ya Kidiplomasia

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Balozi Modest J. Mero (kulia) na Mwakilishi wa Kudumu wa Bosnia na Herzegovina katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Ivica Dronjic wakiweka saini Makubaliano ya kuanzisha Mahusiano ya Kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bosnia na Herzegovina. Makubaliano hayo ambayo yatazingatia Mkataba wa Vienna wa masuala ya mahusiano ya kidiplomasia wa Mwaka 1961 uliwekwa saini New York, Marekani tarehe 25 Januari 2019.  
Afisa wa Ubalozi, Bibi Lilian Mukasa akitoa maelekezo ya namna Waheshimiwa Mabalozi watakavyosaini Makubaliano ya kuanzisha mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi zao.
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Balozi Modest J. Mero (kulia) na Mwakilishi wa Kudumu wa Bosnia na Herzegovina katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Ivica Dronjic wakibadilishana Nyaraka ya Makubaliano baada ya wawili hao kuweka saini.




Friday, January 25, 2019

Tanzania yashinda Tuzo Maonesho ya Kimataifa ya Utalii, India


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tanzania yashinda Tuzo Maonesho ya Kimataifa ya Utalii, India
Ubalozi wa Tanzania, New Delhi, Taasisi za Serikali na kampuni binafsi mbalimbali za utalii nchini zimeshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Mwaka 2019 nchini India yajulikanayo kama OTM 2019 [Outbound Travel Mart-2019] kwa lengo la kutangaza na kutafuta fursa mpya za soko la utalii nchini humo.
Maonesho hayo maarufu na makubwa kabisa katika ukanda wa Asia-Pasifiki yalianza tarehe 23 Januari, 2019 na yamemalizika leo tarehe 25 Januari, 2019, Maonesho haya hufanyika kila mwaka katika Jiji la Mumbai na kushirikisha taasisi mbalimbali za utalii duniani.
Taasisi za Serikali zinazoshiriki ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Kituo cha Kutangaza Utalii wa Zanzibar India [Zanzibar Tourism Promotion Centre]. Kwa upande wa kampuni binafsi ni Leopard Tours, Zara Tours, Ngarawa Hotel and Resort, DOTCOM Safaris Ltd na Jackal Adventures.
Katika Maonesho hayo, Banda la Tanzania limeibuka Mshindi wa Kwanza kwa upande wa Banda bora lilopambwa kwa unadhifu na kuvutia watu wengi [The winner of Best Decoration Award].
Balozi wa Tanzania nchini India Mhe. Baraka Luvanda amesema kuwa maonesho hayo ni fursa adhimu kwa nchi kutangaza vivutio vya utalii ambapo wafanyabiashara wapatao 15,000 wanaojishughulisha na masuala ya utalii walishiriki kutoka katika mataifa zaidi ya 50 duniani. Washiriki wamepata fursa ya kupeana taarifa muhimu kuhusu mwelekeo na maendeleo ya biashara ya utalii katika maeneo mbalimbali duniani, vivutio vipya pamoja na kufanya biashara.
Akiwa katika maonesho hayo, Balozi Luvanda alieleza kuwa maonesho yalisaidia washiriki kukutana na wadau na kuanzisha uhusiano wa kibiashara unaotarajiwa kufungua soko la utalii nchini baada ya wadau hao kupata maelezo ya kutosha kuhusu vivutio vilivyopo nchini na faida zake. Kwa ujumla, India ina soko kubwa la utalii. Tunategemea idadi ya watalii kutoka India wanaokwenda Tanzania itaongezeka mara dufu baada ya kuanza kwa safari za ndege za Shirika la Ndege la Tanzania [Air Tanzania] moja kwa moja kutoka Tanzania kuja India ambapo zinategemewa kuanza kabla ya mwezi wa Juni 2019.

‘Nachukua fursa hii kwa dhati kuwapongeza sana Maafisa wote walioshiriki katika Banda letu la Tanzania la Maonesho kwa kazi nzuri iliyowezesha ushindi huo wa kwanza kwa upande wa Banda bora lilopambwa kwa unadhifu na kuvutia watu wengi [The winner of Best Decoration Award]”, alisema Balozi Luvanda.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
25 Januari 2019
Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Utalii wa India, Mhe. K. J. Alphons akiwa katika banda la Tanzania. Kulia kwake ni Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akiwa na washiriki wengine katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Mwaka 2019 Jijini Mumbai, India tarehe 23 Januari, 2019

Picha ya pamoja ya washiriki baada ya kupokea Tuzo ya ushindi wa kwanza kwa upande wa Banda bora la maonesho lilipambwa kwa unadhifu na kuvutia watu wengi [The Winner of Best Decoration Award] katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Mwaka 2019 Jijini Mumbai, India tarehe 25 Januari, 2019.

Wageni mbalimbali wanatembelea banda la Tanzania ili kupata maelezo kuhusu vivutio vya utalii nchini.

Wageni katika banda la Tanzania wakipata maelezo kuhusu fursa na vivutio vya utalii nchini.




Naibu Waziri awasilisha taarifa ya Wizara ya utekelezaji wa majukumu kwa Kamati ya Bunge ya Nje, Ulinzi na Usalama



Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara kwa Kipindi cha Julai hadi Desemba, 2018 mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) (hawapo pichani) kilichofanyika kwenye Ofisi za Bunge, Dodoma tarehe 25 Januari, 2019. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan M. Mwinyi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), Mhe. Mussa Azan Zungu akizungumza wakati wa kikao kati ya Wajumbe wa Kamati ya NUU na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kulia ni Katibu wa Kamati
Sehemu ya Wakurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Salum Mwinyi Rehani akichangia jambo wakati wa kikao kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kushoto ni Mhe. Ruth Mollel, Mjumbe wa Kamati hiyo.
Mjumbe wa Kamati, Mhe. Fakharia Shomar Khamis nae akichangia hoja wakati wa kikao kati ya Kamati ya NUU na Wizara
Sehemu nyingine ya Wakurugenzi kutoka Wizarani wakifuatilia kikao


Wakurugenzi kutoka Wizarani wakisoma nyaraka mbalimbali wakati wa kikao

Juu na chini ni Wakurugenzi kutoka Wizarani
Wajumbe wa Kamati ya NUU wakifuatilia kikao
Kikao kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 
Mjumbe wa Kamati, Mhe. Prosper Mbena akichangia jambo wakati wa kikao
Mjumbe wa Kamati, Mhe. Janeth Masaburi nae akichangia jambo
Mhe. Mboni Mhita ambaye ni Mjumbe wa Kamati akitoa ushauri kwa Wizara kuhusu kuboresha masuala mbalimbali katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi


Mjumbe wa Kamati ya NUU, Mhe. Shamsi Vuai Nahodha nae akizungumza
Wajumbe wa Kamati wakifuatilia kikao
Watumishi kutoka Wizarani wakifuatilia kukao

Thursday, January 24, 2019

Mama Shamim Khan atunukiwa tuzo ya heshima nchini India

Mbunge wa zamani na aliyekuwa Naibu Waziri kwenye Wizara mbalimbali nchini, Mama Shamim Khan akitunukiwa Tuzo ya Juu (Pravasi Bharatiya Samman Award ) na Rais wa India, Mhe. Ram Nath Kovind tarehe 23 Januari, 2019. Kushoto kwake ni Waziri Mkuu wa Mauritius, Mhe. Pravid Kumar Jugnauth ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa Mkutano wa 15 wa Diaspora wa India uliofanyika katika mji wa Varanasi, Utter Pradesh nchini humo.
Rais wa India, Mhe. Ram Nath Kovind akihutubia katika hafla ya kuhitimisha Mkutano wa 15 wa Diaspora wa India [15thPravasi Bharatiya Divas 2019] uliofanyika tarehe 23 Januari, 2019 katika mji wa Varanasi, Uttar Pradesh nchini India 
Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkubwa wa 15 wa Diaspora wa India uliofanyika katika mji wa Varanasi, Utter Pradesh, India
Picha ya pamoja



Mama Shamim Khan katika picha ya pamoja na Afisa Ubalozi wa Tanzania, New Delhi, Dkt. Kheri Goloka baada ya kupokea Tuzo tarehe 23 Januari, 2019.
=======================================================================


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Yah: Mama Shamim Khan atunukiwa tuzo ya juu ya heshima na Mhe. Ram Nath Kovind, Rais wa India

Mbunge wa zamani na aliyekuwa Naibu Waziri kwenye Wizara mbalimbali nchini, Mama Shamim Khan ametunukiwa Tuzo ya Juu ya Heshima (Pravasi Bharati yan Samman Award) na Rais wa India, Mhe. Ram Nath Kovind. Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa Mkutano wa 15 wa Diaspora wa India (15th Pravasi Bharatiya Divas 2019) uliofanyika kwenye mji wa Varanasi, Uttar Pradesh tarehe 23 Januari, 2019.

Mkutano huo ambao ulifunguliwa na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi  uliwahusisha viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya India akiwemo Waziri Mkuu wa Mauritania, Mhe. Pravid Kumar Jugnauth, Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Sushma Swaraj, Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Mambo ya Nje ya India, Mhe. Gen [Dr.) V. K. Singh na Waziri Kiongozi wa Jimbo la Utter Pradesh, Mhe. Yogi Adityanath.

Mama Shamim Khan ametunukiwa tuzo hiyo kutokana na mchango wake mkubwa kwa jamii hususan katika masuala ya akina mama na kudumisha amani na uhusiano mzuri wa madhehebu ya dini mbalimbali nchini. 

Wakati akimtunuku tuzo hiyo, Rais Kovind alieleza kutambua mchango mkubwa wa Mama Shamim Khan katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Watanzania wenye asili ya India wanaoishi nchini Tanzania na Serikali ya Tanzania katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi zao. Aidha, alimpongeza kwa utumishi uliotukuka. 

Kwa upande wake, Mama Shamim Khan alimshukuru sana Rais Kovind na kueleza kufarijika kwake kwa kutunukiwa Tuzo hiyo ambayo ni heshima kubwa kwake. Aidha, Mama Shamim Khan alipongeza juhudi za Serikali ya India kwa kuendelea kudumisha ushirikiano wa kidugu na wa muda mrefu uliopo baina ya Tanzania na India na amemuomba Mhe. Rais Kovind kuendelea kusaidia juhudi za Serikali ya Mhe.Rais Dkt. John P. Magufuli katika kuwaletea maendeleo watanzania.

Tuzo hiyo hutolewa kwa raia wenye asili ya India ambao wametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi wanazoishi na India. Hivyo hii imekuwa ni heshima kubwa sio tu kwa Mama Shamim Khan bali kwa Tanzania kwa ujumla.  Mama Shamim Khan aliongozana na Afisa Ubalozi wa Tanzania nchini India, Dkt. Kheri Goloka kwenye hafla hiyo.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
24 Januari 2019





Wednesday, January 23, 2019

Balozi wa Tanzania, Ujerumani awasilisha hati za utambulisho nchini Bulgaria

Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani ambaye anawakilisha pia nchini Bulgaria , Mhe. Dkt. Abdallah Posi akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Bulgaria, Mhe. Rumen Radev. Hafla hiyo ilifanyika Ikulu ya nchi hiyo hivi karibuni.
Mhe. Balozi Dkt. Posi akizungumza na Mhe. Rais Radev mara baada ya kuwasilisha hati za utambulisho
Mhe. Balozi Dkt. Posi akiagana na Mhe. Rais Radev mara baada ya kuwasilisha hati za utambulisho


Mhe. Balozi Dkt. Posi akiwa mbele ya gwaride la heshima alipowasili Ikulu ya Bulgaria kwa ajili ya kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais wa nchi hiyo.