Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiagana na Balozi wa Oman hapa Nchini Mhe. Ally Abdallah Almahruqi,mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha Sultan wa Oman,Sultan Qaboos bin Said.
Thursday, January 16, 2020
PROF. KABUDI ASAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO YA SULTAN WA OMAN
Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiagana na Balozi wa Oman hapa Nchini Mhe. Ally Abdallah Almahruqi,mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha Sultan wa Oman,Sultan Qaboos bin Said.
Wednesday, January 15, 2020
SERIKALI YAAGIZA CHUO CHA DIPLOMASIA KUTOA ELIMU KWA VITENDO ZAIDI
Serikali
imekitaka Chuo cha Diplomasia kutoa taaluma ya vitendo kwa wanafunzi
wanaojiunga na chuo hicho ili kuwawezesha wahitimu kuwa na mchango katika Taifa
hususani wakati huu wa utekelezaji wa sera ya Diplomasia ya Uchumi.
Akihutubia
mahafali ya 22 ya Chuo cha Diplomasia, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) ambaye ni Mgeni Rasmi
katika mhafali hayo, amesema Serikali itafurahi kusikia chuo kinatoa mafunzo ya
stratejia, jiopolitiki na demokrasia pamoja na haki za binadamu hasa kwa
muktadha wa kiafrika.
Waziri
Kabudi ameongeza kuwa taaluma inayotolewa na Chuo hicho isiwe ya nadharia pekee
bali iambatane na vitendo ili elimu hiyo itumike kusaidia kufafanua masuala ya
Kidiplomasia na uhusiano wa Kimataifa yanayotokea duniani.
"Nakiagiza
Chuo kuandaa mpango mkakati wa mafunzo kwa vitendo ili tuangalie ni jinsi gani
Wizara inaweza kusaidia. Aidha, Chuo kipitie mitaala yake mara kwa mara kama
ilivyopendekezwa ili kisipitwe na wakati. Dunia inabadilika kwa kasi. Nasi
hatuna budi kwenda kwa kasi hiyo," Amesema Prof. Kabudi.
Prof.
Kabudi ameongeza kuwa, ni vyema Chuo kikawa mstari wa mbele kutoa mafunzo hayo
kwa wanadiplomasia, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, na wafanyabiashara
waliopo hapa nchini.
"Nimefarijika
kusikia kuwa mmefanya mazungumzo na Chuo cha ISRI cha Angola kwa nia ya kufikia
makubaliano ya kutoa mafunzo ya lugha ya Kiswahili nchini Angola ambapo rasimu
ya Hati ya Makubaliano imeandaliwa na inasubiri kusainiwa," Amesema Prof.
Kabudi.
Prof.
Kabudi aliongeza kuwa, Serikali inatambua kwamba Balozi za Iran, Libya, Urusi,
Indonesia na China zimekuwa zikitumia wigo huu wa ushirikiano na kubadilishana
uzoefu, kutoa mada mbalimbali chuoni hapo. Aidha, alitumia fursa hiyo
kuzikaribisha ofisi nyingine za kibalozi hapa nchini kutembelea Chuo cha
Diplomasia na kutoa uzoefu wao kwa vinafunzi pamoja na wakufunzi. Hivyo basi,
ni vyema menejimenti ya Chuo kutoa mwaliko kwa Balozi zote na wawakilishi wa
kudumu wa Mashirika ya Kimataifa hapa nchini kuja kutoa uzoefu wao kwani nayo
itakuwa sehemu ya diplomasia ya ulimwengu.
Awali
akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Drkt. Faraji Mnyepe amesema wahitimu 453 wametunikiwa
vyeti baada ya kupata mafunzo na kufuzu ambapo kati yao 98 ni wa ngazi ya
Astashahada ya Msingi, 119 ni wa Stashahada ya kawaida, 130 ni wa Shahada, 83
ni wa Stashahada ya Uzamili, 45 Stashahada ya uzamili wa diplomasia ya uchumi.
"Nina
imani kuwa wahitimu wa leo kama wale wa miaka ya iliyopita, wameiva ipasavyo
katika fani za mahusiano ya kimataifa, Diplomasia na Stratejia. Naamin pia kuwa
mtakuwa rasilimali kubwa kwa Taifa letu katika fani mlizosomea" Amesema
Dkt. Mnyepe.
Dkt.
Mnyepe ameongeza kuwa, katika mwaka wa masomo 2019/20 chuo kimeweza kuongeza
udahili wa wanafunzi kutoka 1029 kwa 2018/19 hadi kufikia 1275 kwa mwaka wa
masomo 2019/20 ambapo pamoja na mambo mengine juhudi zinaendelea katika kutanua
wigo wa udahili kwa kuanziasha udahili wa mwezi Machi pamoja na kuanzisha
program mpya.
"Katika mwaka wa masomo 2019/20 chuo pia
kimeweza kupanua mawanda ya program zake kwa kuongeza idadi ya program za muda
mrefu. Chuo kimeanzisha Stashahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Amani na
Udhibiti wa Migogoro ambapo kwa sasa program hii inaendeshwa Dar es Salaam na
Dodoma," Amesema Dkt. Mnyepe.
Chuo
cha Diplomasia kilianzishwa rasmi tarehe 13 Januari 1978 kwa kusainiwa
Makubaliano yaliyofanywa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi zetu mbili wa wakati
huo, Mhe. Benjamini William Mkapa wa Tanzania na Mhe. Joaquim Chissano wa
Msumbiji. Kwa miaka yote hiyo, Chuo cha Diplomasia kimejikita kuwaandaa
wanadiplomasia, wanastratejia na wabobezi wengi wa masuala ya Uhusiano wa
Kimataifa.
Chuo
kilitumika kuwaandaa wapigania uhuru wa nchi ya Msumbiji na baadae kilipanua
huduma zake na kutumika kuwaandaa pia wapigania uhuru wa nchi za Angola,
Zimbabwe, Namibia n.k.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), ambaye pia alikua mgeni rasmi wa Mahafali ya 22 ya
Chuo cha Diplomasia, Dar es Salaam, akifungua rasmi Mahafali hayo yaliyofanyika
katika viwanja vya Chuo hicho Kurasini Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika MasharikiDkt. Faraji
Mnyepe akifuatiwa na Kaimu
Mkurugenzi wa Chuo, Dkt. Jeremia Ponera.
Baadhi
ya wanafunzi wakisubiri kutunikiwa
|
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji
Mnyepe akisoma hotuba yake kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi
|
Baadhi ya wahadhiri wa Chuo cha Diplomasia wakiwa wamesimama huku wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza
kwa mahafali
|
Baadhi ya Mabalozi na viongozi waandamizi wa Serikali
wakiwa wanaimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza kwa Mahafali ya 22 ya chuo cha
Diplomasia Jijini Dar es Salaam
|
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.
Palamagamba John Kabudi (Mb), akimkabidhi zawadi mmoja kati ya wanafunzi
walifaulu vizuri masomo yake |
Tuesday, January 14, 2020
NAIBU WAZIRI DKT NDUMBARO AFANYA MAZUNGUMZO NA MWAKILISHI MKAZI WA ICRC
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi (Head of Regional Delegation) wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (International Committee of the Red Cross – ICRC) katika Nchi za Tanzania,Kenya na Djibouti Bw. Olivier Dubois.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam,ambapo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuthamini mchango wa ICRC katika utoaji wa huduma na misaada ya kibinadamu hapa nchini hasa katika kambi za wakimbizi zilizopo hapa Nchini.
Amesisitiza kuwa Tanzania ikiwa ni mwanachama hai wa ICRC itaendelea kutimiza wajibu wake wa Kitaifa na Kimataifa na kwa kuzingatia Sheria za kimataifa zilizopo chini ya ICRC,sheria za Tanzania na mkataba wa uenyeji (Head Quarter Agreement) kati ya Tanzania na ICRC uliosainiwa mwaka 2001.
Kwa upande wake Bw. Dubois ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuishirikisha ICRC katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali hususani ile inayohusu utoaji wa misaada ya kibinadamu (Humanitarian assistance) kwa kushirikiana na Chama cha Msalaba Mwekundu – Tanzania (Tanzania Red Cross Society – TRCS).
Ameongeza kuwa ICRC itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau wengine katika utoaji wa huduma kwa wakimbizi walioko hapa nchini,wafungwa/mahabusu waliopo magerezani,mafunzo kwa vyombo vya ulinzi na usalama hususani wakati wa ulinzi wa amani (Training on International Humanitarian Law during peace keeping mission).
Bw. Dubois ameambatana na Bi. Andrea Heath mwakilishi Mkaazi wa ICRC – Tanzania.
Thursday, January 9, 2020
SERIKALI YAWATAKA MABALOZI KUZINGATIA SHERIA, TARATIBU ZA NCHI
Tanzania
imewataka Mabalozi, Makaimu Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa
kuzingatia sheria za nchi pamoja na mikataba ya kimataifa ili kuhakikisha kuwa
wanatekeleza majukumu yao nchini kwa ufanisi na ufasaha.
Akiongea katika mkutano na Mabalozi, Makaimu
Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema
kuwa mahusiano ya Tanzania na nchi nyingine yanajengwa katika misingi ya
mkataba wa Viena, Mkataba wa umoja wa mataifa na sheria mbalimbali, hivyo ni
vizuri mabalozi kuzingatia taratibu hizo.
"Sisi kama tumesisitiza kuwa ni vyema mabalozi
na wawakilishi wa nchi zao wakafuata taratibu, mila pamoja na desturi zilizopo
katika mikataba hiyo ili kuhakikisha shughuli zao ndani ya Tanzania zinaendana
na kufuatana na mkataba wa Viena, mkataba wa umoja wa mataifa lakini pia kunga,
mila na desturi za kibalozi," Amesema Prof. Kabudi.
Aidha, Waziri Kabudi aliongeza kuwa Tanzania
kupitia mkutano huo imeanza ukurasa mpya wa mahusiano na uendeshaji wa shughuli
za Serikali na balozi pamoja na mashirika ya kimataifa yaliyopo Tanzania.
"………tunepata nguvu mpya baada ya mabalozi wote
kueleza kuridhika kwao kwa hali ya juu sana na hatua ambazo Serikali ya
Tanzania imechukua kupambana na rushwa, kupambana na ubadhirifu wa mali za
umma, hatua ambazo Tanzania imechukua katika kuimarisha makusanyo ya kodi
lakini pia kusimamia matumizi ya fedha za ndani pamoja na zile zinazotolewa na
nchi mbalimbali katika maendeleo ya Tanzania," Amesema Prof. Kabudi.
Katika mkutano huo, Waziri Kabudi amewahamasisha
mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa hapa nchini kuhusu kuhamia Makao
Makuu ya Nchi Dodoma kwa kuwaeleza maendeleo yaliyofikiwa kuhusu ujenzi wa
miundombinu mbalimbali muhimu na kwamba wakati umefika wa kuharakisha kuhamia
Dodoma kwa wakati muafaka kwa kuwa maendeleo yaliyofikiwa nayatoa fursa ya kuwawezesha
wao kuhamia jijini Dodoma.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mabalozi hao hapa
Nchini ambae pia ni Balozi wa Comoro Dkt. Ahamada Mohamed ameipongeza Tanzania
kwa kuitisha mkutano huo mapema ikiwa ni siku tisa tu tangu kuanza kwa mwaka
mpya wa 2020 kwa nia ya kubadilishana mawazo na kusikiliza changamoto za
mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa pia kuwaelezea hatua za utekelezaji
za masuala ya maendeleo chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli jambo
linalowapa fursa mabalozi hao kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi hapa nchini.
Nae balozi wa Kenya hapa Nchini Mhe. Dan Kazungu
ambaye pia Kiongozi wa Mabalozi wa Bara la Afrika amesema wao kama mabalozi
hawawezi kujua mipango, vipaumbele na changamoto za serikali bila ya kuelezwa
na kutaka mikutano ya namna hiyo kufanyika mara kwa mara jambo ambalo linatoa
uelewa na muelekeo wa utendaji kazi wa serikali
na hivyo kusaidia kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kwa kutambua
fursa na changamoto zilizopo.
Awali akiwakaribisha mabalozi katika mkutano huo,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.
Faraji Mnyepe, aliwataka mabalozi kuhakikisha kuwa wanazingatia taratibu na
kanuni za nchi ili kuhakikisha shughuli zao ndani ya Tanzania zinaendana na
kufuatana na mkataba wa Umoja wa Mataifa.
"Nawasihi sana tufanye kazi kwa kuzingatia
taratibu za nchi pamoja na sheria na mikataba kwa manufaa ya nchi yetu
(Tanzania) na nchi zenu ili tuweze kuendelea kuimarisha uhusiano wa
kidiplomasia baina yetu kwa maendeleo endelevu" Amesema Dkt. Mnyepe
Mkutano huo umehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro,Katibu Mkuu
Dkt Faraji Mnyepe na Mkuu wa Itifaki Balozi, Kanali Wilbert Ibuge, mabalozi 28,
Makaimu Mabalozi 12 na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa 10.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe akiongea na mabalozi, (hawapo pichani) wakati wa mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na mabalozi, manaibu
mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa katika mkutano uliofanyika
leo jijini Dar es Salaam
Wednesday, January 8, 2020
PROF. KABUDI AKUTANA, KUFANYA MAZUNGUMZO NA MWAKILISHI WA UNICEF NCHINI TANZANIA
...Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro akutana, Balozi
mteule wa Ujerumani nchini
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John
Kabudi (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la
Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Shalini
Bahuguna katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Waziri Kabudi amemweleza Bi. Shalini Bahuguna kuwa UNICEF imekuwa na
mchango mkubwa sana kwa kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kukuza, kulinda na kutimiza haki za watoto.
"Kwa ujumla UNICEF imekuwa ikisaidia Tanzania kufanikisha agenda
zake za maendeleo endelevu ya kulinda, kukuza na kutunza haki za watoto…..na
tunaamini watoto hawa ni taifa la kesho," Amesema Prof. Kabudi
Waziri Kabudi amemueleza Bi. Bahuguna kuwa
tangu mwaka 2016 Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na UNICEF, imefanikiwa
kuboresha sekta za elimu na afya ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya
upatikanaji wa huduma bora za kijamii, kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa
Ukimwi na kuboresha huduma za maji katika mikoa mbalimbali ikiwemo, Dar es
Salaam, Mbeya, Iringa, Kigoma, Njombe na Songwe.
Kwa
upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto
(UNICEF) nchini, Bi. Bahuguna amesema kuwa UNICEF itaendelea kushirikiana na
Serikali ili kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kulinda haki za watoto.
"Haki za watoto katika taifa ni
jambo muhimu sana, hivyo UNICEF itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania
kuhakikisha kuwa haki za watoto zinalindwa pamoja na kupatiwa mahitaji
muhimu," Amesema Bi. Bahuguna.
Katika tukio jingine, Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amekutana
na kufanya mazungumzo na Balozi Mteule wa Ujerumani Mhe. Balozi Regine Hess.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha
uhusiano wa kihistoria wa Tanzania na Ujerumani ambao ulijengwa tangu enzi za
Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambapo Tanzania na Ujerumani zina
historia ndefu na zimekuwa zikishirikiana kwa miaka mingi katika nyanja za
kiutamaduni, kiuchumi na afya.
Katika mazungumzo hayo, pamoja na mambo
mengine, Mhe. Naibu Waziri alisisitiza umuhimu wa ushirikiano unaolenga kuleta
tija katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya mataifa haya mawili.
Balozi Mteule wa Ujerumani Mhe. Balozi
Regine Hess akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) wakati alipomtembelea na kufanya nae
mazungumzo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiongea na Balozi
Mteule wa Ujerumani Mhe. Balozi Regine Hess wakati Balozi Hess alipomtembelea
Naibu Waziri katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
|
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John
Kabudi (Mb) akiongea na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la
kuhudumia watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Shalini Bahuguna katika
Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
|
Mwakilishi
Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini
Tanzania, Bi. Shalini Bahuguna akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi katika
Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
|
Mwakilishi
Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini
Tanzania, Bi. Shalini Bahuguna akimkabidhi nakala ya Hati ya Utambulisho Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John
Kabudi (Mb) leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
|
Tuesday, January 7, 2020
MFANYABIASHARA KUTOKA INDIA YUKO NCHINI KUANGALIA FURSA ZA UWEKEZAJI
MFANYABIASHARA KUTOKA INDIA YUKO NCHINI KUANGALIA FURSA ZA UWEKEZAJI
Dodoma, 7 Januari 2020
Mfanyabiashara kutoka nchini India, Bw.Vivek Agarwala yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku saba kuanzia tarehe 6 hadi 12 Januari 2020. Bw. Agwarala ambaye amekuja kuangalia fursa za uwekezaji nchini, atafanya mazungumzo na Uongozi wa Benki ya CRDB, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) pamoja na kutembelea maeneo kadhaa kwa lengo la kupata maelezo kuhusu taratibu na fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.
Maeneo yatakayotembelewa na mfanyabiashara huyo ni Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA) Dar es Salaam, Mkoa wa Simiyu ambapo ataangalia uwezekano wa kupata eneo la ekari elfu mbili (2,000) kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha mpunga na ujenzi wa kiwanda zao hilo. Bw. Agarwala atatembelea maghala ya pamba ili kujiridhisha kabla ya kununua kiasi cha robota laki moja (100,000) ambayo aliahidi kununua wakati alipofanya mazungumzo na Uongozi wa Benki ya CRDB mwezi Desemba 2019.
Bw. Agarwala pia atatembelea machimbo ya Tanzanite, mkoani Manyara, Kiwanda cha Karatasi cha Mufindi kilichopo mkoani Iringa na kuangalia uzalishaji maparachichi ili kujenga kiwanda cha kusindika zao hilo kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi.
Ujio wa mfanyabiashara huyo ni matokeo ya juhudi za Ubalozi wa Tanzania nchini India ambao uliratibu ziara ya kikazi iliyofanywa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji-Uendeshaji na Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts iliyofanyika nchini India mwezi Desemba mwaka jana. Ziara hiyo ililenga kutafuta wawekezaji kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo soko la pamba nchini humo.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali.
Friday, December 27, 2019
Mhe. Waziri Kabudi akutana na kupokea nakala za Hati za Utambulisho za Mabalozi Wateule wa Algeria na Ujerumani
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John
Kabudi (Mb) amekutana, kufanya mazungumzo na kupokea nakala za Hati ya Utambulisho
ya Balozi Mteule wa Algeria Mhe. Ahmed
Djellal pamoja na Balozi Mteule wa Ujerumani Mhe. Balozi Regine Hess.
Prof. Kabudi amekutana na mabalozi hao wateule leo jijini Dar es
Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, kabla ya kukabidhiwa nakala za hati za
utambulisho kukoka kwa mabalozi hao, Prof. Kabudi amefanyaa mazungumzo na Mabalozi
wateule ambapo mazungumzo hayo yaliyolenga kuimarisha uhusiano kati ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria pamoja
Shirikisho la Ujerumani.
Waziri Kabudi alimweleza Balozi mteule
wa Algeria nchini Tanzania kuwa Tanzania na Algeria zimeendelea kuwa na
uhusiano mzuri na wa kihistoria tangu miaka ya 1960 wakati wa harakati za
ukombozi wa bara la Afrika dhidi ya ukoloni…"Misingi ya uhusiano wa
Tanzania na Algeria ulijengwa na Waasisi wa Mataifa haya mawili, Hayati Mwl.
Julius Nyerere na Hayati Ahmed Ben Bella wa Algeria," Amesema Prof. Kabudi
Waziri Kabudi ameongeza kuwa, Algeria
imeendelea kuwa na Ubalozi wake hapa nchini Tanzania tangu mwaka 1964 ikiwa ni
miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa kufungua ubalozi hapa nchini. Mwaka 1981
nchi hizi mbili zilianzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC)
ambayo imechangia kuimarisha na kukuza ushirikiano katika masuala mbalimbali
ikiwemo diplomasia, ulinzi, elimu, madini, nishati na michezo.
"Mimi
Balozi Mteule nitashughulikia na kuhakikisha kwamba uwekezaji na biashara
unaofanywa kati ya Algeria na Tanzania unakuwa wa manufaa kwa pande zote mbili
lengo likiwa ni kukuza sekta ya biashara hapa Tanzania" Amesema Mhe.
Balozi Djellal
Katika tukio jingine, Prof. Kabudi
amepokea nakala za Hati ya Utambulisho za Balozi Mteule wa Shirikisho la
Ujerumani hapa nchini, Mhe. Balozi Regine Hess ambaye amemweleza Waziri Kabudi
kuwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Ujerumani ni mzuri na
kuongeza kuwa jukumu lake kubwa kwa sasa ni kuendeleza uhusiano huo.
Balozi Regine Hess ameyasema hayo
wakati akikabidhi nakala za Hati ya Utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb).
Balozi Regine Hess amesema
kuwa mbali na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Ujerumani,
ushirikiano mzuri uliopo wa uwekejzaji, biashara, utalii na elimu utaendelea
kuimarika na kutoa zaidi fursa za maendeleo kwa Tanzania.
"Kuna baadhi ya wawekezaji kutoka
Ujerumaani ambao wameshaonesha nia ya kutaka kuwekeza Tanzania, hivyo
nitawasiliana nao na kuweza kujua wamefikia wapi kwani Tanzania ina sifa nzuri.
Jukumu langu nikiwa Balozi hapa ni kukuza na kuendelea kuimarisha uhusiano wa
kidiplomasia baina ya Ujerumani na Tanzania, hivyo nitajitahidhi niwezavyo
kufanikisha jukumu hilo," Amesema Balozi Hess.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akisoma nakala ya Hati ya Utambulisho
mara baada ya kukabidhiwa na Balozi Mteule wa Shirikisho la Ujerumani hapa
nchini katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akisoma nakala ya Hati ya Utambulisho
mara baada ya kukabidhiwa na Balozi Mteule wa Shirikisho la Ujerumani hapa
nchini Mhe. Balozi Regine Hess katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
|
Balozi Mteule wa Shirikisho la Ujerumani Mhe.
Balozi Regine Hess akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) kabla ya kuwasilisha nakala ya Hati
ya Utambulisho. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini
Dar es Salaam.
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akimkaribisha Balozi Mteule wa
Shirikisho la Ujerumani Mhe. Balozi Regine Hess alipowasili katika Ofisi ndogo
za Wizara jijini Dar es Salaam kuwasilisha nakala ya Hati ya Utambulisho kwa
mhe. waziri
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na Balozi mteule wa
Algeria nchini Tanzania Mhe. Balozi Ahmed Djellal kabla ya kuwasilisha nakala ya
Hati ya Utambulisho. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara
jijini Dar es Salaam.
|
Balozi mteule wa Algeria nchini Tanzania Mhe.
Balozi Ahmed Djellal akimkabidhi nakala ya Hati ya Utambulisho Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb)
leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Subscribe to:
Posts (Atom)